Mpendwa mwana wa Mungu, tuko tena pamoja katika ile habari ya furaha ndiyo kushirikishana mapendo ya Mungu kwa njia ya Neno lake. Leo ndipo tunahitimisha kipindi cha Noeli kwa Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana na tunaanza kipindi cha kawaida cha mwaka wa Kanisa. Kumbe leo pia ni Dominika ya kwanza ya kipindi cha Mwaka wa Kanisa.
Katika
somo la kwanza Nabii Isaya anatupeni habari juu ya mtumishi wa Mungu
ambaye anapokea Roho wa Mungu na kazi yake itakuwa kuwahukumu mataifa
kwa haki. Ni nuru na mwanga kwa mataifa. Sifa yake nyingine ni mtulivu
na mnyenyekevu na hakati tamaa kwa maana mkono wa Mungu uko juu yake.
Mtumishi huyu anakabidhiwa Roho wa Mungu kwa sababu ya kazi ya kimungu
ambayo ni kujenga amani na kuunganisha vilivyovunjika.
Kadiri ya Injili ya Luka 4: 18-19 mtumishi huyu ni Yesu Kristu. Anakuja kwa ajili ya kutangaza mwaka wa Bwana
ambapo wafungwa na vipofu wataondolewa katika shida zao. Kristu
amekwisha fika kwetu kazi yetu sasa ni kupokea ujumbe wake. Namna ya
kupokea ujumbe ni kuitika kwanza ule mpango wa Yohane Mbatizaji na Isaya
wa kutengeneza njia ya Bwana, kuondoa visiki na mabonde. Tunapaswa
kufanya hivyo kwa sababu tunasikia kuwa huyu ajaye hatumii nguvu bali upendo na hivi anahitaji ushirikiano. Kwa jinsi hiyo ni kuweka ubatizo wetu katika matendo.
Mtume
Petro akielewa vema nia na mpango wa Mungu anasimama kama tusomavyo
katika kitabu cha Matendo ya Mitume na kusema hakika Mungu hana
upendeleo cha msingi ni kufanya bidii ya kumcha Bwana. Oneni jinsi
ambavyo neno la Mungu linavyopiga kasi, anasema Mtume Petro, si tu kwa
Wayahudi bali kwa ajili ya wote. Lakini kwa nini fundisho hili?, Ni kwa
sababu kulikuwa na upinzani dhidi ya ubatizo wa wapagani. Kumbe Mtume
Petro anasema, Kristu mpakwa mafuta wa Bwana amepiga kazi ya kichungaji
baada ya kutiwa mafuta na Roho wa Bwana bila kubagua. Ni fundisho kwetu
kujiimarisha katika utume na kuimarisha umoja kamili na watu wote milki
ya Mungu. Toeni bure kwa maana mmepewa bure.
Katik Injili ya
Marko tunapata fundisho la unyenyekevu wa Yohane Mbatizaji na
unyenyekevu wa Kristu. Yohane Mbatizaji anakiri udogo wake ambao ni wa
chini kabisa. Maana hata kushindwa kushika gidamu ya viatu vya Yesu
Kristo. Anatufundisha moja kwa moja kuwa safari
ya kumpenda Mungu yatudai kushuka mpaka sakafuni. Mkombozi mwenyewe pia
ni kielelezo kingine cha hali ya juu kuhusu unyenyekevu. Anajishusha
kwanza na anakuwa mtu, kana kwamba hiyo haitoshi anaamua kubatizwa
wakati hana doa la dhambi. Anatufundisha kujishusha kukaa pamoja na
wadhambi, maana tunabatizwa ili kuokolewa katika uvuli wa dhambi ya
asili kwanza na kuweza kupokea neema za Mungu.
Bwana anapobatizwa yafaa tuangalie mambo yaliyo tokea. Jambo
la kwanza ni kupasuka kwa mbingu, ambalo linatupa habari ileile ya
Nabii Isaya katika Dominika za majilio. Nabii anauliza mbona umetufanya
tukose kukutii? Mbona umetuacha hata tukasahau kukucha wewe Bwana? Is.
63:15-19. Isaya anauliza haya maswali kwa maana ni kama hakuna upatano
kati ya mbingu na nchi. Sasa tendo la kupasuka kwa mbingu ni ishara ya
mapatano kati ya mbingu na nchi na mpatanishi ni Kristu katika uwezo wa
Utatu Mtakatifu.
Jambo la pili ni alama
ya njiwa, alama hii yatukumbusha kile kilichotokea wakati wa mafuriko
ya Nuhu. Wakati huo mbingu na dunia vilifungwa na njiwa alipotokea akiwa
na tawi la mzeituni ilimaanisha kuwa amani imerejeshwa. Ndiyo kusema
kwa ishara ya njiwa kuna amani, ni Roho Mtakatifu afanyaye kazi katika
Yesu Kristu chanzo cha amani. Mpendwa jambo la pili kuhusu njiwa katika
agano la kale alimaanisha nguvu waliyopewa Manabii na hivi Kristu
waziwazi ana nguvu hiyo kwa ajili ya kutenda kazi ya Mungu.
Sauti
kutoka juu yamaanisha kuwa Kristu ni wa juu na pia Mungu anaongea na
watu wake kwa njia yake aliye mwanae mpenzi. Mpendwa msikilizaji yafaa
kukumbuka pia jambo jingine nalo ni lile la Joshua
anapowavusha wana wa Israeli pale Jordani, anapovuka mto anapokea Roho
wa Mungu ili apate nguvu ya kuwafikisha salama katika nchi ya ahadi. Ni
katika mantiki hiyohiyo Masiha anapotoka majini Roho wa Mungu anashuka
juu yake ili awaongoze wana wa Mungu katika uhuru na kweli ili wafike
mbinguni. Watu wanaoongozwa na Bwana kuelekea kwenye uhuru na kweli ndo
sisi, wajibu wetu ni kusikia sauti ya mchungaji mwema. (Yn. 10)
Mpendwa
ninakutakieni heri na baraka tele katika sikukuu ya ubatizo wa Bwana na
nakuomba usisahau wajibu wako ulioupokea kwa njia ya ubatizo, na kwa
namna hiyo utakuwa unasherehekea pia ubatizo wako kila siku ya maisha
yako.
Tumsifu Yesu Kristo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
-
Mkoa wa Njombe ni moja kati ya mikoa Tanzania, ukiwa umeanzishwa rasmi mwaka 2012. Umepakana na mikoa ya jirani ya Morogoro, Ruvuma, Mbeya...
-
Isidore Bakanja, ambaye alitoa maisha yake kwa ajili ya imani ya Kikristo, Akiongozwa na maisha rahisi kama layman Katoliki wakati wa mauaj...
-
Mwandishi wa kitabu cha Kumbukumbu la Torati ambamo tunapata somo la kwanza anatualika kutambua kuwa Mungu haachi kutimiza ahadi yake ya ...
No comments:
Post a Comment