Tuesday, June 24, 2014

Kardinali Pengo aweka jiwe la msingi la Chuo Kikuu MUCO Bagamoyo!

Kanisa Katoliki nchini Tanzania linaendelea kuwekeza kikamilifu katika sekta ya elimu ili kuwasaidia watanzania kuwa na majiundo kamili ili kukabiliana barabara na changamoto za maisha, ili hatimaye, Tanzania iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Shirika la Roho Mtakatifu ambalo kwa miaka mingi limewekeza na kuona mafanikio makubwa katika sekta ya elimu nchini Tanzania, sasa limeanza kujielekeza katika kuanzisha Kitivo cha Sayansi kitakachokuwa chini ya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augostino cha Tanzania, SAUT. Kitivo hiki kitajulikana kama “Marian University College”, kwa kifupi MUCO, ambacho kinajengwa kwenye mji mkongwe wa Bagamoyo, Mkoani Pwani, nchini Tanzania.

Hivi karibuni, Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Chuo kikuu cha MUCO na kwamba, mwezi Septemba, 2014 kitaanza kuandikisha wanafunzi, wakati huo huo ujenzi wa majengo mengine ukiendelea kukamilishwa hatua kwa hatua. Katika hafla ya kuweka jiwe la msingi, Kardinali Pengo amesema, nchi ambayo haina wataalam wa sayansi, kwa hakika itachechemea katika ushindani wa maendeleo na mataifa mengine. Umefika wakati kwa watanzania kujiekeza zaidi katika masuala ya kisayansi ili kupata maendeleo endelevu yanayogusa mahitaji msingi ya binadamu: kiroho na kimwili.

Akizungumza katika tukio hili Padre Florentin Mallya, Makamu mkuu wa Shirika la Roho Mtakatifu Afrika Mashariki amesema, MUCO itaendelea kushirikiana na SAUT, hadi pale mchakato wa kukiwezesha Chuo kikuu cha MUCO kujitegemea na kuwa Chuo kikuu kamili. Kuanzishwa kwa MUCO ni kujibu kwa dhati changamoto inayotolewa na Serikali ya Tanzania kwa sekta binafsi kusaidia mchakato wa kukuza na kuendeleza sekta ya elimu hususan katika mchepuo wa sayansi, ili kujibu mahitaji makubwa yanayoendelea kujitokeza ndani na nje ya Tanzania katika masuala ya elimu.

Huu ni mwendelezo wa huduma ya elimu inayotolewa na Shirika hili katika shule zake za awali na sekondari ambazo kwa miaka mingi zimeendelea kupeta nchini Tanzania kutokana na wanafunzi wanaohitimu katika shule hizi kuwa na kiwango kikubwa cha ufaulu kwenye mitihani. Wazazi waliokuwa wanahaha kuwatafutia watoto wao mahali pazuri zaidi pa kusoma, sasa MUCO itakuwa ni jibu lao makini.

Ni kutokana na changamoto zote hizi, Shirika la Roho Mtakatifu liliomba ushirikiano na Serikali ya Tanzania ili kutekeleza azma hii kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watanzania tangu shule za msingi hadi chuo kikuu. Shirika linapania kuendelea kutoa kiwango bora cha elimu kwa kutambua kwamba, hii ni sehemu ya Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Shirika linaiomba Serikali ya Tanzania pamoja na wazazi kuendelea kuonesha mshikamano katika kufanikisha malengo ya maboresho ya elimu nchini Tanzania.

No comments:

Post a Comment

NCHI YANGU FAHARI YANGU TOUR