Saturday, February 21, 2015

Masomo ya Dominika ya Kwanza ya Kwaresima Mwaka 'B' wa Kanisa 2015

21

 FEBRUARY
 Jumapili ya 1 ya Kwaresima Masomo ya Mwaka "B".
SOMO  1: Mwa. 9:8 - 15

Somo katika kitabu cha Mwanzo.
Mungu akamwambia Nuhu, na wanae pamoja naye, akisema, mimi, tazama, nalithibitisha agano langu nanyi, tena na uzao wenu baada yenu; tena na kila kiumbe hai kilichoko pamoja nanyi; ndege na mnyama wa kufungwa, na kila mnyama wa mwitu katika nchi. Na agano langu nitalithibitisha nanyi; wala kila chenye mwili hakitafutwa tena kwa maji ya gharika, wala hakutakuwa tena gharika,baada ya hayo, kuiharibu nchi. Mungu akasema, hii ndiyo ishara ya agano nifanyalo kati yangu na ninyi, na kila kiumbe hai kilichoko pamoja nanyi, kwa vizazi vyote hata milele; Mimi nauweka upinde winguni, nao utakuwa ni ishara ya agano kati yangu na nchi. Hata itakuwa nikitanda mawingu juu ya nchi, upinde utaonekana winguni, nami nitalikumbuka agano langu, lililoko kati yangu na ninyi, na kila kiumbe hai katika wote wenye mwili, wala maji hayatakuwa gharika tena kuwaharibu wote wenye mwili.

WIMBO WA KATIKATI. Zab. 25:4-9, (k) 10. 
K. Njia zote za Bwana ni fadhili na kweli, kwao walishikao agano lake na shuhuda zake..

read more....
SOMO  2: 1Pet. 3:18 - 22
Somo katika Waraka wa kwanza wa Mtume Petro kwa watu wote.

Kristo aliteswa mara moja kwa ajili ya dhambi, mwenye haki kwa ajili ya wasio haki, ili atulete kwa Mungu; mwili wake akauawa, bali roho yake akahuishwa, ambayo kwa hiyo aliwaendea roho waliokaa kifungoni, akawahubiria; watu wasiotii hapo zamani, uvumilivu wa Mungu ulipokuwa ukingoja, siku za Nuhu, safina ilipokuwa ikitengenezwa; ambamo ndani yake wachache, yaani, watu wanane, waliokoka kwa maji. Mfano wa mambo hayo ni ubatizo, unaowaokoa ninyi pia siku hizi; (siyo kuwekea mbali uchafu wa mwili, bali jibu la dhamiri safi mbele za Mungu), kwa kufufuka kwake Yesu Kristo. Naye yupo mkono wa kuume wa Mungu, amekwenda zake mbinguni, malaika na enzi na nguvu zikiisha kutiishwa chini yake.
  INJILI.Mk. 1:12-15.
Somo katika Injili ilivyoandikwa na Marko.
Roho alimtoa Yesu aende nyikani. Akawako huko jangwani siku arobaini, hali akijaribiwa na shetani; naye alikuwa pamoja na wanyamawa mwitu, na malaika walikuwa wakimhudumia. Hata baada ya Yohane kutiwa gerezani, Yesu akaenda Galilaya, akihubiri Habari njema ya Mungu, akisema, Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni na kuiamini injili.

No comments:

Post a Comment

NCHI YANGU FAHARI YANGU TOUR