Katika Ukristo vipaji vya Roho Mtakatifu ni misimamo tunayotiwa na Roho Mtakatifu wa kuangaza, kuimarisha na kuzoesha akili na utashi wetu ili kushirikiana naye katika mambo ya utumishi wa Mungu.
Kusudi tujue kweli muundo wa Kiroho unaotuwezesha kuishi kama wana wa Mungu, haitoshi tuyajue maadili. Ni lazima tuzingatie pia vipaji vya Roho Mtakatifu, pasipo kusahau namna mbalimbali za kupata msaada wa Mungu.
Orodha ya vipaji ya Roho Mtakatifu kuanzia juu:
- 1. hekima
- 2. akili (kipaji)
- 3. shauri (kipaji)
- 4. nguvu (kipaji)
- 5. elimu (kipaji)
- 6. ibada (kipaji)
- 7. uchaji wa Mungu.
Hekima ni kipaji cha Roho Mtakatifu cha kutusaidia tupende na kufurahia mambo ya Mungu. Akili ni mwanga wa Roho Mtakatifu wa kutusaidia tumjue zaidi Mungu na ukamilifu wake pamoja na kuelewa ufunuo wake. Shauri ni kipaji cha Roho Mtakatifu kinachotuelekeza kuchagua siku zote mambo yenye kufaa zaidi kwa sifa ya Mungu na kwa wokovu wetu. Nguvu ni kipaji cha Roho Mtakatifu kinachotutia moyo wa kushika sana amri za Mungu na mambo ya utumishi wake tusiogope watu wala matukano wala mateso wala kufa. Elimu ni kipaji cha Roho Mtakatifu kinachotutia maarifa ya mambo ya ulimwengu huu, kwa kutambua mapungufu yake pamoja na mitego, werevu na udanganyifu wa shetani akitujaribu mwenyewe au kwa kupitia vitu kama watu. Ibada ni kipaji cha Roho Mtakatifu kinachotufanya tumpende Mungu kama Baba yetu mwema na watu wote kama ndugu; kwa msingi huo kutimiza utumishi wa Mungu na yote yale yenye kumpa Mungu sifa na heshima. Uchaji wa Mungu ni kipaji cha Roho Mtakatifu kinachotutia hofu ya kumchukiza Mungu kwa dhambi kama vile mtoto mwema aogopavyo kumtia baba yake uchungu.
Ushuhuda wa Biblia
Ufunuo kuhusu vipaji vya Roho Mtakatifu unapatikana hasa katika dondoo la Isa 11:2 ambalo linamhusu kwanza Masiya, halafu kwa kumshiriki yeye linawahusu waadilifu wote ambao Yesu aliahidi kuwapelekea Roho Mtakatifu: “Roho ya Bwana atakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha Bwana”. Kipaji cha ibada hakitajwi katika lugha asili ya Kiebrania, bali katika tafsiri za Septuaginta na Vulgata. Halafu, Isaya 11:3 kwa Kiyahudi inataja tena “kumcha Bwana”, ambapo katika Agano la Kale “kumcha Bwana” na “ibada” ni maneno mawili yenye maana karibu ileile. Hivyo kuanzia karne III mapokeo yanashika idadi ya vipaji saba.
Katika kitabu cha Hekima tunasoma: “Naliomba, nikapewa ufahamu; nalimwita Mungu, nikajiliwa na roho ya Hekima. Naliichagua kuliko fimbo za enzi na viti vya enzi, wala mali sikudhani kuwa ni kitu ikilinganishwa nayo; wala sikuifananisha na kito cha thamani, mradi dhahabu yote ya nchi ni kama mchanga kidogo mbele yake, na fedha itahesabiwa kama udongo. Naliipenda kupita afya njema na uzuri wa sura, hata zaidi ya nuru nikataka kuwa nayo, kwa maana mwangaza wake haufifii kamwe. Na pamoja nayo nikajiliwa na mema yote jamii… ingawa sijajua ya kama yeye ndiye aliyeyazaa… Maana yeye amekuwa hazina kwa wanadamu isiyowaishia; nao wale waitumiao hujipatia urafiki na Mungu… na tangu kizazi hata kizazi huwaingilia roho takatifu, huwafanya wanadamu kuwa rafiki za Mungu na manabii” (Hek 7:7-11,12,14,27).
Ufunuo wa Agano la Kale umetimilizwa na Mwokozi: “Mkinipenda, mtazishika amri zangu. Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; ndiye Roho wa kweli… anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu… huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia” (Yoh 14:15-17,26). Mtume Yohane, akitaka kuwakinga waamini dhidi ya wazushi, akaongeza, “Nanyi mmepakwa mafuta na Yeye aliye Mtakatifu… Nanyi, mafuta yale mliyoyapata kwake yanakaa ndani yenu, wala hamna haja ya mtu kuwafundisha; lakini kama mafuta yake yanavyowafundisha habari za mambo yote, tena ni kweli wala si uongo” (1Yoh 2:20,27). Katika Maandiko yapo pia madondoo kuhusu kipaji kimojakimoja.
Ushuhuda wa mapokeo
Mababu wa Kanisa waliyafafanua mara nyingi maneno hayo na kutamka wazi kuwa vipaji saba vya Roho Mtakatifu vimo ndani ya waadilifu wote. “Hivyo vipaji vya Roho Mtakatifu kwetu ni kama chemchemi ya Kimungu tunapochota ujuzi hai wa amri za maisha ya Kikristo, na kwa njia yake tunaweza kujua pia kama Roho Mtakatifu anakaa ndani mwetu” (Katekisimu ya Mtaguso wa Trento). Ushuhuda muhimu wa Mapokeo kuhusu vipaji saba unapatikana katika liturujia ya Pentekoste: “Wape waamini wako, / wenye tumaini kwako, / paji zako zote saba” (sekwensya “Uje Roho Mtakatifu”). “Mtoa wa vipaji saba... / tia nuru akilini / na upendo mioyoni” (utenzi “Uje Roho Muumbaji”).
Ushuhuda huo ulielezwa vizuri na Papa Leo XIII, “Mwadilifu anayeishi kwa neema inayotia utakatifu na kutenda kwa njia ya maadili kama kwa vipawa mbalimbali, anahitaji kabisa vipaji saba, ambavyo vinaitwa kikamilifu zaidi vipaji vya Roho Mtakatifu. Kwa vipaji hivyo roho ya mtu inainuliwa na kuwezeshwa kutii kwa urahisi na mapema zaidi miangaza na misukumo ya Roho Mtakatifu. Vipaji hivyo vina nguvu kubwa hata kumwongoza mtu kwenye utakatifu mkuu; ni bora hivi hata kudumu mbinguni pia, ingawa kwa kiwango cha juu zaidi. Kwa njia yake roho inaongozwa na kuhimizwa kujipatia heri za Kiinjili, ambazo ni maua yanayochanua kwa wakati wake, dalili tangulizi za heri ya milele... Kwa kuwa vipaji ni vikubwa hivyo navyo vinaonyesha wema mkuu wa Roho Mtakatifu kwetu, vinatudai tumuonyeshe heshima na utiifu mkuu kabisa.
Tutafikia kwa urahisi hatua hiyo tukijitahidi zaidi na zaidi kumjua, kumpenda na kumuomba... Tunapaswa kumpenda Roho Mtakatifu kwa kuwa ni Mungu... tena kwa kuwa ni upendo wenyewe, asili, wa milele, kwa sababu hakuna kinachopendeza kuliko upendo... Yeye atatujalia kwa wingi zawadi zake za kimbingu, hasa kwa sababu utovu wa shukrani unafunga mikono ya mfadhili, lakini moyo wa shukrani unaifungua tena... Tunapaswa kumuomba mfululizo na kwa tumaini kubwa atuangaze zaidi na zaidi na kuwasha ndani mwetu moto wa upendo wake, ili kwa kutegemea imani na upendo tutembee kwa ari kuelekea tuzo la milele, kwa kuwa ndiye amana ya urithi wetu”.
Maelezo ya Thoma wa Akwino
Mwalimu wa Kanisa huyo alifundisha hasa matatu: 1° kwamba vipaji ni misimamo ya kudumu, lakini tofauti na maadili; 2° kwamba ni vya lazima kwa wokovu; 3° kwamba vinashikamana na upendo na kukua pamoja nao.
1° “Ili kutofautisha vipaji na maadili mbalimbali tunapaswa kufuata lugha ya Biblia inayoviita si vipaji bali roho” kusudi tuelewe kuwa vinapatikana ndani mwetu kwa uvuvio wa Mungu au msukumo kutoka juu wa Roho Mtakatifu. Ni lazima tuzingatie kwamba binadamu ana mambo mawili yanayomuongoza: moja limo ndani mwake, yaani akili, lingine liko nje, yaani Mungu. “Ni wazi kwamba chochote kinachosukumika kinatakiwa kulingana na lile linalokisukuma; na ukamilifu wake ni urahisi wa kusukumwa nalo. Basi, kadiri hilo lilivyo bora, ni lazima kinachosukumwa kiwe kikamilifu zaidi ili kupokea msukumo wake. Hatimaye ni wazi kwamba maadili ya kiutu yanamkamilisha mtu katika kujiongoza kwa akili yake katika maisha ya ndani na ya nje. Basi unahitajika ndani mwake ukamilifu wa juu ambao umuandae kusukumwa Kimungu, na namna hizo kamilifu zinaitwa vipaji si tu kwa kuwa tunamiminiwa na Mungu, bali pia kwa sababu kwa njia yake mtu anawezeshwa kupokea mara uvuvio wa Kimungu, alivyosema Isaya (50:5): ‘Bwana Mungu amenizibua sikio langu, wala sikuwa mkaidi, wala sikurudi nyuma’. Ndiyo sababu wengine wanasema vipaji vinamkamilisha binadamu vikimuandaa kutenda mambo bora kuliko ya maadili”.
Hapo tunaona kuwa vipaji vya Roho Mtakatifu si matendo wala si misukumo au misaada ya kupita ya neema, bali ni misimamo ya kudumu tunayomiminiwa, inayotuweka tayari kupokea uvuvio wa Mungu, kama vile tanga zinavyowezesha chombo kwenda kwa nguvu ya upepo. Kwa utayari huo wa kupokea misukumo vinatusaidia kutenda mambo yale bora ambayo ukamilifu wake unaonyesha kwamba yanategemea vipaji kuliko maadili.
Mfano huo ulitolewa na Yesu Kristo mwenyewe aliposema, “Upepo huvuma upendako, na sauti yake waisikia, lakini hujui unakotoka wala unakokwenda; kadhalika na hali yake kila mtu aliyezaliwa kwa Roho” (Yoh 3:8). Hatujui vizuri upepo unaovuma umetokea wapi na utasikika mpaka wapi; vilevile hatujui vizuri uvuvio wa Kimungu unaanzia wapi, na utatufikishia ngazi gani ya ukamilifu tukiufuata kwa uaminifu. Tusiwe kama wanamaji wazembe wasiotweka tanga wakati wa kufaa.
Vipaji vinatofautiana na maadili kama wanavyotofautiana wanaoviongoza, yaani Roho Mtakatifu na akili iliyoangazwa na imani; hiyo ni miongozo na kanuni tofauti. Utendaji wa kibinadamu unafuata kanuni ya kibinadamu, utendaji upitao maumbile unafuata kanuni ya Kimungu, yaani uvuvio wa Roho Mtakatifu. Hata busara iliyoinuliwa na upendo inatenda kwa kuzingatia mifuatano ya mawazo, tofauti na kipaji cha shauri kinachotuandaa kupokea uvuvio maalumu usioihitaji. Kwa mfano, tukiuliziwa siri fulani, busara inasita kuona namna ya kutunza siri hiyo bila ya kusema uongo, kumbe uvuvio wa Roho Mtakatifu unaondolea wasiwasi (taz. Math 10:19). Vilevile, imani inaambatana tu na kweli tulizofunuliwa, kumbe kipaji cha akili kinatuwezesha kuona vilindi vya kweli hizo, na kile cha hekima kinatuwezesha kuonja utamu wake.
2° Vipaji vya Roho Mtakatifu ni vya lazima kwa wokovu wa milele. “Maana Mungu humpenda yeye tu akaaye na Hekima” (Hek 7:28). “Miongoni mwa ndugu awatawalaye ana heshima, bali machoni pa Bwana ni wao wamchao” (YbS 10:20). Sasa kipaji bora ni hekima, na cha mwisho ni uchaji wa Mungu.
Maadili ya Kimungu yanajilinganisha na namna ya kibinadamu ya akili na utashi wetu, na hivyo yanatuacha katika hali isiyotosha kwa lengo letu kuu lipitalo maumbile, ambalo tunahitaji kulijua kwa namna hai, ya kuchimba na kuonja, na ambalo tunatakiwa kulilenga kwa ari zaidi. Imani hata ikiwa kubwa inaendelea kuwa na upungufu kwa sababu tatu za msingi: 1) yale inayoyaamini ni giza kwake, haiyaoni moja kwa moja, ila “kwa kioo kwa jinsi ya fumbo” (1Kor 13:12); 2) inayafikia kwa njia ya matamko mbalimbali ya Kanisa, kumbe Mungu ni sahili kabisa; 3) inayafikia kinadharia, kwa kukiri au kukanusha maneno fulanifulani, kumbe Mungu aliye hai anatakiwa kujulikana kama kwa mang'amuzi. Tumaini linashiriki upungufu wa imani, na vilevile upendo, kwa kuwa imani ndiyo inayoupatia la kupenda. Zaidi tena busara ina upungufu, kwa kuwa inahitaji kufuata mawazo, kutafuta sababu za kutenda, ili kuelekeza maadili ya kiutu; mara nyingi inasita isijue la kufanya, ikihitaji mwanga kutoka juu, k.mf. ili kushinda vishawishi visivyotambulikana au vikali na vya muda mrefu.
“Akili ya binadamu, hata baada ya kukamilishwa na maadili ya Kimungu, haiwezi kujua yale yote inayohitaji kuyajua, wala haiwezi kuepuka kila upotovu. Mungu tu aliye na ujuzi wote na enzi zote anaweza kufidia ujinga na upumbavu, ugumu wa moyo na kasoro nyinginezo tulizo nazo. Ili kutuondolea kasoro hizo tumejaliwa vipaji vya Roho Mtakatifu, vinavyotuwezesha kupokea vizuri uvuvio wa Kimungu... Kwa njia ya maadili ya Kimungu na ya kiutu, binadamu hajakamilika kuhusu lengo lake kuu linalopita maumbile asihitaji daima kusukumwa na Roho Mtakatifu kutoka juu”. Haja hiyo ni ya kudumu, ndiyo sababu vipaji ni misimamo ya kudumu tunayomiminiwa.
Sisi tunatumia vipaji kwa mfano wa utiifu, ili kupokea na kutekeleza vizuri agizo kutoka juu, lakini hatuwezi kuwa na uvuvio huo kila tunapotaka. Upande huo vipaji vinatufanya tusitende wenyewe, bali kwa Roho Mtakatifu. Hivyo ni wazi kuwa vipaji, kama vile utiifu, ni misimamo ya kudumu ya mwadilifu.
3° Kwa kuwa vipaji ni vya lazima kwa wokovu, vinashikamana na upendo. Roho Mtakatifu haji ndani mwetu pasipo vipaji vyake, ambavyo vinaendana na upendo na kupotezwa pamoja nao kwa dhambi yoyote ya [[mauti]. Basi, vipaji ni sehemu ya muundo wa Kiroho wa neema inayotia utakatifu, ambayo kwa sababu hiyo inaitwa “neema ya maadili na vipaji”. Kama vile maadili ya kumiminiwa yanavyokua pamoja kwa mfano wa vidole vya mkono, vipaji pia vinakua pamoja. Hakuna mwenye kiwango kikubwa cha upendo wa Mungu, inavyotakiwa na ukamilifu, asiye na vipaji vya Roho Mtakatifu kwa kiwango hichohicho.
Huo muundo wa Kiroho, ambao ni chanzo cha uzima wa milele, una thamani kubwa kuliko ile ya macho, ya afya na ya akili kwa maana mwadilifu akipotewa navyo hapotewi na hazina hiyo ambayo kifo chenyewe hakiwezi kumnyang'anya. Ni thamani kubwa kuliko ile ya karama (kufanya miujiza n.k.) kwa kuwa hizo ni alama za nje tu ambazo zinaweza kuelekeza njia ya kumfikia Mungu, lakini haziwezi kutuunganisha naye inavyofanya neema ya utakaso.
No comments:
Post a Comment