Tuesday, April 16, 2013

ZIARA YA UINJILISHAJI 26-30/06/2013

Wapendwa VIWAWA, tunawakaribisha kushiriki katika ziara ya uinjilishaji, itakayofanyika katika jimbo la mbulu Parokia ya daudi.
Lengo kubwa la ziara hii ni kwenda kuinjilishaji wa Kina ambapo kwa kushirikiana na walezi wetu pamoja na mwenyeji wetu tutachambua mambo yafuatayo:
  1.  Ufundishaji wa dini ulio utoaji wa Elimu katika kweli. 
  2. Mapokeo ya Mwaka wa Imani kwa Vijana
  3. Hali ya Utii na Unyenyekevu(maadili ya Vijana)
  4. Utume wetu wa vijana(maswala ya jamii, siasa na uchumi)
  5. Na mengine mengi  
waweza tafakari mafundisho haya ya dini
Kanisa linapofundisha juu ya Mungu au linapozungumza juu ya Mungu linatoa elimu katika ukweli, elimu inayolenga kumjenga Mwanadamu katika ubinadamu wake. Tangu mwanzo Kanisa limejikita katika Elimu si kwa sababu nyingine yoyote bali kumwinua binadamu katika ubinadamu akapate kujifahamu yeye ni nani, ametoka wapi na kwa nini yuko pale alipo. Mtaguso Mkuu wa Vatikan umesisitiza pia juu ya mfungamano kati ya uinjilishaji na utoaji wa Elimu.

Baba Mtakatifu Benedikto XVI anakazia uzito ukweli huu anapozungumzia utume msingi wa Kanisa wa uinjilishaji unaotoa kipaumbele katika elimu na kuwianisha na malengo ya Taifa lolote kuendeleza na kuiinua jamii katika hadhi inayotegemewa. Ikumbukwe kwamba Kanisa katika utume wake linaoanisha daima dhana za imani na akili kwamba imani huiangaza akili kutambua ukweli na hivyo kumfanya binadamu kuutambua ukweli ulio msingi wa maisha adilifu yampasayo kuishi.

Baba Mtakatifu Benedikto XVI anakazia kuwepo kwa muungano kati ya uinjilishaji na utoaji wa elimu hasa nyakati hizi ambapo elimu dunia inaelekea kumpoteza mwanadamu katika ulimwengu. Hivyo amelialika Kanisa kulichukulia makini suala la uenezaji wa Imani kufungamana na utoaji wa elimu ili kweli elimu itoe ujuzi na maarifa ya kumwendeleza mtu mzima kiroho na kimwili.

Baba Mtakatifu Benedikto XVI ametahadharisha kuwa mfumo wa elimu hivi sasa umeshindwa kutoa malezi bora kwa kizazi kipya kiasi kwamba imedhihirika wazi uwepo wa mmomonyoko wa maadili katika jamii. Elimu inayotolewa ni elimu maarifa tu bila thamani za maisha.

Nyakati hizi watu wengi wanaogopa kusema ukweli na badala yake kukimbilia propaganda za kidunia na utumbuaji wa maisha tu. Matokeo yake watu wanapumbazwa na propaganda za biashara na kuishia kufikiria kwamba maisha ni ponda mali kufa kwaja bila kuangalia thamani halisi ya maisha ya Mwanadamu.

Ulimwengu wa leo unatoa elimu amabayo haimwajibishi mwanadamu katika matendo yake na baadaye anapokutana na changamoto za maisha anakosa mwelekeo na kuishia kuchukua hatua zisizo za kibinadamu kwani ndani yake kakosa utu kageuka kitu ambacho kikikosa thamani yake hutupwa jalalani au kuchomwa moto. Baba Mtakatifu na Kanisa zima lazima liguswe na hili kwani utume wake si kuokoa roho tu bali na mwili pia ambao ndilo hekalu la roho hapa duniani.

Wajibu wa Kanisa kujikita katika utoaji Elimu ni kuboresha mazingira ya maisha ya mwanadamu. Baba Mtakatifu anasema Kanisa litawajibishwa na Bwana iwapo halitapigania kujenga utu wa mwanadamu jinsi ile alivyokusudiwa na Muumba. Hivi sasa kumekosekana heshima kwa ubinadamu hivi kwamba, watu hawathamini tena zawadi ya maisha, wanaona kama mzigo, au kitu cha kufanyia utafiti kwenye maabara kwa malengo ya kiburi tu; mimba kutupwa ovyo, biashara zilizokithiri za viungo na miili ya binadamu, na watoto kuuzwa kama bidhaa. Iko hatari hapa ya ubinadamu kukengeuka kama enzi za Sodoma na Gomora. Hivyo Kanisa lililo Mwili wa Kristo halina budi kusimama kidete kurudisha tena hadhi na thamani ya binadamu iliyo hatarini kupotea.

Baba Mtakatifu Benedikto XVI amemnukuu Baba Mtakatifu Paulo VI, kuwa Mwanadamu wa leo husikiliza zaidi ushuhuda kuliko mafundisho ya mwalimu, vinginevyo Mwalimu atasikilizwa kwa sababu anatoa ushuhuda. Hivyo amelitaka Kanisa kutumia ushuhuda wa maisha katika utoaji wa elimu kwa jamii. Maisha ya ushuhuda yanayoshuhudia ukweli wa Imani na maisha, ndicho kifundishio pekee kwa jamii ya leo.

Changamoto kwa Kanisa na Wanakanisa ni kujitoa mhanga kutoa mifano hai ya maisha yaliyojengwa katika dhamiri iliyo safi, hai na adilifu. Maisha ya utakatifu, usafi, unyenyekevu, upole, amani, haki na mshikamano ndizo silaha pekee za kumfikisha Yesu Mkombozi wa dunia kwa watu.

       Wahi sasa achukue form na ada ya ushiriki ni tshs 150,000 tu ziara itaanza tarehe 26-30/06/13 na mwisho wa kukusanja michango ni tarehe 29/05/12



 Mpendwa Kijana , Nakutakia kheri na Baraka katika kumshuhudia Yesu katika ulimwengu wa leo ambao unaonekana kupoteza maarifa. Shime Mkristu mwenzangu twende tukalirudishe lile tumaini la Kristu kwa watu hawa kwani sisi tumeona mwanga basi tuupeleke mwanga huu na kwa wengine.



No comments:

Post a Comment

NCHI YANGU FAHARI YANGU TOUR