Tuesday, June 24, 2014
Mtakatifu Gaspar mtume hodari wa Damu Azizi ya Yesu, rafiki na mtetezi wa wanyonge! (precios bloods fathers in Tanzania)
Yafuatayo ni mahubiri yaliyotolewa na Padre Reginald Mrosso, Mkuu wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Vikarieti ya Tanzania katika Maadhimisho ya Siku kuu ya Mtakatifu Gaspar del Bufalo, Mwanzilishi wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 21 Oktoba.
Katika Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki tunasoma hivi “Mungu aliye mkamilifu bila mpaka na mwenye heri ndani yake mwenyewe, katika mpango wa wema wake tu, alimwumba mtu kwa hiari yake apate kumshirikisha uzima wake wenye heri. Kwa sababu hiyo, wakati wote, na mahali pote yupo karibu na mwanadamu. Humwita mwanadamu na kumsaidia ili amtafute, amjue, na ampende kwa nguvu zake zote. Anawakusanya watu wote, ambao dhambi iliwatawanya, katika umoja wa familia yake, Kanisa. Ili apate kukamilisha hayo, wakati ulipotimia alimpeleka Mwanawe kama Mwokozi na Mkombozi. Ndani ya Mwanawe na kwa njia yake anawaita watu wafanyike kuwa wana wake katika Roho Mtakatifu, na hivyo wawe warithi wa uzima wake wenye heri”.
Mtume Petro – 1Pet. 1: 13-21 – anatuita tuiishi dhamiri hii. Sisi tunayo matumaini yanayotuhimiza tuwe watakatifu. Sisi tumekombolewa si kwa fedha au dhahabu, bali kwa DAMU YA KRISTO. Hivyo tuishi kama watakatifu kwa mfano wa Mungu aliyetuita katika imani.
Hapa tunatambua kuwa Mungu amekuja kati yetu na amekaa nasi na kila mmoja wetu anaalikwa kuishi na kuutangaza uzima huu mpya. Mtakatifu Gaspari del Bufalo alitambua vizuri kabisa mpango huu wa Mungu kwa ajili ya wokovu wa mwanadamu. Aliweka katika matendo ufahamu huo akitoa ushuhuda na hata kumwaga damu yake kama Kristo kwa ajili ya ndugu zake.
Leo tunakaa hapa pamoja kusali na kutafakari juu ya ukuu huu Mungu na upendo wake kwetu lakini zaidi pia tunatafakarishwa juu ya wajibu wetu mbele ya Mungu na watu wake.
Mtakatifu Gaspari alipoanzisha Shirika alichagua tasaufi ya Damu takatifu iwe karamu yetu ikiongozwa na vipengele vikuu vine – agano, kikombe, msalaba na upatanisho. Katika adhimisho la Jubilee kuu ya Mwaka 2015 Shirika limechagua maandalizi ya adhimisho hilo kuu kwa kufanya tafakari ya kina juu ya uwepo wake na ushuhuda wake hapa duniani. Maadhimisho kuelekea Jubilei hii kuu yalianza rasmi mwaka 2013 kuelekekea 2015 kwenye kilele – mambo ambayo tunayafanya:
Mwaka wa kwanza – 2012-2013 -Kuangalia historia yetu tulikotoka na uaminifu kwa karama yake.
Mwaka wa pili – 2013-2014 - Kuangalia wakati wetu wa sasa – ni kwa jinsi gani tunaishi karama ya upatanisho katika dunia ya leo.
Mwaka wa tatu – 2014-2015 - Kuangalia utume wetu – ni kwa namna gani tunaweza kutoa jibu kwenye kilio cha damu.
Leo tunakutana katika adhimisho la sadaka takatifu ya misa tukiwa pamoja na kama taifa la Mungu linaloamini uwepo wake Mungu Baba mwenyezi. Na dhamira yetu kuu mwaka huu ni upatanisho. Tunajiuliza je upatanisho maana yake nini? Upatanisho ni tendo la uponyaji. Ni tendo linalorudisha mahusiano kati yetu na Mungu na kati yetu.
Uwepo wa Kristo umeleta wokovu wa milele. Neno wokovu linaeleza dhana ya kuwekwa huru. Kwa kutupatanisha naye, tumepewa wajibu mpya kumtumikia Mungu mzima.
Zaburi ya 85 inatukumbusha tena wajibu wetu wa kutafuta upatanisho na Mungu na watu wake. Utuponye tena Ee Mungu, mwokozi wetu…. Wokovu wake ni karibu na wenye kumcha, utukufu wake utakaa katika nchi yetu, wema na uaminifu zitakutana, haki na amani zitabusiana. Uaminifu utachipuka katika nchi, na haki itachungulia kutoka mbinguni. Naye Bwana atatoa yaliyo mema, na nchi yetu itatao mazao, haki itatangulia mbele ya Bwana, wokovu utafuata nyayo zake.
Kama walivyofanya wana wa Israeli katika sala hii, wanamkubusha Mungu fadhila zake kwao na zikijumuisha msamaha wa hatia zao. Wanatambua makosa yao na wanaomba Mungu awajenge upya tena. Hapa baada ya kutoka utumwani wanatambua ubaya wa dhambi na balaa zake na wanataka kujijenga upya na kuanza upya katika yote. Wajibu wetu leo ni kujenga na kuendeleza huo ufalme mpya wa Mungu ulioletwa kwa njia ya Kristo na kanisa lake.
Baba Mtakatifu mwenye heri Yohani Paulo II katika mojawapo ya mafundisho yake anaeleza kuwa - ukombozi wa mwanadamu umefanyika kwa Kristo kumwaga damu yake. Kwake yeye sisi tumefanywa wana – Efe. 1:3…ametuchagua kabla ya kuumbwa ulimwengu ili tuwe wake. Na kwa njia yake tumepokea neema ya kuwa wana na kuwa watakatifu. Hii zawadi ya neema imeletwa kwetu kwa njia ya Kristo.
Na kwa namna hii Mungu Baba amefanya mageuzi makubwa kwetu – ukombozi toka utumwa wa dhambi, ukombozi kwa njia ya damu yake, msamaha wa dhamhi kwa neema yake na kuwa wana katika Mwanaye. Kifo cha Kristo msalabani, tendo kuu kabisa la upendo na umoja, humwaga kwetu mwanga mkuu na kutujalia busara ya kimungu.
Katika lugha ya kibiblia – akili au ufahamu huelezwa au kuonekana katika pendo na kwa maana hiyo pendo hutuingiza katika fumbo la mapenzi yake Mungu ambapo lengo lake ni wokovu – mwisho wake ukiwa ni kuunganisha yote mbinguni na duniani chini ya Kristo. Anahitimisha akisema au tukialikwa au tukimwomba Mungu atujalie neema ya kuona, kutafuta na kutafakari mema ya mbinguni na si ya hapa duniani.
Narudia tena, sisi ambao tumepatanishwa na Damu ya Kristo tumepewa wajibu mpya.
Mtume Paulo katika - 2Kor. 5:17-21 – basi mtu akiwa katika Yesu Kristo ni kiumbe kipya. Ya kale yamepita, mapya yamefika. Hayo yote yanatoka kwa Mungu. Yeye ametupatanisha naye kwa ujumbe wa Kristo, akatukabidhi sisi kazi ya usuluhishaji. Yaani, Mungu ameipatanisha dunia naye katika Kristo, kusudi asiwahesabie watu tena makosa yao. Akaliweka neno la upatanisho ndani yetu. Basi, tumekuwa wajumbe mahali pa Kristo, kwa maana ni Mungu anayeonya kwa huduma yetu. Na ombi tunalotoa kwa jina la Kristo ndilo mpatanishwe na Mungu. Yeye amemfanya yule asiyejua dhambi kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili na sisi tuwe uadilifu wa Mungu katika yeye.
Sisi leo kama Mtakatifu Gaspari tunaalikwa kutafakari vyema nguvu ya upendo wa Kristo aliyemwaga damu yake na akatupatanisha na Mungu. Tendo hili la Mungu ni pendo takatifu na hivyo basi sisi tunaomwamini Mungu tuna lazima ya kuingia katika falsafa hii ya wokovu. Huu ni utume wa Kanisa na kila mkristo. Sisi tumesamehewa makosa yetu kwanza na Mungu. Ni wajibu, ni lazima, si hiari. Je mimi, wewe, sisi ni sababu ya upatanisho?
Ili upatanisho utokee ni lazima mambo manne yawepo; ukweli, huruma, haki na amani. Na tujiulize sote tulioko hapa leo je tunazo sifa hizo katika maisha yetu.
Kristo kwa kumwaga damu yake ametukomboa toka mauti na kutupatanisha tena na Mungu Baba. Mara nyingi tunapofikiria kuhusu sakramenti ya upatanisho tunatingwa. Huwa tunatatizwa zaidi na ubaya au ukubwa dhambi zetu. Kwa hiyo tunakata tamaa, Kwa hakika tafakari yetu ingetakiwa itambue kwanza huruma ya Mungu ambayo ni kuu kuliko dhambi zetu.
Kama tutafikiria zaidi juu ya dhambi zetu na kuogopeshwa sana kama vile hutujapatanishwa naye Kristo, basi hatuna cho chote cha kuadhimisha, au cha kusherehekea au kinachotuwajibisha. Upatanisho hautatafutwa wala kupatikana. Tafakari yetu kuu na ya kwanza ni juu ya huruma ya Mungu isiyo na mwisho, isiyopunguka, na ikiwa hivyo basi tuna kila sababu ya kufurahi na kushangilia. Tufikirie kwa mfano Injili ya Luka sura 15: kondoo aliyepotea, shilingi iliyopotea, mwana mpotevu.
Fundisho hilo ni juu ya huruma kuu ya Mungu. Hata kama tumekata tama, Mungu husamehe, Mungu hufurahi na hukamilika katika kusamehe. Kristo amekufa ili kudhihirisha pendo hilo kuu la Mungu kwetu. Huo ndio upendo kamili.
Sisi tumekombolewa kwa Damu yake Kristo. Sisi tuliokuwa na dhambi tumekombolewa. Sisi ambao hatukustahili tena upendo wake Mungu, tumetakaswa kwa neema yake. Haijalishi wingi na ukubwa wa dhambi zetu, huruma ya Mungu ni kuu zaidi. Mungu ametupatanisha naye. Hiyo ndiyo furaha yetu. Somo la Injili latukumbusha uwepo wa majaribu lakini pia ipo nguvu ya ushindi kama tukibaki pamoja na Kristo. – katika somo la Injili sala ya Yesu kuhusiana na majaribu, wafuasi wanaahidi kushiriki kikombe cha mateso. Lakini baadaye unapatikana wokovu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
-
Mkoa wa Njombe ni moja kati ya mikoa Tanzania, ukiwa umeanzishwa rasmi mwaka 2012. Umepakana na mikoa ya jirani ya Morogoro, Ruvuma, Mbeya...
-
Mwandishi wa kitabu cha Kumbukumbu la Torati ambamo tunapata somo la kwanza anatualika kutambua kuwa Mungu haachi kutimiza ahadi yake ya ...
-
Isidore Bakanja, ambaye alitoa maisha yake kwa ajili ya imani ya Kikristo, Akiongozwa na maisha rahisi kama layman Katoliki wakati wa mauaj...
No comments:
Post a Comment