Saturday, April 13, 2013

Msitafute njia ya mkato katika maisha!




Katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya mwezi mmoja tangu Baba Mtakatifu Francisko alipochaguliwa kuliongoza Kanisa, Jumamosi, tarehe 13 Aprili 2013 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu iliyohudhuriwa na Wanajeshi wa Kikosi cha Zimamoto cha Vatican na Watawa wa Upendo kwenye Kikanisa cha Domus Sanctae martha, kilichoko mjini Vatican.

Papa amewakumbusha kwamba, hata katika mahangaiko, mateso na shida mbali mbali anazoweza kukabiliana nazo mwamini, kamwe asithubutu kutafuta njia ya mkato bali wajiaminishe kwa Mwenyezi Mungu. Waamini wa Kanisa la Mwanzo, kadiri ya Matendo ya Mitume, walijikuta wanaanza kulalamikiana na kubaguana katika huduma mambo ambayo yalikuwa yanadhohofisha umoja na mshikamano wa upendo miongoni mwa wafuasi wa Kristo. Mitume wakachukua uamuzi wa kuwakutanisha na kujadiliana kwa pamoja na hatimaye, wakapata suluhisho la matatizo yao.

Mitume walibainisha kwamba, dhamana yao ya kwanza ni kusali na kutangaza Habari Njema ya Wokovu; kumbe Mashemasi saba walioteuliwa walipewa dhamana ya kutoa huduma ya upendo ambayo ni mwendelezo wa huduma na mshikamano wa upendo unaofanywa na Mama Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Kristo yuko daima pamoja na wafuasi wake na kamwe hawezi kuwaacha wakaangamia.

Baba Mtakatifu anasema, hivi ndivyo ilivyotokea pale mitume wake walipokuwa wameelemewa na hofu pamoja na woga, akawatokea na kuwaambia wasiogope. Hata kama waamini wanakosea, wasikate tamaa, bali watambue kwamba, Yesu yuko pamoja nao. Wachunguze pale walipokosea, wajiwekee mikakati ya kusahihisha na kurekebisha pamoja na kujipa moyo wa kusonga mbele kwa imani na matumaini zaidi. Waamini kamwe wasitafute njia ya mkato katika maisha!

No comments:

Post a Comment

NCHI YANGU FAHARI YANGU TOUR