Saturday, March 30, 2013

Kauli mbiu ya Maadhimisho ya Pasaka kwa Mwaka 2013

Kauli mbiu ya Maadhimisho ya Pasaka kwa Mwaka 2013 nchini Tanzania ni: Amani na Maendeleo!



Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salama akitoa ujumbe wake wa Siku kuu ya Pasaka kwa Mwaka 2013 inayokwenda sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, anawaalika Wakristo kwa namna ya pekee kabisa kuombea amani, umoja na mshikamano wa kitaifa, hasa kutokana na kushamiri kwa vitendo vya choko choko za kidini nchini Tanzania zilizopelekea: madhulumu na mauaji ya viongozi wa kidini pamoja na uchomaji moto wa nyumba za Ibada.

Kinzani za kidini zinazoendelea nchini Tanzania ni changamoto kwa Wakristo na Waislam kukutana na kujadiliana mustakabali wa Tazania. Kwa vile Serikali inayowajibu wa kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na utulivu inapaswa kuwapo ili kufuatilia majadiliano haya.

Kwa miaka mingi Wakristo na Waislam nchini Tanzania wameishi na kupendana kama ndugu na wala tofauti zao za kidini halikuwa ni jambo la kuwagawa! Lakini mambo yamebadilika katika miaka ya hivi karibuni kiasi cha kuwafanya watu kuanza kujiuliza, hivi kweli ni nani anayehusika na uchochezi wa vurugu za kidini na kwa manufaa ya nani?

Majadiliano ya kidini ni njia muafaka inayoweza kumaliza choko choko za kidini, kila upande ukilijadili suala hili katika ukweli, upendo na haki. Kardinali Pengo anaendelea kuwasihi Wakristo na watanzania wenye nia njema kuepukana na kishawishi cha kutaka kulipiza kisasi kutokana na madhulumu wanayokabiliana nayo. Anasema, ulinzi na usalama wakati wa Maadhimisho ya Juma kuu ni kazi na jukumu la Serikali, kumbe anatumaini kwamba, Wakristo wataweza kuadhimisha Mafumbo ya Imani yao kwa amani na utulivu.

Kardinali Pengo anasema, atakwenda Kanisa kuadhimisha Mafumbo ya Ukombozi, kama ni kufa ni afadhali afie Kanisani na wala hataacha kwenda kusali kwa sababu ya vitisho vya ulipuaji wa Makanisa vilivyozagaa nchini Tanzania wakati huu.

Kardinali Pengo amevishauri vyombo vya dola kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya ukweli, uwazi na maadili ya kazi. Anasema, Serikali haiwezi kuacha Tanzania kutawaliwa na "wahuni wachache" wanaoleta vurugu kwa kisingizio cha dini na kukazia kwamba, hatua madhubuti hazina budi kuchukuliwa ili haki, amani na utulivu viweze kudumishwa.

Itakumbukwa kwamba, Waziri mkuu Mizengo Pinda wa Tanzania na ujumbe wake walipotembelea Radio Vatican hivi karibuni alibainisha kwamba, Serikali ya Tanzania inatarajia tarehe 4 Aprili 2013 kukutana na viongozi wa kidini na wadau mbali mbali ili kwa pamoja kuweza kujadili mustakabali wa Tanzania kwa kuangalia amani na utulivu kama nyenzo muhimu katika ustawi na maendeleo ya Tanzania.

Friday, March 29, 2013

Hii ndiyo Aleluya kuu lazima


IBADA YA ALHAMISI KUU-POPE FRANCIS

Nimewapeni mfano, nanyi hudumianeni kwa ukarimu na upendo!



Baba Mtakatifu Francisko, Jioni ya Alhamisi kuu, tarehe 28 Machi 2013 ameadhimisha Ibada ya Karamu ya Mwisho, katika Gereza la Watoto la "Casal del Marmo," lililoko mjini Roma kwa kuwaosha miguu watoto kumi na wawili, kielelezo cha upendo wa Kristo unaomwilishwa katika huduma kwa jirani, lakini zaidi kwa wale wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Katika mahubiri yake kwa vijana hawa, amewashirikisha upendo ulioneshwa na Yesu Kristo, Siku ya Alhamisi kuu, alipoweka mavazi yake kando, akaanza kuwaosha mitume wake miguu, kitendo ambacho kilimshangaza Mtume Petro, kiasi cha kutaka kukataa katu katu kuoshwa miguu na Yesu, lakini akafafanuliwa maana yake, kiasi kwamba, akaweza hata kuridhika na uamuzi uliotolewa.

Yesu ambaye ni Mwalimu na Bwana, Nafsi ya Pili ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, ndiye aliyetekeleza kitendo hiki cha unyenyekevu, ambacho kilikuwa kinafanywa na watumwa! Akawaachia mfano wa kuigwa na kuendelezwa, kwa kutambua kwamba, uongozi ni huduma hasa kwa wanyonge na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Ni mwaliko wa kumegeana upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo, aliyewapenda watu wake upeo kiasi cha kuyamimina maisha yake pale juu Msalabani. Huduma ya upendo, iwachangamotishe waamini na watu wenye mapenzi mema kujikita katika msamaha na upatanisho unaopaswa kububujika kutoka katika undani wa mtu mwenyewe.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kama Padre na Askofu wa Roma, anajisikia kuwajibika kuwaonjesha huruma na upendo wa Kristo kwa njia ya huduma inayopata chimbuko lake kutoka katika moyo wake na wala si jambo la kutaka kujionesha mbele ya watu.

Kwa maneno machache, hii ni imani katika matendo, inayowachangamotisha waamini na watu wenye mapenzi mema, kusaidiana kwa hali na mali; wakiungana kwa pamoja kutafuta mafao ya wengi. Huduma ya upendo ni changamoto endelevu inayotolewa na Yesu aliyekuja kutumikia na kuyamimina maisha yake kwa ajili ya ukombozi wa wengi.

Thursday, March 21, 2013

KIPINDI CHA KWARESIMA

Bibilia na Kipindi cha Kwaresima

Katika Agano la Kale Musa ndiye aliyeongoza Waisraeli. Sisi tunakumbuka na kufuata safari yao ya ukombozi, walipokaa jangwani miaka 40 ili kuelimishwa kinaganaga juu ya yale yatokanayo na maneno 10 ambayo Musa alipewa na Mungu alipofunga siku 40 juu ya mlima Sinai.
Hayo yalikamilishwa na Yesu katika Agano Jipya kama kiongozi na mkombozi wa wote. Kabla hajaanza utume wake, yeye pia alifunga siku 40 jangwani akijilisha matakwa ya Baba ili ayatekeleze na kuwatangazia watu wote.

Juhudi za Kwaresima

Kufuatana na hayo yote Kanisa linafunga siku 40 katika jangwa la kiroho. Wakati wa Kwaresima linawaongoza waamini katika safari ya kujirekebisha kulingana na Neno la Mungu la Agano la Kale na la Agano Jipya. Wote wanahimizwa kufunga safari hiyo kadiri ya hali yao: kwanza wale wanaojiandaa kubatizwa usiku wa Pasaka (hasa kwa kufanyiwa mazinguo matatu yanayofuatana katika Dominika III, IV na V), lakini pia waliokwishabatizwa, ambao kabla ya hapo wanatakiwa kutubu na kuungama dhambi ili warudie kwa unyofu ahadi za ubatizo.
Makundi yote mawili watakula pamoja Mwanakondoo ili kuishi upya kwa upendo, jambo litakalofanya hata wasio Wakristo wafurahie Pasaka.
Kazi za urekebisho zinahitaji juhudi za pekee. Vivyo hivyo kwa ukombozi wa kiroho Kwaresima inadai bidii nyingi pande mbalimbali: katika kufunga, kutoa sadaka, kusali na kusikiliza Neno la Mungu hasa wakati wa ibada. Hayo yote yanahusiana na kusaidiana.
Mkristo akijinyima chakula cha mwili anajifunza kufurahia zaidi mkate wa Neno la Mungu na wa ekaristi, tena anatambua zaidi anavyopaswa kuwahurumia wenye njaa na shida mbalimbali. Toba inahimizwa isiwe ya ndani na ya binafsi tu, bali pia ya nje na ya kijamii: itokane na upendo na kulenga upendo kwa kurekebisha kasoro upande wa Mungu (sala), wa jirani (sadaka) na wa nafsi yetu (mfungo).
Mfungo, yaani kujinyima tunavyovipenda na hata tunavyovihitaji, uwe ishara ya njaa yetu ya Neno la Mungu, ya nia yetu ya kushiriki mateso ya Yesu yanayoendelea katika maskini, ya kulipa kwa dhambi zetu na kuachana nazo. Sadaka inayotokana na sisi kujinyima inampendeza Mungu kuliko ile isiyotuumiza; msaada unaweza kutolewa pia kwa kutetea haki za binadamu dhidi ya wanyanyasaji. Sala inastawi kwa kusikiliza sana Neno la Mungu hasa kwa pamoja (katika familia, jumuia, liturujia n.k.). Ndiyo maana wakati wa Kwaresima Kanisa linazidisha nafasi za kulitangaza na hivyo kuelimisha wote kuhusu mambo makuu ya imani na maadili yetu.

Kwaresima katika liturujia.

Kuna mpangilio kabambe wa masomo ya Misa, hasa ya Dominika, ili wote wafuate hatua kuu za historia ya wokovu (somo la kwanza) na kuchimba ukweli wa ubatizo (mwaka A), agano na fumbo la Kristo (mwaka B) na upatanisho (mwaka C). Kwa njia hiyo tunatangaziwa jinsi Mungu anavyotuokoa; pia upande wetu kuanzia Dominika ya kwanza tunajielewa kuwa watu vishawishini ambao tunapaswa kushinda kwa kumfuata Yesu, si Adamu: kwenda jangwani ili kumtafuta Bwana na matakwa yake.
Kilele cha safari ya Kwaresima ni Dominika ya Matawi, tunapoingia Yerusalemu pamoja na Yesu anayekwenda kufa na kufufuka kwa ajili yetu. Liturujia ya siku hiyo ina mambo mawili: kwanza shangwe (katika maandamano), halafu huzuni (kuanzia masomo, ambayo kilele chake ni Injili ya Mateso).
Baada ya Kwaresima kwisha, tutapitia tena historia ya wokovu katika kesha la Pasaka ambapo hatua zote zinaangazwa na ushindi wa Kristo mfufuka.

JUMA KUU LA PASAKA

Juma kuu


Juma kuu ni juma la mwaka ambalo Ukristo unaadhimisha kwa namna ya pekee matukio makuu ya historia ya wokovu, kuhusiana na mwisho wa maisha ya Yesu huko Yerusalemu, uliofuatwa na ufufuko wake.
Katika madhehebu mengi, juma hilo linaanza na Jumapili ya matawi ambapo linaadhimishwa kwa shangwe tukio la Yesu Kristo kuingia huo mji mtakatifu kama mfalme wa Wayahudi huku akipanda punda na kushangiliwa na umati wa wafuasi wake, waliofurahia hasa alivyomfufua Lazaro wa Betania.
Lakini Yesu alieleza kuwa ufalme wake si wa dunia hii, na kuwa yeye hakuja kutumikiwa bali kutumikia na kutoa uhai wake uwe fidia ya umati.
Hivyo siku zilizofuata alikabili kwa hiari mateso na kifo kutoka kwa wapinzani wake na kwa mamlaka ya Ponsio Pilato, na hatimaye akafufuka mtukufu usiku wa kuamkia Jumapili.
Kabla ya hapo Yesu alijumlisha hayo matukio yajayo katika karamu ya mwisho aliyokula pamoja na mitume wake 12, akiwaachia agizo la kufanya daima karamu ya namna hiyo kama ukumbusho wake.
Basi, kuanzia Alhamisi kuu jioni hadi Jumapili ya Pasaka jioni Wakristo wanaadhimisha siku tatu kuu za Pasaka, zinazofanya ukumbusho wa Yesu mteswa, mzikwa na mfufuka.

Wednesday, March 20, 2013

IBADA YA MATAWI

Katika mwaka wa Kanisa wa madhehebu mbalimbali ya Ukristo, Jumapili ya matawi inaadhimishwa jinsi Yesu Kristo alivyoingia Yerusalemu ili kufa na kufufuka kwa wokovu wa binadamu wote. Siku hiyo alishangiliwa na umati kwa kutumia matawi, ndiyo asili ya jina.
Ndiyo mwanzo wa Juma kuu linaloadhimisha matukio makuu ya historia ya wokovu kadiri ya imani ya Wakristo.
Tangu mwaka 1985 siku hiyo Kanisa Katoliki linaadhimisha pia "Siku ya kimataifa ya vijana"

Kulikuwa Jumapili ya Matawi hasubihi, na kijana wa familia moja alikuwa amepatwa na mafua, na hivyo hakuweza kwenda Kanisani pamoja na wana familia wengine. Aliachwa nyumbani. Basi wana familia waliporuri kutoka sherehe za Jumapili walifika nyumbani na matawi yao. Yule kijana akawauliza umaana wa matawi yale. Mama akamjibu, “Umati ulimshangia Yesu akipita kwa kuinua ya matawi juu. Basi yule kijana akajibu kwa mshangao, Jumapili ya pekee ambao sikuweza kwenda Kanisani, na Yesu anakuja binafsi!” Kwa sherehe za Jumapili hii ya Matawi, Kanisa huadhimisha ukubusho wa Bwana Yesu wakati aliingia Yerusalemu mahali atakapokamilisha fumbo la Pasaka, yaani, mateso, kufa na kufufuka kwake. Kwa maandamano ya matawi Jumapili hii, tunaanza rasmi Wiki Takatifu tukielekea Pasaka. Maandamano yenyewe humshangilia Yesu, ambaye hivi punde kwa kifo na ufufuko wake, atarudi kwenye utukufu wa Baba. Jumapili ya Matawi ina pande mbili, yaani pande moja ya furaha na nyingine ya mateso. Tunaona kwanza Yesu akiingia Yerusalemu kwa shangwe na furaha, na pia hivi punde atateswa. Yule anayeingia Yerusalemu kwa shangwe, ndiye pia atayehukumiwa na umati afe msalabani kwa ajili ya dhambi zetu. Hivyo Yesu ndiye mfano maalum wa kutuonyesha jinsi safari yetu ya imani itakapokuwa hapo mwisho, yaani kujinyenyekesha na kuteswa hadi kukubali kufa msalabani, ili Mungu atufufue siku ya mwisho.

Kwenye Injili juu ya Mateso ya Bwana iliyoandikwa na Mtk. Luka tunashirikishwa kwenye mchezo wa kuwiga juu wa ukombozi wetu, lakini mchezo wenyewe ni wa hali ya juu sana. Yesu ndiye anayechukua mahali pa katikati kwenye mchezo huu. Mtk. Luka anatuonyesha kwamba Yesu anateseka na kufa asipokuwa na kosa hata moja (Lk 23:4, 14-15, 22). Yesu anateswa na kuuawa na hadui zake ambao sio Warumi, lakini Mayahudi wenzake (Lk 22: 3,31,53). Maandishi ya Luka juu ya mateso na kufa kwa Yesu umaana wake hasa ni Habari Njema juu ya huruma na usamaho wa Mungu Baba. Hivyo Injili yenyewe ni kama mujiza wa vile Baba huendelea kuonyesha huruma wake kwa wote. Hivyo Yesu anaponya sikio la askari aliyekatwa na Petro; Yesu anamwangalia Petro kwa huruma wakati alimkana mara tatu; na Yesu anamuhurumia mwizi aliyekuwa amehukumiwa kufa msalabani. Kwenye mateso yake huko gethsemani, wakati alikuwa akichekelewa na umati na mateso yake yote msalabani, Yesu ni ishara ya Mungu baina ya watu wake; na pia kama chombo kinachoonyesha upendo na huruma wa Mungu. Kuna ujumbe gani tungepeleka nyumbani Jumapili hii? 1) Tunapotafakari juu ya mateso na kifo cha Bwana, tuyaone pia kwenye maelfu ya watu wetu barani Afrika wanaoteswa na kufa bila kosa lolote. Pia tukumbuke mateso yetu binafsi. 2) Kwenye mateso ya Yesu tunaonyeshwa kwamba Mungu katika upendo na huruma wake hawezi kutuacha peke. Pia tunagundua kwamba hapo mwisho, mateso yatageuzwa kuwa furaha, na kifo kuwa maisha mapya. 3) Tukumbuke kwamba ni kwa ajili ya dhambi zetu Yesu anahukumiwa kufa msalabani, na ni kwa ajili ya upenda na huruma wa Mungu tunapata maondoleo ya dhambi tukitubu na kuungama dhambi zetu.


 ABEL R. REGINALD.

Tuesday, March 19, 2013

PICTURE ZA HIJA YA VIJANA - BAGAMOYO 2013

 Vijana wakiwa kwenye njia ya msalaba wakielekea kituo cha mwisho ndani ya kanisa la Bagamoyo.



Viongozi wa Parokia ya Boko kutoka kulia ni Eppie Mwikola-Mhazin, Flora Magele-Mwenyekit Msaidizi, Abel Reginald-Mwenyekiti, Frida Meeda-Katibu na Timoth Jafethy-Katibu Msaidizi






NCHI YANGU FAHARI YANGU TOUR