Wednesday, March 23, 2016

KWANINI WAZEE WA ZAMANI WALIISHI MIAKA MINGI: YAJUE MADHARA YA MAFUTA YAKUPIKIA

CHAKULA ni moja ya mahitaji muhimu katika mwili wa mwanadamu, kwa ajili ya kuupatia nguvu, kulinda na kujenga mwili. Kwa kawaida, vyakula vingi anavyokula mwanadamu vinaandaliwa kwa kutumia mafuta ya kupikia, hali inayosababisha wapishi wengi kushindwa kuandaa vyakula kama hawana mafuta ya kupikia.
Mafuta ya kupikia yana faida na madhara kulingana na aina na wingi wa mafuta. Hata hivyo, kwa kawaida, mafuta yasiyokuwa na viwango vya ubora hupatikana kwa bei nafuu, na ndiyo hayo ambayo hupendwa kutumiwa na familia nyingi kutokana na uwezo wa kipato.
Kutokana na hali ngumu ya maisha inayozikabili familia nyingi nchini, wengi wetu hatujali aina ya vyakula tulavyo, wala vyakula tunavyonunua vina viambato gani na kiasi gani. Wengi tunaangalia gharama na upatikanaji wa bidhaa, basi.
Ni mafuta gani bora yanayofaa kupikia chakula?
Ili kuwa makini na afya zetu, ni vizuri kutafuta na kuchagua mafuta ya kupikia kwa umakini na busara zaidi. Kama nilivyodokeza hapo juu na katika machapisho mengine ya FikraPevu kwamba ulaji wa mafuta una faida na hasara zake. Moja ya madhara ya ulaji wa mafuta bila uangalifu, ni kutofanya kazi vizuri kwa ubongo pamoja na kuziba mishipa ya damu.
Katika soko la mafuta ya kupikia nchini, kuna aina nyingi tu za mafuta. Hata hivyo, kisayansi mafuta yote hayo ymegawanyika katika sehemu kuu mbili tu. Mosi, ni mafuta ya kupikia yanayotokana na asili ya wanyama, na pili, ni mafuta yanayotokana na mimea ya asili.
Mafuta yenye asili ya wanyama
Mafuta yenye asili ya wanyama, kwa asili, huwa yameganda katika joto la kawaida. Mafuta haya ni pamoja na anayotokana na nyama iliyonona na nyama ya nundu. Mafuta ya samli, siagi, jibini na maziwa yenye mafuta.
Aina hii ya mafuta ina athari kwa mtumiaji, ikiwa ni pamoja na kupata magonjwa ya moyo, kuwa na uzito uliozidi na unene uliokithiri, huweza kusababisha ugonjwa wa kisukari na kadhalika. Kwa hiyo, ni muhimu kiafya, kila binadamu akajitahidi kupunguza utumiaji wa aina hii ya mafuta yenye asili ya wanyama.
Mafuta yatokanayo na mimea
Mafuta mengi yatokanayo na mimea huwa hayagandi na muda wote yanakuwa katika hali ya kimiminika katika joto la kawaida. Kwa kawaida, mafuta haya haya, tofauti nay ale ya wanyama, yana ‘lehemu.’
Aina ya mafuta aina hii yanayotokana na mimea ya asili, ni pamoja na mafuta ya soya, ufuta, karanga, alizeti, mawese, pamba, nazi, korosho, kweme na mbegu za maboga.
Katika afya ya sayansi, mafuta haya ndiyo bora zaidi kwa kupikia kwa sababu husaidia kuboresha afya ya mwili. Hata hivyo, pamoja na kuwa mafuta bora zaidi, inashauriwa kuyatumia kwa kiasi kidogo.
‘Lehemu’ ni nini na ina madhara gani mwilini?
‘Lehemu’ ni moja ya kiambata kinachopatikana kwenye mafuta ya kupikia, ambacho kitaalamu inajulikana kwa jina la ‘Cholesterol.’ Kiambata hiki hupatikana kwa wingi kwenye mafuta ya kupikia yanayotokana na asili ya wanyama.
Kiambata hiki, pamoja na kusababisha madhara makubwa ya kiafya, lakini kinahitajika mwilini kwa kiasi kidogo. Kwa kawaida kiambata hiki kinatakiwa kiwe chini ya 200mg/dl. Hata hivyo, ni vigumu kwa binadamu kujitambua ni kiasi gani cha kiambata hiki kilichoko mwilini mwake hadi pale atakapoonana na Daktari na kupima.
Moja ya madhara ya kuwa na kiasi kikubwa cha lehemu mwilini, ni kuwa na mkusanyiko wa mafuta katika mishipa ya damu, hali inayoweza kusababisha damu kushindwa kupita kwa urahisi katika mishipa ya mwanadamu.
Hali hiyo ikimpata mwanadamu, huweza kusababisha tatizo la shinikizo kubwa la damu na ugonjwa wa moyo. Hatari nyingine ni mafuta kuziba mishipa midogo ya damu yenye mawasiliano ya moja kwa moja na moyo au ubongo, hali inayoweza kusababisha ugonjwa wa kiharusi pamoja na kifo.
Nini kifanyike ili kujilinda na athari hizo za kiafya zinazosababishwa na lehemu?
Kwanza kabisa punguza matumizi ya nyama, mayai, jibini na maziwa yasiyotolewa mafuta kabla ya kutumiwa. Jiepushe kula maini, moyo, firigisi na figo. Kama mtu anaiishi katika mazingira ambayo nyama nyekundu kama vile ya ng'ombe ndiyo mboga kuu, basi mtu huyo anapaswa kuhakikisha kwamba kiasi cha nyama nyekundi kinacholiwa hakizidi nusu kilo kwa wiki.
Ongeza matumizi ya vyakula vyenye makapi-mlo kwa wingi, kama vile nafaka zisizokobolewa kwa mfano unga wa dona, ulezi, uwele, mtama, vyakula vya jamii ya kunde, mbogamboga na matunda. Kwa kawaida vyakula vyenye makapi-mlo kwa wingi, huwa havina mafuta mengi.
Ni muhimu pia kwa binadamu kujiepusha na ulaji wa mafuta yanayotokana na wanyama, kujiepusha na ulaji wa nyama zilizonona na kuwa na mafuta mengi, kuepuka ulaji wa ngozi ya kuku na siagi pia.
Mazoezi ya mwili angalau dakika 30 kila siku, ni muhimu kwa aina yoyote ya ulaji wa mafuta bila kujali kwamba yana asili ya wanyama au mimea. Inahauriwa mazoezi hayo yawe yale ynayomtoa mtu jasho jingi, kama vile kukimbia kila siku umbali fulani wa kilomita.

No comments:

Post a Comment

NCHI YANGU FAHARI YANGU TOUR