Nafasi Ya Mume Na Mke
Mungu amepanga kwamba familia ya Kikristo iwe katika mfumo fulani. Kwa sababu mfumo huo unaleta uthabiti katika maisha ya familia, Shetani hufanya kazi sana kupotosha mpango aliokusudia Mungu.Kwanza kabisa ni kwamba, Mungu amepanga mume awe kichwa cha familia. Hii haimpi mume ruhusa ya kutawala mke wake na watoto katika ubinafsi. Mungu amewaita waume kupenda, kulinda, kutimiza mahitaji na kuongoza familia zao kama kichwa. Pia, Mungu alikusudia wake wawe watiifu kwa uongozi wa waume zao. Hili ni wazi, kama Maandiko yanavyosema.
Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu. Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili. Lakini kama vile Kanisa limtiivyo Kristo, vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika kila jambo (Waefeso 5:22-24).Mume si kichwa wa mkewe kiroho – Yesu ndiye mwenye nafasi hiyo. Yesu ni kichwa wa kanisa kiroho, na mke wa Kikristo ni mshirika wa kanisa sawa na mume wake ambaye ni Mkristo pia. Ila, katika familia, mume Mkristo ndiye kichwa wa mke wake na watoto, nao wanapaswa kutii na kunyenyekea mamlaka yake hayo aliyopewa na Mungu.
Je, mke anapaswa kumtii mumewe kwa kiwango gani? Kama Paulo anavyosema, ni katika kila jambo. Wakati pekee anaporuhusiwa kuvunja sheria hiyo ni kama mume wake anamtaka kuvunja Neno la Mungu au kufanya kitu ambacho kinapinganana dhamiri yake. Ni wazi kwamba hakuna mume Mkristo atakayemtaka mke wake kufanya chochote kinachovunja Neno la Mungu au kwenda kinyume na dhamiri yake. Mume si Bwana kwa mkewe – Yesu tu ndiye mwenye nafasi hiyo maishani mwake. Kama itafikia uchaguzi kuhusu nani wa kumtii, anapaswa kuchagua kumtii Yesu.
Waume wanapaswa kukumbuka kwamba Mungu hayuko upande wao mara zote. Kuna wakati ambapo Mungu alimwambia Ibrahimu afanye kama alivyoambiwa na Sara mkewe (ona Mwanzo 21:10-12). Maandiko pia yanataja jinsi Abigaili alivyoacha kumtii Nabali mumewe, aliyekuwa mpumbavu, na kwa kufanya hivyo aliepusha tatizo (ona 1Samweli 25:2 – 38).
Neno La Mungu Kwa Wanaume
Mungu anawaambia hivi waume:Enyi waume, wapendeni wake zetu kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake… Vivyo hivyo imewapasa waume nao kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe, maana hakuna mtu anayeuchukia mwili wake popote; bali huulisha na kuutunza kama Kristo naye anavyolitendea Kanisa. Kwa kuwa tu viungo vya mwili wake. … Lakini kila mtu ampende mke wake kama nafsi yake mwenyewe; wala mke asikose kumstahi mumewe (Waefeso 5:25, 28-30, 33).Waume wanaagizwa kuwapenda wake zao kama Kristo anavyolipenda Kanisa. Si wajibu mdogo huo! Mke yeyote atajinyenyekeza kwa furaha kabisa kwa mtu anayempenda kama Yesu – aliyetoa uhai Wake kwa sababu ya upendo wa kujitoa. Sawa na jinsi Kristo anavyoupenda mwili Wake – yaani Kanisa – ndivyo na waume wanavyotakiwa kumpenda mwanamke ambaye ni “mwili mmoja” nao (Waefeso 5:31). Kama mume Mkristo anampenda mkewe kama anavyopaswa, atamtimizia mahitaji yake, atamtunza, atamheshimu, atamsaidia, atamtia moyo, na atatumia muda kuwa naye. Akishindwa katika wajibu wake kumpenda mkewe, mume huyo yuko hatarini kuzuia majibu ya maombi yake mwenyewe.
Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima kama chombo kisicho na nguvu na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe (1Petro 3:7. Maneno mepesi kukazia).Kihalisi ni kwamba hapajawahi kuwepo na ndoa isiyokuwa na kutokuelewana na shida mbalimbali. Ila, kwa kujitoa na kukuza tunda la Roho katika maisha yetu, waume na wake wanaweza kujifunza kuishi kwa maelewano na amani, na kufikia mahali pa kutambua baraka zinazozidi kuongezeka za ndoa ya Kikristo. Kila mwenzi anaweza kukua na kufikia ukomavu mkubwa katika kufanana na Kristo kutokana na matatizo yasiyoepukika yanayotokea katika ndoa zote.
Kwa maelezo zaidi juu ya wajibu na majukumu ya waume na wake, tazama Mwanzo 2:15-25; Mithali 19:13; 21:9, 19; 27:15, 16; 31:10-31; 1Wakor. 11:3; 13:1-8; Wakolosai 3:18, 19; 1Timo. 3:4, 5; Tito 2:3-5; 1Petro 3:1-7.
Tendo La Ndoa
Mungu ndiye mwanzilishi wa tendo la ndoa, na ni dhahiri kwamba aliliumba ili kustarehesha na kusaidia katika uumbaji. Pamoja na hayo, Biblia inatamka wazi kwamba tendo la ndoa ni la kufurahiwa na wale walioungana pamoja katika agano la ndoa, la kudumu.Kukutana kimwili nje ya mipaka ya ndoa huitwa zinaa au uasherati. Mtume Paulo alisema kwamba wale watendao mambo kama hayo hawataurithi ufalme wa Mungu (ona 1Wakor. 6:9-11). Ingawa Mkristo anaweza kujaribiwa na pengine kufikia kuanguka katika tendo la uzinzi au uasherati, atajisikia hatia kubwa sana rohoni mwake, itakayompelekea kutubu.
Paulo pia alitoa mafundisho wazi kabisa kuhusu majukumu ya mume na mke kwa mwenzake, kuhusu tendo la ndoa.
Lakini kwa sababu ya zinaa, kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke na awe na mume wake mwenyewe. Mume na ampe mkewe haki yake, na vivyo hivyo mke na ampe mumewe haki yake. Mke hana amri juu ya mwili wake, bali mumewe. Vivyo hivyo, mume hana amari juu ya mwili wake, bali mkewe. Msinyimane isipokuwa mmepatana kwa muda, ili mpate faragha kwa kusali; mkajiane tena, Shetani asije akawajaribu kwa kutokuwa na kiasi kwenu (1Wakor. 7:2-5).Mistari hii inaweka wazi kabisa kwamba tendo la ndoa lisitumiwe kama “zawadi” na mume au mke, maana hakuna mwenye mamlaka juuya mwili wake mwenyewe.
Tena, tendo la ndoa ni zawadi kutoka kwa Mungu. Si dhambi wala najisi inapokuwa katika ndoa. Paulo aliwatia moyo Wakristo wenye ndoa kushirikiana kimwili. Tena, tunapata ushauri huu kwa waume Wakristo katika kitabu cha Mithali:
Chemchemi yako ibarikiwe; nawe umfurahie mke wa ujana wako. Ni ayala apendaye na paa apendezaye; maziwa yake ytakutoshe siku zote; na kwa upendo wake ushangilie daima (Mithali 5:18, 19).[1]Kama wanandoa Wakristo wanataka kufurahia mahusiano kimwili yenye kutosheleza, waume na wake wanahitaji kuelewa kwamba kuna tofauti kubwa sana kati ya wanaume na wanawake kwa habari ya kushirikiana kimwili. Kiasili, mwanamume ni mtu wa kimwili sana kwa habari ya kukutana kimwili. Asili ya mwanamke kwa habari ya kukutana kimwili ni kitu cha hisia. Wanaume husisimka na kuwa tayari kukutana kimwili na mwanamke kwa kuona tu (ona Mathayo 5:28). Wanawake wao husisimka na kuwa tayari kukutana kimwili kwa mahusiano ya karibu sana, na kwa kuguswa na kushikwa-shikwa (ona 1Wakor. 7:1). Wanaume huvutiwa na wanawake wanaowapendeza macho; ila wanawake huvutiwa na wanaume wanaowapendeza kwa sababu zaidi ya kuvutia kimwili. Hivyo, wanawake wenye busara hupendeza ili kuwavutia waume zao wakati wote. Na waume wenye hekima huonyesha upendo wao kwa wake zao kutwa nzima kwa kuwakumbatia na kuwatendea mambo ya ukarimu, badala ya kuwatazamia wake zao “kuwa tayari” kwa ghafula wakati wa usiku.
Kiwango cha ashiki ya mwanamume kukutana kimwili na mwenzake huongezeka kulingana na kuongezeka kwa mbegu za uzazi katika mwili wake. Kiwango cha ashiki ya mwanamke huongezeka au kupungua kutegemeana na siku zake za mwezi. Wanaume wana uwezo wa kusisimka na kuwa tayari kukutana kimwili na mwanamke, na kufikia kilele cha tendo la ndoa baada ya muda mfupi sana – nukta chache tu au dakika, ila wanawake huchukua muda mrefu. Ingawa mwanamume yuko tayari kimwili kukutana na mwanamke upesi sana, mwili wa mwanamke unaweza usiwe tayari, mpaka baada ya nusu saa au zaidi. Basi, waume wenye hekima huchukua muda katika kuanza kuwasisimua wenzao kwa kuwapapasa, kuwabusu na kuwashika-shika sehemu za mwili ambazo zinasisimua, ili kumsababisha mwanamke kuwa tayari kukutana kimwili. Ikiwa hajui sehemu zinazohusika, amwulize. Tena, anapaswa kujua kwamba, japo yeye anaweza kufikia kilele cha tendo la ndoa mara moja tu, mwenzake anaweza kufikia kilele cha tendo la ndoa mara nyingi. Mume anapaswa kuhakikisha kwamba mwenzake anapokea anachotaka.
Ni muhimu sana kwa waume Wakristo na wake zao kuzungumza kuhusu mahitaji yao kwa uwazi, na kujifunza juu ya tofauti zao kiasi wanachoweza. Mahusiano kimwili kati ya waume na wake yanaweza kuwa baraka inayozidi kuongezeka kutokana na mawasiliano ya miezi mingi na miaka, na kugunduana na kuzoeana.
Watoto Wa Familia Ya Kikristo
Watoto wanapaswa kufundishwa jinsi ya kunyenyekea na kutii kabisa wazazi wao Wakristo. Wakifanya hivyo, wameahidiwa maisha marefu na baraka zao.Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana, maana hii ndiyo haki. Waheshimu baba yako na mama yako; amri hii ndiyo amri ya kwanza yenye ahadi, Upate heri, ukae siku nyingi katika dunia (Waefeso 6:1-3).Akina baba Wakristo kama vichwa wa familia zao, wanapewa wajibu wa msingi kabisa kwa ajili ya kuwafundisha watoto wao, hivi:
Nanyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu; bali waleeni katika adabu na maonyo ya Bwana (Waefeso 6:4).Ona kwamba wajibu wa baba ni wa namna mbili: kuwalea watoto wake katika adabu na maonyo ya Bwana. Hebu tuanze kwa kutazama haja ya kuwafundisha watoto adabu.
Nidhamu Ya Watoto
Mtoto asiyetiwa nidhamu atakapokuwa mtu mzima atakuwa mbinafsi na muasi kwa mamlaka. Watoto wanapaswa kutiwa nidhamu wakati wowote wanapoacha kwa makusudi kutii sheria halali zilizowekwa na wazazi wao. Watoto wasiadhibiwe kwa makosa au kutowajibika kwa sababu ya utoto. Lakini, watakiwe kukabiliana na matokeo ya makosa yao na kutowajibika kwao, na kwa njia hiyo kuwasaidia kujiandaa kwa ajili ya uhalisi wa maisha ya utu uzima.Watoto wadogo wanapaswa kuadhibiwa kwa kiboko, kama Neno la Mungu linavyofundisha. Lakini watoto wachanga wasipigwe viboko. Hii haina maana kwamba watoto wachanga waruhusiwe kufanya wanachotaka. Inatakiwa tangu wanapozaliwa wajue kwamba mama na baba ndiyo wenye mamlaka. Wanaweza kufundishwa wakiwa wadogo sana maana ya neno “hapana” kuwakuwakataza tu kufanya kitu wanachofanya, au wanachotaka kufanya. Wakianza kuelewa maana ya neno “hapana”, wanaweza kuchapwa kofi dogo tu matakoni ili kuwasaidia kuelewa vizuri zaidi wanapoendelea kufanya kile ambacho wazazi wanasema kisifanywe. Kama hayo yatafanyika kwa utaratibu na mara kwa mara, watoto watajifunza kuwa watiifu tangu umri mdogo sana.
Pia, wazazi wanaweza kuonyesha mamlaka yao kwa kutounga mkono tabia zisizotakiwa za watoto wao. Mfano ni kuwapa mara moja kitu wanachotaka, wakilia. Kufanya hivyo ni kuwafundisha watoto walie ili wapate matakwa yao. Au, kama wazazi watakubaliana na madai ya watoto wao kila mara wanaponuna au kukasirika ni kwamba wanawatia moyo kuendelea na tabia hiyo isiyotakiwa. Wazazi wenye hekima huunga mkono tabia nzuri tu katika watoto wao.
Kuchapa kiboko kusilete madhara kimwili, ila kusababishe maumivu ya kutosha kumfanya mtoto yule asiyetii kulia kwa muda kidogo. Kwa njia hiyo, mtoto atajifunza kuunganisha uchungu na kutokutii. Hata Biblia inaunga mkono hilo.
Yeye asiyetumia fimbo yake humchukia mwanawe; bali yeye ampendaye humrudi mapema. … Ujinga umefungwa ndani ya moyo wa mtoto; lakini fimbo ya adhabu itaufukuzia mbali. … Usimnyime mtoto wako mapigo; maana ukimpiga kwa fimbo hatakufa. Utampiga kwa fimbo, na kumwokoa nafasi yake na Kuzimu. … Fimbo na maonyo hutia hekima; bali mwana aliyeachiliwa humwaibisha mamaye (Mithali 13:24; 22:15; 23:13-14; 29:15).Wazazi wanaposimamia sheria zao, hawana haja ya kuwatisha watoto ili kuwafanya watii Mtoto anapoacha kutii kwa makusudi, achapwe fimbo. Ikiwa mzazi atatishia tu kumchapa mtoto wake ambaye si mtii, anachofanya ni kuunga mkono uasi wa mtoto wake. Matokeo ni kwamba mtoto anajifunza kutokujali utii mpaka vitisho vya wazazi wake vya maneno vinapofikia kiwango fulani cha sauti.
Baada ya kiboko, mtoto anapaswa kukumbatiwa na kuhakikishiwa upendo wa mzazi aliyemchapa.
Mlee Mtoto
Wazazi Wakristo wanapaswa kutambua kwamba wana wajibu wa kuwafundisha na kuwalea watoto wao, kama tunavyosoma katika Mithali 22:6, kwamba: “Mlee mtoto katika njia impasayo, naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee” (maneno mepesi kukazia).Kulea (au kufundisha) si kuadhibu tu mtoto anapoacha kutii, bali ni kumpongeza pia wakati anapofanya vizuri. Watoto kila wakati wanahitaji kusifiwa na wazazi wao ili kuunga mkono tabia zao njema, na mambo mazuri wanayofanya. Watoto wanahitaji kuhakikishiwa mara kwa mara kwamba wanapenda, wanakubalika na kufurahiwa na wazazi wao. Wazazi wanaweza kuonyesha upendo wao kwa kusifu, kuwakumbatia na kuwabusu watoto, na kwa kutumia muda mwingi nao.
“Kulea” maana yake “kufanya atii.” Basi, wazazi Wakristo wasiwape watoto wao uchaguzi kama watakwenda kanisani au kuomba kila siku au hapana. Watoto hawana ufahamu wa kutosha kujua kinachowafaa, au kilicho bora. Ndiyo sababu Mungu aliwapa wazazi. Wazazi watakaofanya bidii na kuweka juhudi na nguvu zao kuhakikisha kwamba watoto wao wanalelewa vizuri, wana ahadi kutoka kwa Mungu kwamba watoto wao hawataacha njia iliyo sawa hata wakiwa wakubwa, kama tulivyosoma katika Mithali 22:6.
Pia, watoto wanapaswa kuongezewa majukumu wanavyozidi kukua. Lengo la mzazi mwenye kufanikiwa ni kumwandaa mtoto hatua kwa hatua ili kuwajibika kabisa akiwa mtu mzima. Mtoto anapozidi kukua, apewe uhuru zaidi wa kujiamulia mambo yake mwenyewe. Tena, yule kijana mkubwa anapaswa kuelewa kwamba daima akubali wajibu utokanao na maamuzi yake, na kwamba wazazi wake hawatakuwepo siku zote “kumwokoa” katika matatizo.
Wajibu Wa Wazazi Kufundisha
Kama tusomavyo katika Waefeso 6:4, akina baba si tu kwamba wanawajibika kuwafundisha adabu watoto wao, bali pia wanatazamiwa kuwafundisha katika Bwana. Si wajibu wa kanisa kumpa mtoto mafundisho kuhusu maadili ya KiBiblia, tabia za Kikristo au theolojia – ni kazi ya baba. Wazazi wanaoachia wajibu wote kwa mwalimu wa Shule ya Jumapili awafundishe watoto wao kuhusu Mungu wanakosea sana. Mungu aliwaamuru Waisraeli hivi, kwa njia ya Musa:Na maneno haya ninayokuamuru leo yatakuwa katika moyo wako; nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii na kuyanena uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo (Kumbu. 6:6, 7. Maneno mepesi kukazia).Wazazi Wakristo wawafundishe watoto wao kuhusu Mungu tangu wakiwa wadogo, wakiwaambia Yeye ni nani na anawapenda kiasi gani. Watoto wadogo wafundishe habari za kuzaliwa kwa Yesu, maisha Yake, kifo na kufufuka Kwake. Watoto wengi wanaweza kuelewa ujumbe wa Injili wanapokuwa na umri wa miaka mitano au sita, na wanaweza kufanya uamuzi wa kumfuata Kristo. Baada ya hivyo (wakiwa na miaka sita au saba, na wakati mwingine hata wakiwa wadogo zaidi), wanaweza kupokea ubatizo wa Roho Mtakatifu na kunena kwa lugha kama ishara kwamba wamejazwa. Pamoja na hayo, hatuwezi kuweka sheria kuhusu jambo hili kwa sababu kila mtoto yuko tofauti. Ila hoja ni kwamba, wazazi Wakristo wanapaswa kutoa nafasi ya kwanza kwenye kuwafundisha watoto wao mambo ya kiroho.
Amri Kumi Za Kuwapenda Watoto Wako
1). Usiwatie watoto wako mahali pagumu (ona Waefeso 6:4). Watoto wasitazamiwe kutenda kama watu wazima. Ukitazamia mengi kupita kiasi kutoka kwa watoto wako, wataacha kujitahidi kukupendeza maana wanajua haiwezekani.2). Usilinganishe watoto wako na watoto wengine. Wajulishe jinsi unavyofurahia sifa zao za kipekee na karama au vipaji vyao kutoka kwa Mungu. Wakubali wao kama wao.
3). Wape majukumu nyumbani, ili wajue kwamba wao ni sehemu muhimu sana ya familia hiyo. Kufanikiwa ni matofali yanayojenga kujiamini katika maisha ya mtu.
4). Tumia muda kuwa na watoto wako. Hiyo inawajulisha kwamba wao ni wa maana kwako. Kuwapa vitu haichukui nafasi ya wewe kujitoa kwao. Tena, watoto hushawishiwa zaidi na wale wanaokaa nao muda mwingi.
5). Ikibidi useme kitu kibaya, jaribu kukisema kwa uzuri. Mimi sikuwahi kuwaambia watoto wangu kwamba ni “wabaya” walipoacha kunitii. Badala yake, nilikuwa namwambia hivi kijana wangu, “Wewe ni mtoto mzuri, na watoto wazuri hawafanyi ulichofanya!” (Kisha nilikuwa namchapa kiboko.)
6). Tambua kwamba, neno “hapana” linamaanisha “ninakujali”. Watoto wanaporuhusiwa mambo yao kila wakati wanatambua kwama hujali kiasi cha kutosha kuwakataza chochote wakati wowote.
7). Tazamia watoto wako kukuiga wewe. Watoto hujifunza kwa mifano ya wazazi wao. Mzazi mwenye busara hawezi kumwambia mtoto wake, “Fanya ninavyokwambia. Usifanye kama ninavyofanya mimi.”
8). Usiwaokoe watoto wako na matatizo yao yote. Ondoa mawe yanayoweza kuwakwaza tu; acha mawe ya kukanyagia yabakie mbele yao.
9). Mtumikie (na kumfuata) Mungu kwa moyo wako wote. Nimeona kwamba watoto wa wazazi waliopoa kiroho huwa hawamfuati Mungu wakiwa watu wazima. Watoto Wakristo wa wazazi ambao hawajaokoka, na watoto wa wazazi Wakristo waliojitoa kabisa kwa Mungu huendelea na wokovu hata “wakiondoka kwenye kiota” – nyumbani.
10). Wafundishe watoto wako Neno la Mungu. Mara nyingi wazazi hutoa nafasi ya kwanza kwa elimu ya watoto wao, na kushindwa kuwapa elimu ya muhimu zaidi wanayoweza kupata – elimu ya Biblia.
Nafasi Ya Huduma, Ndoa Na Familia
Pengine kosa kubwa la kawaida kabisa lifanywalo na viongozi wa Kikristo ni kutokujali ndoa zao na familia zao kwa sababu ya kujitoa kwenye huduma. Wanajihesabia haki kwa kusema kwamba kujitoa kwao “ni kwa ajili ya kazi ya Bwana.”Kosa hili hurekebika wakati mtumishi anayefanya wengine kuwa wanafunzi anapotambua kwamba utii wake halisi na kujitoa kwake kwa Mungu huonekana kwa mahusiano yake na mke wake na watoto. Mtumishi hawezi kudai kwamba amejitoa kwa Mungu ikiwa hampendi mke wake kama Kristo anavyolipenda kanisa, au kama atapuuzia kutumia muda unaotakiwa na watoto wake, ili kuwalea na kuwakuza katika kicho na kumcha Bwana.
Tena, kumpuuza mwenzi na watoto kwa sababu ya “huduma” ni ishara ya huduma ya kimwili kabisa, inayofanywa kwa nguvu za mtu binafsi. Wachungaji wengi wenye makanisa wanaobeba mizigo mizito ni mfano wa hili, maana wanajichosha ili kuhakikisha kwamba kila utaratibu wa kanisa unakwenda vizuri.
Yesu aliahidi kwamba mzigo Wake ni mwepesi na nira Yake ni laini (ona Mathayo 11:30). Hamwiti mtumishi yeyote kuonyesha anavyopenda dunia au anavyolipenda kanisa kwa kutowapenda watu wa familia yake. Sifa mojawapo ya mzee ni kwamba, “awe mwenye kuisimamia nyumba yake vema” (1Timo. 3:4). Mahusiano yake na familia yake ni kipimo cha uwezo wake kufanya huduma.
Wale walioitwa kufanya huduma za kusafiri na ambao inawabidi kuwa nje ya nyumbani mara kwa mara lazima watumie muda wa ziada kufikiri kuhusu familia zao wanapokuwa nyumbani. Washirika wengine katika mwili wa Kristo wafanye kinachowezekana ili kufanikisha hilo. Mtumishi anayefanya wengine kuwa wanafunzi anatambua kwamba watoto wake mwenyewe ndiyo wanafunzi wake wa kwanza. Akishindwa hapo, hana haki ya kujaribu kuwafundisha wengine walio nje ya nyumbani mwake kuwa wanafunzi.
No comments:
Post a Comment