Wednesday, January 28, 2015

Dhamana na nafasi ya Baba kwenye Familia

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 28 Januari 2015 ameendelea na Katekesi yake kuhusu Familia, kwa kuangalia: utu, dhamana na nafasi ya Baba wa familia, jina ambalo Wakristo wamefundishwa na Yesu mwenyewe kumwita Mwenyezi Mungu; jina lenye utajiri mkubwa wa mahusiano katika jamii.

Read More 

Jambo la kusikitisha anasema Baba Mtakatifu katika jamii mamboleo, kuna mgogoro wa dhana ya uelewa wa Ubaba ambao kwa wengi unaonekana kuwa ni mtu mwenye madaraka na hata wakati mwingine ni mtu mkatili; mambo yanayochanganya kuhusu uelewa na dhamana ya Baba ndani ya familia.

Baba Mtakatifu anasema, leo hii inawezekana kuzungumzia kuhusu "kutokuwepo" kwa Baba kama kielelezo katika jamii, lakini ikumbukwe kwamba, dhamana na nafasi ya Baba ni muhimu sana katika familia, kwani wao ni mfano na mwongozo kwa watoto katika hekima na fadhila. Bila ya uwepo wa Baba, watoto wengi wanajisikia kuwa "yatima", wakiachwa huku wanatangatanga na hivyo kukosa mwelekeo wa makuzi pamoja na maendeleo yao.

Baba Mtakatifu anasema, hata jamii ina wajibu wa kuhakikisha kwamba, inawalinda na kuwatunza watoto, ili wasibaki na kujisikia kuwa ni yatima, bila mawazo, tunu msingi za maisha, matumaini na fursa za kazi na ukweli mtimilifu katika maisha ya kiroho. Yesu aliwaambia wafuasi wake kwamba, kamwe hatawaacha yatima. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuimarisha na kupyaisha tena utambuzi wa ubaba na hivyo kuanza mchakato wa kupata mababa wema kwa ajili ya mafao na ustawi wa familia, Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake. 

Baba Mtakatifu Francisko akizungumza na waamini pamoja na mahujaji kwa lugha mbali mbali amewataka kumsikiliza kwa makini Yesu anayewafunulia Mwenyezi Mungu kama Baba anayewapenda na kuwaunda wote ili waweze kuwa ndugu wamoja. Waamini waendelee kujifunza kutoka kwa watakatifu ili kuishi kwa nguvu ya sala, huku wakijitahidi kushughulikia wokovu wa ndugu zao. Roho Mtakatifu awasaidie ili waweze kuwa kweli ni watakatifu. 

Baba Mtakatifu amezikumbuka na kuziombea familia mbali mbali zinazoogelea katika shida na magumu ya maisha, zitambue kwamba, wao ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya Jumuiya za Kikristo. Ukosefu wa upendo, dhana na uelewa wa Baba ndani ya familia unaweza kugumisha mchakato wa kujenga mahusiano na Mwenyezi Mungu ambaye ni Baba. 

Waamini wanaalikwa kusali kwa ajili ya baba katika familia, ili waweze kutekeleza dhamana na wajibu wao kikamilifu pamoja na kuendelea kuwa ni alama ya upendo kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawataka waamini na mahujaji wanaotembelea kwenye Makaburi ya Watakatifu Petro na Paulo, wapate mwamko na ari mpya ya kutaka kushuhudia Ukristo wao katika familia na jamii kwa ujumla wake. 

Katika kumbu kumbu ya Mtakatifu Thoma wa Akwino, Padre na Mwalimu wa Kanisa, Baba Mtakatifu anawataka vijana kujielekeza zaidi katika masomo, ili kunoa akili na utashi wao kwa ajili ya huduma ya Injili. Imani ya Mtakatifu Thoma, iwasaidie wagonjwa kumkimbilia Yesu hata katika nyakati za majaribu; upole wake uwe ni kielelezo cha mahusiano mema kati ya wanandoa ndani ya familia. 

No comments:

Post a Comment

NCHI YANGU FAHARI YANGU TOUR