Mama Kanisa pia anaadhimisha Jubilee ya miaka 5o tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipotoa Tamko kuhusiana na Maisha ya Kitawa: Perfect Caritatis, yaani Upendo Mkamilifu, Waraka uliowataka Watawa kupyaisha maisha yao, kwa kutoa nafasi ya kwanza katika maisha ya kiroho, mashauri ya Kiinjili, maisha ya kijumuiya pamoja na malezi makini kwa wale wote wanaotaka kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.
Haya ni matukio makuu yatakayoliwezesha Kanisa kufanya tafakari ya kina katika maisha na utume wa Watawa sehemu mbali mbali za dunia. Mwaka wa Watawa Duniani unazinduliwa rasmi, Jumamosi jioni tarehe 29 Novemba 2014 kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Makuu, lililoko mjini Roma kwa Ibada na Mkesha wa Sala, kuanzia saa 1:00 Usiku. Tarehe 30 Novemba, 2014, Jumapili ya kwanza ya Kipindi cha Majilio, kutafanyika Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, kuanzia saa 4:00 asubuhi kwa saa za Ulaya.
Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume linasema kwamba, matukio haya ni muhimu sana katika uzinduzi wa Mwaka wa Watawa Duniani, kwa kujiweka chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria, Mama wa Mungu na msimamizi wa maisha ya kitawa. Hiki ni kipindi cha matumaini, sala na tafakari ya kina kuhusu matendo makuu ya Mungu katika maisha ya Watawa wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya Mungu na jirani zao, kwa kutambua kwamba, imani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ambayo Watawa wanapenda kuwamegea na kuwashirikisha wengine.