Thursday, January 7, 2016

BONDE LA MTO MSIMBAZI(bomoa bomoa kuendelea)

BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limesema kazi ya ubomoaji nyumba zilizoko katika Bonde la Mto Msimbazi itaendelea leo katika maeneo ambayo hayako kwenye zuio lililotolewa na Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam,  Mkurugenzi Mkuu wa NEMC,  Bonaventure Baya,   alisema zuio lililopo mahakamani linahusu nyumba 681 tu, hivyo wataendelea na kazi  katika maeneo yote  yaliyobaki.
Alisema mpango wa ubomoaji wa majengo  katika bonde hilo ulianzishwa na serikali kwa lengo la kusafisha bonde na mto huo na mazingira yanayozunguka ili kunusuru maisha ya wananchi kupanua uwezo wa mto huo.
“Bonde la Msimbazi halifai kwa ujenzi wa makazi kwa kuwa kuna madhara ambayo ni pamoja na mafuriko ya mara kwa mara, uchafuzi wa mto huo unahatarisha afya za wananchi kutokana na taka nyingi na zikiwemo majitaka toka viwandani na makazi ambayo hutupwa katika bonde hilo,” alisema Baya.
Akizungumzia sababu ya Serikali kufanya ubomoaji huo alisema, Serikali ilishachukua hatua mbalimbali katika miaka ya nyuma ikiwemo ya kuwapa waathirika wa mafuriko viwanja  mbadala  katika eneo la Mabwepande pamoja na vifaa vya ujenzi, lakini baadhi ya wananchi waliviuza na kurejea mabondeni.
“Zoezi hili ni la kitaifa litafanyika kwa nchi nzima kwa awamu mbalimbali kwa kuwa kuna uharibifu mkubwa unaondelea hususani katika mito kutokana na uchimbaji holela wa mchanga na madini, utupaji majitaka toka katika makazi na viwandani hali inayosababisha maji ya mito kuwa na sumu,” alisema Baya.
Mkurugenzi huyo wa NEMC, alizitaja sekta za Serikali zinazohusika katika kazi hiyo ni pamoja na taasisi yao ambayo ipo chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Idara ya Mipango Miji, halmashauri za manispaa za Dar es Salaam,  Idara ya Misitu, Jeshi la Polisi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Idara ya Usalama wa Taifa.
Wakati hayo yakiendelea jana maofisa wa NEMC waliuweka alama ya X katika nyumba 300 kuanzia eneo la Kipawa hadi Gongolamboto.

No comments:

Post a Comment

NCHI YANGU FAHARI YANGU TOUR