Leo Jumamosi, tarehe tarehe 10
Januari 2015 Askofu
msaidizi Titus Mdoe wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, ametoa Daraja la Ushemasi kwa Watawa wanne wa
Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, C.PP.S., Ibada iliyoadhimishwa kwenye Parokia ya Mtakatifu Nicholaus, Kunduchi,
Mtongani, Jimbo kuu la Dar es Salaam.
Hawa ni Majandokasisi
waliohitimu masomo yao ya falsafa na taalimungu na tarehe 9 Januari 2015
wamepokelewa rasmi kuwa ni Wamissionari wa Shirika la Damu Azizi ya
Yesu, katika Ibada iliyoongozwa na Mheshimiwa Padre Reginald Mrosso,
C.PP.S. Mkuu wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Vikarieti
ya Tanzania.
Yafuatayo ni mahubiri aliyoyatoa katika Ibada ya
Misa Takatifu kwa ajili ya kuwapokea Frt. Lauriano Januari Mushi,
Innocent Emmanuel Miku, John Eleuteri Mlay pamoja na Emmanuel Joseph
Makusaro kuwa Wamissionari. Ibada hii imefanyika kwenye Parokia ya
Mtakatifu Nicholaus, Kunduchi, Mtongani, Jimbo kuu la Dar es Salaam.
Read More
Katika
barua yake kwa ajili ya Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa uliozinduliwa
Jumapili ya kwanza ya Kipindi cha Majilio Nov. 2014 na unaotarajiwa
kufungwa rasmi tarehe 2 Feb. 2016, Siku kuu ya kutolewa Bwana Hekaluni
sanjari na Siku ya Watawa Duniani, Baba Mtakatifu Francisko anaanza na
maneno haya; napenda kusema neno moja kwenu na neno hilo ni furaha.
Popote walipo watawa, ipo pia furaha. Wale wote waliosikia sauti ya
Bwana wanaalikwa kufurahi: wimbo wetu wa katikati leo unatualika
tufurahi kwa sababu sisi ni watu wa ufufuko na watu wake Mungu – Zab.
95: kwa sababu dunia imeuona wokovu wa Mungu. Ninyi vijana wapendwa mko
hapa kwa sababu mnaamini katika huo ufufuko, katika huo uzima wa milele
wa kimungu.
Leo tunamshukuru Mungu kwa sababu ndugu zetu hawa
wamefikia hatua hii kubwa katika maisha yao ya wito na ya Kanisa kwa
ujumla katika kumtumikia Mungu na watu wake. Tunasoma maneno haya
katika - Zab. 100:3 – jueni kwamba Bwana ndiye Mungu, ndiye aliyetuumba,
nasi tu watu wake, taifa lake na kondooo wa malisho yake. Ufahamu huu
ni muhimu sana katika maisha ya mwanadamu ye yote. Ni chanzo cha wito
mbalimbali katika maisha ya kawaida na katika kanisa. Ye yote yule
anayetambua Mungu ni nani, atapata mwelekeo wa kimungu katika maisha
yake. Asiyetambua hilo, hupoteza mwelekeo wa kimungu katika maisha yake.
Mtume
Paulo katika - 1 Tim. 6:15-16 – anaandika hivi – wakati wake mwenye
heri atalidokeza tokeo la yeye aliye peke yake mtawala, Mfalme wa
wafalme, Bwana wa mabwana, Yeye peke yake hawezi kufa. Amekaa katika
mwanga usiosogeleka. Hakuna mwanadamu aliyemwona, wala awezaye kumwona.
Heshima na enzi ya milele ni yake. Amina. Tunaona kuwa ufalme na utawala
wa kweli ni wake.
Ufahamu huu unatupelekea kutambua kuwa
tumeitwa kumtumikia yeye tu na si kitu kingine cho chote kile – Mt. 4:10
– Yesu akamwambia, nenda zako shetani, kwa maana imeandikwa– umwabudu
Bwana Mungu wako, ukamtumikie yeye peke yake. Na katika Kumb. 6:13 –
ndiye Bwana Mungu wako utakayemwogopa, ndiye utakayemtumikia na kuapa
kwa jina lake.
Somo la kwanza toka Nabii Isaya – “Injili ya
Ufalme wa Mungu” - mwandishi anaandika neno hili wakati Waisraeli
wamekuwa huru toka Babeli - linaelezea habari ya ukombozi. Waisraeli
wanatoka katika utumwa. Wanafurahi. Nanyi pia tafakarini sana hali yenu –
mjiweke huru kwa ajili ya Mungu. Yule aliyeufahamu ukombozi wa Mungu,
anajiweka huru kwa ajili yake. Nanyi kuweni huru siku zote kwa ajili ya
kumtumikia Mungu na mumtumikie kwa furaha siku zote za maisha yenu.
Nabii Isaya– anatambua kuwa thamani ya maisha iko katika uhuru wa
kimungu. Huo ndio uhuru wa kweli na wenye kuleta wokovu.
WHO IS A CONSECRATED PERSON?
He
is a person who has an experience of God and especially as an Absolute.
One who deeply aware of his encouter with God and having received a
special gift which is divine and trinitarian. This is more than reading
or hearing about God (Cf. Mk 8:27-29 – ungamo la Petro – baada ya Yesu
kuwauliza – watu wasema mimi ni nani? ). And because in encoutering God
he knows himself, then the experience of his weakness, fragility and
suffering leads him to see God as an Absolute — God is all, man is
nothing. Hence, the first task of consecrated person is to reveal the
primacy of God to the world. All vocations reveal the mystery of Christ:
the lay vocation reveals the face of Christ facing towards the world,
the priestly vocation reveals the face of Christ facing towards the
community and the consecrated vocation reveals the heart of Christ
turned towards the Father. The consecrated person lives for God and only
for God. The first value of our vows is to sing the primacy of God in
our lives.
Waraka wa Kitume Injili ya Furaha,“Evangelii Gaudium”
uliochapishwa na Baba Mtakatifu Fransisko unatoa kipaumbele cha kwanza
kwa furaha ya Injili, kwa kuwaalika waamini kushirikisha furaha yao
inayopata chimbuko kutoka katika huruma na upendo wa Mungu kwa wanadamu.
Katika mwono huu, Kristo ni kiini cha Injili na kwamba, Kanisa
linaalikwa kufanya mageuzi makubwa kama sehemu ya Uinjilishaji.
Baba
Mtakatifu Francisko anaendelea kusema – furaha ya Injili inajaza mioyo
na maisha ya wale wanaokutana na Kristo. Pamoja na Yesu Kristo, furaha
inazaliwa upya tena. Sura ya 4 – mwanzoni - ya waraka wa Pili wa Mtume
Paulo kwa Wakorintho – inazungumzia juu ya watumishi kwa ajili ya
Kristo. Mstari wa sita – kwani Mungu aliyesema, Mwanga ung’ae kutoka
gizani, ndiye yeye anayeng’aa mioyoni mwetu tupate kwa mwanga wake
kuutambua utukufu wa Mungu uliopo usoni mwa Yesu Kristo. 2 Kor. 4: 6….
Mnaalikwa muwe mwanga wake Kristo. Kwa maisha yenu na ushuhuda wenu wa
maisha, Kristo aendelee kuonekana duniani. Maisha haya mnayotaka kufuata
yawe changamoto kwa wale wote ili wanapowaona ninyi wazidi kumpenda na
kumtumikia Mungu Baba.
Katika barua kwa mwaka wa watawa – Baba
Mtakatifu Francis anamtaja wazi Mtakatifu Francisko wa Assisi kama mfano
wa kuigwa, yeye aliyefanya Injili iwe njia yake ya maisha, akafanya
imani ikakua na akahuisha kanisa na jamii, akaifanya iwe ya kindugu
zaidi, lakini daima akiongozwa na Injili na ushuhuda wa maisha yake.
Nanyi yapokeeni na yatimizeni mapenzi ya Bwana kama mtakatifiu Francis.
Na imani yenu ionekane katika matendo yenu. Lengo lenu liwe tu ni
kutangaza habari njema kwa kila kiumbe.
Neno la Mungu katika
somo la Injili leo liwaongoze na kuwatafakarisha sana - Yesu ndiye
masiha aliyepakwa mafuta, ambaye kadiri ya maandiko ya manabii ‘ndiye
aliyepelekwa kuwatangazia maskini habari njema na kuutangaza mwaka wa
Neema – Lk. 4, 18-19, pia katika Isa. 61: 1-2 - ‘Roho wa Bwana yu juu
yangu, kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema.
Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, na vipofu kupata kuona
tena, kuwaacha huru waliosetwa, na kutangaza mwaka wa Bwana
uliokubaliwa. Baada ya kusoma, akafunga kile kitabu, akampa mtumishi,
kisha akaketi, watu wote wakamkodolea macho. Naye akaanza kuwaambia,
andiko hili mlilolisikia limetimia leo’.
Nanyi ingieni katika
programu hii ya kimasiha ya Yesu Kristo. Yaani muwe watangazaji mahiri
wa ufalme wake na kuutangaza daima mwaka wa Bwana. Ujumbe huu bado u hai
hata leo. Msijihangaishe na lo lote lile lililo nje ya programu hii.
Katika kumfuata Kristo – Baba Mtakatifu katika barua yake kwa
Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa anaendelea kusema – kuweni na mwanga na
furaha, ng’aeni furaha. Isa. 66: 10-14 – shangilia pamoja na Yerusalemu,
pigeni vigelegele kwa ajili yake, enyi nyote mnaomlilia, furahini,
furahini pamoja naye ninyi nyote mlioomboleza kwa ajili yake Ili mpate
kunyonya na kushibishwa maziwa ya faraja yake, na kufurahishwa kwa
maziwa yake matukufu.
Maana, Bwana asema hivi; nitatiririsha
amani na utulivu pande zote kama mto; nao utukufu wa mataifa kama kijito
kifurikacho. Nanyi mtapata kunyonya, mtabebwa kifuani, na kubembelezwa
juu ya magoti yake, mfano wa mwana anayefarijiwa na mama yake, ndivyo
nami nitawafariji, nanyi mtafarijiwa moyo katika Yerusalemu. Kwa kuona
hayo, moyo wenu utafurahi, na mifupa yenu itasitawi mfano wa majani
mabichi na mkono wa Bwana utajulikana kwa watumishi wake, nayo ghadhabu
yake kwa maadui zake.
Wote watakaoshiriki karamu hii ya Bwana na
mwaliko huu mtakatifu watapata uzima wa milele. Ninyi mnataka kuingia
katika karamu hii. Furahini pamoja na Bwana na furaha hiyo izae matunda
katika maisha yenu.
Naye Mtakatifu Gaspari anatupa changamoto
nyingine katika maisha ya ufuasi. Alipoanzisha Shirika la Wamisionari wa
Damu Azizi ya Yesu alialika wafuasi wake wawe na upendo mkuu akisema
‘upendo ni kifungo kwa wamisionari wake’. Wakifungwa na upendo, Gaspari
aliamini Wamisionari wake wataweza kueneza kwa maisha yao Tasaufi ya
damu azizi. Tena watakuwa tayari kutoa huduma ya Neno la Mungu. Akinukuu
maneno toka waraka wa Paulo kwa waefeso 1;6-8 – Atukuzwe Mungu, Baba wa
Bwana wetu Yesu Kristo …katika yeye ametuchagua kabla ya kuwekwa
misingi ya ulimwengu kusudi tuwe watakatifu na bila doa mbele yake
katika upend.
Mtakatifu Gaspari aliamini kuwa upendo ukiwepo
kazi ya Mungu itaendelezwa. Nasi tumwaminio tutapata uzima wa milele.
Katika maisha yake alieneza sifa na utukufu wa neema hizi za Mungu,
neema ambayo inatoka kwa mwanae mpendwa Kristo Yesu. Kutoka kwake Kristo
tunaona ukombozi wetu na tuna msamaha wa dhambi. Nanyi muwe na upendo
mkuu kwa Mungu Baba na Mwanae anayewajalia roho ya kutaka kumtumikia
yeye kwa ulimwengu wa leo wenye changamoto nyingi za maisha.
Ninyi
leo mnakuwa Wamisionari wanashirika. Mtakatifu Gaspari hakuona ibada
kwa Damu azizi ya Yesu kama ibada nyingine ya kawaida, bali aliona ni
kama kiini kabisa cha dini. Mtakatifu Gaspari mwenyewe anasema, ‘ni njia
salama ya kufikia utakatifu binafsi na chachu ya maisha mapya ya jumuia
na nguvu imara ya kazi ya kitume.
Pengine twaweza kujiuliza
kama Kristo alishamwaga damu yake kwa ajili yetu sote, nafasi yangu ni
ipi leo katika kuutangaza upendo huu wa Kristo? Kwa nini nihangaike
kufanya mengi kama Kristo tayari ameshatukomboa? Waraka wa mtume Paulo
kwa Wakolosai 1:24 unatupatia jibu “ nayatimiliza katika mwili wangu
yale yaliyopungua katika mateso kwa ajili ya mwili wake yaani kanisa
lake”
Nihitimishe homilia hii nikinukuu tena maneno ya Baba
Mtakatifu Francis katika barua yake kwa Mwaka wa Watawa, akisema –
nataka niseme neno moja kwenu, nalo ni furahini. Po pote walipo watawa
na watu wa maisha ya wakfu, waseminari, wanaume na wanawake, vijana, ipo
furaha, ipo daima furaha. Ni furaha ya upya, furaha ya kumfuata Kristo,
furaha ambayo Roho Mtakatifu atupatia. Siyo furaha ya ulimwengu. Somo
la pili la leo linatoa mwelekeo – Ebr. 13:12-15, 20-21- habari juu ya
maisha mapya katika ufufuko.
Sisi tumepatanishwa na Mungu kwa
njia ya kifo cha mwanawe, tumeokolewa kwa ufufuko wake. Sisi ni viumbe
vipya. Ni watu wa ufufuko. Mnapoaanza maisha mapya katika shirika letu
na ndani ya kanisa – jitahidini nanyi kuwa wapya katika yote – ishini
maisha ya ufufuko. Maneno ya Petro Mtume yawaongoze“tuishi kama
watakatifu kwa mfano wa Mungu aliyetuita katika imani”.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
-
Mkoa wa Njombe ni moja kati ya mikoa Tanzania, ukiwa umeanzishwa rasmi mwaka 2012. Umepakana na mikoa ya jirani ya Morogoro, Ruvuma, Mbeya...
-
Mwandishi wa kitabu cha Kumbukumbu la Torati ambamo tunapata somo la kwanza anatualika kutambua kuwa Mungu haachi kutimiza ahadi yake ya ...
-
Isidore Bakanja, ambaye alitoa maisha yake kwa ajili ya imani ya Kikristo, Akiongozwa na maisha rahisi kama layman Katoliki wakati wa mauaj...
No comments:
Post a Comment