Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 20 Oktoba 2013 amewataka waamini na watu wenye mapenzi mema kujenga utamaduni wa kusali bila kuchoka; kwa kupaaza sauti kwa Mwenyezi Mungu, usiku na mchana kwani hiki ni kielelezo cha imani makini kwa Mwenyezi Mungu ambaye daima anasikiliza kwa makini na upendo mkuu na anayafahamu mahitaji ya waja wake.
Baba Mtakatifu amewahakikishia waamini waliokuwa wamefurika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kwamba, Yesu anaendelea kufanya hija na wafuasi wake na wala hayuko mbali nao katika mapambano dhidi ya dhambi na kwamba, sala ni silaha muhimu inayomfanya mwaminifu kutambua na kuonja uwepo endelevu wa Kristo katika hija ya maisha yake hapa duniani.
Yesu anawakirimia wafuasi wake huruma na msaada wanaohitaji, kwa kutambua kwamba, mapambano dhidi ya dhambi si jambo la lelemama, bali linahitaji uvumilivu na udumifu katika sala kama alivyofanya Musa katika somo la kwanza, Jumapili ya ishirini na tisa ya kipindi cha Mwaka C wa Kanisa. Mwenyezi Mungu ni mwenza na nguvu katika mapambano haya na kwamba, sala ni kielelezo cha ushuhuda wa imani kwa Mwenyezi Mungu.
Baba Mtakatifu anasema, ikiwa kama waamini watauzima moto wa imani, kwa hakika watatembea katika giza totoro, kiasi kwamba, watapoteza dira na mwelekeo wa maisha.
Baba Mtakatifu amewapongeza wanawake wanaosimama kidete kulinda na kutetea misingi ya haki na amani kwa ajili ya familia zao bila kuchoka wala kukata tamaa. Hiki ni kielelezo cha imani thabiti, ujasiri na mfano wa kuigwa katika maisha ya sala, changamoto ya kuendelea kusali daima kama ushuhuda wa imani tendaji kwa Mwenyezi Mungu anayewapenda waja wake pamoja na kuwahamasisha kushikamana naye katika mapambano dhidi ya dhambi, ili kuweza kuyashinda malimwengu kwa njia ya wema.
Mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Baba Mtakatifu Francisko aliwakumbusha waamini kwamba, Mama Kanisa Jumapili iliyopita ameadhimisha Siku ya 87 ya Kimissionari Duniani. Utume wa Kanisa ni kuhakikisha kwamba, linawasha moto wa imani uliowashwa kwa mara ya kwanza na Yesu mwenyewe duniani. Ni moto wa imani kwa Mwenyezi Mungu ambaye ni mwingi wa huruma na mapendo. Huu ni moto ambao waamini wanapaswa kuwagawia wengine ili mioyo iweze kupata joto la ujumbe wa Mungu.
Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwashukuru wale wote wanaoshiriki kwa hali na mali katika kutegemeza shughuli za kimissionari sehemu mbali mbali duniani, lakini kwa namna ya pekee, wale wanaomsaidia Khalifa wa Mtakatifu Petro kueneza Injili sehemu mbali mbali za dunia. Mama Kanisa yuko karibu na wamissionari walioenea sehemu mbali mbali za dunia, wanatekeleza dhamana na wajibu wao katika hali ya ukimya pasi na makeke! Ni watu wanaojitosa kimasomaso kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.
Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu amemkumbuka Afra Martineli, mmissionari aliyefanya kazi za kitume nchini Nigeria kwa miaka mingi, akapendwa na wengi; lakini hivi karibuni aliuwawa kikatili nchini Nigeria. Watu wengi wamelia na kuomboleza kifo cha Afra Martineli. Hii ni kwa sababu alitangaza Injili ya Kristo kwa njia ya ushuhuda wa matendo yake, kwa kuanzisha shule, mahali ambapo aliwasha moto wa imani na kwamba, amevipiga vita vilivyo vizuri na sasa mwendo ameumaliza.
Baba Mtakatifu amemkumbuka pia Mwenyeheri Stefano Sàndor aliyetangazwa kuwa Mwenyeheri jumamosi iliyopita, huko Budapest kutokana na mchango wake mkubwa kwa majiundo ya vijana kiroho na kimwili.Mwenyeheri Sàndor alikabiliana uso kwa uso na utawala wa Kinazi, wakati ulipoanza madhulumu dhidi ya Kanisa. Akauwawa kikatiliki akiwa na umri wa miaka 39. Mama Kanisa anaishukuru Familia ya Wasaelisiani na Kanisa Katoliki nchini Hungaria.
Baba Mtakatifu Francisko amewakumbuka na kuonesha uwepo wa karibu kwa wananchi wa Ufilippini waliokumbwa na tetemeko la ardhi lililosababisha maafa makubwa kwa maisha na mali ya watu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kuwaombea wananchi hao wakati huu mgumu katika historia ya maisha yao.
Baba Mtakatifu, mwishoni amewashukuru wadau mbali mbali walioshiriki katika "Mbio za Imani" kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, jumapili iliyopita; mbio za Marathoni zilizoandaliwa na Baraza la Kipapa la Utamaduni na wadau mbali mbali kutoka Italia. Baba Mtakatifu amewakumbusha kwamba, mwamini ni mwanariadha wa maisha ya kiroho.
No comments:
Post a Comment