Baba Mtakatifu Francisko amemteua Monsinyo Liberatus Sangu kutoka Jimbo Katoliki la Sumbawanga, kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Shinyanga, Tanzania. Kabla ya uteuzi wake, Askofu mteule Sangu alikuwa ni Afisa mwandamizi katika Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu mjini Vatican.
Askofu mteule Liberatus Sangu alizaliwa kunako tarehe 19 Februari 1963, Kijijini Mwazye, Jimbo Katoliki la Sumbawanga. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi kwenye Seminari kuu la Kibosho, Jimbo Katoliki Moshi na Segerea, Jimbo kuu la Dar es Salaam, akapadrishwa kunako tarehe 9 Julai 1994.
Katika maisha yake kama Padre, Askofu mteule Sangu amewahi kuwa Mlezi wa Seminari ndogo ya Kaengesa, Jimbo Katoliki la Sumbawanga kuanzia mwaka 1994 hadi mwaka 1995. Akateuliwa kuwa Paroko wa Parokia ya Matai kuanzia mwaka 1995 hadi mwaka 1996. Kati ya Mwaka 1996 hadi mwaka 1999 alikuwa mjini Roma kwa masomo ya juu na kujipatia shahada ya Uzamili katika taalimungu ya Sakramenti za Kanisa, kutoka katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Mtakatifu Anselmi, kilichoko mjini Roma.
Kuanzia mwaka 1999 hadi mwaka 2000, aliteuliwa kuwa Msimamizi wa Parokia ya Mwanzye. Kuanzia mwaka 2000 hadi mwaka 2007 akateuliwa kuwa ni Mkurugenzi wa miito Jimbo Katoliki la Sumbawanga; mlezi katika mwaka wa malezi na mkurugenzi wa utume wa vijana, Jimbo Katoliki Sumbawanga. Kunako mwaka 2007 hadi mwaka 2008 aliteuliwa kuwa Paroko wa muda Parokiani Sopa. Kuanzia mwaka 2008 hadi uteuzi wake, amekuwa akitekeleza utume wake kama Afisa mwandamizi, Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu mjini Vatican.
Itakumbukwa kwamba, Jimbo Katoliki la Shinyanga, Tanzania kuanzia mwaka 2012 limekuwa wazi kufuatia kifo cha Askofu Aloysius Balina.
No comments:
Post a Comment