Sunday, November 2, 2014

Siku ya Marehemu tarehe 02/11(Mungu amewekeza siri ya upendo katika Fumbo la KIFO!)

Kifo ni kitendawili ambacho binadamu ameshindwa kabisa kukitegua. Anabaki kuhoji na kujihoji bila kupata jibu la kwa nini anakufa. Mbele ya kifo binadamu anabaki kutoa visingizio vya kujitetea na kulaumu, hatimaye anakiona kifo kuwa mwiko

Zamani mwiko ulikuwa masuala ya „mapenzi”, kumbe kifo na misiba hakikuwa kitu cha kuogopa sana. Lakini sasa ni kinyume, mambo ya mapenzi yamegeuka kuwa kitu cha kawaida kabisa isipokuwa kifo kimekuwa kiboko chetu.

Watu tunakiogopa na pengine hatutaki hata kukisikia. Tunapolazimika kwenda msiba basi tunawaachia wengine walipambe jeneza maua, nasi tukisubiri kwenda kutia sahihi kwenye kitabu cha maombolezo na kutoa rambirambi kwenye bahasha kisha kukaa mbani na jeneza huku tukizungumza chinichini. Sanasana tunajisahaulisha kwa kuimba nyimbo za maombolezo au kusikiliza nyimbo za Injili. Tunaogopa kabisa kukizungumzia kifo au walau kukijadili. Mbele ya kifo binadamu tunabaki kulaumiana, kushikana uchawi na hasa tunamlaumu Mwenyezi Mungu.

Mathalani, kuna baadhi ya wakristu wa kale hata wa sasa walisali na kuomba msaada kwa Mungu au kwa kupitia watakatifu fulani kusudi waepushwe na kifo. Sala hizo zinapoacha kupokelewa, binadamu anachukia, na kumlaumu Mungu. Kristu aliwahi pia kulaumiwa pale alipokataa mwito wa Marta na Maria walipomwomba aenda kwao kumponyesha kaka yao Lazaro aliyekuwa mgonjwa. Yesu akaenda huko kwa kuchelewa kusudi siku nne baada ya kifo. Siku ile alipojionesha msibani, Maria na Marta wakamjia juu na kumlaumu sana. “Bwana ungalikuwapo ndugu yetu asingalikufa”. Hata katika nafasi hiyo, bado hatutaki kulijibu swali ni sababu gani Yesu alifika duniani. Je Yesu alifika duniani ili kuendeleza uhai huu wa kibaolojia au kushinda mauti?

Tukitaka kujua ukweli wa mwenendo mzima wa maisha yetu, hatuna budi kuangalia pia hatima yake, yaani kuelewa kwamba maisha yetu yana mwanzo (yaani kuzaliwa) na yana ukamilifu wake. Ama sivyo tutaendelea kukiogopa kifo, nacho kitaendelea kupeta na kutuogofya zaidi.

Ndugu zangu, tulishukuru Kanisa limetutengea mwezi mzima wa Novemba tulioishauanza ili tukitafakari kitendawili hiki cha kifo. Asiyetaka kukitafakari kifo anaonywa na methali ya kiswahili isemayo: “Asiyejua kufa na atazame kaburi.” Kwa hiyo tunaalikwa pia kwenda makaburi mara nyingi kuwaona wenzetu walioishapambana na kifo, nao watatusaidia kutafakari vizuri zaidi fumbo hilo la kifo.

Hebu tujaribu kutafakari kidogo na kupata jibu stahiki juu ya kifo na hatima ya maisha yetu. Tuanze utafiti wetu na Wayahudi, hasahasa manabii na wanazaburi. Wenzetu walianza utafiti mpya juu ya kifo wakitegemeza hoja zao juu ya kitu hiki “upendo”. Yaani kama Mungu aliingia katika mahusiano na binadamu na kufanya naye maagano iwe kwa njia ya manabii wa aina yoyote ile ni kwa sababu Mungu alimpenda binadamu na hivi akataka kuwa na mawasiliano naye. Ukimpenda mtu kwa dhati, huwezi ukamwacha tu kienyeji.

Hiyo ndiyo sheria ya upendo. Kwa hiyo ukisema: “Mungu ninakupenda”, naye akikuambia “Ninakupenda”, basi upendo huo hauwezi kwisha. Namna hii ya kufikiri, ina nguvu sana katika maisha. Katika Agano la kale, Mungu anawaambia wayahudi: “Wewe una thamani machoni pangu, nami ninakupenda” (Isaya). Hapo yaonesha wazi kuwa Mungu anao mradi wa kumpenda kiumbe chake kwa sababu amemwumba. Kwa hiyo katika Injili, tunaona kuwa katika mradi huo, Mungu amewekeza katika upendo kwa njia ya udalali ambao ni yeye mwenyewe katika nafsi ya pili ya Mungu, Yesu Kristu.

Injili ya leo imechukuliwa toka mazungumzo juu ya chakula cha uzima Ekaristi. Mradi huo wa Mungu umeanishwa kwa neno moja tu “Mapenzi”. Neno hilo limetamkwa na Yesu karibu mara nne: “sikushuka kutoka mbinguni ili niyafanye mapenzi yangu”; halafu, “bali niyafanye mapenzi yake aliyenipeleka”; halafu tena “Mapenzi yake aliyenipeleka ni haya”; na mwisho “Kwa kuwa mapenzi yake baba yangu ni haya”.

Hebu tumwangalie kwa undani Dalali aliyekabidhiwa kutekeleza mradi wa Mungu kwa wanadamu anasema: “Wote anipao Baba watakuja kwangu; wala yeyote ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe”. Hivi ndiyo Mungu anavyomwaminisha Yesu mradi huo wa mapendo kwa binadamu. Mungu anauaminisha ubinadamu wote kwa Yesu bila masherti. Kwa hiyo ili kuelewa maana ya kifo na ukombozi toka kifo, yabidi tuingie katika mradi huo wa mahusiano ya upendo (mapenzi) na Yesu.

Hoja ya msingi ya kuingia katika mahusiano hayo ni ile anayoisema Yesu mwenyewe, “Kwa kuwa mimi sikushuka kutoka mbinguni ili niyafanye mapenzi yangu, bali mapenzi yake aliyenipeleka.” Hivi ni dhahiri kwamba Yesu amefika duniani kama dalali ili kutekeleza mradi wa Mungu, yaani kunadisha na kuendeleza mahusiano hayo ya upendo. Mungu amemdhamini Kristu mwanae mradi mzima wa upendo. Kama anavyothibitisha Yesu mwenyewe: “Mapenzi yake aliyenipeleka ni haya, ya kwamba katika wote alionipa nisimpoteze hata mmoja, bali nimfufue siku ya mwisho.” Hapo ndipo palipojaa uhondo! Maana yake bila Kristu, hatuwezi kupata jibu sahihi juu ya kifo, jibu linalookoa na kuelewa mwisho au hatima yetu. Na Yesu aliye mdhamini wa mradi huo hataki kujiangusha mwenyewe anaposema, “Katika wote alionipa nisimpoteze hata mmoja, bali nimfufue siku ya mwisho” anamaanisha kwamba atatuwapelekesha hao aliokabidhiwa hadi kieleweke.

Kufufuliwa siku ya mwisho, kadiri ya mwinjili Yohane haimaanishi mwisho wa dunia, bali ni Kalvario, juu ya msalaba siku ile anaposulibiwa na kufa. Tendo la mwisho la Yesu la upendo ni pale alipoitoa roho na maisha yake ya kimungu, nguvu ya upendo aliyoitolea yote kabisa wakati wa uhai wake na kuihitimisha pale msalabani. Siku hiyo ya mwisho anaitoa roho yake na maisha yale ya milele yanaingia kwenye mahusiano ya daima na Mungu, na maisha hayo hayana mwisho. Hayo ndiyo mapenzi ya Mungu.

Mradi huo unatekelezeka tu endapo tutamtambua Mungu katika Kristu: “Kwa kuwa mapenzi yake Baba yangu ni haya, ya kwamba kila amtazamaye Mwana na kumwamini yeye, awe na uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho.”
Maana yake, upendo huo wa Baba utatekelezeka kwa namna tatu: kwanza kwa yule “amtazamaye Mwana,” kumbe yatubidi kuona au kutazama. Kuutazama au kuuona huu mradi wa Mungu na kumtambua Kristu ambaye ndiye mdhamini mkuu wa Mungu. Halafu yabidi “kumwamini Yesu”, yaani kutoa ushuhudi wa binafsi kwa huyo mdhamini pekee. Kisha matokeo ya kumtambua na kuishi kama alivyoishi huyo mdhamini yatakuwa ni “kufufuliwa naye”.

Kwa hiyo katika maisha yetu yatubidi tuyadhihirishe hayo mahusiano ya mapendo na Mungu kwa njia ya Kristu mdhamini wa mapendo. Kwa wale wenzetu walioishazaliwa kwa Baba, yaani waliofariki, wameutambua tayari uso wa Yesu na kumwaminia hivi sasa wamepokea maisha ya kimungu. Kwao hao sisi leo tunawapa ushirikiano kwa kuwa karibu sana nao, na siyo leo tu bali daima. Kama maisha yao hayakuwa makamilifu, sisi tuwaombee yaani kuwaonesha upendo, kwani Mungu amewekeza upendo katika Yesu Kristu.

Saturday, November 1, 2014

Ben Kiko enzi za uhai wake


 



Ben Kiko Hatunaye tena!

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Waziri wa Habari, Vijana Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Dkt. Fenela Mukangara kuomboleza kifo cha aliyekuwa Mtangazaji na Mwandishi Mkongwe na Mahiri hapa nchini wa iliyokuwa Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) ambayo kwa sasa ni TBC Taifa, Ben Hamis Kikoromo maarufu kama Ben Kiko.

Ben Kiko amefariki dunia usiku wa kuamkia tarehe 31 Oktoba, 2014 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) Jijini Dar es Salaam alikokuwa amelazwa akiendelea na matibabu ya figo baada ya kuhamishiwa hapo akitokea Hospitali ya Jeshi ya Milambo Mkoani Tabora. “Nimeshtushwa, nimesikitishwa na kuhuzunishwa sana kutokana na taarifa za kifo cha Mwanahabari na Mtangazaji huyu Mahiri ambaye ametoa mchango mkubwa wa kihabari kwa Taifa letu”, amesema Rais Kikwete akiomboleza msiba wa Ben Hamis Kikoromo.

“Namkumbuka Marehemu Ben Kiko, enzi za uhai wake, kama Mtangazaji aliyekuwa na mvuto mkubwa kwa wasikilizaji wake kutokana na namna yake ya kipekee ya kuripoti matukio hususan katika kipindi kilichojizolea umaarufu mkubwa wakati huo cha MAJIRA kilichokuwa kikirushwa hewani na Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD)”.

Wakati wa vita dhidi ya Nduli Idi Amin wa Uganda mwaka 1978, Ben Hamis Kikoromo alifanya kazi kubwa kwa Taifa kwani aliweza kuripoti matukio mbalimbali kutoka katika uwanja wenyewe wa vita, na hivyo kuliwezesha Taifa na wananchi kwa ujumla kuhabarika vilivyo na matukio yaliyokuwa yakiendelea.

“Kutokana na msiba huu mkubwa, pokea salamu zangu za Rambirambi kutoka dhati ya moyo wangu kwa kumpoteza mmoja wa Waandishi na Watangazaji Mahiri katika Tasnia ya Habari hapa nchini.

Vilevile kupitia kwako, naomba Salamu zangu za Rambirambi na pole nyingi ziifikie Familia ya Marehemu Ben Hamis Kikoromo kwa kupoteza Kiongozi na Mhimili Madhubuti wa Familia. Nawaomba Wanafamilia wote, ndugu na Jamaa wa Marehemu wawe wavumilivu na wenye subira wanapoomboleza kifo cha mpendwa wao huku wakitambua kuwa yote ni mapenzi yake Mola”, amesema Rais Kikwete.

Amewahakikishia Wanafamilia kuwa yuko pamoja nao katika muda wote wa maombolezo, na anamuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aipokee na kuilaza mahala pema peponi Roho ya Marehemu Ben Hamis Kikoromo, Amina.

Aidha Rais Kikwete ametuma Salamu za Rambirambi kwa Wanahabari kote nchini ambao kwa hakika msiba wa Ben Kiko utakuwa umewagusa kwa karibu. Hata hivyo amesema kuondoka kwa Ben Kiko kusiwe chanzo cha wao kukata tamaa, bali kifo chake hakina budi kuwa chachu katika kujituma zaidi, na wawe tayari kuiga yote mazuri aliyoyafanya Marehemu enzi za uhai wake hapa duniani hususan katika Taaluma ya Uandishi wa Ha

Chelsea, Arsenal safi

*Liverpool waoga kichapo kwa Newcastle
Chelsea wameendeleza rekodi ya kutofungwa baada ya kuwachapa QPR 2-1, Arsenal wakavuna pointi tatu na mabao matatu bila majibu kwa Burnley huku Liverpool wakipoteza mechi.
Chelsea sasa wanaongoza kwa tofauti ya pointi nne, baada ya kufikisha 26 katika michezo 10, wakiwa mbele ya Southampton. Diego Costa alirejea dimbani baada ya kukosekana katika mechi nne zilizopita, lakini hakufunga bao.
QPR walicheza vyema na kuwabana wenyeji, kwani hadi dakika ya 74 mabao yalikuwa 1-1, Chelsea wakaja kubahatika kwa bao la penati la Eden Hazard dakika moja baadaye na kutoka na ushindi. Bao jingine lilifungwa na Oscar wakati la QPR lilifungwa na Charlie

ncastle
Kocha Jose Mourinho amesema hakufurahia ushindi huo akisema timu yake hawakucheza vizuri, tofauti na alivyotarajia. Kocha wa QPR, Harry Redknapp alisononeshwa na penati iliyotolewa, akisema haikuwa haki.
Katika mechi nyingine Arsenal wamewafurahisha washabiki wao kwa kuwatandika Burnley 3-0 kwa mabao mawili ya Alexis Sanchez ambaye kwa msimu huu amefikisha 10 wakati furaha nyingine ilikuwa kwa beki kinda Calum Chambers aliyefunga bao lake la kwanza tangu aanze kuchezea timu ya wakubwa.
Theo Walcott alicheza kwa mara ya kwanza tangu alipoumia Januari, akichukua nafasi ya Alex Oxlade-Chamberlain dakika 10 kabla ya mechi kumalizika na Arsene Wenger anasema alivyocheza ni dhahiri atarudi kwenye hali yake ya kawaida mapema.
Newcastle wameendelea kufufuka ambapo wamefanikiwa kuwalaza Liverpool 1-0, hali inayozidi kumfedhehesha kocha wa Liverpool, Brendan Rodgers na kumpa ahueni kubwa yule wa Magpies, Alan Pardew.
Bao pekee la mchezo lilifungwa na Perez Guiterez katika dakika ya 73, ukiwa ni ushindi wa tatu mfululizo wakati Liverpool wamefikisha mechi mbili bila ya kufunga hata bao moja. Watu walikuwa wakimwangalia Mario Balotelli awe mkombozi wa Liver, lakini sasa amefikisha mechi nane pasipo kuzifumania nyavu.

1414871851910_wps_16_Chelsea_Manager_Jose_Mour

Siku kuu ya Watakatifu Wote!

Tunakuletea habari njema ya furaha tunapotafakari pamoja Neno la Mungu katika sherehe ya Watakatifu wote. Mama Kanisa akitaka kuhitimisha mwaka wa Kanisa kwa furaha anaona ni vema awaoneshe watoto wake lengo la maisha ya kikristu yaani ni kuelekea maisha ya utakatifu, maisha ya ya milele mbinguni. 

Kumbe, Mama Kanisa amependa kila tarehe 1Novemba ya kila mwaka, sherehe hii iadhimishwe katika Kanisa zima la ulimwengu. Adhimisho hili ni mwaliko kwetu kuchuchumalia maisha yanayotimiza mapenzi ya Mungu, maisha ya ufufuko ambayo Mtume Paulo anatuambia daima akisema basi mkishafufuliwa mkayatazame yaliyo ya juu!

Mpendwa, yafaa kutambua watakatifu ni akina nani? Watakatifu ni wale wanaokaa na Mungu katika kiti chake cha enzi kadiri tusomavyo katika kitabu cha Ufunuo. Ni marafiki wa kweli au tunaweza kusema ni marafiki wa dhati au wa kina. Katika lugha yangu ya kihaya Watakatifu tunaweza kuwalinganisha na “Abatahanju” yaani wale ambao huingia ndani ya nyumba mpaka sebule ya nyuma na hata jikoni.

Ni wale ambao hula chakula pamoja na mkuu wa familia, na hivi wanafurahi pamoja na Mungu Baba huko mbinguni. Ni wale ambao Injili ilikuwa chakula chao cha kila siku walipokuwa duniani na walijikabidhi katika mikono ya Mungu na kuwa mali yake. Ni wale walioishi heri nane mafundisho ya Kristu aliyoyatoa pale mlimani. Ni wale ambao walitunza neema ya UTAKASO waliyoipokea wakati wa Ubatizo.

Ni wale ambao walimpenda Mungu kwa moyo wao wote, kwa akili yao yote na kwa nguvu zao zote na kisha wakampenda jirani aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Ni wale ambao katika ubinadamu wao walikubali mateso wakitambua na kujua siri ya furaha watakayoipata milele. Sasa wanafurahia matunda ya msalaba wa Kristu. Kwa kifupi ni wale walioshika vema amri kuu ya mapendo.

Ili basi nasi tuweze kufikia hali hiyo iliyo heri na furaha upeo, somo la kwanza linaweka mwaliko kwa watu wote kuwa, ili mmoja aweze kupokea heri za milele yaani utakatifu, ni lazima kufua mavazi katika Damu ya Mwanakondoo. Ni lazima kukinywea kikombe kimoja cha Damu Takatifu iliyo thamani ya wokovu kwa wote. Ndiyo kusema ni kuishi kwa kutimiza mapenzi ya Mungu.

Kwa kufua mavazi katika Damu ya Mwanakondoo kunamwondoa mtu katika dhiki ya dhambi na dhiki ya upungufu wa upendo mkamilifu. Mmoja ananyakuliwa toka taabu ya ulimwengu geugeu na kuvikwa mavazi meupe ndiyo utakaso mkamilifu unaowezesha kuimba baraka na utukufu na hekima na shukrani na heshima na uweza na nguvu zina Mungu wetu hata milele na milele. Amina. Huu ni wimbo wa sifa kwa Mungu ambao unaweza kuimbwa na walio wake, ndiyo watakatifu.

Katika Injili ya Mathayo tunapata mafundisho ya Yesu mlimani yaani Heri Nane. Bwana anaonesha njia ya kufikia utakatifu, njia ya kuishi mapenzi ya Mungu. Anaainisha namna ya kufika mbinguni, akisema, wanaheri wale walio maskini wa roho maana ufalme wa mbinguni ni wao. Wanaheri wenye upole maana watairithi nchi. Anazidi kukazia utakaso wa roho akisema heri wenye moyo safi maana hao watamwona Mungu. Hizi ni baadhi ya heri nane za mlimani njia kamilifu ya kufikia utakatifu.

Kwa kuzitafakari heri nane tunaweza kusema mambo makuu mawili ni lazima katika kufikia utakatifu. Jambo la kwanza ni kujitenga na chachu ya ulimwengu. Kumbuka Bwana anasali na kusema tuko ulimwenguni lakini sisi si wa ulimwengu. Hii yamaanisha kujitenga na kile kinachopingana na injili ya Bwana, na hivi kuwa maskini wa roho. Kumbe mkristu anapaswa ajisikie daima kinyume na mawimbi ya ulimwengu yanayopingana na Injili. Jambo la pili ni lile la kupokea kikombe cha mateso daima na kulitangaza jina la Bwana.

Mateso haya hugeuka na kuwa furaha katika maisha ya mkristu sasa anapoishi na baadaye. Mtakatifu lazima aoneshe sura ya Kristu mteswa na mwenye furaha kwa ajili ya ukombozi wa ulimwengu. Mtakatifu ni lazima amwilishe Heri Nane katika maisha yake na hivi zingae daima na kuwa kielelezo cha maisha ya upendo. >>>>
Endelea hapa

Katiba Mpya ya watanzania isome hapa

Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 ya Jimbo Katoliki Mahenge.

Jimbo Katoliki la Mahenge, Tanzania, linaadhimisha kilele cha Jubilee ya miaka 50 tangu lilipoanzishwa kunako mwaka 1964 na Marehemu Askofu Elias Mchonde aliyekuwa Askofu msaidizi wa Jimbo la Dar es Salaam akateuliwa kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo Katoliki la Mahenge na kuliongoza Jimbo hili kuanzia wakati huo hadi mwaka 1969 alipofariki dunia. Baadaye Jimbo limeongozwa na Askofu Nikas Kipengele tangu mwaka 1970 hadi mwaka 1971; Askofu Patrick Iteka kuanzia mwaka 1973 hadi mwaka 1993.
Askofu Agapiti Ndorobo akapewa dhamana ya kuwaongoza waamini wa Jimbo Katoliki la Mahenge tangu mwaka 1995 hadi wakati huu, Jimbo linapomwimbie Mwenyezi Mungu utenzi wa shukrani na sifa kwa kuadhimisha Jubilee ya Miaka 50 ya uwepo wake. Askofu Ndorobo ameliongoza Jimbo kwa miaka 19 sasa. Katika mahojiano maalum na Radio Vatican anabainisha: mafanikio na changamoto anazokabiliana nazo katika kuwaongoza, kuwafundisha na kuwatakatifuza Watu wa Mungu Jimboni Mahenge.Itakumbukwa kwamba, Jimbo Katoliki la Ifakara lililoanzishwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI kunako mwaka 2012 na Askofu Salutaris Melchior Libena kuteuliwa akuwa Askofu wake wa kwanza ni matunda ya Jimbo Katoliki la Mahenge ambalo hapo awali lilikuwa na Parokia 38 lakini baada ya kuligawa ili kurahisisha shughuli za kichungaji kwa Watu wa Mungu, sasa Jimbo Katoliki la Mahenge lina Parokia 22, likiwa na waamini zaidi ya 215, 000 lakini hapo awali lilikuwa na waamini 487, 000.

Askofu Ndorobo anasema kwamba, katika kipindi cha miaka 50 ya uwepo wa Jimbo Katoliki la Mahenge kumekuwepo na maendeleo makubwa katika medani mbali mbali za maisha, lakini zaidi ni upendeleo kwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Kuna vituo vya kutunzia wagonjwa wa kifafa, kituo cha wagonjwa wa Ukoma pamoja na kituo cha Watoto Yatima.

Jimbo Katoliki la Mahenge linamiliki na kuendesha Sekondari 5; Vituo vya Afya na Zahanati 9 na kwamba kuna mpango mkakati wa kuanzisha Hospitali ili kujibu kilio cha watu wenye shida na mahangaiko wanaolazimika kutembea umbali mrefu ili kutafuta tiba kwa magonjwa yanayowasumbua, lengo ni kuendelea kutangaza Injili ya Uhai, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Askofu Ndorobo anakiri kwamba, Jimbo la Mahenge limeendelea kuwa na miito mbali mbali ya maisha ya: Kipadre, Kitawa na Ndoa. Kuna vyama vya miito vinavyosaidia mchakato wa malezi ya miito ndani ya Kanisa, kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko, unaowachangamotisha vijana kupenda kushiriki katika maisha ya Kipadre, Kitawa na Ndoa takatifu.

Askofu Ndorobo anasema miaka 19 ya utume wake kama Askofu wa Jimbo Katoliki Mahenge amekumbana na changamoto nyingi, lakini katika mahojiano na Radio Vatican anagusia changamoto kuu mbili, yaani umuhimu wa Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo na Maisha ya Sala na Kisakramenti. Anasema, kwa miaka hii yote amependa kukazia umuhimu wa waamini kushiriki katika maisha ya Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo kwani hizi ni shule ya Sala, Neno la Mungu na kielelezo cha imani tendaji.

Huu ndio mwelekeo ambao anapenda kuuendeleza hata baada ya maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 ya Jimbo Katoliki Mahenge. Anasema, amependa kukazia umuhimu wa waamini kushiriki kikamilifu katika maisha ya Sala na Sakramenti za Kanisa ili waweze kujichotea neema na baraka; waweze kuonja huruma na upendo kutoka kwa Mwenyezi Mungu, tayari kufanya mabadiliko ya kina katika maisha yao, kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu. Viongozi wawe ni mfano bora wa maisha ya sala na Sakramenti za Kanisa, ili wao wakiishaimarika, waweze pia kuwaimarisha ndugu zao katika imani, matumaini na mapendo.

NCHI YANGU FAHARI YANGU TOUR