Monday, January 12, 2015

Mwongozo wa Sinodi ya Maaskofu kuhusu Familia arehe 4 hadi tarehe 25 Oktoba 2015

Mama Kanisa ameanza hija kuelekea maadhimisho ya Sinodi ya kumi na nne ya kawaida ya Maaskofu itakayofanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 4 hadi tarehe 25 Oktoba 2015 kwa kuongoza na kauli mbiu “Wito na Utume wa Familia katika Kanisa na Ulimwengu mamboleo”.
Read More
Hili ni tukio muhimu sana linaoonesha umoja na mshikamano wa Mama Kanisa na ni mwendelezo wa maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu iliyofanyika Mwezi Oktoba 2014.

Kwa sasa, hiki ni kipindi cha kusali, kutafakari na kushirikisha mang’amuzi mbali mbali, kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu. Tayari Sekretarieti kuu ya Sinodi imekwisha kutuma Mwongozo kwa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki, Sekretarieti ya Vatican, Taasisi na wadau mbali mbali wanaojibidisha katika kutangaza Injili ya Familia duniani. Mwongozo huu ni matunda ya Hati ya Mababa wa Sinodi maalum ya Maaskofu. Tafakari, maoni na ushauri kutoka kwa Familia ya Mungu, yanapaswa kuifikia Sekretarieti kuu ya Sinodi tarehe 15 Aprili 2015, ili kuandaa Hati ya Kutendea kazi, “Instrumentum Laboris”.

Mwongozo umeandikwa kwa mfumo wa maswali, kwa kuuliza swali na msingi, Je, hati hii inaelezea ukweli wa maisha ya familia katika jamii ya wakati huu au kuna mambo ambayo hayakupewa kipaumbele na hivyo kusahaulika? Mambo ambayo yanapaswa kuingizwa katika tafakari ya Mababa wa Sinodi? Maswali yaliyoulizwa yanapania kutoa fursa kwa Mabaraza ya Maaskofu kujadili kwa kina na mapana ukweli kuhusu maisha ya familia.

Kuhusu hali ya kijamii na kitamaduni, Waamini wanahamasishwa kuchunguza kwa umakini mkubwa, ikiwa kama Kanisa mahalia linashirikishwa kikamilifu katika mbinu mkakati wa kuendeleza tunu msingi za maisha ya kifamilia, ili kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza dhidi ya tamaduni za watu mahalia. Waamini wanaulizwa ikiwa kama Kanisa linaonesha ukweli katika kukabiliana na changamoto za nyakati hizi; mbinu gani ziweze kutumika ili kuzuia mmong’onyoko wa tunu msingi za maisha ya kifamilia.

Je, Kanisa linaweza kuzisaidia namna gani familia kuweza kutekeleza dhamana na wajibu wake katika jamii ambayo imemezwa mno na malimwengu, kiasi hata cha kudharau mtindo asilia wa maisha ya ndoa unaofumbatwa katika upendo thabiti kati ya Bwana na Bibi katika Sakramenti ya Ndoa kwa lengo la kuendeleza kizazi?

Makanisa mahalia yanahimizwa kuangalia ni kwa jinsi gani Wakleri wanavyoweza kufundwa, ili kuweza kuzisaidia familia za Kikristo kushuhudia ukuu wa upendo katika maisha ya ndoa kwa vijana wa kizazi kipya. Waamini wanaombwa kuangalia kwa kina na mapana changamoto za kichungaji, hasa zaidi miongoni mwa watu wanaoishi nje ya mfumo wa maisha ya Kikristo au kati ya watu ambao hawajabatizwa.

Injili ya Familia haina budi kutazamwa mintarafu miwani ya Maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kama ambavyo Mababa wa Sinodi katika ujumbe wao walivyokazia, kama sehemu ya mchakato unaopania kuonesha utimilifu wa wito na utume wa Familia. Hapa swali msingi ni kuhusu dhamana na nafasi kwa wachungaji kutumia Maandiko Matakatifu katika kuibua mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji kwa kuonesha ujasiri na uaminifu.

Waamini wanaswalishwa ni kwa jinsi gani wanavyoweza kushuhudia tunu msingi za maisha ya ndoa na familia? Ni dhambi gani inapaswa kuepukwa? Ni changamoto zipi ambazo wachungaji wanakabiliana nazo katika kukuza uelewa na ukomavu, ili hatimaye, wanandoa watarajiwa waweze kufunga Sakramenti ya Ndoa; kwa kutambua na kuthamini umuhimu, uzuri na udumifu wa kifungo cha Sakramenti ya Ndoa, ili kuvuka kikwazo cha mapungufu yanayojitokeza katika kukuza mahusiano kati ya wanandoa na mahusiano na Mwenyezi Mungu.

Mababa wa Sinodi wanawauliza waamini, Je, wanaweza kufahamu namna gani dhamana na utume wa Familia katika Mpango wa Kazi ya Ukombozi? Je, wachungaji wanaweza kuwasaidia kwa kiasi gani wanandoa kutambua kwamba, Sakramenti ya Ndoa si kizingiti bali ni uzoefu wa utimilifu wa maisha ya Ndoa katika kukuza na kudumisha dhamana na utume wa kimissionari katika familia sanjari na kuendeleza dhamana ya Uinjilishaji.

Mwongozo wa Sinodi unawauliza waamini ni kwa namna gani wanaweza kusaidiwa kuyafahamu Mafundisho ya Kanisa kuhusu Familia, ili kuondokana na uwili ambao unaoweza kujitokeza kati ya k ile ambacho waamini wanakiri pamoja na uhalisia wa maisha yao. Hapa waamini wanapaswa kufahamu kwa kina umuhimu wa kifungo cha Sakramenti ya Ndoa kwamba ni udumifu na mshikamano wa dhati kati ya wanandoa unaopania kuwapatia furaha na utimilifu wa mtu binafsi katika maisha ya ndoa.

Mababa wa Sinodi wanakiri kwamba, Ndoa na Familia si suala tu la ukweli na uzuri wake. Familia nyingi zinaandamwa na madonda makubwa pamoja na madhaifu; mambo ambayo yanalihamasisha Kanisa kuwasaidia na kuwasindikiza kwa njia ya huruma, uvumilivu bila kubeza tunu msingi za Kiinjili. Je, waamini wanaweza kufahamu ni kwa jinsi gani hakuna mtu ambaye anatengwa na huruma pamoja na upendo wa Mungu? Je, ukweli huu unaweza kumwilishwa namna gani katika shughuli na mikakati ya Kiinjili; Je, waamini wanaweza kushirikishwa kwa namna gani zaidi ili kufahamu tunu msingi za kiutu na kimaadili zinazojitokeza katika mifumo mbali mbali ya ndoa, ili kuweza kufikia utimilifu wa maisha ya Sakramenti ya Ndoa ya Kikristo.

Mababa wa Sinodi wanawataka waamini kuzama zaidi na kuendeleza mambo msingi yaliyoibuliwa na kujadiliwa wakati wa Maadhimisho ya Sinodi Maalum ya Maaskofu, kama chachu ya mwamko mpya wa kutangaza kwa ujasiri zaidi Injili ya Familia. Waamini wanaulizwa, Je, Familia zinahusishwa kikamilifu katika kuwafunda Mapadre au hata katika kukuza mchakato wa ushirikiano kwa ajili ya huduma kati ya Kanisa na Serikali, Taasisi za Kisiasa na Kijamii katika ngazi ya kitaifa na kimataifa. Waamini wanaulizwa, Je, ni kitu gani kifanyike ili kukuza na kudumisha ushirikiano wa pande hizi mbili pamoja na kusimama kidete kupinga mambo yote yanayosigana na tunu msingi za maisha ya ndoa na familia katika masuala ya: kitamaduni, kiuchumi na kisiasa!

Maandalizi ya wanandoa watarajiwa pamoja na kuwasindikiza wanandoa wapya katika maisha yao ya ndoa; ni mambo ambayo yanahitaji kufanyiwa upembuzi yakinifu, ili kuliwezesha Kanisa kufanya tafakari ya kina kama sehemu ya maboresho ya kuwahusisha Wanajumuiya katika maandalizi ya maisha ya ndoa na familia. Mwongozo unatoa angalisho pia kwa ajili ya waamini wanaoishi katika ndoa za Serikali au wale ambao wanaishi katika kile kinachoitwa “uchumba sugu”.

Haya ni mambo ambayo kimsingi yanapata chimbuko lake katika masuala ya kitamaduni, sababu za kiuchumi; mapokeo au vijana wa kizazi kipya kushindwa kufanya maamuzi magumu kuhusu kifungo cha ndoa hadi kifo kitakapowatenganisha. Mababa wa Sinodi wanauliza, Je, waamini wanaweza kusaidiwa namna gani ili kutambua na kukumbatia ukweli huu katika maisha yao?

Mababa wa Sinodi wanasema kuna haja ya kuwa na sanaa ya kuwasindikiza waamini katika maisha ya Kikristo ili hatimaye, waweze kufikia utimilifu pamoja na kuzihusisha familia za Kikristo kubeba Msalaba wa kuwasaidia wanafamilia ambao wanakumbana na madonda makubwa katika maisha na utume wao. Mababa wa Sinodi wanaangalia ni kwa jinsi gani ambavyo pale ambapo familia zimeonesha mpasuko mkubwa wa kiimani, ndoa inaweza kuvunjwa. Je, Kanisa linaweza kuwahudumia na kuwasaidia namna gani wanandoa walioachana na kuamua kuoa au kuolewa tena. Je, hawa wanaweza kusaidiwa kwa namna gani ili kuondokana na vizuizi hivi ambavyo wakati mwingine si muhimu sana?

Mwongozo wa Sinodi unawauliza Maaskofu, Je, Kanisa linaweza kuwasaidia kwa namna gani watu wenye mwelekeo ushoga na usagaji; wanaohitaji huduma za kichungaji mintarafu Mwanga wa Injili; watu wenye mahusiano na familia ambao kimsingi wanahitaji kuangaliwa kwa jicho la kichungaji?

Mwishoni, Mwongozo wa Sinodi, unajikita katika dhamana ya kuendeleza maisha kama tunu msingi ya wito na utume wa familia. Hapa Mababa wa Sinodi wanauliza ni kwa jinsi gani wanafamilia wanaweza kuendeleza majadiliano katika ukweli na uwazi kuhusiana na masuala ya: sayansi ya maadili maumbile; namna ya kuasili watoto pamoja na madhara yanayojitokeza kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Mababa wa Sinodi wanawauliza Maaskofu, Je, wanaweza kuwasaidia wazazi kwa kiasi gani ili kuwarithisha watoto wao imani, mintarafu utambulisho wa Kikristo; Je, wanaweza kutekeleza kwa kiasi gani wajibu huu msingi, ili dhamana ya malezi iweze kupata mwangwi hata katika maisha ya kisiasa na kijamii.

No comments:

Post a Comment

NCHI YANGU FAHARI YANGU TOUR