Ujumbe wa Baba Mtakatifu Benedikto XVI kwa Siku ya Vijana Duniani 2013
Nendeni ulimwenguni kote mkayafanye mataifa yote kuwa ni wanafunzi wangu ndiyo kauli mbiu inayoongoza maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani itakayoadhimishwa Rio de Janeiro, Brazil, mwezi Julai 2013.
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anachukua fursa hii kuwaalika vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia kushiriki katika tukio hili muhimu katika maisha ya imani. Sanamu ya Kristo Mfalme inayopendezesha mji wa Rio de Janeiro, Brazil, ikiwa na mikono wazi, ni kielelezo cha mwaliko wa Kristo ambaye yuko tayari kuwapokea wote wanaomwendea na kwamba, moyo wake unaonesha upendo wa hali ya juu kabisa kwa kila kijana.
Huu ni mwaliko kwa vijana wenyewe kujiachilia mikononi mwa Kristo. Baba Mtakatifu anawaalika vijana kushirikisha mang’amuzi haya kwa vijana wenzao watakaoshiriki katika maadhimisho ya siku ya vijana duniani kwa mwaka 2013 nchini Brazil. Vijana wanapaswa kupokea na kuukumbatia upendo wa Kristo, ili waweze kuwa ni mashahidi wa upendo huu ambao unatakiwa kwa kiasi kikubwa ulimwenguni.
Baba Mtakatifu anasema kwamba, vijana wengi kutokana na kipaji chao cha kujitolea wamesaidia kwa namna ya pekee katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu na maendeleo ya ulimwengu huu kwa njia ya kutangaza Habari Njemaya Wokovu. Ni watu wenye ari inayopata chimbuko lake kutoka katika Injili ya upendo wa Mungu unaojionesha kwa njia ya Kristo; walitumia nyenzo na vifaa mbali mbali vilivyokuwepo kwa wakati ule, pengine duni kuliko hali ilivyo kwa sasa.
Vijana wanaendelea kujiuliza umuhimu na maana ya maisha pamoja na hali ngumu wanayokabiliana nayo. Matatizo na changamoto wanazokumbana nazo katika hija ya maisha, vijana wanajiuliza ikiwa kweli wanaweza kufanya jambo lolote?
Mwanga wa Imani anasema Baba Mtakatifu unaondoa giza hili kwa kutambua kwamba, maisha ya binadamu ni jambo nyeti sana kwani ni matunda ya upendo wa Mungu. Mungu anawapenda wote hata wale ambao wamekengeuka na kupoteza imani yao. Mwenyezi mungu anaendelea kuwasubiri kwa utulivu. Ndiyo maana alimtoa Mwanaye wa pekee ili aweze kufa na kufufuka kutoka katika wafu ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika utumwa wa dhambi.
Mama Kanisa anapoendelea kutekeleza dhamana na utume wake wa Uinjilishaji anawategemea vijana, kwani wao ni Wamissionari wa kwanza kabisa miongoni mwa vijana wenzao. Mara baada ya maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, Papa Paulo wa sita, alitoa ujumbe kwa vijana ulimwenguni, akiwataka kujenga dunia bora zaidi, kuliko ilivyokuwa kwa wakati ule. Mwaliko huu bado ni endelevu hata leo hii, licha ya muda kuendelea kuyoyoma kwa kasi. Maendeleo ya sayansi na teknolojia yanawezesha mwingiliano wa vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia.
Utandawazi wa mwingiliano huu unaweza kuwa na mwelekeo chanya katika kukuza ubinadamu, ikiwa kama utasimikwa katika upendo wa dhati na badala ya kujikita katika vitu! Ni upendo tu, unaoweza kusheheni katika mioyo ya watu, kwa sababu Mungu ni upendo. Mwanadamu anapomsahau Mwenyezi Mungu, anapoteza tumaini na upendo kwa wengine. Ndiyo maana kuna haja ya kumshuhudia Mungu ili watu wengine waweze kuonja uwepo wake. Wokovu wa watu wote na kila mmoja unategemea kwa kiasi kikubwa upendo huu.
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku ya VIjana Duniani anawakumbusha kwamba, wito wa kimissionari ni muhimu sana kwa ajili ya hija ya imani, wanapotangaza Injili pamoja na kuwawezesha wao wenyewe kukua na kukomaa kikristo wakishikamana na Kristo. Hawataweza kuwa waamini ikiwa kama hawawezi kuinjilisha. Kuwa mmissionari maana yake ni kuwa kwanza kabisa mfuasi wa Kristo, kwa kumsikiliza kwa makini na hatimaye, kumfuasa.
Baba Mtakatifu anawaalika vijana kufanya tafakari ya kina kuhusu karama walizokirimiwa na Mwenyezi Mungu ili waweze kuzitumia kwa ajili ya jirani zao; wajifunze kusoma historia ya maisha ya kila mmoja wao na kuchuchumilia utajiri urithi mkubwa waliobahatika kuupata kutoka kwa vizazi vilivyopita, kwa kutambua kwamba, wanaunganishwa na umati mkubwa wa watu waliotangaza na kurithisha imani ambayo wanapaswa kuwamegea wengine. Kama Wamissionari wanapaswa kutambua Mapokeo ya Imani ya Kanisa. Vijana wanapaswa kutambua kile wanacho amini ili kuweza kukitangaza.
Yesu aliwatumwa mitume wake kwenda ulimwenguni kote ili kutangaza Habari Njema kwa kila kiumbe, yule atakayeamini na kubatizwa atapata uzima wa milele. Kuinjilisha maana yake ni kutangaza Habari Njema ya Wokobu ambayo ni Yesu Kristo mwenyewe. Kadiri watakavyomfahamu Kristo ndivyo watakavyokuwa na hamu ya kutaka kumtangaza zaidi na zaidi; kwa kumpenda na kuvutwa kwake ili kuwa naye karibu zaidi, kwani ana nguvu ya upendo inayoongoza utume wa kutangaza Injili. Roho wa Bwana anawataka kujitoa katika ubinafsi wao na kuwa tayari kwenda Kuinjilisha, daima wakijikita katika nguvu ya upendo wa Mungu, inayowabandua kutoka katika ubinafsi, ulimwengu, matatizo na mazoea yao binafsi.
Kristo mfufuka anasema Baba Mtakatifu, anawatuma Mitume wake kutolea ushuhuda wa uwepo wake unaoyakomboa mataifa, kwani Mwenyezi Mungu ni mwingi wa upendo na anataka kila mtu aweze kuokoka na kamwe asipotee! Vijana wanaalikwa kufungua macho yao ili kuona makando kando yao. Mataifa wanayoalikwa kuyatangazia Habari Njema si nchi nyingine duniani; bali ni kila sehemu ya maisha yao; kama vile familia, jumuiya mahali pa masomo na kazi; makundi ya marafiki zao na “vijiwe” wanapotumia muda wao wa ziada. Utangazaji wa Injili ya Kristo kwa njia ya furaha inamaanisha kugusa kila sehemu ya maisha.
Baba Mtakatifu anapenda kukazia kwa namna ya pekee, Uinjilishaji katika sekta ya mawasiliano ya jamii, hasa katika mtandao, unaotumiwa kwa kiasi kikubwa na vijana, wanaotekwa kwa urahisi zaidi na njia za mawasiliano ya jamii, ili kuweza kuwajibika katika kuuinjilisha ulimwengu wa mtandao.
Sehemu ya pili ni safari na uhamiaji, kwani vijana wengi wanasafiri kwa sababu mbali mbali kama vile masomo na kazi na wakati mwingine ni kwa ajili ya kujifurahisha. Lakini pia kuna mamillioni ya watu, wengi wao wakiwa ni vijana, wanaosafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine wakitafuta fedha au kutokana na sababu mbali mbali za kijamii. Hili linaweza kuwa ni jukwaa pia la kushirikishana Injili.
Baba Mtakatifu anawakumbusha vijana kwamba, kutangaza habari Njema ya Wokovu ni dhamana inayohusu maisha yao yanayogeuzwa kuwa ni alama za upendo, unaofanana na ule wa Kristo. Vijana wanapaswa kujiandaa vyema kama yule Msamaria mwema, kwa kuwa makini kwa watu wanaokutana nao, ili kuwasikiliza, kuwaelewa na kuwasaidia. Kwa njia hii wanaweza kuwaongoza watu wanaotafuta maana ya maisha kwenda nyumbani mwa Mungu, yaani Kanisa, mahali ambapo matumaini na wokovu ni makazi yake.
Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo na Katekesi makini, wanaweza kuwafanya wengine kuwa ni wafuasi, kwa kuwaongoza wengine ili waweze kukutana na Yesu Kristo kwa njia ya Neno na Sakramenti zake. Kwa njia hii, wanaweza kumwamini na kupata fursa ya kuweza kumfahamu Mungu na hatimaye, kuishi katika neema yake. Baba Mtakatifu anawaalika vijana kumwomba Roho Mtakatifu ili aweze kuwasaidia; kuwaonesha njia ya kumfahamu na kumpenda Kristo kwa ukamilifu zaidi, wakijitahidi kuwa wagunduzi wanapotangaza Injili.
Baba Mtakatifu anawatia moyo vijana kamwe wasikate tamaa wanapojisikia kwamba ni dhaifu na wanyonge kiasi cha kushindwa kuinjilisha, wasikate tamaa, bali watambua kwamba, uinjilishaji si utume unaotegemea karama na uwezo wao. Wanapaswa kuwa waaminifu na watii ili kuitikia wito unaojikita katika nguvu ya Mungu. Vijana wanatakiwa kuyasimika maisha yao katika sala na maisha ya Kisakramenti, kwani uinjilishaji wa kweli ni matunda ya sala na unaenziwa pia kwa sala.
Vijana wajifunze kuzungumza na Mungu ili hatimaye, waweze kuzungumza kuhusu Mungu. Maisha ya imani ya vijana yapate chimbuko lake katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, pamoja na kujitahidi kupokea Sakramenti ya Upatanisho mara kwa mara. Kwa wale ambao bado hawajaimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara, waongeze juhudi ya kuipokea sakramenti hii, kwani kama ilivyo pia Sakramenti ya Ekaristi Takatifu ni Sakramenti za utume, kwani zinawakirimia nguvu na mapendo ya Roho Mtakatifu ili kuweza kuungama imani. Vijana wanaalikwa kushiriki kikamilifu katika Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu.
Ikiwa kama vijana watafuata njia hii kwa ukamilifu, Yesu mwenyewe atawawezesha kuwa waaminifu kwa Neno ili waweze kutolea ushuhuda amini na wenye nguvu kwake Yeye. Wakati mwingine watajaribiwa ili kuonesha udumifu, pale neno la Mungu linapokatiliwa au kukumbana na upinzani. Baba Mtakatifu anatambua mateso na dhuluma ambayo baadhi ya vijana wanakabiliana nazo sehemu mbali mbali za dunia kiasi kwamba, hawawezi hata kidogo kutolea ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake kutokana na ukosefu wa uhuru wa kidini. Kuna baadhi yao ambao tayari wamekwisha yamimina maisha yao kwa sababu tu ni Wakristo. Baba Mtakatifu anawataka vijana kuwa imara katika imani yao, daima wakitambua kwamba, Yesu Kristo yuko pamoja nao katika kila jaribu la maisha.
Vijana wanalihitaji Kanisa ili kuweza kuwa imara katika imani yao ya Kikristo. Hakuna mtu anayeweza kutolea ushuhuda wa Injili peke yake, kwani Yesu aliwatuma wafuasi wake kwa pamoja. Hivyo, ushuhuda wa imani daima unatolewa ba Jumuiya ya Kikristo na utume wao unaweza kuzaa matunda kwa njia ya umoja unaomwilishwa ndani ya Kanisa. Ni kwa njia ya umoja na upendo kwa jirani, wengine wanaweza kuwatambua kwamba, wao ni wafuasi wa Kristo.
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya siku ya vijana duniani kwa mwaka 2013 anawaalika vijana kusikiliza kutoka katika undani wa mioyo yao sauti ya Yesu inayowaita kutangaza Injili. Kama sanamu ya Yesu Kristo Mfalme inavyoonesha pale Rio de Janeiro, ni moyo ambao umefunguka kwa upendo kwa kila mtu na mikono yake iko wazi kuwafikia watu wote. Ni changamoto kwa vijana wenyewe kuwa ni moyo na mikono ya Yesu, kwa kutolea ushuhuda wa upendo huu sanjari na kuwa ni wamissionari kwa vijana wa kizazi kipya, wanaowajibishwa na upendo ambao uko wazi kwa wote.
Baba Mtakatifu anahitimisha ujumbe wake kwa kusema kwamba, mwaliko anaoutoka kwa vijana ni kwa ajili ya dunia nzima, lakini zaidi kwa vijana wanaoishi Amerika ya Kusini. Katika maadhimisho ya mkutano wa tano wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Amerika ya Kusini, uliofanyika mjini Aparecida kunako mwaka 2007, Maaskofu walizindua kampeni ya utume Barani humo. Vijana wanaunda idadi kubwa ya wananchi wa Amerika ya Kusini. Hawa ni rasilimali muhimu sana kwa Kanisa na Jamii, changamoto ya kutangaza kwa ari zaidi imani kwa vijana wenzao kutoka sehemu mbali mbali za dunia.
No comments:
Post a Comment