Dar/Dodoma. Kikao cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jana usiku kilivunjika baada ya vurugu kutawala ukumbini humo.
Vurugu hizo zilianza saa 04:42 usiku hadi saa
04:49 usiku wakati Spika Anne Makinda alipolazimika kuahirisha Bunge
hadi leo saa tatu asubuhi.
Chanzo cha vurugu ni kutokana na ugumu wa
kutokukubaliana na azimio la tisa, lililolenga kumwajibisha moja kwa
moja Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Azimio la PAC lilitaka Waziri Muhongo aadhibiwe
kwa kufukuzwa kazi kutokana na tuhuma zilizokuwa zinazomkabili ikiwamo
kulidanganya Bunge.
Hata hivyo, baadhi ya wabunge wengi wakiwa wa CCM
walitaka waziri huyo asiadhibiwe na Bunge bali achukuliwe hatua na
mamlaka iliyomteua.
Wakati ubishani huo ukiendelea, ikiwa imefika saa
4.42 usiku Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe
alisimama na Spika Makinda alimruhusu kuzungumza.
“Bunge kufikisha saa tano kasoro ni historia,
lakini leo (jana) kuna uzito wa kiti na uzito wa wabunge kwa mamlaka
ambayo yako ndani yao. Panaonekana kuna maamuzi mengine ya kulinda watu.
Kwa nini leo tuna kigugumizi. Tunapata wakati mgumu kuendelea kushiriki
kikao cha kulindana. Kwanini mnalinda wezi,” ilikuwa ni kauli ya Mbowe.
Mara baada ya kutoa kauli hiyo, wabunge wote wa
upinzani walisimama na kuanza kupiga kelele kwamba wezi
waondoke…tunataka fedha zirudi…tunataka fedha zirudi…vijana
msilale…vijana msilale.
Wakati wabunge hao wakiendelea kuimba, wabunge wa
CCM wao walikuwa wakizunguka zunguka huku wengine wakitoka ndani ya
Ukumbi wa Bunge.
Hata hivyo, wabunge wa upinzani waliendelea
kusimama, kuimba na kupiga makofi, huku wabunge wa CCM wakimpongeza
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele kwa kuruka kihunzi
alichokuwa amewekewa na kamati ya PAC.
Kutokana na hali hiyo wabunge wengine walisimama
vikundi vikundi, huku Waziri wa Nchi, Sera, Uratibu na Bunge, William
Lukuvi, na Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka walikuwa
wakiwasihi wabunge wa upinzani wasiondoke bungeni.
Spika Makinda alisimama na kusema, “Mheshimiwa Mbowe kuondoka mapema ni mambo ya kitoto, semeni mnataka Bunge lifanye nini.”
Hata hivyo, kauli hiyo ya Makinda haikuwafanya wabunge hao
kuacha walichokuwa wakikifanya, bali walibaki ndani ya ukumbi wakiwa
wamesimama hadi ilipofika Saa 04:49 usiku wakati Spika Makinda
aliposimama na kusema, “Waheshimiwa wabunge naahirisha kikao cha bunge
hadi pale tutakaposhauriana.”
Kuvunjika kwa kikao hicho kinaweka njia panda
hatima ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
Frederick Werema ambao Bunge lilikuwa halijafikia kufanya maazimio ya
hatima yao.
Hoja ya baadhi ya wabunge wa CCM walikuwa wakitaka
mapendekezo yaliyotolewa na Mbunge wa Bariadi (CCM), Andrew Chenge
kuhusu hatima ya Pinda na Werema yapite.
Chenge alipendekeza kuwa, “Kuhusu suala la Waziri
wa Nishati na Madini lifikishwe kwa mamlaka ya uteuzi kwa hatua zaidi
(wakimaanisha Rais).”
Pendekezo ambalo lilipingwa na upinzani kwa kile
walichoeleza kuwa Bunge linaweza kuwawajibisha kama ambavyo limewahi
fanya hivyo. Spika Makinda akijibu hoja ya Bunge kuwawajibisha alisema;
“Mnajua waheshimiwa wabunge huko nyuma mawaziri walikubali wenyewe,
lakini hawa wamekataa ndiyo maana tunaona haya yanatokea.”
Awali, Bunge hilo limemwachia Rais Jakaya Kikwete
kufanya uamuzi wa kuwawajibisha, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na
Madini, Eliakim Maswi baada ya kuadhimia kuwa suala lake lifikishwe kwa
Rais kwa hatua zaidi.
Mjadala wa kuchukuliwa hatua kwa Maswi uliwagawa
wabunge na kuwafanya kujadili kwa zaidi ya dakika 30, kufikia uamuzi huo
ambao hata hivyo ulipingwa na baadhi ya wabunge.
Hata hivyo, Bunge limemwokoa Naibu Waziri wa
Nishati na Madini, Stephen Masele kwa kuona kuwa kauli yake aliyoitoa
haikuwa na madhara yoyote hivyo hahusiki kwa vyovyote vile kwenye sakata
hilo.
Hatua ya kuwashughulikia viongozi hao na wengine
kuokolewa ilifikiwa baada ya mvutano mkali wa pande mbili ndani ya Bunge
katika kukubaliana na mapendekezo ya kamati ya PAC.
Baada ya muda wabunge na mawaziri walioanza kuingia kwenye magari yao na kuondoka bila kujua nini kitaendelea leo.