POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam
imeanzisha msako mkali, kuwatafuta watu waliohusika na mauaji ya
Mhasibu wa Kanisa Katoliki Parokia ya Makoka jijini Dar es Salaam, Sista
Cresencia Kapuri (50), ambao utahusisha vikosi vyote vya Polisi. Vikosi
hivyo ni Usalama Barabarani, askari wa doria wanaotumia pikipiki na
magari, wapelelezi na askari Polisi wa kawaida.
Mauaji ya mtawa huyo, yalitokea juzi mchana katika eneo la Ubungo Riverside,
jijini humo, ambapo alipigwa risasi na watu wanaodaiwa kuwa ni
majambazi na kumpora Sh milioni 20 pamoja na nyaraka mbalimbali za
ofisi.
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Mkoa wa Dar es Salaam, Suleiman
Kova, aliwaambia waandishi wa habari ofisi kwake jana kuwa Sista
Cresencia wakati anapigwa risasi, alikuwa ameongozana na wenzake, ambao
ni Sista Brigita Mbaga (32) na dereva wao Mark Mwarabu, aliyekuwa
akiendesha gari aina ya Toyota Hilux Pick-Up, yenye namba T213 CJZ.
Kova
alisema wakati watawa hao, wakitoka katika Benki ya CRDB Tawi la
Mlimani City, walipofika Ubungo Riverside kulipa deni la chakula katika
duka la Thomas Francis,
ndipo walitokea watu hao wawili wanaodaiwa kuwa ni majambazi wakiwa na
pikipiki, ambayo haikusomeka namba, huku mmoja akiwa na bunduki aina ya
SMG.
“Yule
dereva wa gari la masista walimpiga risasi katika kidole gumba cha
mkono wa kulia na kisha kumpiga mtawa huyo risasi ya kifuani na kupora
kiasi hicho cha fedha na nyaraka hizo,” alisema Kova.
Alisema
kuwa jambo kubwa walilogundua ni kuwa matukio mengi ya ujambazi, hasa
unaohusisha wananchi kuporwa kiasi kikubwa cha fedha, yanaanzia katika
mabenki, hivyo kuna uwezekano wa watu ambao si waaminifu, wanafanya
uhalifu huo.
Alisema kuwa katika matukio ya aina hiyo, majambazi huwafuatilia wateja wanapoingia au kutoka katika benki mbalimbali.
Alisema imeonekana kwamba mara nyingi benki, zinapohitaji kusafirisha pesa nyingi, hutumia askari au taasisi nyingine za usalama kusafirisha fedha zao.
No comments:
Post a Comment