Thursday, May 29, 2014

SHEREHE YA KUPAA BWANA MWAKA "A" masomo dominika 01/06/2014 jumapili



01
   JUNI 
 SHEREHE YA KUPAA BWANA MWAKA "A"


RATIBA ZA IBADA
KIGANGO CHA BOKO.
IBADA YA MISA YA KWANZA 12:15 – 1:45 ASUBUHI
IBADA YA MISA YA PILI 2:00 – 3:50 ASUBUHI
IBADA YA MISA YA TATU SAA 4:00-5:20 ASUBUHI
KIGANGO CHA MBWENI.
IBADA YA MISA YA KWANZA 1:15 – 2:55 ASUBUHI
IBADA YA MISA YA PILI 3:00 – 4:50 ASUBUHI
KIGANGO CHA MT. RAFAEL.
IBADA YA MISA YA KWANZA 1:00 – 2:55 ASUBUHI
IBADA YA MISA YA PILI 3:00 – 4:50 ASUBUHI
KIGANGO CHA ANTHONY WA PADUA – MBWENI TETA.
IBADA YA MISA NI 3:00 – 5:00ASUBUHI
ZAB:47:1-2,5-6,7-8
SOMO LA 1: Mdo. 1:1-11

Kitabu kile cha kwanza naliandika, Theofilo, katika habari ya mambo yote aliyoanza Yesu kufanya na kufundisha, hata siku ile alipochukuliwa juu, alipokuwa amekwisha kuwaagiza kwa Roho Mtakatifu wale Mitume aliowachagua; wale alowadhihirisha mafsi yake, kwa dalili nyingi, baada ya kuteswa kwake, ya kwamba yu hai, akiwatokea muda wa siku arobaini, na kuyanena mambo yaliyohusu ufalme wa Mungu. Hata alipokuwa amekutana nao aliwaagiza wasitoke Yerusalemu, bali waingoje ahadi ya Baba, ambayo mlisikia habari zake kwangu; ya kwamba Yohane alibatiza kwa maji, bali ninyi mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu baada ya siku hizi chache. basi walipokutanika , wakamuliza, wakisema, Je! Bwana, wakati huu ndipo unapowarudishia Israeli ufamle? Akawaambia, si kazi yenu kujua nyakati wala majira, Baba aliyoyaweka katika mamlaka yake mwenyewe. Lakini mtapokea nguvu, ikiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa Nchi. Akiisha kusema hayo, walipokuwa wakitazama, akainuliwa, wingu likampokea kutoka machoni pao. Walipokuwa wakikaza macho mbinguni, yeye alipokuwa akienda zake, tazama watu wawili wakasimama karibu nao, wenye nguo nyeupe, wakasema Enyi watu wa Galilaya, mbona mmesimama mkatazama mbinguni? Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda juu mbinguni, atakuja jinsi iyo hivyo mlivyomwona akienda zake mbinguni.

Somo 2:Efe.1:17-23

Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu awape ninyi Roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye; macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo; na ubora wa ukuu wa uweza wake ndani yetu tuaminio jinsi ulivyo; kwa kadiri ya utendaji wa nguvu za uweza wake; aliotenda katka kristo alipomfufua katika wafu, akamweka mkono wake wa kuume katika ulimwengu wa roho; juu sana kuliko ufamle wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajalwo, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia; akavitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote.

INJILI:Mt. 28:16-20

Wale wanafunzi kumi na moja walikwenda Galilaya mpaka mlima ule aliowaagiza Yesu. Nao walipomwona, walimsujudia; lakini baadhi yao waliona shaka. Yesu akaja kwao, akawaambia, nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi sikuzote, hata ukamilifu wa dahari.

Matangazo mbali mbali
Jumapili hii tarehe 01/06/14 kutakuwa na kikao cha vijana wote wanaoshiriki ziara ya uinjilishaji parokia za Dareda, Sanu, Daudu na endabashi, kikao kitafanyikia parokiani Saa 4:00 asubuhi mara baada ya ibada ya pili.
zaidi......

jdhibitisha ushiriki wako kwenye ziara ya Dareda 01-07/07/14 kwa kulipa ada ya ushiriki sasa ni tshng 150000 lipa kwa mhazini wako jumuiya, kigango au parokia.....tunawatakia maandalizi mema.

Monday, May 26, 2014

Ziara ya Baba Mtakatifu Francisco Israel

Hotuba ya Papa kwa Mufti Mkuu wa Jeresalemu


Jumatatu Baba Mtakatifu Francisiko, aliifungua ratiba yake ya Hija katika nchi Takatifu kwa kukutana na Mufti Mkuu wa Jeresalem , katika Msikiti Mkuu wa Jerusalem.

Na katika nyayo za watangulizi wake, na hasa katika mwanga wa Paul VI , aliyefanya hija hii miaka hamsini iliyopita, na hivyo kuwa Papa wa kwanza kutembelea Nchi Takatifu ,pia alitamani sana kufanya hija hii ya kutembelea maeneo ambayo yamemshuhudia Yesu akiyaishi maisha haya ya kidunia. Na kwamba hija yake isingekuwa kamili bila ya kukutana na kutafakari pamoja na watu wanao ishi katika nchi hii. Na hivyo kwa heshima na taadhima ameweza kukutana na Mufti Mkuu wa Jerusalem , na Waislamu wengine , wake kwa waume.

Hotuba ya Papa ilielekeza mawazo kwa Ibrahimu , ambaye aliishi kama Mhujaji wa imani katika nchi hiI ambayo Waislamu, Wakristo na Wayahudi wanamtabua Ibrahimu kuwa Baba yao wa Imani, ingawa kila mmoja, humwabudu Mungu Mmoja katika njia tofaut. Ibarahim ni mfano mkubwa sana wa jinsi ya kumfuata Mungu kwa imani kuu.

Papa amewatia moyo waamini wote kwamba, katika Hija hii ya kidunia, hatuko peke yetu. Kwa Wakristo, kwa njia ya msalaba, huungana na waamini wa dini nyingine , kushiriki na kutembea pamoja na hata kuishi pamoja kama sehemu njia ya kutimiza mapenzi ya Mungu. Papa alitoa shukurani zake za dhati kwa wote walio wezesha mkutano huo na kwa ukarimu wao ulioonyesha kwamba , hija ya maisha, ni yetu sote binadamu . .
Papa aliomba uwepo wa mawasiliano ya kidugu na kubadilishana mawazo , kama hatua yenye kutoa mwanya wa chaguzi na nguvu mpya, katika kukabiliana na changamoto katika maisha ya kawaida, na wao kama viongozi waweze kuwa msitari wa mbele likabiliana na changamoto kwanza.

Alisema, hawawezi kusahau ,ukweli kwamba Hija ya Ibrahimu, pia ilikuwa ni wito kwa uadilifu : Mungu alimtaka aishuhudie imani yake kimatendo. Na hivyo , pia wao, kama viongozi, wangependa kuwa mashahidi wa utendaji wa Mungu katika dunia yetu. Aliomba kukutana kwao kutia shime vuguvugu la ndani la kusambaza wito huu na katika kuwa mawakala wa amani na haki” . Papa aliwasihi katika zawadi ya sala pia kujifunza kuwa na huruma kuu, kumheshimu kila mmoja na kupendana kama kaka na dada ! Pia kujifunza kuelewa maumivu mwingine !
Na jina la Mungu lisitumiwe kama chombo cha kuhalisha vurugu na maonevu, balijina hilo liwe kichocheo cha utendaji wa pamoja kwa ajili ya kujenga haki na amani!
Aidha Baba Mtakatifu , majira ya asubuhi, alikutana na Rabbi Wakuu wawili wa Israel, na pia alitembelea Makao makuu ya Rais wa Israel.
Baba Mtakatifu majira ya jioni kabla ya kuongoza Ibada ya Misa itakayokamilisha Hija yake katika nchi Takatifu , anakutana na Mapadre watawa na waseminaristi katika Kanisa la Getsemani.

Tuesday, May 6, 2014

Dominika ya 4 ya pasaka mwaka “A”. tarehe 11/05/2014

JUMAPILI DOMINIKA YA 4 ya Pasaka ya Mwaka A.
      RATIBA ZA IBADA 
KIGANGO CHA MH. ISIDORI BAKANJA- BOKO.
MISA YA KWANZA 12:15-2:00 ASUBUHI
MISA YA PILI     SAA 2:00-4:00 ASUBUHI
MISA YA TATU SAA 4:00-5:30 ASUBUHI
KIGANGO CHA MT. FRANCIS WA ASIZ-MBWENI 
MISA YA KWANZA SAA 1:10-3:00 ASUBUHI
MISA YA PILI SAA 3:00-4:30 ASUBUHI

KIGANGO CHA MT. RAFAEL-MBWENI MALINDI
SAA 1:00-3:00 ASUBUHI.
MISA YA PILI SAA 3:00-5:00

KIGANGO CHA ANTHONY WA PADUA-MBWENI TETA
MISA NI SAA 3:00-5:00.


SOMO 1. Mdo.2:14a, 36 – 41
Siku ya Pentekoste Petro akasimama pamoja na wale kumi na mmoja, akapaza sauti yake, akawaambia, basi nyumba yote ya Israel na wajue yakini ya kwamba Mungu amemfanya Yesu huyo mliyemsulubisha kuwa Bwana na Kristo. Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na Mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu? Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie. Akawashuhudia kwa maneno mengine mengi sana na kuwaonya, akisema, jiokoeni na kizazi hiki chenye ukaidi. Nao waliolipokea neon lake wakabatizwa; na siku ile wakaongezeka wata wapata elfu tatu.


WIMBO WA KATIKATI; Zab. 23:1-6

(Kitikio)
Bwana ndiye mchungaji wangu sitopungukiwa na kitu au Aleluya


SOMO 2: 1Pet. 2:20b – 25
Kustahimili, mtendapo mema na kupata mateso, huu ndiyo wema hasa mbele za Mungu. Kwa sababu ndio mlioitiwa; maana Kristo naye aliteswa kwa ajili yenu, akawaachia kielelezo, mfuate nyanyo zake. Yeye hakutenda dhambi, wala hila haikuonekana kinywani mwake. Yeye alipotukanwa, hakurudisha matukano; alipoteswa, hakuogopa; bali alijikabidhi kwake yeye ahukumuye kwa haki. Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu yam ti; ili, tukiwa wafu kwa mambo ya dhambi, tuwe hai kwa mambo ya haki; na kupigwa kwake mliponywa. Kwa maana mlikuwa mnapotea kama kondoo; lakini sasa mmemrudia Mchungaji na Mwangalizi
wa roho zenu.



 SHANGILIO. Yn. 10:14
Mimi ndimi mchungaji mwema; nao walio wangu nawajua; nao walio wangu wanijua mimi
Aleluya


INJILI.:Yn. 10:1-10
Yesu aliwaambia Wayahudi, Amin, amin, nawaambieni, Yeye asiyeingia mlangoni katika zizi la kondoo, lakini akwea penginepo, huyo ni mwizi naye ni mnyang’anyi. Aingiaye mlangoni ni mchungaji wa kondoo. Bawabu humfungilia huyo, na kondoo humsikia sauti yake; naye huwaita kondoo wake kwa majina yao, na huwapeleka nje. Naye awatoapo nje kondoo wake wote, huwatangulia; na wale kondoo humfuata, kwa maana waijua sauti yake. Mgeni hawatamfuata kabisa, bali watamkimbia; kwa maana hawazijui sauti za wageni. Mithali hiyo Yesu aliwaambia; lakini wao hawakuelewa na mambo hayo aliyowaambia. Basi Yesu aliwaambia tena, Amin, amin, nawaambieni, Mimi ndimi mlango wa kondoo. Wote walionitangulia ni wevi na wanyang’anyi; lakini kondoo hawakuwasikia. Mimi ndimi mlango; mtu akiingia kwa mimi, ataokoka; ataingia na kutoka, naye atapata malisho. Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kasha wawe nao tele.


Mdo - kitabu cha Matendo ya Mitume
1Pet - kitabu cha waraka wa kwanza  wa mtu Petro kwa watu wote
Yn -  kitabu cha muinjili Yohana.

Na Abel Reginald……………….niwatikieni maandalizi mema ya Dominika


usikose kuhudhuria kwenye kikao cha Halmashauri ya VIWAWA Parokia ya Boko mara baada ya Misa ya kwanza Kigangoni Rafael 

Tuesday, April 29, 2014

MASOMO YA JUMAPILI DOMINIKA YA 3 YA MWAKA A TAREHE 04/05/2014

JUMAPILI DOMINIKA YA 3 ya Pasaka ya Mwaka A.
      RATIBA ZA IBADA 
KIGANGO CHA MH. ISIDORI BAKANJA- BOKO.
MISA YA KWANZA 12:15-2:00 ASUBUHI
MISA YA PILI     SAA 2:00-4:00 ASUBUHI
MISA YA TATU SAA 4:00-5:30 ASUBUHI
KIGANGO CHA MT. FRANCIS WA ASIZ-MBWENI 
MISA YA KWANZA SAA 1:10-3:00 ASUBUHI
MISA YA PILI SAA 3:00-4:30 ASUBUHI

KIGANGO CHA MT. RAFAEL-MBWENI MALINDI
SAA 1:00-3:00 ASUBUHI.
MISA YA PILI SAA 3:00-5:00

KIGANGO CHA ANTHONY WA PADUA-MBWENI TETA
MISA NI SAA 3:00-5:00.


MASOMO 

SOMO 1:Mdo.2:14,22-28
Petro alisimama pamoja na wale kumi na moja,akapaza sauti yake, akawaambia, enyi watu wa Uyahudi, ninyi nyote mkaao Yerusalemu, lijueni jambo hili, mkasikilize maneno yangu, Yesu wa Nazareti, mtu aliyedhihirishwa kwenu na Mungu kwa miujuza na ajabu na ishara, ambazo Mungu alizifanya kwa mkono wake kati yenu, kama ninyi wenyewe mnavyojua; mtu huyu aliotolewa kwa shauri la Mungu lilikusudiwa, na kwa kujua kwake tangu zamani, ninyi mkamsulubisha kwa mikono ya watu wabaya, mkamwua; ambaye Mungu alimfufua, akaufungua uchungu wa mauti, kwa sababu haikuwezekana ashikwe nao. Maana Daudi ataja habari zake. Nalimwona Bwana mbele yangu siku zote, kwa kuwa yuko upande wa mkono wangu wa kuume, nisitikisike. Kwa hiyo moyo wangu ukapendezewa, ulimi wangu ukafurai; tena mwili wangu nao utakaa katika matumaini. Kwa maana hutaiacha roho yangu katika kuzimu; wala hutamtoa mtakatifu wako aone uharibifu. Umenijulisha njia za uzima; utanijaza furaha kwa uso wako.

SOMO 2: 1Pet. 1:17-21
Ikiwa unamwita Baba, yeye ahukumuye kila mtu asipo upendeleo, kwa kadri ya kazi yake, enendeni kwa hofu katika wakati wenu wa kukaa hapa kama wageni. Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhambi; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa Baba zenu; bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo. Naye amejulikana kweli tangu zamani, kabla haijawekwa misingi ya dunia; lakini alifunuliwa mwisho wa zamani kwa ajili yenu; ambao kwa yeye mmekuwa wenye kumwamini Mungu, aliyemfufua katika wafu akampa utukufu; hata Imani yenu na tumaini lenu liwe kwa Mungu.

INJILI. :Lk. 24:13-35
Siku ile watu wawili miongoni mwa wafuasi wa Yesu walikuwa wakienda kijiji kimoja, jina lake Emau, kilichokuwa mbali na Yerusalemu kama mwendo wa saa mbili. Nao walikuwa wakizungumza wao kwa wao habari za mambo hayo yote yaliyotokea. Ikawa katika kuzungumza na kuulizana kwao Yesu mwenyewe alikaribia, akaandamana nao. Macho yao yakafumbwa wasimtambue. Akawaambia, ni maneno gani haya tangu yalipotendeka mambo haya; tena wanawake kadha wa kadha wa kwetu walitushitusha, walivyokwenda kaburini asubuhi na mapema, wasiuone mwili wake; wakaja wakasema ya kwamba wametokewa na malaika waliosema kwamba yu hai. Na wengine walikuwa pamoja nasi walikwenda kaburini wakaona vivyo hivyo kama wale wanawake walivyosema, ila yeye hawakumwona. Akawaambia, enyi msiofahamu, wenye mioyo mizito ya kuamini yote waliyoyasema manabii! Je! Haikupasa Kristo kupata mateso haya na kuingia katika utukufu wake? Akaanza kutoka Musa na manabii wote, akawaeleza katika maandiko yote mambo yaliyomhusu yeye mwenyewe. Wakakaribia kile kijiji walichokuwa wakienda, naye alifanya kama anataka kwendelea mbele. Wakamshawishi wakisema, kaa pamoja nasi, kwa kuwa kumekuchwa, na mchana unakwisha. Akaingia ndani kukao nao. Ikawa alipokuwa ameketi nao chakulani, alitwaa mkate, akaubariki, akaumega,akawapa.yakafumbuliwa macho yao, wakamtambua; kasha akatoweka mbele yao. Wakaambiana, je! Mioyo yetu haikuwaka ndani yetu hapo alipokuwa akisema nasi njiani, kutufunulia maandiko? Wakaondoka saa ile ile, wakarejea Yerusalemu,wakawakuta wale kumi na moja wamekutanika, wao na wale waliokuwa pamoja nao, wakisema, Bwana amefufuka kweli kweli, naye amemtokea Simoni. Nao waliwapa habari ya mambo yale ya njiani, na jinsi alivyojitambulisha nao katika kuumega mkate.


  1.  form za ziara ya uinjilishaji parokia ya Dareda na ziara ya mbuga ya wanyama ya ngorongoro zipo tayari na nafasi zimebaki chache wahi sasa nafasi ikiwa kama kijana mkatoliki askari kamili wa Yesu,...twende tuungane pamoja katika kumtangaza yeye aliye njia ya uzima na ukweli mchango na tshs 180,000 tu na mwisho wa kupokea michango ni tarehe 18/06/2014.
  2. tunawakumbusha vijana wote kuendelea kulipa ada kwa maendeleo ya chama chetu..... mapendo sana malipo kwa njia ya benk kwa jina na number hii :viwawa parokia ya boko account no 01524526820100 crdb bank tegeta branch
JIANDAE NA ZIARA YA UINJILISHAJI MWAKA 2014.....................

Tuesday, March 25, 2014

Ujumbe wa Kwaresima Mwaka 2014 Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania




kwa wasomaji wa Blog yetu tunawaletea ujumbe wa Kwaresima kwa Mwaka 2014 kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania unaoongozwa na kauli mbiu "Ukweli utawaweka huru. Yn. 8:32". Maaskofu wanazungumzia kuhusu umuhimu wa wongofu wa kweli unaomweka mwamini huru; wajibu wa kuuishi, kuulinda na kuusimamia ukweli kishuhuda mintarafu hali halisi ya Tanzania.

UTANGULIZI

Wapendwa Taifa la Mungu,


“Ukweli utawaweka huru”. Safari ya maisha ya mwanadamu ni safari ya kutafuta uhuru, uhuru ambao unamfungua mtu kutoka katika minyororo inayomfunga na kumfanya kuwa mhudumu wa mazingira na hali yake. Chimbuko la uhuru wa kweli ni Mungu mwenyewe katika mpango wake wa milele na huruma yake ya milele. Mungu ndiye asili na chanzo cha uhuru wa kweli na tunafanywa kuwa huru kweli pale tunapoamua kwa dhati kuupokea ukweli utokao kwa Mungu. Mungu ndiye ukweli wenyewe: “Ukweli wowote, bila kujali anayeusema, unatoka kwa Roho Mtakatifu”, na popote tunapoukuta ukweli huo ni mali ya Mungu.


Wapendwa Taifa la Mungu, tunapoanza safari ya Kwaresima ya mwaka huu, sisi Maaskofu wenu, tungependa kuwakumbusheni ninyi na watu wote wenye mapenzi mema juu ya umuhimu wa kuishi katika ukweli. Kuuishi ukweli na kuishi maisha yaliyojengwa juu ya msingi wa ukweli ni kushiriki hasa maisha ya Mungu. Kama tunataka kujenga jamii yenye utu, haki, amani, upendo na mshikamano wa kweli, ni lazima tuanze kwanza kujenga dhamiri zinazothamini na kuuenzi ukweli. Pasipo ukweli jamii itasambaratika kwa sababu itakuwa imejengwa bila msingi.


Wapendwa Taifa la Mungu, Ukweli utawapeni uhuru kwa kuwa toka kuumbwa kwa ulimwengu, Mungu aliye ukweli wenyewe alipanga na kunuia kwamba mwanadamu aliyemuumba kwa sura na mfano wake, aishi katika uhuru kamili akimiliki na kuutiisha ulimwengu wote (Mwa 1:28 ). Ni katika ukweli tunamjua, tunampenda na kumtumikia Mungu. Ni katika ukweli tunadhihirisha kuwa tumeitwa kuwa wana huru katika ufalme wa Baba wa milele.


Ukweli na uhuru ni dhana zinazoenda pamoja. Penye ukweli pana uhuru na penye uhuru pana ukweli. Kama vile mtu huru awezavyo kuuishi ukweli kwa kuwa uhuru wake humfanya ajitegemee kifikra, kimaamuzi na kiutendaji ndivyo pia jamii ya watu na hata taifa huru liwezavyo kujitegemea kifikra, kimaamuzi na kiutendaji.


Kwa maisha, kifo na ufufuko wa Kristo, waamini wamewekwa huru na wanaitwa kuutafuta na kuusimamia ukweli. Waamini wanaalikwa kuutafuta, kuujua na kuulinda ukweli katika nyanja zote za maisha.


SURA YA KWANZA
WONGOFU WA KWELI HUTUWEKA HURU


Mungu alipenda kujifunua kwa wanadamu kupitia manabii na mwanawe wa pekee Bwana wetu Yesu Kristo. Hata leo, Roho Mtakatifu analiongoza Kanisa katika kuendelea kuujua ukweli wa kiimani katika safari ya pamoja ya kiroho kuelekea uhuru kamili wa roho zetu. Ukweli wa kiimani huleta uhuru wa kiroho. Mwaka uliopita Kanisa liliadhimisha Mwaka wa Imani ikiwa ni sehemu ya kuwakumbusha wanakanisa wote juu ya wajibu wao wa kiimani katika Kanisa na katika jamii.

Kwa kuishi ipasavyo imani yetu ya kikristo tunashiriki wajibu wa kuujenga Ufalme wa Mungu ambao mojawapo ya nguzo zake saba za msingi ni ukweli! Hakika, ufalme wa Mungu, kama Mama Kanisa anavyotangaza katika utangulizi wa Misa ya sherehe ya Kristo Mfalme ni ufalme wa UZIMA na KWELI, ufalme wa NEEMA na UTAKATIFU, ufalme wa HAKI, MAPENDO na AMANI. Mungu wetu ni UKWELI na ni MKWELI. Tunasadiki na kukiri kwamba hadaganyi wala hadanganyiki. Imani ni wajibu wa kushiriki kuujenga Ufalme wa Mungu, ufalme ambao msingi wake ni ukweli, kwa sababu Mungu ni ukweli.

Mwanadamu aliyekombolewa kwa damu ya thamani kubwa sana ya Kristo iliyomwagika pale Kalvari, amepata kurudishiwa hadhi ya kuwa mwana huru wa Mungu akikombolewa kutoka utumwa wa dhambi. Uhuru anaoupata mwanadamu una gharama kubwa na thamani kubwa. Uhuru wa kweli ni uhuru ndani ya Mungu; ni uhuru katika Mungu. Uhuru wa kweli huambatana na utii wa sheria ya Mungu na uwajibikaji unaodai unyenyekevu na nidhamu ya hali ya juu. Uhuru huu ni kinyume na uhuru usio na mipaka ambao jamii ya sasa inadai,uhuru ambao hupingana na malengo ya Muumba na taratibu na miongozo halali mbele za Mungu iliyowekwa na jamii.
Kanisa, ukweli na uhuru

Kanisa ambalo ni ishara ya wokovu na alama ya uwepo hai wa Kristo aliye njia, ukweli na uzima katika ulimwengu wa sasa ni sisi tulioalikwa kuwa Familia ya Mungu. Kwa kumkiri Kristo na kwa kubatizwa kwetu tumekuwa Rafiki na wadau wake Yesu Kristo (Yn 15: 14). Kwa namna hiyo sisi sote Familia ya Mungu – Wakleri, Watawa na Waumini Walei – tu chombo mikononi mwa Kristo kwa kushiriki kikamilifu kazi ya Kristo ya kuwakomboa watu.

Kwa mantiki hiyo, Kanisa linao wajibu wa kwanza kabisa kuulinda ukweli, kuusimamia, kuushi na kuutangaza. Kanisa ni chombo kiletacho wokovu kwa ulimwengu na kuwaweka huru wanadamu walio katika utumwa unaojidhihirisha katika sura mbalimbali kama vile, umasikini, ufisadi, rushwa, ushirikina, magonjwa, siasa chafu, kutokuwajibika, ubinafsi,nk.

Kanisa ni chombo cha Kristo cha kuwaletea watu uhuru wa kweli. Roho wa Bwana, aliye juu ya Yesu (Lk 4:18,19) yuko pia juu ya Kanisa lake ambalo analituma kuwafungulia watu vifungo vyao mbalimbali na kuwaachia huru waliosetwa (Lk 4:18-19).

Ukweli kama tunu ya kimungu lazima uote mizizi katika mioyo ya wanadamu walioumbwa kwa sura na mfano wake (Kut 1:26). Ni wajibu wa kila mwanadamu kuutafuta ukweli na kuujua. Kwa njia ya ufahamu, mwanadamu anaalikwa kuutafuta ukweli kwani ndio njia pekee ya kumweka huru na kuufikia wokovu. Maana Mungu amemwachia mwanadamu uhuru kusudi aifuate nia yake (YBS 14:15), na hivyo amtafute Muumba wake kwa hiari, na hatimaye aufikie ukamilifu ulio bora na wenye heri, pasipo shuruti na kwa kuambatana na Mungu. Kanisa linamsaidia mwandamu kufanikisha kuufikia ukweli na kwa uhuru kupitia neema za Mungu.



SURA YA PILI
WAJIBU WA KUUISHI, KUULINDA NA KUUSIMAMIA UKWELI KISHUHUDA

Waamini waliowekwa huru na Kristo, wanao wajibu wa kuujua ukweli, kuutafuta, kuulinda na kuusimamia kwa lengo la kuleta huru wa kweli kwa manufaa ya wote. Huko ndiko kuwa mfuasi wa Kristo aliyesema: “Mimi nilikuja ulimwenguni; ili niishuhudie kweli. Kila aliye wa hiyo kweli hunisikia sauti yangu” (Yn 18:38).

Jamii leo hii imegawanyika juu ya uhuru ambao wanajamii wanapaswa kuwa nao. Wazazi wanaamini kuwa uhuru ni kutenda jambo lolote bila kubughudhiwa na yeyote, hata kama tendo hilo ni kinyume na misingi ya maadili. Watoto wanataka uhuru binafsi katika kupanga na kuamua mambo yanayowahusu. Watoto wasingependa kupokea malezi na maelekezo iwe ni ya wazazi au ya jamii. Vijana wanapenda kuamua mambo yao kama wanavyoona, wakipuuzia uzoefu na ushauri wa wakubwa wao. Tujiulize: Je, huu ndiyo uhuru tuutafutao? Katika mazingira kama haya kinachotafutwa si uhuru bali kuishi kwa kuheshimu vionjo binafsi. Ni muhimu sana kwa wanafamilia kuwa na uhuru wa pamoja katika kupanga na kuamua masuala kifamilia.

Tukijiruhusu kama wanajamii kuishi katika uholela upendo unatoweka. “Usikubali kitu chochote kuwa ni ukweli kama kinakosa upendo. Na usikubali kitu chochote kuwa ni upendo kama kinakosa ukweli! Hali moja bila nyingine ni uongo unaoharibu”. Kwa sababu “ni katika ukweli tu ndipo upendo inang’aa, ni katika ukweli tu ndipo tunapoweza kuuishi upendo kwa hakika”.
SURA YA TATU
HALI HALISI YA TAIFA LETU


Taifa lenye umri wa miaka 50 ya uhuru ni taifa lililokwishavuka uchanga. Ni taifa kijana lililo katika umri wa kujenga juu ya misingi iliyowekwa kwa manufaa ya wote. Ni taifa linalojitegemea. Bila msingi huo, mengine yote, hata kama yanaonekana yanang’aa yatakuwa yanasaliti mustakabali wa kweli wa taifa letu. Tusijidanganye. Bila msingi wa kujitegemea na kutafuta manufaa ya wote (common good) taifa hili litaanguka. Kama halianguki leo, kesho ni lazima litaanguka. Tunajiuliza, uko wapi ujasiri wa Taifa letu? Imepotelea wapi fahari ya kujitawala, si kisiasa tu, bali kiuchumi, kifikira na kijamii? Imepotelea wapi ile mbegu ya uzalendo iliyopandwa na waasisi wa taifa letu? Imeishia wapi heshima ya kuthamini utu, kuheshimu imani ya asiyeamini kile nisichokiamini na kutafuta ufumbuzi halisi wa matatizo yanayotukabili?


Tumepoteza dira ya kujitegemea kimaamuzi na kimkakati. Tumefikia mahali pa kuamini kwamba maendeleo yataletwa kwa kaulimbiu zinazobadilika badilika kila siku. Katika mazingira ya sasa, watu wachache, kwa sababu binafsi na kwa manufaa binafsi wanapotosha ukweli na kutafuta njia za kulinda maslahi yao kwa kutumia mifumo isiyokubalika, lakini inayosimikwa na kuhalalishwa ili kulinda maslahi binafsi. Hali hii inajidhihirisha kupitia matumizi mabaya ya madaraka, mikataba mibovu, kupindisha sheria, kufumbia macho uhalifu, nk. Uhuru wa kweli haujengeki katika misingi dhaifu ya ubinafsi na haulengi kumfanya mtu yeyote yule awe juu ya sheria za haki na taratibu za uadilifu. Na kimsingi, hakuna maendeleo ya kweli kama watu hawaheshimu haki ya msingi ya kuujua ukweli na kuishi kadiri ya ukweli huo.

Katika mazingira kama haya Kanisa haliwezi kukaa pembeni na kutazama tu kwa sababu nalo lina wajibu wa kuijenga jamii. Kanisa lina wajibu wa kuangalia, kuboresha na kuikosoa mienendo ya kijamii na kisiasa inayohatarisha ustawi wa jamii nzima na hivyo kuathiri kazi ya Kristo ya kumkomboa mwanadamu na kuusimika Ufalme wa Mungu; ufalme unaojidhihirisha katika kutamalaki kwa ukweli, haki na amani. Kanisa litaendelea kusisitiza ukweli huu kwamba; “Ili kuunda maisha ya kisiasa yaliyo kweli ya kibinadamu, hakuna lililo bora zaidi kuliko kustawisha ndani ya watu hisia za haki, upendo na huduma kwa manufaa ya wote”. Hapa tungependa kuelezea mambo machache yanayoivuruga nchi yetu.
Uvunjifu wa amani

Taifa letu linazidi kupoteza tunu bora ya amani ambayo waasisi wa taifa letu wametuachia. Katika siku za karibuni yamekuwepo matukio ya mauaji, watu kumwagiwa tindikali kwa sababu ya imani yao au visasi na hata mauaji kwa kutumia mabomu. Uhasama wa kidini na matukio ya kijasusi na ugaidi dhidi ya raia yanaonekana kushamiri. Kumekuwapo na matumizi makubwa ya nguvu upande wa vyombo vya dola vikitumia silaha za moto na za kivita. Wimbi la wananchi kutotii sheria na taratibu za nchi linakua. Tunakwenda wapi?

Amani lazima ilindwe ndani na nje ya mipaka ya nchi yetu. Hata hivyo, amani sio tunu inayojitegemea peke yake kwa kuwa amani ya kweli inazaliwa ndani ya mioyo yenye kujali misingi ya utu, haki, heshima, ukweli na umoja. Fikra tofauti na hizo, huzaa mioyo potofu, na mioyo potofu haiwezi kutoa amani.
Rushwa na madawa ya kulevya

Mapambano dhidi ya rushwa na madawa ya kulevya yamegeuka kuwa wimbo unaochosha kwa sababu hakuna dhamira ya dhati ya kuitokomeza. Uongozi wa juu unapotamka hadharani kuwafahamu watoa rushwa, wapokea rushwa na wafanyabiashara wa madawa ya kulevya lakini hakuna hatua zozote zinazochukuliwa ni hali inayotisha sana. Wakati umefika ambapo lazima tuwe wakweli kuhusu mapambano dhidi ya rushwa na madawa ya kulevya. Hatuwezi kuwa huru kuhusu rushwa na madawa ya kulevya kama hatujawa wakweli kuhusu mapambano dhidi ya rushwa na madawa ya kulevya. Wanaopiga vita rushwa majukwaani, ndio wanaoomba na kupokea nje ya jukwaa. Isitoshe rushwa ndiyo ngazi waliyoitumia na wanayoitumia kufika jukwaani. Katika mazingira kama haya hatujengi Taifa bali tunalibomoa na historia itatuhukumu. Hatuna budi kuunda misingi imara ya utawala bora. Tukumbuke daima kuwa utawala bora bila uwajibikaji na kuwajibishana ni kiini macho.
Kukua kwa matabaka katika jamii

Tofauti kubwa sana za kiuchumi zinazidi kupanua utengano wa kimatabaka kati ya wenye nguvu za kiuchumi na wasio na kitu. Wenye nguvu kiuchumi sasa wanamiliki uchumi, wanamiliki siasa na hatima ya fukara, na kwa fedha wananunua haki ya wanyonge.


Mgawanyo mbovu wa rasilimali za nchi unatisha. Ardhi inamilikiwa na wachache kwa kivuli cha uwekezaji mkubwa huku wananchi wakiahidiwa ajira kwa kuwa vibarua kwenye mashamba hayo badala ya kuwezeshwa kumiliki ardhi na kuitumia kwa faida. Haya ni masuala yanayomtia hofu mtu yeyote anayejali na kuthamini mustakabali wa taifa letu.
Siasa kuingilia weledi

Tatizo la siasa kutawala mifumo ya ujenzi wa misingi ya maendeleo linakua kwa kiwango cha kutia hofu. Kwa mfano, siasa na wanasiasa wanaathiri mfumo wa utoaji wa elimu nchini kiasi cha kulifanya taifa hili kuwa kama taifa lisilojali mustakabali wake. Yamekuwepo maneno mengi na mipango ya zimamoto isiyofanyiwa utafiti wa kina na utendaji umekuwa hafifu sana. Uthabiti katika kusimamia utekelezaji wa mipango ya maendeleo hauonekani na badala yake porojo zimetawala. Imejitokeza hali ya wale waliopewa dhamana ya kusimamia masuala ya elimu kwa mfano kukosa unyenyekevu wa kuwasikiliza na kushauriana na wataalamu katika nyanja hizi. Kila mara zinaibuka sera ambazo msingi wake ni ubunifu usiozingatia weledi na hivi kuifanya elimu kudidimia.
Mchakato wa Katiba mpya

Katiba kama moyo wa taifa ni chombo kinachopaswa kutengeneza misingi ya mfumo wa maisha mazima na uhai wa Taifa letu. Ukweli wote na uhuru wote wa Taifa unabebwa na Katiba. Iwapo mchakato wa katiba mpya hautaendeshwa kwa ukweli na uhuru, hatutaweza kupata katiba yenye kubeba ukweli na uhuru wote kuhusu taifa letu. Tunarudia tena kutamka kuwa zoezi hili adhimu na la muhimu kwa mustakabali wa Taifa limeharakishwa mno. Sasa tunaona zoezi zima limehodhiwa na wanasiasa. Mchakato wa katiba mpya unadai kuwepo kwa fadhila ya kijamii ya kutafuta manufaa ya wote (common good). Katiba si mali ya wanasiasa bali ni mali ya wananchi. Tunapenda kuialika jamii yote kuitendea haki nchi yetu. Tukae chini na tuzipime kila hatua zetu katika zoezi hili na tuone kama zinakidhi kipimo cha «Hekima, Umoja na Amani». Hekima ituongoze kulinda umoja wa Taifa letu na utuepushe na kishawishi cha kubaguana na kutengana. Kwa kuzingatia hilo umoja huo utatuongoza katika njia ya amani.

Uharibifu wa mazingira

Tishio kubwa la kimaangamizi kwa vizazi vijavyo linatokana na ukweli kuwa kumekuwepo na uharibifu mkubwa wa mazingira. Maendeleo yanagharama yake. Kiu ya kweli ya maendeleo ni lazima iambatane na ulazima wa kuwa makini katika kutunza mazingira na uthabiti wa uumbaji. Vyanzo vya maji na kingo za mito zimeharibiwa kwa kuruhusu shughuli za kilimo kufanyikia maeneo hayo, kwa kuruhusu makazi ya watu, viwanda kujengwa na kuruhusu takataka ya sumu kutoka viwandani na migodini kutiririkia kwenye vyanzo vya maji, nk. Ukataji wa miti umeshamiri na baadhi ya misitu ya asili imepotea. Kwa sababu hiyo tumechangia sana katika kusababisha mabadiliko ya tabia nchi ambayo athari zake sasa zinajionesha waziwazi. Ukame, njaa, mafarakano kati ya wakulima na wafugaji na kuenea kwa jangwa ni vitisho vilivyo dhahiri mbele yetu. Huu ni ukweli kuwa tumeshindwa kuzingatia agizo la Mungu la kuitawala na dunia kuutiisha ulimwengu. Tunahitaji sasa kubadilika ili ukweli utawale, tupate uhuru kamili kwa kuwajibika kuyalinda na kuyatunza mazingira kwa faida ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.
Ni wajibu wetu Waamini Wakatoliki kuulinda ukweli na kuusimamia kiushuhuda. Jitahada za namna hii zina gharama yake kwa kuwa zinahitaji ujasiri wa kinabii na utayari wa kuteseka na hata ikibidi kutoa sadaka kubwa ya uhai.
HITIMISHO

Wapendwa Taifa la Mungu, tunapenda kuwahimiza kwa maneno haya tukisema: “Inunue kweli, wala usiiuze. Naam, hekima na mafundisho na ufahamu” (Mith 23:23). Ukweli ni msingi wa lazima na unapaswa kuwa wa kudumu kwa tendo lolote ili liweze kuitwa kuwa ni adilifu. Ukweli unapaswa kuzijenga dhamiri zetu ili kumsaidia mwanadamu kupata mwanga unaofukuza mikanganyiko.


Katika ulimwengu usiojali ukweli, uhuru unapoteza msingi wake na mwanadamu anakuwa mhanga wa vurugu ya vionjo na kutawaliwa kwa hila, iliyojidhihirisha waziwazi au iliyojificha. Hivi ni mwaliko kwetu sote “tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, Kristo” (Efe 4:15). Kwa sababu upendo “haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli” (1Kor 13:6).










Ni sisi Maaskofu wenu,

Mhashamu Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Iringa
Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Dar es Salaam
Mhashamu Askofu Mkuu Josaphat Lebulu, Arusha
Mhashamu Askofu Mkuu Paul Ruzoka, Tabora
Mhashamu Askofu Mkuu Yuda Thaddaeus Ruwa’ichi, Ofm Cap, Mwanza,
Mhashamu Askofu Telesphor Mkude, Morogoro
Mhashamu Askofu Gabriel Mmole, Mtwara

Mhashamu Askofu Bruno Ngonyani, Lindi
Mhashamu Askofu Anthony Banzi, Tanga
Mhashamu Askofu Agapiti Ndorobo, Mahenge
Mhashamu Askofu Evaristo Chengula, IMC, Mbeya
Mhashamu Askofu Augustino Shao, CSSp, Zanzibar
Mhashamu Askofu Damian Kyaruzi, Sumbawanga

Mhashamu Askofu Severine NiweMugizi, Rulenge-Ngara
Mhashamu Askofu Desiderius Rwoma, Bukoba
Mhashamu Askofu Method Kilaini, Bukoba
Mhashamu Askofu Damian Dallu, Geita
Mhashamu Askofu Ludovick Minde, OSS, Kahama
Mhashamu Askofu Alfred Leonard Maluma, Njombe

Mhashamu Askofu Castor Paul Msemwa, Tunduru-Masasi
Mhashamu Askofu Beatus Kinyaiya, Ofm Cap, Mbulu
Mhashamu Askofu Michael Msonganzila, Musoma
Mhashamu Askofu Issack Amani, Moshi
Mhashamu Askofu Almachius Rweyongeza, Kayanga
Mhashamu Askofu Rogath Kimaryo, CSSp Same
Mhashamu Askofu Salutaris Libena, Ifakara
Mhashamu Askofu Eusebius Nzigilwa, Dar es Salaam
Mhashamu Askofu Renatus Nkwande, Bunda
Mhashamu Askofu Gervas Nyaisonga, Dodoma
Mhashamu Askofu Bernadin Mfumbusa, Kondoa
Mhashamu Askofu John Ndimbo, Mbinga
Mhashamu Askofu Titus Mdoe, Dar e
s Salaam.

Tuesday, March 11, 2014

UJUMBE WA BABA MTAKATIFU FRANCISCO KWA KIPINDI CHA KWARESMA 2014

Mama Kanisa anakianza kipindi cha Kwaresima, yaani siku arobaini za toba na wongofu wa ndani; kusali na kufunga; kusoma na kulitafakari Neno la Mungu pamoja na kumwilisha imani katika matendo, kwa Jumatano ya Majivu. Waamini wanakumbushwa kwamba, wao ni mavumbi na mavumbini watarudi tena.

Hizi ni nyakati za toba na zimewekwa na Mama Kanisa kwa ajili ya mazoezi ya maisha ya kiroho; zinajikita katika liturujia ya toba, kuhiji kama ishara ya toba, kujinyima kwa hiyari kama sehemu ya kufunga na kutoa sadaka kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii; ni mwaliko wa kushiriki kidugu kazi za mapendo na kimissionari zinazotekelezwa na Mama Kanisa.

Ujumbe wa Kwaresima kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa Mwaka 2014 unaongozwa na kauli mbiu “Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, Jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba, ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake”. Huu ni mwaliko kwa waamini kuonesha moyo wa ukarimu kwa jirani zao kama ilivyokuwa nyakati za Mtakatifu Paulo aliyewahimiza Wakorintho kuwasaidia ndugu zao waliokuwa wanateseka mjini Yerusalemu.

Baba Mtakatifu katika tafakari hii anaonesha jinsi ambavyo Mwenyezi Mungu ambaye ni tajiri na mwingi wa rehema kwa njia ya Yesu Kristo, Mwanaye wa pekee amejinyenyekesha na kuwa maskini, ili aweze kuwa karibu na binadamu kwa njia ya Fumbo la Umwilisho. Hiki ni kielelezo cha upendo wa Mungu ambao ni neema na baraka inayotolewa kwa binadamu anayependwa na Mwenyezi Mungu, kiasi cha hata Kristo kujisadaka maisha yake.

Huu ndio upendo unaoshirikisha, unajenga na kuimarisha umoja na udugu kwa kuvunjilia mbali kuta za utengano. Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Mwenyezi Mungu amefikiri na kutenda kama binadamu katika mambo yote isipokuwa hakutenda dhambi.

Kwa njia ya umaskini wa Yesu, Mwenyezi Mungu amependa mwanadamu aweze kutajirika, hii ndiyo mantiki ya Fumbo la Umwilisho na Fumbo la Msalaba. Alibatizwa mtoni Yordani si kwa vile alikuwa anahitaji toba, wongofu wa ndani na msamaha, bali alipenda kuonesha mshikamano wa dhati na binadamu mdhambi kwa kujitwika dhambi zake mabegani mwake, ili aweze kuwafariji, kuwaokoa na kuwakomboa kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake wa Kwaresima kwa Mwaka huu anasema, Yesu alijifanya kuwa jirani na Msamaria mwema, kwa kuguswa na mahangaiko ya binadamu, ili hatimaye, aweze kumwonjesha huruma na mapendo yanayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Utajiri wa Yesu unajionesha kwa namna ya pekee kwa kumtegemea Baba yake wa mbinguni, katika kutekeleza mapenzi yake na hatimaye kuvikwa taji la utukufu. Yesu anatambua kwamba, ni Mwana pekee wa Mungu, Masiha anayewaalika wafuasi wake kujitajirisha kutoka kwake na kushiriki udugu na kujitahidi kuchuchumilia utakatifu wa maisha kwa kuishi kama watoto wa Mungu na ndugu zake Kristo.

Kila wakati Mwenyezi Mungu anaendelea kumkomboa mwanadamu kutoka katika umaskini wake kwa njia ya umaskini wa Yesu, kwa kuonja na kuguswa na umaskini wa jirani zao tayari kujifunga kibwebwe kusaidia kupambana na umaskini: wa hali, kipato na maadili. Umaskini ni kielelezo cha kukosa imani, mshikamano na matumaini. Umaskini wa kipato unawakumba wote wanaoishi katika mazingira ambayo ni kinyume kabisa cha utu na heshima ya binadamu.

Hawa ni watu wanaopokonywa haki na mahitaji msingi kama vile: chakula, maji, malazi, huduma bora za afya, fursa za kazi na ajira, maendeleo na ukuaji wa kitamaduni. Kanisa linaendelea kujisadaka kwa ajili ya kupambana na umaskini wa kipato katika mikakati yake ya kichungaji inayopania kumkomboa mtu mzima: kiroho na kimwili. Kanisa linaiona na kuitambua sura ya Kristo miongoni mwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Kanisa linapania kuhakikisha kwamba, utu na heshima ya binadamu vinaendelea kupewa kipaumbele cha pekee kwa kukomesha ubaguzi ambao wakati mwingine ni chanzo kikuu cha umaskini. Kanisa linahimiza matumizi bora ya rasilimali ya dunia kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Jamii iongozwe katika misingi ya haki, usawa, kiasi na ushirikiano.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kuna umaskini wa kimaadili, unaomfanya mwanadamu kuwa ni mtumwa wa dhambi, ulevi wa kupindukia, mcheza kamari na mtazamaji wa picha za ngono. Hili ni kundi la watu lililopoteza dira na mwelekeo wa maisha kwa kukata tamaa! Ni watu wanaoogelea katika utupu kwa kukosa fursa za ajira pamoja na kuendelea kudhalilishwa utu na hehima yao kama binadamu: wanakosa chakula na malazi; hawana haki ya kupata huduma bora katika sekta ya elimu, afya na maendeleo. Matokeo yake ni watu kuelemewa mno na umaskini wa kimaadili kiasi hata cha kutema zawadi ya maisha!

Umaskini huu ni chanzo kikuu cha myumbo wa uchumi kimataifa na matokeo yake ni umaskini na utupu wa maisha ya kiroho. Hali hii inajionesha pale mwanadamu anapomn’goa Mwenyezi Mungu katika maisha na vipaumbele vyake, kiasi hata cha kutema upendo na huruma yake. Hapa mwanadamu anadhani kwamba, anaweza kujitegemea mwenyewe na wala haitaji msaada kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Lakini ikumbukwe kwamba, ni Mungu peke yake anayeweza kukomboa na kumwokoa mwanadamu.

Baba Mtakatifu anasema, Injili ni dawa inayoponya umaskini wa maisha ya kiroho, changamoto na mwaliko kwa kila Mkristo kuhakikisha kwamba, anashiriki kutangaza Injili ya Kristo katika medani mbali mbali za maisha, ili watu waonjeshe upendo na huruma ya Mungu; ili hatimaye, waweze kushirikishwa maisha ya uzima wa milele. Waamini wawe ni watangazaji amini wa Injili ya Furaha inayojikita katika huruma na matumaini; mwanga na faraja kwa wote wanaotembea katika giza na uvuli wa mauti. Ni mwaliko wa kumfuasa Kristo aliyethubutu kuwaendea maskini; akaonesha sifa ya kuwa mchunga mwema kwa kumwendea Kondoo aliyekuwa amepotea, ili kumwonjesha upendo wake. Kwa kushikamana na Yesu, waamini wanaweza kuwa na ujasiri wa kushiriki katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya na maendeleo endelevu.

Baba Mtakatifu Francisko katika Kipindi hiki cha Kwaresima anawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuonesha ushuhuda wa pekee kwa maskini wa hali, maadili na maisha ya kiroho wanaokutana nao kila siku ya maisha yao, ili waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Yesu Kristo. Kwaresima ni muda muafaka wa kujisadaka kwa ajili ya kuwasaidia wengine, kwa kutambua kwamba, kwa njia hii pia tunafanya toba.

Waamini wanaweza kuwatajirisha jirani zao na hivyo kushiriki katika mchakato wa kuganga na kuponya umaskini unaomwandama binadamu. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, waamini wataweza kukitumia kipindi hiki cha Kwaresima ili kupata neema na baraka zinazobubujika kutoka kwa Kristo mwenyewe!

Ujumbe huu umehaririwa na

Padre Richard A. Mjigwa.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican

NCHI YANGU FAHARI YANGU TOUR