Hatua za mwisho mwisho kabla ya Papa Mpya kutokeza hadharani!
Padre Federico Lombardi msemaji mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro unakamilika kwa Kardinali kupata theluji mbili ya kura zote halali zilizopigwa. Baada ya hapo, Dekano wa Makardinali ambaye wakati wa uchaguzi ni kardinali Giovanni Battista Re, atamuuliza Kardinali aliyechaguliwa kama anakubali kisheria kwamba, amechaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Baada ya hapo, ataulizwa jina ambalo atalitumia katika utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Wakati wote huu, Mshehereheshaji mkuu wa Papa ndiye atakayekuwa anachukua rasmi taarifa zinazotolewa na Papa Mteule akisaidiwa na Washereheshaji wengine wawili wanaokuwepo mahali hapo kama Mashahidi. Seehemu hii ya mchakato ikikamilika, hapo karatasi zilizotumika kwa ajili ya kupigia kura zinachomwa na hapo moshi mweupe unatoka kuashiria kwamba Kanisa limempata Papa Mpya.
Papa Mpya ataelekea kwenye "Chumba cha machozi" neno ambalo pengine linaonesha ile hali ya ndani anayokuwa nayo Kardinali baada ya kuambiwa kwamba, amechaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Anaporudi kwenye Kikanisa cha Sistina, Injili inayozungumzia Ukulu wa Mtakatifu Petro inasomwa, Makardinali wanasali kwa kitambo kidogo na hapo Makardinali moja baada ya mwingine wanaanza kwenda kula kiapo cha utii kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, wakati wote huu, Makardinali na Papa wanaendelea kumshukuru Mungu kwa kuimba utenzi wa shukrani, Te Deum.
Padre Lombardi anasema, Papa Mpya kabla ya kwenda kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro kutoa baraka zake kwa mji wa Roma na Ulimwengu kwa ujumla, "Urbi et Orbe" atapitia kwanza kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Paulo kusali kwa kitambi kifupi na baadaye atawasalimia na kuwapatia baraka zake za kitume waamini, mahujaji na wote watakaokuwa wamekusanyika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro. Papa mpya ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kusimikwa kwake, siku yoyote inayoonekana inafaa zaidi!
No comments:
Post a Comment