Thursday, February 12, 2015

Askofu mteule wa jimbo la Shinyanga amekiri Kanuni ya Imani na kula kiapo cha utii kwa Kanisa anapotekeleza dhamana na wajibu wake wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu,


Askofu mteule Liberatus Sangu wa Jimbo Katoliki Shinyanga, Jumanne tarehe 10 Februari 2015 katika Ibada ya Liturujia ya Neno la Mungu, iliyoongozwa na Askofu mkuu Savio Hon Tai-Fai, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu amekiri Kanuni ya Imani na kula kiapo cha utii kwa Kanisa anapotekeleza dhamana na wajibu wake wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu, huku akiwa ameungana na Maaskofu wenzake.
Read More..............  
Ibada hii imehudhuriwa pia na Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu mkuu mwambata na Rais wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa pamoja na baadhi ya Watu wa Familia ya Mungu kutoka Tanzania. Ibada hii imeadhimishwa kwenye Kikanisa cha Mwenyeheri Kardinali Newman kilichoko kwenye Makao Makuu ya Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, mahali ambapo kwa kawaida Maaskofu wateule wanakiri na kula kiapo cha utii kwa Kanisa.
Katika kiapo cha utii, Askofu mteule Sangu ameahidi kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa Kanisa; kulinda amana ya Mafundisho ya Kanisa na kuwasaidia wale wote wanaokengeuka kuufahamu ukweli wa imani ya Kanisa Katoliki. Atajitahidi kuwa ni Mchungaji mwema, akifuata mfano wa Yesu Kristo Kuhani mkuu. Atasimamia nidhamu kadiri ya Sheria za Kanisa na Kanuni katika maadhimisho ya Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa.
Askofu mteule Sangu ameapa kwamba, atasimamia mali ya Kanisa kwa uaminifu na kuonesha upendo na mshikamano wa pekee na Mapadre pamoja na Mashemasi ambao ni wasaidizi wake wa karibu na kwamba, atajitahidi kukuza na kuendeleza miito mitakatifu ndani ya Kanisa; pamoja na kuhamasisha ari na moyo wa shughuli za kimissionari zinazotekelezwa na Watawa mbali mbali Jimboni mwake. Mwishoni, atawajibika kwa Baba Mtakatifu na Baraza la Maaskofu Katoliki katika utekelezaji wa majukumu yake kadiri ya Sheria za Kanisa.

No comments:

Post a Comment

NCHI YANGU FAHARI YANGU TOUR