Majilio (pia: Adventi) ni kipindi cha liturujia ya madhehebu mbalimbali ya Ukristo (kama vile Kanisa Katoliki, ya Waorthodoksi, Waanglikana na Walutheri) kinatangulia sherehe ya Noeli na kuanza mwaka wa liturujia. Kinaweza kudumu kati ya siku 22 na 40.
Jina lake kwa Kilatini ni adventus maana yake ujio (wa Yesu Kristo), lakini jina la Kiswahili ni sahihi zaidi kwa sababu linadokeza kuwa ujio wa Yesu ni kwa ajili yetu na kuwa alikuja zamani, anakuja kila siku na atakuja kwa utukufu mwisho wa dunia.
Maana ya Majilio katika Maisha ya Binadamu
Sisi binadamu hatuwezi kuishi daima katika hali ileile bila ya matazamio. Hasa kijana anatarajia mambo mapya tena mema. Hivyo tunajitahidi kuyapata. Asiyetazamia chochote amevunjika moyo, hana hamu ya kuishi. Lakini matazamio ya kibinadamu yakimfikia mtu hayamridhishi moja kwa moja. Kristo tu anatimiza hamu zote kwa kumkomboa kutoka unyonge. Majilio yanatukumbusha kila mwaka matarajio ya kweli na hivyo yanaamsha hamu ya kuishi kwa bidii ya kiroho.
Majilio katika liturujia ya Katoliki
Katika mwaka wa liturujia ya Kanisa la Katoliki, sherehe ya Noeli inaandaliwa na kipindi cha Majilio ambacho kina mambo mawili: kinakumbusha Mwana wa Mungu alivyotujilia mara ya kwanza, na papo hapo kinatuandaa kumpokea atakapotujilia tena siku ya mwisho. Kufuatana na hayo kina sehemu mbili: hadi tarehe 16 Desemba kinahusu zaidi kurudi kwa Bwana; siku nane za mwisho kinatuelekeza moja kwa moja kuadhimisha kuzaliwa kwake.Urefu wa Majilio unategemea siku inayoangukia Noeli, kwa kuwa ni lazima yawe na Jumapili nne. Hivyo basi yanaanza kwa Masifu ya Jioni ya kwanza ya Jumapili inayoangukia tarehe 30 Novemba au tarehe ya jirani zaidi; yanakwisha kabla ya Masifu ya Jioni ya kwanza ya Noeli.
Kwa jumla ni kipindi cha toba: rangi yenyewe ni zambarau; haziruhusiwi sherehe za fahari; ala za muziki na maua vinaweza kutumika kwa kiasi tu. Masharti hayo yanalegezwa katika Jumapili ya tatu kwa sababu ya furaha ya kuona tunakaribia sherehe yenyewe.
Katika kipindi hicho tunaadhimisha tumaini la Israeli lililotimizwa Yesu alipokuja katika unyenyekevu wa umbile letu; pia tunangojea arudi kwa utukufu. Kama alivyotekeleza ahadi mara ya kwanza, atazitekeleza pia mara ya pili, ingawa kwake miaka elfu ni kama siku moja tu. Kati ya majilio hayo mawili, Bwana anatujilia mfululizo kifumbo katika sakramenti (hasa ekaristi) na katika maisha ya kila siku kwa njia ya matukio na watu (hasa maskini). Basi tunapaswa kuwa tayari daima kumpokea ili siku ya mwisho tukamlaki, naye atukaribishe kwenye uzima wa milele. Pia tunapaswa kumuomba aje kutukomboa, yeye aliye tumaini letu.
Katika safari ya Majilio watu watatu wanatuongoza tukutane na Yesu: 1. Isaya nabii wa tumaini, mwenye kipaji cha kutokeza matazamio ya binadamu na kumhakikishia atatimiziwa na Mwokozi. 2. Yohane Mbatizaji, mwenye kuhimiza toba kwa kuwa tunapaswa kupindua maisha yetu ili tukutane vema na Kristo. 3. Maria, bikira aliyekuwa tayari kumpokea Masiya kwa upendo na kushirikiana naye katika kutimiza mpango wa wokovu.
Tukiwafuata hao watatu tunaweza kujipatia maadili yale yanayotuandaa kumpokea Mwokozi anapotujilia: ndiyo matunda maalumu tunayotarajiwa kuyachuma wakati wa Majilio: 1. Kukesha katika imani, sala na kutambua ishara za Bwana kutujilia katika nafasi yoyote ya maisha na mwishoni mwa nyakati. 2. Kuongoka kwa kufuata njia nyofu. 3. Kushuhudia furaha inayoletwa na Yesu kwa kuwa na upole na uvumilivu kwa wenzetu, kwa tumaini la kuwa bidii zetu zinawahisha ufalme wa Mungu wenye heri isiyo na mwisho. 4. Kutunza unyenyekevu kwa kufuata mifano ya maskini wa Injili ambao ndio waliompokea Mkombozi.
No comments:
Post a Comment