Friday, October 16, 2015

Deo Filikunjombe afariki dunia kwenye ajali ya Chopa

 Tanzia : Deo Filikunjombe afariki dunia kwenye ajali ya Chopa
Aliyekuwa mbunge wa jimbo la Ludewa, Deo Filikunjombe ambaye alikuwa anatetea nafasi hiyo kupitia chama cha Mapinduzi(CCM), amefariki kwenye ajali ya helikopta iliyotokea jana usiku ndani ya Pori la Akiba la Selous lililopo eneo la Kilombero mkoani Morogoro. Filikunjombe ni mmoja wa abiria wanne waliokuwa ndani ya chopa hiyo ambao wamethibitishwa kupoteza maisha. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jerry Silaa,Meya wa Manispaa ya Ilala anayemaliza muda wake, Capt.William Silaa baba mzazi wa Jerry ndiye aliyekuwa rubani wa chopa hiyo ambaye naye amepoteza maisha. “Kwa masikitiko makubwa nimepokea taarifa rasmi kutoka kwa timu ya uokoaji imefanikiwa kufika eneo la ajali na kukuta abiria wote na rubani wamepoteza maisha,” ilisomeka sehemu ya taarifa ya Jerry Silaa. “Nimepoteza Baba na rubani mzuri wa nchi yetu Capt.William Silaa,nimepoteza rafiki na kiongozi wangu Mhe.Deo Filikunjombe. Nawapa pole wote waliopoteza ndugu zao. Nawaombea marehemu mapumziko ya Amani.” “Nawashukuru wote walioshirikiana na familia kusaidia uokozi,” . “Namshukuru Mhe.Rais Jakaya M Kikwete, Dr.John Pombe Magufuli, IGP Ernest Mangu, Katibu Mkuu MU Dr.Meru, Kampuni ya Everest Aviation ,Wabunge, MaDC, Maafisa wa TCAA na wote walioshiriki kuwatafuta wahanga wa tukio hili,” ilimaliza sehemu ya Taarifa ya Silaa Wakati Taifa bado likiwa limeshikwa na butwaa kutokana na vifo vya aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara Dr Abdallah Kigoda, aliyezikwa jana na siku hiyohiyo kutokea kifo cha Dr Emanuel Makaidi, Mwenyekiti wa NLD na mgombea ubunge jimbo la Masasi, leo tena Taifa linaamka na kushuhudia kumpoteza kijana shupavu aliyekuwa miongozi mwa wabunge mahiri kuwahi kutokea ndani ya chama cha Mapinduzi, Deo Filikunjombe. Ni misiba..misiba..misiba, hakika uchaguzi wa mwaka huu unatengeneza historia ya aina yake na ya kuhuzunisha. Filikunjombe anakuwa mgombea ubunge wa sita kufariki ndani ya kipindi kisichozidi majuma sita. Mungu ailaze roho yake mahali pema, AMEN

No comments:

Post a Comment

NCHI YANGU FAHARI YANGU TOUR