Thursday, October 31, 2013

Sherehe za Nadhari za kwanza Wanovisi wa Shirika la Carmelite sisters

Wanavosisi watano wa shirika la masista wakarmel wamisionari wa Mt. teresia wa Mtoto Yesu, watarajia kufunga naziri za kwanza za kitawa, ambao ni
  1. Betrice Faustine Urio
  2. Dorice Kalebi Tarimo
  3. Emeritha Joseph Kavishe.
  4. Hemilete Masika Sivatungika
  5. Salange Kavuke Syaghuswa.
 Ibada itafanyika katika Parokia ya Ekaristi Takatifu Lushoto, siku ya Ijumaa ya tarehe 01/11/2013,siku ya  Sherehe ya Watakatifu wote, Na itaongozwa na Askofu wa Jimbo la Tanga: Mhashamu Askofu Anthony Banzi.
 Na baada ya Ibada itafuata Tafrija fupi ya kuwapongeza katika nyumba ya wito wa kitawa ya Jumuiya ya Bikira Maria wa Mlima Karmel - lushoto KIALO,

Mungu awaongeze na Mt. Teresia wa Mtoto Yesu awe Mlinzi wako...

Tuesday, October 29, 2013

MASOMO YA DOMINIKA YA 31 YA MWAKA C. JUMAPILI TAREHE 03/11/13

JUMAPILI DOMINIKA YA 31 ya Mwaka C.
      RATIBA ZA IBADA 
KIGANGO CHA MH. ISIDORI BAKANJA- BOKO.
MISA YA KWANZA 12:15-2:00 ASUBUHI
MISA YA PILI     SAA 2:00-4:00 ASUBUHI
MISA YA TATU SAA 4:00-5:30 ASUBUHI
KIGANGO CHA MT. FRANCIS WA ASIZ-MBWENI 
MISA YA KWANZA SAA 1:10-3:00 ASUBUHI
MISA YA PILI SAA 3:00-4:30 ASUBUHI

KIGANGO CHA MT. RAFAEL-MBWENI MALINDI
IBADA NI MOJA TU ITAANZA SAA 3:00-5:00 ASUBUHI.


KIGANGO CHA ANTHONY WA PADUA-MBWENI TETA
MISA NI SAA 3:00-5:00.




DOMINIKA 31 ya mwaka C (masomo)
SOMO 1. HEK. 11:22- 12:2
Ulimwengu wote mbele zako Bwana, ni kama chembe moja katika mizani, na mfano wa tone moja la umande lishukalo asubuhi juu ya ardhi. Lakini wewe unawahurumia watu wote, kwa sababu unao uweza wa kutenda mambo yote; nawe wawaachilia wanadamu dhambi zao, ili wapate kutubu. Kwa maana wewe wavipenda vitu vyote vilivyopo, wala huchukii kitu cho chote ulichokiumba. Kwa kuwa hungalifanya kamwe kitu cho chote kama ungalichukia; tena kitu cho chote kingaliwezaje kudumu, ila kwa mapenzi yako? Au kitu kisichoumbwa nawe kingaliwezaje kuhifadhika? Lakini wewe unaviachilia vyote, kwa kuwa ni vyako, Ee Mfalme mkuu, mpenda roho za watu; maana roho yako isiyoharibika imo katika vyote. Kwa hiyo wawathibitishia kidogo kodogo hatia yako, wale wanaokengeuka kutoka katikala  njia njema; wawaonya, ukiwakumbusha kwa mambo yale yale wanayokosa, ili waokoke katika ubaya wao, na kukuamini wewe Bwana.

SOMO 2. 2THE. 1:11- 2:2
Kwa hiyo twawaombea ninyi sikuzote, ili Mungu wetu awahesabu kuwa mmekustahili kuitwa kwenu, akatimiza kila haja ya wema na kila kazi ya imani kwa nguvu; jina la Bwana wetu Yesu litukuzwe ndani yenu, nanyi ndani yake, kwa neema ya Mungu wetu na ya Bwana Yesu Kristo. Basi, ndugu, tunakusihini, kwa habari ya kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo, na kukusanyika kwetu mbele zake, kwamba usifadhaishwe upesi hata kuicha nia yenu, wala msisitushwe, kwa roho, wala kwa neno, wala kwa waraka unaodhaniwa kuwa ni wetu, kana kwamba siku ya Bwana imekwisha kuwapo.

INJILI. LK. 19:1-10
Yesu alipoingia Yeriko alipita katikati yake. Na tazama, palikuwa na mtu, jina lake Zakayo, mkubwa mmoja katika watoza ushuru, naye ni tajiri. Huyu alikuwa akitafuta kumwona Yesu ni mtu wa namna gani, asiweze kwa sababu ya umati wa watu, maana ni mfupi wa kimo. Akatangulia mbio, akapanda juu ya mkuyu apate kumwona, kwa kuwa atakuja kupita njia ile. Na Yesu, alipofika mahali pale, alitazama juu, akamwambia, Zakayo, shuka upesi, kwa kuwa leo imenipasa kushinda nyumbani kwako. Akafanya haraka, akashuka, akamkaribisha kwa furaha. Hata watu walipoona, walinung’unika wote, wakisema, ameingia kukaa kwa mtu mwenye dhambi. Zakayo akasimama,  akamwambia Bwana, Tazama, Bwana nusu ya mali yangu nawapa maskini, na ikiwa nimenyang’anya mtu kitu kwa hila namrudishia mara nne. Yesu akamwambia, leo wokovu umefika nyumbani humu, kwa sababu huyu naye ni mwana wa Ibrahimu. Kwa kuwa mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuoka kile kilichopotea.
             
  1.  Jumapili ya tarehe 03/11/13 tutakuwa na kikao cha halmashauri ya VIWAWA Parokia, kikao kitaanza mara baada ya misa ya pili...mahali na parokiani boko fika bila kukosa.
  2. Kigango cha mt. Raphael jumapili tarehe 3/11/2013 ni siku ya mnada wa mavuno waamini wote, ndugu jamaa na marafiki unaalikwa kuungano nao.
  3. jiandae na semina ya vijana wote wa parokia ya boko pamoja na parokia jirani tarehe 23/11/2013 taarifa kamili utazipata jumapili.


  1. tunawakumbusha vijana wote kuendelea kulipa ada kwa maendeleo ya chama chetu..... mapendo sana malipo kwa njia ya benk kwa jina na number hii :viwawa parokia ya boko account no 01524526820100 crdb bank tegeta branch
JIANDAE NA ZIARA YA UINJILISHAJI MWAKA 2014.....................

Monday, October 28, 2013

MJUE Kardinal Polycarp Pengo

Polycarp Pengo ni kardinali wa pili kutoka Tanzania, akiwa aliteuliwa mara baada ya kifo cha Laurean Rugambwa, kardinali wa kwanza kutoka kusini kwa Sahara.

Maisha yake.

Alizaliwa Mwazye (mkoa wa Rukwa) tarehe 5 Agosti 1944.
Baada ya masomo ya ngazi mbalimbali, alipewa upadrisho mwaka 1971 na Askofu Charles Msakila wa Jimbo Katoliki la Sumbawanga, akasoma teolojia ya maadili huko Roma, Italia, akijitwalia digrii ya udaktari mwaka 1977.
Kisha kufundisha somo hilo kwa muda mfupi kwenye seminari kuu ya Kipalapala (mkoa wa Tabora), alichaguliwa kuwa gombera wa seminari kuu ya Segerea hadi mwaka 1983.
Aliteuliwa askofu wa Nachingwea tarehe 11 Novemba 1983, akapewa daraja takatifu hiyo na Papa Yohane Paulo II tarehe 6 Januari 1984.
Tarehe 17 Oktoba 1986 alihamishiwa jimbo jipya la Tunduru-Masasi.
Tarehe 22 Januari 1990 alifanywa askofu mwandamizi wa Dar-es-Salaam na mwaka 1992, kardinali Laurean Rugambwa alipojiuzulu, akawa askofu mkuu.
Aliteuliwa na Yohane Paulo II kuwa kardinali tarehe 21 Februari 1998, akikabidhiwa parokia ya Nostra Signora de La Salette mjini Roma.
Pamoja na majukumu mbalimbali katika idara za Papa, tangu mwaka 2007 hadi 2013 alikuwa mwenyekiti wa Umoja wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki ya Afrika na Madagaska

Historia (Kanisa Katoliki)

Imani

, Imani,


Ingawa kwa Kiswahili neno imani lina maana mbalimbali (k.mf. "huruma"), ile kuu inahusiana na kitenzi kuamini, kinachofanana na kusadiki. Hapo ni kukubali ukweli wa jambo lisiloweza kuthibitishwa.
Katika dini msingi wake ni mamlaka ya Mungu aliyeshirikishwa ukweli huo kwa njia ya ufunuo maalumu ili kumsaidia binadamu amjue yeye, ajifahamu pamoja na maisha yake duniani na ahera.
Kwa msingi huo, au wa namna hiyo, mtu anaweza kushikilia jambo bila ya uthibitisho mwingine, ingawa pengine Ukristo unatia maanani pia akili katika ujuzi wa ukweli.
Kadiri ya Mtume Paulo imani ikifuatana na tumaini na upendo ni adili kuu mojawapo, msingi, mzizi na chanzo cha wokovu.

Roho ya imani katika maisha ya kiroho

Kila mara mtu anafuata ama umbile, asipopita fikra za kibinadamu tu, ama imani, anapolenga mbinguni kwa njia ya utakatifu. Roho hizo zinazotuongoza maishani ni namna maalumu za kupima, kuona, kuhisi, kupenda, kushabikia, kutaka na kutenda. Basi, roho ya imani ni kupima yote kwa mtazamo wa juu ambao unapita maumbile na kutegemea mamlaka ya Mungu katika kujifunua, na ukweli wake katika kutushirikisha utukufu. Tunaelewa zaidi roho ya imani tukiangalia iliyo kinyume chake, yaani upofu wa roho unaozuia mtu asione mambo ya Mungu isipokuwa kidunia na kutoka nje. Hivyo Israeli haikuelewa uteuzi wake kadiri ya ukweli wa Mungu ulio wa juu kuliko ukabila au ubaguzi wowote.
Imani ina mitazamo mipana kuliko huo kutokana na usahili wake unaoshiriki hekima ya Mungu. Juu sana kuliko mifuatano ya mawazo, ni tendo sahili ambalo tunamsadiki Mungu anayefunua na papo hapo anajifunua. Kwa tendo hilo lipitalo maumbile tunaambatana naye pasipo udanganyifu na hivyo katika giza tunalenga kutazama mambo ya Mungu, juu kuliko hakika zote za kibinadamu. Hakika inayotokana na imani tuliyomiminiwa na Mungu, inapita hata hakika ya akili tunayoweza kujipatia kwa kuzingatia miujiza inayothibitisha ufunuo wake.
Imani ni zawadi ya Mungu: “Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu” (Ef 2:8). Ni kama hisi ya Kiroho inayotuwezesha kusikia ulinganifu wa mafumbo aliyotufumbulia, yaani kusikia sauti yake kabla hatujakaribishwa kumuona uso kwa uso.
“Lakini sisi hatukuipokea roho ya dunia bali Roho atokaye kwa Mungu, makusudi tupate kujua tuliyokirimiwa na Mungu, nayo twayanena, si kwa maneno yanayofundishwa kwa hekima ya kibinadamu, bali yanayofundishwa na Roho, tukiyafasiri mambo ya rohoni kwa maneno ya rohoni. Basi, mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu; maana kwake huyo ni upuuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni. Lakini mtu wa rohoni huyatambua yote, wala yeye hatambuliwi na mtu. Maana, ni nani aliyefahamu nia ya Bwana, amwelimishe? Lakini sisi tunayo nia ya Kristo” (1Kor 2:12-16). Ili ifanye hivyo imani inasaidiwa na vipaji vya akili na hekima, lakini yenyewe ndiyo inayotufanya tushike Neno la Mungu pasipo udanganyifu.
Ingawa mafumbo yake ni ya giza kwetu, adili la imani ni bora kuliko ujuzi mwangavu walionao malaika kwa umbile lao, kwa sababu imani tunayomiminiwa inalingana na uzima wa milele, kwa kuwa ndiyo mbegu yake. Malaika wenyewe walihitaji zawadi hiyo waweze kulenga hali ipitayo maumbile waliyoitiwa.
Mungu anapotujalia imani, anapenya roho yetu na kusema nayo si kwa mifuatano ya maneno, bali kwa wazo la ghafla. Imani ikifika, tunaachana na mfuatano wowote wa mawazo tuliokuwanao pamoja na sababu zake: tunaviweka chini ili imani ivikalie kama mtawala. Imani ikiangaza akili kwa mng’ao wa kweli zake, mara utashi unahisi joto la upendo wa Mungu.

Imani tuliyomiminiwa inatakiwa kustawi hadi kifo

Imani inatakiwa kukua kila siku. “Imani inaweza ikawa kubwa ndani ya Mkristo mmoja kuliko ndani ya mwingine, upande wa akili kutokana na hakika na imara kubwa zaidi katika kushika ufunuo, na upande wa utashi kutokana na utayari na utiifu au tumaini kubwa zaidi” kwa kuwa “imani tunayomiminiwa inalingana na zawadi ya neema, ambayo si sawa kwa wote” (Thoma wa Akwino). Yesu Kristo aliwasema wanafunzi wake kuwa “wa imani haba” (Math 6:30); kumbe alimuambia mwanamke Mkananayo, “Mama, imani yako ni kubwa!” (Math 15:28).
Imani inaweza kukua kwa upana na kwa dhati au nguvu. Inapanuka tunapozidi kujifunza yale yote Kanisa linayoyafundisha: wanateolojia wanayajua wazi, lakini si kwamba imani yao ni ya dhati na ya nguvu kadiri ilivyoenea. Kumbe tunakuta watakatifu wasiojua mengi katika hayo, lakini wanapenya mafumbo yalivyofumbuliwa na Injili kwa usahili. Mitume wa Yesu walimuomba imani hiyo waliposema, “Tuongezee imani” (Lk 17:5). Yesu akawaambia, “Yoyote mtakayoomba katika sala mkiamini, mtapokea” (Math 21:22). Tutayapokea hasa tukijiombea kwa udumifu yaliyo ya lazima au ya kufaa sana kwa wokovuwetu, kama vile ustawi wa maadili.

Ubora na uwezo wa imani

Thamani ya imani inapimwa na matatizo inayoyashinda katika majaribu: “Kwa imani Ibrahimu alipojaribiwa, akamtoa Isaka awe dhabihu… yeye aliyeambiwa: Katika Isaka uzao wako utaitwa, akihesabu ya kuwa Mungu aweza kumfufua hata kutoka kuzimu… Kwa imani walishinda milki za wafalme, walitenda haki, walipata ahad, walifunga vinywa vya simba, walizima nguvu za moto… Wengine walijaribiwa kwa dhihaka na mapigo, naam, kwa mafungo, na kwa kutiwa gerezani; walipigwa kwa mawe, walikatwa kwa misumeno, walijaribiwa, waliuawa kwa upanga; walizungukazunguka wakivaa ngozi za kondoo na ngozi za [mbuzi]], walikuwa wahitaji, wakiteswa, wakitendwa mabaya – watu ambao ulimwengu haukustahili kuwa nao” (Eb 11:17-19, 33-34, 36-38). Mambo kama hayo yanatokea hata siku hizi. “Basi na sisi pia, tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa mbele yetu, tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu” (Eb 12:1-2).
“Mzingatieni Kristo aliyevumilia upinzani wa namna hiyo kutoka kwa wakosefu… Hapo katika tabu yoyote mtaona dawa katika msalaba wa Yesu. Humo mtakuta vielelezo vya maadili yote. Gregori Mkuu alisema tukiyakumbuka mateso ya Yesu hatutaona chochote kuwa kigumu au cha tabu tusiweze kukivumilia kwa subira na upendo” (Thoma wa Akwino). Imani ikistawi inatufanya kwa kawaida tuzidi kuhisi fumbo la Kristo; polepole hisi hiyo ipitayo maumbile inakuwa sala ya kumiminiwa yenye kupenya na kuonja, asili ya furaha na amani: “Furahini katika Bwana sikuzote; tena nasema, Furahini… Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu” (Fil 4:4,7).

Tuishije kwa roho ya imani?

Tunapaswa kuishi hivyo kwa kupima yote kwa mwanga huo wa juu: kwanza Mungu, halafu nafsi yetu, jirani na matukio yote.
Je, kuna haja ya kusema tumzingatie Mungu kwa imani? Bila ya shaka! Kwa kuwa mara nyingi tunamzingatia kwa dhana zisizo na msingi, kwa miguso ya kibinadamu mno na kwa maono yetu, badala ya kupitia ushuhuda alioutoa juu yake mwenyewe. Pengine hata tunaposali tunajisikiliza tu kwa kumkopesha Mungu mawazo yetu yanayotokana na umimi. Tunapojiamini kipumbavu tunaelekea kudhani huruma ya Mungu ni kwa ajili yetu, na haki yake kwa watu tusioelewana nao. Kumbe tukikata tamaa tunatilia shaka kimatendo upendo wa Mungu kwetu na huruma yake kuu. Kwa imani tunamuona Mungu kupitia mafumbo ya maisha na mateso ya Mwokozi na kupitia uhai wa Kanisa linalofanywa upya na ekaristi kila siku. Jicho la imani linasafika zaidi na zaidi kwa ufishaji wa hisi na maono, maoni na matakwa yetu: hapo tu unakuja kuanguka polepole ule utaj wa kiburi unaotuzuia tusione mambo ya Mungu au tuone tu vivuli vyake na tata zake.
Tunapaswa vilevile kujitazama kwa imani. Tukijitazama kibinadamu tu, tunaona ndani mwetu sifa za umbile ambazo mara nyingi tunazizidisha. Baadaye, majaribu yakituonyesha tulivyojidanganya tunavunjika moyo kwa urahisi. Kumbe kwa imani tunakuja kujua utajiri upitao maumbile ambao Bwana ametutia katika ubatizo na kutuongezea kwa ekaristi, yaani thamani ya neema inayotia utakatifu, ya uwemo wa Utatu mtakatifu pamoja na ukuu wa wito wa Kikristo. Tunakuja kujua pia vizuio vya ustawi wa uzima huo, k.mf. usahalifu wa mbegu ya uzima wa milele iliyopandwa ndani mwetu, na kiburi cha kipumbavu. Kwa mtazamo huo wa juu tunakuja kujua mapema kilema kinachotutawala na kivutio maalumu cha neema tulicho nacho, ambavyo cha kwanza kikomeshwe na cha pili kistawishwe.
Lakini tunayesahau zaidi kumtazama kwa imani ndiye jirani. Tunamtazama kibinadamu tu, tukiathiriwa na dhana zisizo na msingi, kiburi, wivu na vilema vingine. Kwa hiyo ndani yake tunakubali yale ambayo yanatupendeza kibinadamu, yanatufaidisha au kutukuza; kumbe tunahukumu yale ambayo yanatukinaisha, yanamfanya bora kuliko sisi na kutushusha. Dhambi ngapi za kuhukumu na kusingizia zinatokana na mtazamo huo uliofunikwa na utaji wa umimi! Tukijifunza kumtazama jirani kwa imani ni faida kubwa pande zote. Hapo tunakuja kuwaona wakubwa wetu kama wawakilishi wa Mungu, na kuwatii kwa moyo pasipo kuwasema. Tunaona kuwa wasiotupendeza wamekombolewa kwa damu ya Kristo, pengine ni viungo vya mwili wake vinavyokaribia moyo wake kuliko sisi: mara nyingi tunaishi miaka pamoja na watu safi tusitambue uzuri wa roho zao. Vilevile, tukija kuwatazama kwa imani wanaotupendeza, pengine tunavumbua wana maadili ya Kimungu kiasi cha kuzidisha na kutakasa mapendo tunayowaonea; pia kwa wema tunaona vizuio walivyonavyo kwa utawala wa Mungu na tunaweza kushauriana nao tusonge mbele katika njia yake.
Hatimaye tunapaswa kutazama kwa imani matukio yote ya maisha yetu, ya furaha na ya uchungu vilevile. Mara nyingi tunaridhika kuyaona upande wa hisi tu, au kwa akili iliyoathiriwa na dhambi. Mara chache tunayazingatia Kimungu, kwa kuona kwamba “katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema” (Rom 8:28): hata katika upinzani, matatizo makubwa yasiyotarajika na dhambi (tukiweza kujinyenyekesha kutokana nazo). Katika kukosewa haki na watu tunaweza kutambua haki ya Mungu ikiadhibu makosa ya siri ambayo hatulaumiwi na mtu; au tunahisi majaribu ya Kimungu, na utakaso unaokusudiwa kupatikana kwa njia ya hayo.
Kabla ya imani yetu kutakaswa kwa majaribu kadhaa ya aina hiyo, tujitahidi kukua katika imani, badala ya kupima yote kibinadamu tu. Ni lazima tujinyime mianga midogo na ya bandia ili tujaliwe ile ya juu; tuache kufuata mno akili yetu ili tuone uangavu mkuu wa mafumbo ya imani na kuishi kulingana nayo. Hivyo tunaelewa kwa nini hatutakiwi kuitikia vishawishi dhidi ya imani, bali kuvikataa au kuviruka kwa kukiri imani kwa dhati zaidi; Bwana anaviruhusu kwa maendeleo yetu tu.



Itaendeleaa ...........................

Sala ya Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya Familia



Maadhimisho ya Mwaka wa Imani kwa ajili ya Familia limekuwa ni tukio la imani kwani kabla ya Misa Takatifu, waamini wengi walipata nafasi ya kuungama ili kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao kwa kutambua umuhimu wa Sakramenti ya Upatanisho.

Mara baada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili, tarehe 27 Oktoba, 2013, Baba Mtakatifu Francisko amesali mbele ye Sanamu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, akiiendea kwa imani thabiti ili kutafakari umoja na upendo wa dhati, ili hatimaye, aweze kuzikabidhi Familia zote za Kikrito ambazo zinapaswa kuonja neema.

Familia Takatifu ni shule makini ya Neno la Mungu, Fadhila, hekima na nidhamu ya maisha ya kiroho. Baba Mtakatifu anaomba ili waamini waweze kuwa na jicho la kuona kazi ya Mungu katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku. Familia Takatifu ni hifadhi aminifu ya Fumbo la Ukombozi.

Baba Mtakatifu anaomba fadhila ya ukimya, moyo wa sala katika familia ili ziweze kuwa kweli ni Kanisa dogo la nyumbani; daima wanafamilia watamani utakatifu pamoja na kuwasaidia kukabiliana na changamoto za maisha, kwa kusikilizana, kuelewana na kusameheana.

Familia Takatifu iwasaidie walimwengu kutambua na kuthamini utakatifu wa maisha na kwamba, Familia ni hazina ambayo haina mbadala. Kila familia ijitahidi kupokea na kuenzi amani kwa ajili ya watoto na wazee; wagonjwa na wapweke; maskini na wote wanaosukimizwa pembezoni mwa Jamii.

Wednesday, October 23, 2013

Washeni moto wa imani duniani!



Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 20 Oktoba 2013 amewataka waamini na watu wenye mapenzi mema kujenga utamaduni wa kusali bila kuchoka; kwa kupaaza sauti kwa Mwenyezi Mungu, usiku na mchana kwani hiki ni kielelezo cha imani makini kwa Mwenyezi Mungu ambaye daima anasikiliza kwa makini na upendo mkuu na anayafahamu mahitaji ya waja wake.

Baba Mtakatifu amewahakikishia waamini waliokuwa wamefurika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kwamba, Yesu anaendelea kufanya hija na wafuasi wake na wala hayuko mbali nao katika mapambano dhidi ya dhambi na kwamba, sala ni silaha muhimu inayomfanya mwaminifu kutambua na kuonja uwepo endelevu wa Kristo katika hija ya maisha yake hapa duniani.

Yesu anawakirimia wafuasi wake huruma na msaada wanaohitaji, kwa kutambua kwamba, mapambano dhidi ya dhambi si jambo la lelemama, bali linahitaji uvumilivu na udumifu katika sala kama alivyofanya Musa katika somo la kwanza, Jumapili ya ishirini na tisa ya kipindi cha Mwaka C wa Kanisa. Mwenyezi Mungu ni mwenza na nguvu katika mapambano haya na kwamba, sala ni kielelezo cha ushuhuda wa imani kwa Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu anasema, ikiwa kama waamini watauzima moto wa imani, kwa hakika watatembea katika giza totoro, kiasi kwamba, watapoteza dira na mwelekeo wa maisha.

Baba Mtakatifu amewapongeza wanawake wanaosimama kidete kulinda na kutetea misingi ya haki na amani kwa ajili ya familia zao bila kuchoka wala kukata tamaa. Hiki ni kielelezo cha imani thabiti, ujasiri na mfano wa kuigwa katika maisha ya sala, changamoto ya kuendelea kusali daima kama ushuhuda wa imani tendaji kwa Mwenyezi Mungu anayewapenda waja wake pamoja na kuwahamasisha kushikamana naye katika mapambano dhidi ya dhambi, ili kuweza kuyashinda malimwengu kwa njia ya wema.

Mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Baba Mtakatifu Francisko aliwakumbusha waamini kwamba, Mama Kanisa Jumapili iliyopita ameadhimisha Siku ya 87 ya Kimissionari Duniani. Utume wa Kanisa ni kuhakikisha kwamba, linawasha moto wa imani uliowashwa kwa mara ya kwanza na Yesu mwenyewe duniani. Ni moto wa imani kwa Mwenyezi Mungu ambaye ni mwingi wa huruma na mapendo. Huu ni moto ambao waamini wanapaswa kuwagawia wengine ili mioyo iweze kupata joto la ujumbe wa Mungu.

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwashukuru wale wote wanaoshiriki kwa hali na mali katika kutegemeza shughuli za kimissionari sehemu mbali mbali duniani, lakini kwa namna ya pekee, wale wanaomsaidia Khalifa wa Mtakatifu Petro kueneza Injili sehemu mbali mbali za dunia. Mama Kanisa yuko karibu na wamissionari walioenea sehemu mbali mbali za dunia, wanatekeleza dhamana na wajibu wao katika hali ya ukimya pasi na makeke! Ni watu wanaojitosa kimasomaso kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.

Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu amemkumbuka Afra Martineli, mmissionari aliyefanya kazi za kitume nchini Nigeria kwa miaka mingi, akapendwa na wengi; lakini hivi karibuni aliuwawa kikatili nchini Nigeria. Watu wengi wamelia na kuomboleza kifo cha Afra Martineli. Hii ni kwa sababu alitangaza Injili ya Kristo kwa njia ya ushuhuda wa matendo yake, kwa kuanzisha shule, mahali ambapo aliwasha moto wa imani na kwamba, amevipiga vita vilivyo vizuri na sasa mwendo ameumaliza.

Baba Mtakatifu amemkumbuka pia Mwenyeheri Stefano Sàndor aliyetangazwa kuwa Mwenyeheri jumamosi iliyopita, huko Budapest kutokana na mchango wake mkubwa kwa majiundo ya vijana kiroho na kimwili.Mwenyeheri Sàndor alikabiliana uso kwa uso na utawala wa Kinazi, wakati ulipoanza madhulumu dhidi ya Kanisa. Akauwawa kikatiliki akiwa na umri wa miaka 39. Mama Kanisa anaishukuru Familia ya Wasaelisiani na Kanisa Katoliki nchini Hungaria.

Baba Mtakatifu Francisko amewakumbuka na kuonesha uwepo wa karibu kwa wananchi wa Ufilippini waliokumbwa na tetemeko la ardhi lililosababisha maafa makubwa kwa maisha na mali ya watu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kuwaombea wananchi hao wakati huu mgumu katika historia ya maisha yao.

Baba Mtakatifu, mwishoni amewashukuru wadau mbali mbali walioshiriki katika "Mbio za Imani" kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, jumapili iliyopita; mbio za Marathoni zilizoandaliwa na Baraza la Kipapa la Utamaduni na wadau mbali mbali kutoka Italia. Baba Mtakatifu amewakumbusha kwamba, mwamini ni mwanariadha wa maisha ya kiroho.

Tuesday, October 22, 2013

MASOMO YA DOMINIKA YA 30 YA MWAKA C TAREHE 27/10/2013

JUMAPILI DOMINIKA YA 30 ya Mwaka C.
      RATIBA ZA IBADA 
KIGANGO CHA MH. ISIDORI BAKANJA- BOKO.
MISA YA KWANZA 12:15-2:00 ASUBUHI
MISA YA PILI     SAA 2:00-4:00 ASUBUHI
MISA YA TATU SAA 4:00-5:30 ASUBUHI
KIGANGO CHA MT. FRANCIS WA ASIZ-MBWENI 
MISA YA KWANZA SAA 1:10-3:00 ASUBUHI
MISA YA PILI SAA 3:00-4:30 ASUBUHI

KIGANGO CHA MT. RAFAEL-MBWENI MALINDI
SAA 1:00-3:00 ASUBUHI.
MISA YA PILI SAA 3:00-5:00

KIGANGO CHA ANTHONY WA PADUA-MBWENI TETA
MISA NI SAA 3:00-5:00.


MASOMO 

 Somo 1:Ybs.35:12-14, 16- 17
Kwa kuwa Bwana ndiye mhukumu wala hakijali cheo cha mtu. Hatamkubali ye yote juu ya maskini, naye ataisikiliza sala yake aliyedhulumiwa. Hatayadharau kamwe malalamiko ya yatima, wala ya mjane amwelezapo habari zake. malalamiko yake aliyeonewa yatapata kukubaliwa, na dua yake itafika hima mbinguni. Sala yake mnyenyekevu hupenya mawingu; wala haitatulia hata itakapowasili; wala haitaondoka hata Aliye juu  itakapoiangalia, akaamua kwa adili, akatekeleza hukumu. Wala Bwana hatalegea, wala hatakuwa mvumilivu kwa mwanadamu.

SOMO 2: 2Tim.4:6- 8, 16- 18
Mimi sasa namiminwa, na wakati wa kufariki kwangu umefika. Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda: baada ya hayo nimewekewa taji ya haki, ambalo Bwana, mhukumu mwenye haki, atanipa siku ile; wala si mimi tu, bali na watu wote pia waliopenda kufunuliwa kwake. katika jawabu langu la kwanza hakuna mtu aliyesimama upande wangu, bali wote waliniacha; naomba wasihesabiwe hatia kwa jambo hilo. lakini Bwana alisimama pamoja nami akanitia nguvu, ili kwa kazi yangu ule ujumbe utangazwe kwa utimilifu, hata wasikie Mataifa yote; nami nikaokolewe katika kinywa cha simba. Bwana ataniokoa na kila neno baya, na kunihifadhi hata nifike ufalme wake wa mbinguni. Utukufu una Yeye na milele. Amina.

INJILI. :Lk.18:9-14
Yesu aliwaambia mfano huu watu wanaojikinai ya kuwa wao ni wenye haki, wakiwadharau wengine wote. Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali, mmoja Farisayo, wa pili mtoza ushuru. Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake.; Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyanganyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote. lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakudhubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifuani akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi. Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.
             
  1.  Jumapili ya tarehe 03/11/13 tutakuwa na kikao cha halmashauri ya VIWAWA Parokia, kikao kitaanza saa tatu asubuhi mahali tutapeana taarifa.


  1. tunawakumbusha vijana wote kuendelea kulipa ada kwa maendeleo ya chama chetu..... mapendo sana malipo kwa njia ya benk kwa jina na number hii :viwawa parokia ya boko account no 01524526820100 crdb bank tegeta branch
JIANDAE NA ZIARA YA UINJILISHAJI MWAKA 2014.....................

NCHI YANGU FAHARI YANGU TOUR