Wednesday, September 17, 2014

MAHUSIANO KABLA YA NDOA

Katika ulimwengu, mahusiano ya karibu ya kimwili kabla na nje ya ndoa yanakubalika, na hata kushabikiwa. Vipindi vya uchumba vinahesabika kama nyakati za wahusika hao wawili kuona kama ‘wanafaana’. Hili mara nyingi linawapelekea katika kuwa na mahusiano ya karibu ya kimwili.
Inasikitisha kwamba katika makanisa mengi vijana wanauiga mtindo huu huu, na wale walio katika nafasi za mamlaka – uongozi wa kanisa, wazazi, nk., hawashughuliki na hili suala kwaumakiniunaohitajika.Vijanawanaachiwa kujiamulia wenyewe mipaka katika hili suala nyeti, badala ya kupewa miongozo ya Kibiblia iliyo wazi.
Hebu tuwe wazi tokea mwanzo ya kwamba Mungu hachanganyikani; Neno lake halijaficha jambo. Ndani mwake, tunaona maono na mpango wake vilivyo dhahiri, kwa watu wake na Kanisa lake. Ni wazi kwamba hataki tujichanganye na ulimwengu na njia zake. Na wala Mungu hataki sheria na kuhukumiana Kanisani mwake, ambavyo havina nguvu yoyote ya kumbadilisha mtu. Anachotaka ni Wakristo wote wahakikishwe na Roho Mtakatifu kuhusu dhambi kupitia Injili ya Yesu Kristo ambayo inaweka mpaka ulio wazi na kutuonyesha tunapaswa tusimame juu ya msingi upi. Hii ndiyo maana ninaamini tunapaswa kurejea kwenye msingi – Neno la Mungu – ili tuone anasemaje juu ya hili suala.
MIILI YETU NI VIUNGO VYA KRISTO
Hebu tuangalie Mungu anavyoiona ndoa na mahusiano nje ya ndoa, na tutaona ya kwamba uhusiano wowote wa kimwili nje ya ndoa, uwe wa aina yo yote ile, unahesabika kuwa ni dhambi machoni pa Mungu. Si suala la ‘Tuweke wapi mipaka?’ kwa sababu tukijaribu kuweka mipaka ya aina yoyote, tutaivuka tu. Ni kama lile tangazo la breki za magari lisemavyo, “Usianzishe jambo ambalo hutaweza kulizuilia!”

1 Wakorintho 6:15 inasema: “Je, hamjui ya kuwa miili yenu ni viungo vya Kristo? Basi nivitwae viungo vya Kristo na kuvifanya viungo vya kahaba? Hasha!” Kwa hivyo, si roho zetu tu zilizounganika na Kristo; nafsi yetu yote ni mmoja naye. Mistari ya 16 – 17 inasema, “Au hamjui ya kuwa yeye aliyeungwa na kahaba ni mwili mmoja naye? Maana asema, ‘Wale wawili watakuwamwilimmoja.’Lakiniyeyealiyeungwa na Bwana ni roho moja naye.”
Paulo hapa anasema waziwazi ya kwamba ni lile tendo la ndoa linalowaunga watu kuwa mwili mmoja, na hili linapaswa kuchukuliwa kwa uzito. Katu hatupaswi kusahau ya kuwa roho zetu, nafsi zetu na miili yetu imeungwa pamoja na Kristo. Siku hizi Wakristo wengi wanafanya wanavyopenda na miili yao, pasipo kutambua madhara ya rohoni yanayotokana na matendo yao. Kwenye kifungu hiki Paulo anaweka utofauti kati ya dhambi ya mwili na dhambi nyingine; katika zinaa unatenda dhambi dhidi ya mwili wako kwa sababu unafanyika kuwa mmoja na yule mnayeunganika naye kimwili. Uzinzi ni uhusiano wowote wa kimwili nje ya ndoa. Uongo, wizi, hasira, nk. ni tofauti; haya ni matunda ya tamaa zetu za kimwili.
Ikiwa Mungu aliamua kuweka utofauti kati ya dhambi katika miili yetu na dhambi nyingine, tunapaswa kuwa makini sana, na kuufahamu moyo wake katika hili suala. Msitari wa 18 unasema, “Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe.” Hatupaswi kusahau ya kuwa miili yetu pamoja na roho zetu vimeungwa na Kristo, na tunapotenda zinaa ni jambo zito sana machoni pa Mungu. Mistari ya 19-20 inatukumbusha ya kuwa mwili wetu ni hekalu la Roho Mtakatifu, na tunahimizwa, “mtukuzeni Mungu katika miili yenu.”
MWILI UNAPASWA KUSULUBIWA
Katika Wagalatia 5:24-25, Paulo anasema, “Na hao walio wa Kristo wameusulibisha mwili pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake. Tukiishi kwa Roho, na tuenende kwa Roho.” Kila Mkristo ana uelewa fulani wa maana ya haya Maandiko. Lakini kwa wale wanaotamani kutembea rohoni, na wako tayari kuoa au kuolewa, yana maana zaidi maishani mwao.

Tumeitwa kuisulubisha miili yetu na tamaa zake. Hii ndio maana tunahitajika kuusikia ujumbe wa Msalaba kila wakati kwa sababu unatukumbusha kujikana nafsi zetu na kuyapoteza maisha. Hakuna nafasi ya kudanganyana, wala kujaribisha mambo… Sisi ni watu waliochaguliwa ambao miili yetu ni mali ya Bwana Yesu Kristo.
Iweje, basi, tuwaze ya kuwa ni sahihi kwa watu wawili waliochumbiana rasmi au vinginevyo, kufanya mambo wanayoruhusiwa kufanya tu mume na mke, eti kwa kuwa wamefikia uamuzi wa kuwa wenza? Uamuzi wa watu wawili wa kuoana huko mbeleni unapaswa umaanishe ya kwamba wataheshiminiana kwa utimilifu mbele za Bwana. Hadi siku ya kuoana, Bwana anawataka waishi maisha safi na matakatifu.
Vijana, sikilizeni… isipokuwa una uhakika moyoni mwako ya kuwa uhusiano umeanzishwa na Mungu, usithubutu kuuingia. Ukitaka kuufahamu mpango wake, na mtu aliyekuandalia kuwa mwenzi wako, fahamu ya kuwa atakufunulia.
Mkishafahamu ya kuwa ni mpango wa Mungu muoane, na ikiwa mnafahamu maisha ya utakatifu mnayopaswa kuishi kabla ya harusi, hakuna hatari. Mnaweza mkachumbiana na kutiana moyo katika kuheshimiana, kwa sababu mmehakikishiwa mioyoni mwenu ya kuwa mnapaswa kuishi maisha matakatifu mbele za Bwana hadi mtakapooana. Utakuwa na kicho kitakatifu cha uwepo wa Mungu katika maisha ya mwenzi wako na kufanyika kielelezo kwa wengine.
Ndio maana unapaswa uthibitike katika kile Mungu anachosema, ili pasiwepo na kubahatisha. Je, kuna mahusiano ya aina yoyote ya kimwili kabla ya ndoa yanayokubalika? Hasha! Neno la Mungu liko wazi sana juu ya hili suala.
MANUKATO YA UHUSIANO SAFI NA MTAKATIFU
Labda tayari uko katika uhusiano wa kimwili nje au kabla ya ndoa, na Bwana anakunenea ya kwamba si sahihi. Ushauri wangu ni kwamba utubu na ufanye uamuzi imara wa kuacha mahusiano yote ya kimwili mara moja; na usigeuke nyuma. Si jambo ambalo linafanyika hatua kwa hatua, wala si jambo la kuchukulia kwa wepesi. Neema ya Mungu ipo kukusaidia. Na ikiwa ninyi wawili mnafahamu mioyoni mwenu ya kuwa mmeandaliwa kuoana, basi jitunzeni hadi siku hiyo, mheshimiane kama vile ndugu wa kiume anavyomheshimu ndugu wa kike kanisani, na katika kufanya hivyo muishi maisha matakatifu na safi. Injili ya Msalaba wa Yesu Kristo inaleta jawabu kwa, na kuchora msitari ulio wazi katika kila jambo tunalokabiliana nalo maishani mwetu. Inatusaidia kuenenda katika uhakikisho, na kwa maana hiyo tunatembea katika ushindi. Wakristo wa kila rika, walio kwenye ndoa na ambao wako bado, wanahitajika wasikilize kwa umakini kile Mungu anachosema katika Neno lake ili waweze kuishi maisha matakatifu na kufanyika vielelezo kwa wengine. Je! si ni jambo la utukufu moyo wako unapokushuhudia ya kuwa kuna hali ya usafi katika uhusiano wa ndugu wanaotaraji kufunga ndoa? Hili linaleta harufu nzuri ya manukato inayopendeza. Je, ni ushuhuda wa jinsi gani wa nguvu ya Injili watu wawili wanapooana juu ya huu msingi!

Ninaamini huu ndio mpango wa Mungu kwa Kanisa lake na kwa watoto wake. Hakuna haja ya kukata tamaa. Mungu yu hai; anaweza kuleta watu wawili pamoja. Anajua ya mbeleni. Anajua kila kitu kuhusu maisha yetu, na shauku yake ni sisi tuishi maisha safi na matakatifu. Ndio maana ni heri kusubiri, kuliko kujaribisha mambo. Fungua moyo wako; mwache Mungu azungumze na wewe na akushawishi. Kwa Yesu Kristo hakuna kuchelewa. Leo inaweza ikawa siku yako ya kumtangazia Bwana ya kuwa unaenda kuishi maisha yako ya Ukristo kabla ya ndoa kwa kulifuata Neno lake.

Tuesday, September 9, 2014

Masista watatu wauawa Burundi

soma hapaBaba Mtakatifu Francisko, amepeleka salaam zake za rambirambi kwa familia za Masista watatu wanashirika la Mtakatifu Xavery, waliouawa katika nyumba yao ya Kamenge, Kaskazini mwa mji wa Bujumbura siku ya Jumapili. Majina ya Marehemu Masista ni Sista Olga Raschietti, Sista Luchia Pulici na Sr Bernadetta Boggian. Wote wanatajwa kuwa raia wa Italia.

Rambirambi za Papa zimetumwa kwa Mjumbe wake wa Kitume nchini Burundi, Askofu Mkuu Evariste Ngoyagoye na nyingine kwa Mama Mkuu wa Shirika la Masista wa Mtakatifu Xavery, akionyesha kusikitishwa sana na kilichotokea kwa Masista hao. Papa anatumaini damu hii ya watu wa Mungu iliyomwangika bure, itaweza kuwa mbegu ya matumaini katika ujenzi wa udugu wa kweli kati ya jamii ya watu wa Burundi. Na ameahidi kuwakumbuka katika sala zake mashahidi hawa wa Injili , na ukaribu wake kwa shirika, na jumuiya ya waamini nchini Burundi.

Mkuu wa Shirika la Watawa Xaverian nchini Burundi, Padre Mario Pulcini, akithibitisha uwepo wa tukio, ameonyesha hisia kwamba ni tukio la wizi. Na kwamba, Sista Lucia na Sista Olga, waliuawa Jumapili mchana wakati Sista Bernadetta, alikwenda kupokea Masista wengine waliowasili katika uwanja wa ndege tokea Italia.

Wakati aliporejea nyumbani alikutana na hali ya ukimya uliompa wasiwasi na baadaye akiwa na Padre Mario waliona wenzao tayari walikuwa wameuawa ndani ya nyumba yao. Na Sista Bernadetta ameuawa usiku wa kuamkia Jumatatu akiwa katika chumba chake.

Askofu Henry, Jimbo la Parma Italia, kwa niaba ya Kanisa lote la Parma, amepeleka pia niaba ya waamini wa Parma , salaam zake za rambirambi kwa Usharika wa Missionari Xaverians, wakiwafariji kwa sala ya imani kwa Bwana wa Maisha. Askofu pia ametoa ombi kwa Wakristo wa Jimbo la Parma na kwa wote wenye mapenzi mema, kuwakumbuka Masista hawa katika sala zao.


Wednesday, August 27, 2014

Ziara ya Uinjilishaji JImbo la Mbulusehemu ya Promo www viwawaboko blogs...

Nembo ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016

Heri wenye rehema maana hao watapata rehema, ndiyo kauli mbiu itakayoongoza maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016 itakayofanyika Jimbo kuu la Cracovia, Poland. Kamati kuu ya maandalizi imechapisha nembo itakayotumika kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani ambayo Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuhudhuria na kushiriki kikamilifu.

Nembo ina rangi kuu tatu: Bluu, Nyekundu na Njano; inaonesha ramani ya Poland na ndani yake kuna Msalaba inayomwonesha Yesu Kristo, kiini cha mkutano huu. Nembo hii inawaalika vijana kujiaminisha mikononi mwa Mungu, utekelezaji wa maneno ya Mtakatifu Faustina Kowalska aliyeeneza Ibada ya Huruma ya Mungu.

Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016 itaanza kutimua vumbi kuanzia tarehe 26 hadi Julai 2014. Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuwasili nchini Poland hapo tarehe 2
8 Julai 2016.

Kambumbu kuchezwa kwa ajili ya kueneza Ujumbe wa amani duniani

Septemba Mosi katika viwanja vya Olympic vya mjini Roma, kutafanyika mashindano ya mpira wa miguu kati ya timu mbili za kidini kwa heshima ya Papa Francisco, kwa ajili ya kutoa ujumbe wa nguvu wa amani duniani. Ni mpango uliowasilishwa siku ya Jumanne kwa wanahabari katika ukumbi wa Makao Makuu ya Redio Vatican. Kati ya walio shiriki katika mkutano huo ni Msgr. Guillermo Karcher, afisa katika Sekretarieti ya Vatican kwa ajili ya khafla za Kipapa , mchezaji wa zamani wa mpira wa miguu Javier Zanetti, wakiwepo pia wachezaji kutoka timu ya Lazio, Cristian Ledesma,na Juan Iturbe wa timu ya Roma.

Mchezo huu utakao fanyika katika uwanja wa Olympic Roma, Mosi Septemba 20:45, si mechi za kipinzani bali ni mchezo wa kirafiki kwa ajili ya kutoa ujumbe wa amani, na washiriki wa mechi hii wanatoka mataifa mbalimbali na watu wa imani mbalimbali . Sehemu ya mapato yake yatatengwa kwa ajili ya kufanikisha miradi ya Papa kwa ajili ya elimu na ustawi wa maisha kwa watu maskini mradi unaofanikishwa na kuendelezwa na taasisi ya "Scholas Occurentes" ambayo ni taasisi ya elimu, mkono wa Papa Francisko katika utoaji wa misaada na chama cha "Pupi" kilicho anzishwa na aliyekuwa Argentina mchezaji wa mpira wa miguu Javier Zanetti na mke wake Paula, kwa ajili udumishaji juhudi za kutoa msaada katika mradi unaoitwa "maisha mbadala". Kwa ajili hii, pia unaalikwa kutoa msaada wako katika juhudi hizi kwa kutuma ujumbe wa SMS namba 45593.

Katika mkutano wa waandishi wa habari, Msgr. Guillermo Javier Karcher, aliwasilisha rasmi salaam za Papa Francisko, ambamo alitoa shukurani zake za dhati kwa mpango huo uliandaliwa kwa ajili ya amani, kama alivyowahi kupendekeza siku za nyuma, uwepo wa mechi ya kirafiki kati ya wachezaji kutoka kila timu na wa dini zote na madhehebu yote Kikristo.Taasisi ya “Scholas Ocurrentes”, ililichukua kwa makini pendekezo hilo na kuandaa mechi hii na pia ina lenga kujenga mtandao kwa ajili ya kubadilishana miradi na maadili elimu kwa ajili ya kuendeleza utamaduni wa mijadala na utamaduni wa amani. Katika mtazamo huo, Papa Francisko alipendekeza kwamba kabla ya kila mchezo, kila timu ipande mti wa mzeituni, kama ishara ya amani , kama ilivyo fanyika katika maadhimisho ya mwaka Mtakatifu 2000, yeye akiwa Askofu Mkuu wa Buenos Aires, alipanda mti katika uwanja wa Plaza de Mayo , akiwa na wanafunzi elfu saba kutoka shule za Kiserikali bila ya utengano wa kidini.
Waandaaji wa tukio hili wanatumaini, mchezo huu wa kwanza wa madhehebu,utaweza kuwa hatua ya mwanzo katika juhudi za kueneza ujumbe wa amani kwa njia ya michezo, kama Papa Francisco alivyo pendekeza. Michezo pamoja na kuwa ni uwanja wa upinzani kati ya timu mbili zinazocheza, lakini ni tukio ambalo daima hufanyika katika hali ya amani na utulivu, kuburudisha na kufurahisha mioyo ya watu. Na hivyo unakuwa ni mfano mzuri wa kuigwa na vyama vya kisiasa , kwamba licha ya kuwa na maoni tofauti katika utendaji lakini katika utofauti huo, unakuwa ni nafasi ya kujenga mazuri kwa ajili ya ustawi wa jamii. Na kuwa mchezaji wa mpira au mwana riadha hakumwondolei mtu imani yake. Imani ni suala linalo ambatana na mtu katika maisha yake yote. Na ndivyo licha ya watu kuwa na imani mbalimbali, wanapaswa kuchanganyika na kucheza pamoja kwa amani na utulivu kama ilivyo timu za mpira katika mechi, hucheza kwa ajili ya manufaa ya wote.


NCHI YANGU FAHARI YANGU TOUR