Sunday, November 3, 2013

Tafakari ya masomo ya leo dominika ya 31 mwaka C 03/11/13

Somo La Kwanza: Hek. 11:22-12:2
Wimbo Wa Katikati: Zab. 145: 1-2, 16-18, 123-14 (K)
Somo La Pili: 2 Thes.1: 11-2:2
Injili: Lk. 19: 1-10
Tafakari y ya masomo:
Injili ya leo, inatuadithia juu ya mtosa ushuru Zakayo. Zakayo alikuwa na mapungufu makuu mawili. Moja, alikuwa na upungufu wa asili, alikuwa mfupi wa kimo. Katika msongamano mkubwa uliokuwa unamfuata Yesu, alikuwa hana nafasi ya kumwona kwani watu warefu wangemzuia. Pili, alikuwa na upungufu wa kijamii. Kazi yake ya kutosa ushuru ilimfanya achukiwe na Wayahudi wenzake. Kwani, watosa ushuru walikuwa wadanganyifu kwa waliwatosa watu ushuru mkubwa zaidi, huku wakijitajirisha na pesa za ziada walizotosa watu. Hivyo basi, hawakupendwa na jamii ya  Wayahudi.

Pamoja na mapungufu haya ya kiasili na hata ya kijamii, ambayo yangekuwa sababu ya kutosha kabisa ya kumzuia Zakayo asimuone Yesu. Zakayo hakukubali, nafasi hii ya kumuona Yesu, impite. Alitoka mbio, akapanda juu ya mkuyu ili amuone Yesu. Yesu alizizawadia juhudi za Zakayo kwa kumuita, “Zakayo, shuka upesi, kwa kuwa leo imenipasa  kushinda nyumbani mwako.”

Yesu anamtumia Zakayo kutuonesha jinsi Mungu anavyozijali juhudi za wale wajitahidio bila kukata tamaa kutokana na mapungufu waliyonayo. Kama Zakayo asingejitahidi kutafuta mbinu za kumuona Yesu, hata kwa kupanda mkuyuni, angekufa bila kutimiza ndoto yake ya kutaka kumuona Yesu. Mara nyingi tumejiona kuwa kutokana na mapungufu yetu hatuwezi kutimiza ndoto zetu maishani. Tunapoteza muda tukisema kama ningekuwa na hili ama lile ningefanya hivi ama vile. Kama ningezaliwa mwanamke ama mwanaume ningefanya hili wala lile. Kama ningezaliwa katika familia iko hivi ningefanya hili ama lile; Kama ningekuwa na uwezo huu ama ule basi mambo yangu yangeenda vizuri; Kama muda huu, ndio ningekuwa mwanafunzi, ningesoma sana ili niwe na maisha mazuri zaidi. Mwanafunzi naye anasema, ningekuwa na akili kama fulani, ningefanya vizuri; ama ningekuwa shule bora zaidi ningesoma kwa bidii sana. Hizi ndoto za mchana hazitatusaidia. Kitakachotusaidia ni kukubali mapungufu yetu na hapo kuangalia ni kitu gani Mungu ametuwekea karibu kitakachotuwezesha kutimiza ndoto zetu. Kama Zakayo asingekuwa mtu wa jitihada, asingeona kuwa angeweza kupanda mtini na hivyo kuyashinda mapungufu yake. Kama Zakayo asingekuwa ni mtu wa maono, mkuyu ungeendelea kubakia mkuyu tu huenda ungekuwa mojawapo ya vikwazo vya kumzuia asimuone Yesu. Angeendelea kulalamika na hata kuulalamikia mkuyu. Zakayo alipoutazama mkuyu aliona jinsi unavyoweza kutumika kuwa kifaa cha kumwezesha kumuona Yesu na siyo kikwazo cha kumuona Yesu. Ufupi wake, japo ulikuwa ni upungufu wa asili ulikuwa sababu yake ya kuzitumia jitihada zake. Zakayo alikuwa na mtazamo chanya katika maisha. Mtazamo huu ulimfanya kuweza kuvibadilisha vizingiti katika njia yake ya maisha na kuvifanya ngazi ya kumwezesha kutimiza ndoto yake katika maisha. 

Sisi pia, inatubidi, kuangalia kwa makini kabisa ni mapugufu gani yanayotufanya tushindwe kutimiza ndoto zetu maishani.(ulevi? Wivu? Tamaa? Hasira? Uwongo? Uadui? Chuki? Uvivu? Nk.) Baada ya kuyaona mapungufu hayo, tuangalie kwa makini, tena sana, ni kitu gani Mungu ametuwekea karibu nasi ambacho kitatufanya tuweze kuyashinda mapungufu haya. Hakuna na tatizo lisilo na suluhu kwa wale wanaoamini. Ila tu ni lazima tukazie macho mapungufu yetu, tuangalie pia na zile nyenzo Mungu alizoweka karibu nasi ambazo zitatuwezesha kukwea na kuvishinda vikwazo hivvyo na baada ya kuviona tumuombe Mungu kwa bidii zote, kwani  yeye alikuja ili tuwe na uzima kamili (Jn 10:10) na siyo mapungufu. Zakayo aliona mti wa mkuyu, wewe pia inakubidi utafute mkuyu wako utakao panda, na hapo utamsikia Bwana akikuambia, “Leo, imenipasa niwe nyumbani mwako.” AMINA

No comments:

Post a Comment

NCHI YANGU FAHARI YANGU TOUR