Thursday, May 7, 2015

MVUA ZAENDELEA KUWATESA WATU DAR



Baada ya mvua ya kubwa ya kama masaa mawili mfululizo,maeneo mengi jijini Dar yamejaa maji na kupelekea adha kubwa kwa wakazi wa jiji hili.Pichani ni eneo la Morogoro Road
Barabara ya Bibi Titi Mohamed mambo yalikuwa namna hii,wenye magari madogo walipita kwa staili ya maji ya shingo

TAHADHARI YA KUWEPO MVUA KUBWA MAENEO YA UKANDA WA PWANI YA NCHI

HALI ILIVYOKUWA ENEO LA SINZA-AFRIKA SANA

Saturday, April 4, 2015

Masomo ya Jumapili ya Paska "mwaka B wa Kanisa (Tarehe 05/04/2015)

05

 APRILI
 Heri ya Paska Masomo ya Mwaka "B".

SOMO  1: Mdo. 10:34, 37- 43
Somo katika kitabu cha Matendo ya Mitume.
  Petro akafumbua kinywa chake, akasema, Jambo lile ninyi mmelijua, lilionea katika Uyahudi wote likianzia Galilaya, baada ya ubatizo aliohubiri Yohane; habari za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu; naye akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana Mungu aikuwa pamoja naye. Nasi tu mashahidi wa mambo yote yaliyotendeka katika nchi ya Wayahudi na katika Yerusalemu; ambaye walimwua wakamtundika mtini. Huyo Mungu alimfufua siku ya tatu, akamjalia kudhihirika, si kwa watu wote, bali kwa mashahidi waliokuwa wamekwisha kuchaguliwa na Mungu, ndiyo sisi, tuliokula na kunywa naye baada ya ufufuka kwake kutoka kwa wafu. akatuagiza tuwahubiri watu na kushuhudia ya kuwa huyu ndiye aliyeamriwa na Mungu awe mhukumu wa wahai na wafu. Huyo manabii wote humshuhudia, ya kwamba kwa jina lake kila amwaminiye atapata ondoleo la dhambi.

WIMBO WA KATIKATI. 
Zab. 118:1-2, 16-17, 22-23. 
1.Aleluya.
            Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema
  kwa maana fadhili zake ni za milele.
           Israeli na aseme sasa,
    Ya kwamba fadhili zake ni za milele.

K. siku hii ndiyo aliyoifanya Bwana, Tutashangilia na kuifurahia.

2. Mkono wa kuume wa Bwana umetukuzwa;
                   Mkono wa kuume wa Bwana hutenda makuu.
     Sitakufa bali nitaishi,
                   Nami nitayasimulia matendo ya Bwana.
(K)
3. Jiwe walilolikataa waashi
                Limekuwa jiwe kuu la Pembeni.
     Neno hili limetoka kwa Bwana,
                Nalo ni ajabu machoni petu (K)

Monday, March 30, 2015

UJUMBE WA BABA MTAKATIFU SIKU YA VIJANA (JUMAPILI YA MATAWI 29/03/2015)

Heri wenye moyo safi maana hao watamwona Mungu ndiyo kauli mbiu inayoongoza maadhimisho ya Siku ya Vijana Kijimbo inayoadhimishwa na Mama Kanisa, Jumapili ya Matawi tarehe 29 Machi 2015 kama sehemu ya maandalizi ya Siku ya 30 ya Vijana Kimataifa itakayoadhimishwa Jimbo kuu la Cracovia, Poland, mwezi Julai 2016.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wa maadhimisho ya Siku ya vijana kijimbo anagusia hamu ya vijana kuwa na furaha na anaendelea kuchambua kwa kina na mapana kauli mbiu ya ujumbe huu kwa kuwakumbusha vijana kwamba, Kristo ni utimilifu wa furaha ya mwanadamu, changamoto kwa vijana kuhakikisha kwamba, wanatunza ndani mwao moyo safi na kamwe wasibeze upendo wa dhati.

Baba Mtakatifu anawataka vijana wakati mwingine kwenda kinyume cha mawimbi ya maisha ya ujana, kwa kutambua kwamba, fainali iko uzeeni. Wawe ni watu makini katika maisha na maamuzi yao na kamwe wasikubali na kumezwa na malimwengu kwani watajikuta wapweke na hawana matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Vijana katika maisha waoneshe ari na moyo wa kupenda kwa dhati.

Hija ya maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Kimataifa huko Cracovia, Poland inaongozwa na Hotuba ya Heri za Mlimani, ambayo kimsingi ni muhtsari wa mafundisho makuu ya Yesu, chemchemi ya furaha ya kweli na amani ya ndani. Baba Mtakatifu anabainisha kwamba, kila mtu duniani yuko kwenye mchakato wa kutafuta furaha ambayo inapata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu anayeijaza mioyo ya waja wake, kama yanayobainisha Maandiko Matakatifu, kielelezo cha umoja na mshikamano kati ya mwamini na nafsi yake; mwamini na Mungu pamoja na jirani zake.

Baba Mtakatifu anaendelea kusema kwamba, dhambi ilipoingia ulimwenguni, ilichafua usafi wa mioyo ya binadamu, kiasi kwamba, dhambi ikawa ni kizingiti cha mwanadamu kuweza kukutana moja kwa moja na Muumba wake; furaha ya kweli ikakosa dira na mwelekeo sahihi; mwanadamu akatumbukia katika huzuni na mahangaiko ya ndani. Mwanadamu akamlilia Mwenyezi Mungu, naye akakisikia kilio chake na kumtuma Mwanaye mpendwa, Yesu Kristo ili aweze kumfungulia mwanadamu malango mapya ya kukutana na Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko anawaambia vijana kwamba, ni kwa njia ya Yesu Kristo wanaweza kupata utimilifu wa wema na furaha ya kweli. Yesu Kristo ndiye mwenye uwezo wa kuzima kiu ya matarajio ya vijana katika maisha, ambao wakati mwingine wanadanganywa na malimwengu kwa kuwapatia njia za mkato.

Baba Mtakatifu Francisko kwa namna ya pekee kabisa anawaalika vijana kuhakikisha kwamba, wanatunza usafi wa moyo kwa kujenga na kudumisha mahusiano mema na matakatifu kati yao na jirani zao. Moyo wa mtu n ikisima cha mawazo na vionjo, changamoto kwa vijana kuhakikisha kwamba, mawazo yao yanakuwa safi pasi na mawaa mbele ya Mungu na binadamu. Moyo safi wenye uwezo wa kujenga mahusiano bora.

Baba Mtakatifu anawaalika pia vijana kujenga utamaduni wa kutunza mazingira kwani hii ni sehemu ya ekolojia ya binadamu, ambayo inapaswa kuwa kweli ni safi, kama kielelezo makini cha mahusiano bora  kati ya mwamini na Muumba wake pamoja na kazi ya uumbaji ambayo Mungu amemkabidhi mwanadamu kuitunza na kuiendeleza. Vijana waonje upendo wa Mungu anayewaangalia kama mboni ya jicho lake!

Baba Mtakatifu anawakumbusha vijana kwamba, ujana ni moto wa kuotea mbali; ni wakati ambapo mbegu ya upendo ambao unajikita katika ukweli, wema na ukuu unaanza kuchanua pole pole katika maisha ya vijana. Baba Mtakatifu anawaangalisha vijana kuwa makini ili mbegu hii ya upendo isije ikachafuliwa na hatimaye kuharibiwa. Hapa vijana wanatakiwa kuwa makini na kamwe wasikubali kuyumbishwa na mawimbi ya maisha ya ujana kwa kubeza upendo, kiasi cha kuugeuza kuwa ni mahali pa kukidhi tamaa za mwili. Lakini ikumbukwe kwamba, upendo wa kweli unajikita katika wema, umoja, uaminifu na uwajibikaji. Vijana wanapaswa kuwa ni wana mapinduzi kwa kwenda kinyume na mawimbi haya potofu na dhidi ya utamaduni wa raha za mpito ambazo mara nyingi zimewaachia vijana machungu katika maisha.

Vijana wawe waaminifu na kuwajibika barabara kwa kuonesha jeuri kwamba, wanafahamu kupenda kwa dhati. Baba Mtakatifu anasema, ana imani kubwa na vijana na kwamba, anawaombea, ili kamwe wasitindikiwe na ujasiri huu. Vijana wanaalikwa kwa namna ya pekee kabisa na Baba Mtakatifu kuhakikisha kwamba, wanamtafuta Mwenyezi Mungu kwa njia ya: sala, tafakari ya Neno la Mungu na upendo kwa jirani. Kusali ni kuongea na kujadiliana na Fumbo la Utatu Mtakatifu yaani: Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu. Vijana wajenge utamaduni na mazoea ya kusali vyema na daima.

Tafakari ya Neno la Mungu imwilishwe kwa njia ya upendo na huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kwa njia hii, vijana wataonja na kutambua uwepo endelevu wa Mungu katika maisha yao; Mungu ambaye anaendelea kutekeleza mpango wake kwa maisha ya kila kijana. Vijana wamkimbilie Mwenyezi Mungu wakiwa na mioyo safi pasi na woga wala makunyanzi mioyoni mwao. Vijana wanaposikia kwamba, wanaitwa na Mwenyezi Mungu katika miito mitakatifu, wasisite kusema, Ndiyo na kwa njia hii wataweza kuwa kweli ni mbegu ya matumaini kwa Kanisa na jamii inayowazunguka. Vijana watambue kwamba, mapenzi ya Mungu katika maisha yao ndicho kiini cha furaha yao ya kweli.

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha ujumbe wake kwa Siku ya Vijana Kimataifa katika ngazi ya kijimbo inayoadhimishwa Jumapili ya Matawi kwa kumshukuru Mtakatifu Yohane Paulo II ambaye miaka thelathini iliyopita alithubutu kuanzisha ndani ya Kanisa Siku ya Vijana Kimataifa. Hii ni hekima ya Kimungu na sauti ya kinabii ambayo imeliwezesha Kanisa kuwashirikisha vijana wengi matunda ya maisha ya kiroho. Mtakatifu Yohane Paulo II msimamizi wa Siku za Vijana Kimataifa, awaombee vijana wakati huu wa maandalizi kuelekea katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Kimataifa itakayofanyika Jimbo kuu la Cracovia, nchini Poland. Bikira Maria aliyejaa neema, uzuri na usafi wote, awasindikize vijana katika hija hii.

Tazama aleleya kuu hapa

Friday, March 27, 2015

Mwazo wa Juma kuu: Furaha, shangwe; mateso na huzuni!

Image result for sunday palms jesus in jerusalemMaadhimisho ya Jumapili ya Matawi, mwanzo wa Juma kuu ni kipindi cha: furaha na shangwe; mateso na huzuni; lakini pia ni kipindi cha matumaini kwa ajili ya ushindi wa Kristo mfufuka. Kanisa lina matumaini makubwa katika ile Siku ya kwanza ya Juma! Kanisa lataka kutuambia nini katika Jumapili hii ya matawi? Mwandishi mmoja anasema – kumfuata Kristo – mpole, kumfia Kristo ili tuweze kuuingia uzima wa milele pamoja naye. Ni lazima kumuiga Kristo katika sadaka ya kifo ili tumuige katika utukufu wa msalaba.
 Swali kubwa ni hili – kwa nini Mungu ameruhusu mateso? Nabii Ayubu – 31:37 – anapoongelea kuhusu mashindano ya mwisho anaomba Mungu ampe majibu. Jibu halionekani katika kitabu hiki cha Ayubu ila kinachoonekana ni kuwa fumbo la mateso lamezwa katika fumbo kuu la upendo la Mungu mwenyewe.
Kwa namna ya pekee, imani ya kikristo inaliishi fumbo hili – upendo mkuu wa Mungu. Haitoi jibu la moja kwa moja ni kwa nini ni kwa njia ya mateso ila twapata maelezo mbalimbali jinsi Mungu anavyotumia njia ya mateso kumkomboa mwanadamu. Mungu hutumia mateso ya mwanadamu ili kumkomboa mwanadamu. Ndiyo maana ya ibada yetu ya leo. Lakini fumbo labaki.
 Wainjili wetu wanaeleza historia ya mateso ya Yesu na kifo, lakini hawatoi jibu ni kwa nini lazima Yesu apitie njia ya mateso ili kutupatia wokovu. Ila wanaeleza matokeo yake kwamba kinachopatikana ni wokovu – matokeo ya mateso na kifo chake Kristo. Yaani matokeo yake ni wokovu wa mwanadamu.
 Mwinjili Marko – Mk. 15:39 – anasema tendo la kifo cha Yesu ndiyo sababu ya imani ya yule Akida – basi yule akida aliyesimama hapo alimwelekea, alipoona ya kuwa alikata roho jinsi hii, akasema, hakika huyu alikuwa mwana wa Mungu.
 Mwinjili Matayo – anaona ufufuko katika kifo cha Yesu – Mt. 27:52-53 – makaburi yakafufuka, ikainuka miili mingi ya watakatifu waliolala. Nao wakiisha kutoka makaburini mwao, baada ya kufufuka kwake, wakauingia mji mtakatifu, wakawatokea wengi.
 Mwinjili Yohani – Yoh. 19:30 – analinganisha kufa kwa Kristo na kutupatia roho – basi Yesu alipokwisha kuipokea ile siki, alisema, imekwisha, akainama kichwa, akaisalimu roho yake.
Mt. Paulo naye anaendelea kusaidia kutoa majibu anapowaandikia Wafilipi katika somo la pilia akiwaambia hivi: mwatakiwa kuwa wapole na wanyenyekevu na kuwa na mtazamo wa Kristo. Naye Kristo anaonesha wazi hilo – anajishusha na kuwa mwanadamu hata kufa msalabani.
  Habari juu ya mateso ya Kristo iko wazi katika somo la Injili. Ushuhuda wa imani anaotoa Mt. Petro juu ya ufuasi uko wazi katika fundisho la Yesu juu ya msalaba – Mk. 8:34-38 – mtu akitaka kuwa mfuasi wangu, ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake .... . Fundisho hili la imani linakamilishwa na maneno ya Yesu mwenyewe – ye yote yule anayetaka kunifuata ni lazima achukue msalaba wake na anifuate. Yawezekana pia katika maandiko haya ya Marko, anatoa mwaliko kwa wafuasi kumfuata Kristo kama anavyotualika.
Wote pamoja, Mwinjili Marko na Mtume Paulo – wanasisitiza haja ya kukubali mateso ili kukamilika katika maisha ya Kikristo. Ila wanaweka wazi kuwa hili si jambo la kibinafsi tu. Wote wanatambua kuwa katika Kristo hupatikana ukamilifu. Yesu kadiri ya Marko na Paulo ni zaidi ya mwalimu anayeongoza wengine tu. Anayefundisha watu ili wapate kuwa hai. Yesu ni uhai wenyewe, ni chanzo cha nguvu yetu sisi ya kumfuata yeye.
Ukiangalia kwa umakini wimbo kwa Kristo katika somo la Pili – jambo hili linakuwa wazi kabisa. Wimbo wazungumza habari ya umungu wake, anayejitoa kabisa na kuchukua aina ya mtumwa. Na baadaye kutukuzwa kwake mbinguni na kupewa jina la Bwana. Mwanazuoni mmoja anaandika hivi – ni nani ambaye angeweza kufanya hivyo? Mfano wa Kristo kujitoa kabisa ulifanywa ili kutoa wokovu. Kwa vile alifanya alichofanya, sisi twaweza kufanya anachotaka sisi tufanye.
Katika Injili ya Marko – na katika sehemu hii ya mateso – tunakutana na jumbe za wokovu zinazoelezea wazi wimbo huo. Ni nani awezaye kubisha kuwa sadaka aliyozungumzia Yesu si yeye mwenyewe? Siku ya karamu ya mwisho anajitoa mwenyewe awe chakula na kinywaji.   Tunaalikwa tuige mfano wa mtumishi mtii anayeteseka. Ndicho tunachoambiwa katika jumapili hii ya matawi. Lakini zaidi twaambiwa kuwa katika Kristo tunayo nguvu ya kuteseka. Kwa kumpokea yeye, tunapokea nguvu ya kufanya kama alivyofanya yeye.
Tutafakarishwe na mfano huu: Ndugu wawili – mdogo alikuwa jambazi na kila aina ya maisha ya ubaya na yasiyofaa kwa jamii. Kaka mkubwa daima alikuwa akitumia kila aina ya ushawishi na maonyo ili ndugu yake aondokane na maisha hayo ya ujambazi. Usiku mmoja huyu ndugu mdogo jambazi akarudi nyumbani mbio na nguo zake zimejaa damu. Mara akamwambia kaka yake nimeua mtu. Lakini mimi sitaki kufa. Dakika chache baadaye nyumba ikawa imezingirwa na polisi. Wote wawili wakajua wazi kuwa hakuna namna yo yote ile ya kutoroka katika mikono ya askari. Yule ndugu jambazi akaanza kulia sikunuia kumuua yule. Mimi sitaki kufa. Alimwambia kaka yake. Kaka mtu akapata wazo. Akachukua nguo za yule ndugu yake jambazi na kuzivaa. Polisi walipoingia ndani wakamkamata, wakamshtaki na kumhukumu kufa kwa sababu ya kuua. Akafa yeye na ndugu yake akabaki. Alikufa kwa ajili ya ndugu yake. Hiki ndicho anachofanya Yesu kwa ajili yetu.
Kilichopo katika somo la leo na adhimisho la leo ni swala la mapendo – upendo wa Mungu kwetu. Sisi tutalipaje upendo huo? Yule ndugu mdogo atalipaje upendo kwa kaka yake aliyekufa badala yake? Ndugu mpendwa, ni lazima majibu ya maswali yetu yapatikane katika Maandiko Matakatifu. Jibu la kidunia kuhusu kifo ni huzuni, karaha, wasiwasi, mashaka, kilio n.k.
 Jibu la Mungu ni tofauti. Ni furaha, ni utukufu, ni uzima mpya. Mbegu isipoanguka na kuchipua, haitazaa. Ni ajabu kweli. Nabii Ayubu anatuambia, mateso yanapoteza uzito wake yanapohusishwa na upendo wa fumbo la Mungu. Peke yetu hatutaweza kuelewa fumbo zito la ukombozi wetu. Ni katika imani tu twaweza kupata jibu. Mtazamo wa haya tufanyayo upo mbele, kwake Mungu. Hatuwezi kufanya mambo yamhusuyo Mungu na kutaka kupata majibu hapa hapa au hapo hapo au jinsi tunavyofikiri au kutaka sisi. Sisi kama tunamwamini Mungu, tumempokea Yesu, basi tuenende kadiri ya amri na maagizo yake na tumpe nafasi atende kazi yake ndani yetu.
Pd. Reginald Mrosso, C.PP.S.

NCHI YANGU FAHARI YANGU TOUR