Friday, October 16, 2015

Lowassa atuma salamu za rambirambi kifo cha Filikunjombe

 Lowassa atuma salamu za rambirambi kifo cha Filikunjombe
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA), Edward Lowassa ametuma salamu za rambirambi kwa chama cha Mapinduzi(CCM) na familia ya aliyekuwa mbunge/mgombea wa jimbo la Ludewa Deo Filikunjombe aliyefariki pamoja na watu wengine watatu katika ajali ya Helikopta iliyotokea jana jioni maeneo ya mbuga ya Selous mkoani Morogoro.
Helikopta hiyo iliyokuwa inaongozwa na Kapt.William Silaa(marehemu) ilidaiwa kupata hitilafu na baadae kupoteza mawasiliano jana jioni ilipokuwa safarini kutoka Dar es salaam kuelekea Njombe.
Helikopta hiyo ilianguka kwenye mbuga ya Selous na kupelekea vifo vya watu wote wanne waliokuwemo.
“Filikonjombe alikuwa Mbunge mahiri aliyesimama imara kutetea maslahi ya wananchi wa jimbo lake la Ludewa na watanzania kwa ujumla,” amesema Lowassa.
“Alikuwa mwiba kwa serikali ya Chama chake CCM kutetea maslahi ya nchi, mfano ni katika kashfa ya Escrow ambapo alikuwa Makamu Mwenyekiti wa kamati iliyochunguza kashfa hiyo.”
“Mwenyezimungu awape moyo wa subira, familia, jamaa, marafiki na wananchi wa Ludewa, katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na mpendwa wao,” amesema Lowassa.
Ni pigo lingine kubwa ambalo katika kipindi kifupi Taifa limepata, huku bado likiwa na kidonda cha kuondokewa na wanasiasa wengine mahiri,Mchungaji Christopher Mtikila, Celina Kombani, Dr Abdallah Kigoda na Dr Emanuel Makaidi aliyefariki jana
Kwa mujibu wa Zitto Kabwe, ambaye ndiye msimamizi wa mazishi ya Filikunjombe, amesema miili ya marehemu wote wanne imehifadhiwa katika Hospitali ya jeshi Lugalo kwa ajili ya kufanyiwa utambuzi na madaktari kutokana na miili hiyo kuwa katika hali mbaya ya kuungua.
Baada ya utambuzi huo, taratibu za mazishi zitaendelea.

No comments:

Post a Comment

NCHI YANGU FAHARI YANGU TOUR