Tuesday, November 18, 2014

Mwaka wa Katekesi Jimbo Katoliki Ifakara

Mwaka wa Imani uliotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita na kuhitimishwa kwa kishindo kikuu na Papa Francisko, lilikuwa ni tukio la neema kubwa kwa maisha na utume wa Kanisa. Ilikuwa ni nafasi kwa waamini kupitia tena Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, ili kuweza kuyapyaisha katika uhalisia wa maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo.

Mwaka wa Imani, ulikwenda sanjari na maadhimisho ya miaka 20 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipochapisha kwa mara ya kwanza Katekesi Mpya ya Kanisa Katoliki, bila kusahau Kitabu cha Sheria za Kanisa; matunda makuu ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Waamini kwa namna ya pekee kabisa walihamasishwa kufanya tafakari ya kina kuhusu Imani wanayoungama katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, Kanisa na Mambo ya nyakati.

Waamini walihimizwa kutambua umuhimu wa maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa, ili waweze kushiriki kikamilifu na hatimaye kujipatia neema na baraka zinazotolewa na Mama Kanisa. Mwaka wa imani, ulikuwa ni nafasi kwa waamini kujikita katika ushuhuda unaoonesha imani tendaji kwa kukumbatia Amri za Mungu kama dira na mwongozo wa maisha yao ya kiroho na maisha ya hadhara.

Waamini kwa mara nyingine tena, walihimizwa na Mama Kanisa kumwilisha imani yao kwa Kristo na Kanisa lake kwa njia ya Sala na Matendo ya huruma. Kwa maneno machache, Mwaka wa Imani, ilikuwa ni fursa ya kutafakari kwa kina na mapana kuhusu: Imani, Sakramenti za Kanisa, Amri za Mungu na Maisha ya Sala. Mwaka wa Imani, kimekuwa ni kipindi cha neema ambacho kimeyasaidia Makanisa mahalia kujiwekea mbinu mkakati wa kuimarisha imani kwa njia ya Sinodi za Majimbo au Mwendelezo wa Maadhimosho ya Mwaka wa Imani kwa kuchagua mada mbali mbali kadiri ya mahitaji ya Kanisa mahalia.

Askofu Salutaris Melchior Libena wa Jimbo Katoliki la Ifarakara, Tanzania, katika mahojiano maalum na Gazeti la AMECEA anasema kwamba, mara baada ya kuadhimisha Mwaka wa Imani, kulionekana kwamba, kunahitaji la kuendelea kuwaimarisha waamini katika Mafundisho tanzu ya Kanisa kwa kujikita hasa zaidi katika Katekesi ya kina, zoezi la kiroho linaloigusa Familia ya Mungu Jimboni Ifakara.
http://viwawaboko.blogspot.com/p/mak.htmlKutokana na hitaji hili msingi, Jimbo Katoliki la Ifakara hapo tarehe 19 Marchi 2013, katika Maadhimisho ya Siku kuu ya Mtakatifu Yosefu mchumba wake Bikira Maria na Msimamizi wa Kanisa la Kiulimwengu, Askofu Libena akazindua Mwaka wa Katekesi Jimbo Katoliki Ifarakara, utakaofungwa rasmi hapo tarehe 19 Marchi 2015, Jimbo Katoliki Ifakara litakapokuwa linaadhimisha Mwaka wa Tatu tangu kuundwa kwake na Baba Mtkatifu mstaafu Benedikto XVI. Ifakara ni kati ya majimbo machanga sana nchini Tanzania, lakini linaendelea kucharuka kwa maendeleo ya watu kiroho na kimwili.

Askofu Libena anasema, Mwaka wa Katekesi umekuwa ni fursa kubwa kwa Familia ya Mungu Jimboni Ifakara kuweza kupyaisha tena mafundisho tangu ya Kanisa, dhamana inayotekelezwa kuanzia kwenye ngazi ya: Familia, Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo, Vigango, Parokia na katika ngazi ya Jimbo. Lengo ni kuhakikisha kwamba, Jimbo Katoliki Ifakara litakapokuwa linaadhimisha kumbu kumbu ya miaka mitatu tangu kuundwa kwake, waamini wawe wameifahamu Katekesi kwa kina na mapana yake.

Jimbo Katoliki Ifakara linapenda kumwilisha imani katika matendo kwa kuwekeza zaidi katika sekta ya elimu ambayo kwa sasa inaonekana inahitaji kupewa uzito wa pekee kutokana na ukweli kwamba, kwa masuala ya afya, Jimbo limejiimarisha kwani kuna Hospitali ya Rufaa yenye vitanda 370 na idadi nzuri ya Zahanati ambazo zinaendelea kutoa huduma bora kwa kuzingatia utu na heshima ya binadamu.

Jimbo Katoliki la Ifakara linamiliki na kuendesha shule kadhaa za msingi, lakini kwa bahati mbaya, linamiliki Sekondari moja tu, changamoto ya kuendelea kuwekeza katika elimu, ili kuweza kuwafunda vijana wa kizazi kipya: kiroho na kimwili, tayari kulitumikia Taifa na Kanisa kwa ujumla.

Itakumbukwa kwamba, Jimbo Katoliki la Ifakara liliundwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI kunako tarehe 14 Januari 2012 na kuzinduliwa rasmi tarehe 19 Marchi 2012 na Askofu Salutarius Libena akawa ni Askofu wa kwanza wa Jimbo Katoliki Ifakara:>>>>>bonyeza hapa soma zaidi hapa

No comments:

Post a Comment

NCHI YANGU FAHARI YANGU TOUR