Tuesday, May 6, 2014

Dominika ya 4 ya pasaka mwaka “A”. tarehe 11/05/2014

JUMAPILI DOMINIKA YA 4 ya Pasaka ya Mwaka A.
      RATIBA ZA IBADA 
KIGANGO CHA MH. ISIDORI BAKANJA- BOKO.
MISA YA KWANZA 12:15-2:00 ASUBUHI
MISA YA PILI     SAA 2:00-4:00 ASUBUHI
MISA YA TATU SAA 4:00-5:30 ASUBUHI
KIGANGO CHA MT. FRANCIS WA ASIZ-MBWENI 
MISA YA KWANZA SAA 1:10-3:00 ASUBUHI
MISA YA PILI SAA 3:00-4:30 ASUBUHI

KIGANGO CHA MT. RAFAEL-MBWENI MALINDI
SAA 1:00-3:00 ASUBUHI.
MISA YA PILI SAA 3:00-5:00

KIGANGO CHA ANTHONY WA PADUA-MBWENI TETA
MISA NI SAA 3:00-5:00.


SOMO 1. Mdo.2:14a, 36 – 41
Siku ya Pentekoste Petro akasimama pamoja na wale kumi na mmoja, akapaza sauti yake, akawaambia, basi nyumba yote ya Israel na wajue yakini ya kwamba Mungu amemfanya Yesu huyo mliyemsulubisha kuwa Bwana na Kristo. Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na Mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu? Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie. Akawashuhudia kwa maneno mengine mengi sana na kuwaonya, akisema, jiokoeni na kizazi hiki chenye ukaidi. Nao waliolipokea neon lake wakabatizwa; na siku ile wakaongezeka wata wapata elfu tatu.


WIMBO WA KATIKATI; Zab. 23:1-6

(Kitikio)
Bwana ndiye mchungaji wangu sitopungukiwa na kitu au Aleluya


SOMO 2: 1Pet. 2:20b – 25
Kustahimili, mtendapo mema na kupata mateso, huu ndiyo wema hasa mbele za Mungu. Kwa sababu ndio mlioitiwa; maana Kristo naye aliteswa kwa ajili yenu, akawaachia kielelezo, mfuate nyanyo zake. Yeye hakutenda dhambi, wala hila haikuonekana kinywani mwake. Yeye alipotukanwa, hakurudisha matukano; alipoteswa, hakuogopa; bali alijikabidhi kwake yeye ahukumuye kwa haki. Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu yam ti; ili, tukiwa wafu kwa mambo ya dhambi, tuwe hai kwa mambo ya haki; na kupigwa kwake mliponywa. Kwa maana mlikuwa mnapotea kama kondoo; lakini sasa mmemrudia Mchungaji na Mwangalizi
wa roho zenu.



 SHANGILIO. Yn. 10:14
Mimi ndimi mchungaji mwema; nao walio wangu nawajua; nao walio wangu wanijua mimi
Aleluya


INJILI.:Yn. 10:1-10
Yesu aliwaambia Wayahudi, Amin, amin, nawaambieni, Yeye asiyeingia mlangoni katika zizi la kondoo, lakini akwea penginepo, huyo ni mwizi naye ni mnyang’anyi. Aingiaye mlangoni ni mchungaji wa kondoo. Bawabu humfungilia huyo, na kondoo humsikia sauti yake; naye huwaita kondoo wake kwa majina yao, na huwapeleka nje. Naye awatoapo nje kondoo wake wote, huwatangulia; na wale kondoo humfuata, kwa maana waijua sauti yake. Mgeni hawatamfuata kabisa, bali watamkimbia; kwa maana hawazijui sauti za wageni. Mithali hiyo Yesu aliwaambia; lakini wao hawakuelewa na mambo hayo aliyowaambia. Basi Yesu aliwaambia tena, Amin, amin, nawaambieni, Mimi ndimi mlango wa kondoo. Wote walionitangulia ni wevi na wanyang’anyi; lakini kondoo hawakuwasikia. Mimi ndimi mlango; mtu akiingia kwa mimi, ataokoka; ataingia na kutoka, naye atapata malisho. Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kasha wawe nao tele.


Mdo - kitabu cha Matendo ya Mitume
1Pet - kitabu cha waraka wa kwanza  wa mtu Petro kwa watu wote
Yn -  kitabu cha muinjili Yohana.

Na Abel Reginald……………….niwatikieni maandalizi mema ya Dominika


usikose kuhudhuria kwenye kikao cha Halmashauri ya VIWAWA Parokia ya Boko mara baada ya Misa ya kwanza Kigangoni Rafael 

Tuesday, April 29, 2014

MASOMO YA JUMAPILI DOMINIKA YA 3 YA MWAKA A TAREHE 04/05/2014

JUMAPILI DOMINIKA YA 3 ya Pasaka ya Mwaka A.
      RATIBA ZA IBADA 
KIGANGO CHA MH. ISIDORI BAKANJA- BOKO.
MISA YA KWANZA 12:15-2:00 ASUBUHI
MISA YA PILI     SAA 2:00-4:00 ASUBUHI
MISA YA TATU SAA 4:00-5:30 ASUBUHI
KIGANGO CHA MT. FRANCIS WA ASIZ-MBWENI 
MISA YA KWANZA SAA 1:10-3:00 ASUBUHI
MISA YA PILI SAA 3:00-4:30 ASUBUHI

KIGANGO CHA MT. RAFAEL-MBWENI MALINDI
SAA 1:00-3:00 ASUBUHI.
MISA YA PILI SAA 3:00-5:00

KIGANGO CHA ANTHONY WA PADUA-MBWENI TETA
MISA NI SAA 3:00-5:00.


MASOMO 

SOMO 1:Mdo.2:14,22-28
Petro alisimama pamoja na wale kumi na moja,akapaza sauti yake, akawaambia, enyi watu wa Uyahudi, ninyi nyote mkaao Yerusalemu, lijueni jambo hili, mkasikilize maneno yangu, Yesu wa Nazareti, mtu aliyedhihirishwa kwenu na Mungu kwa miujuza na ajabu na ishara, ambazo Mungu alizifanya kwa mkono wake kati yenu, kama ninyi wenyewe mnavyojua; mtu huyu aliotolewa kwa shauri la Mungu lilikusudiwa, na kwa kujua kwake tangu zamani, ninyi mkamsulubisha kwa mikono ya watu wabaya, mkamwua; ambaye Mungu alimfufua, akaufungua uchungu wa mauti, kwa sababu haikuwezekana ashikwe nao. Maana Daudi ataja habari zake. Nalimwona Bwana mbele yangu siku zote, kwa kuwa yuko upande wa mkono wangu wa kuume, nisitikisike. Kwa hiyo moyo wangu ukapendezewa, ulimi wangu ukafurai; tena mwili wangu nao utakaa katika matumaini. Kwa maana hutaiacha roho yangu katika kuzimu; wala hutamtoa mtakatifu wako aone uharibifu. Umenijulisha njia za uzima; utanijaza furaha kwa uso wako.

SOMO 2: 1Pet. 1:17-21
Ikiwa unamwita Baba, yeye ahukumuye kila mtu asipo upendeleo, kwa kadri ya kazi yake, enendeni kwa hofu katika wakati wenu wa kukaa hapa kama wageni. Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhambi; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa Baba zenu; bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo. Naye amejulikana kweli tangu zamani, kabla haijawekwa misingi ya dunia; lakini alifunuliwa mwisho wa zamani kwa ajili yenu; ambao kwa yeye mmekuwa wenye kumwamini Mungu, aliyemfufua katika wafu akampa utukufu; hata Imani yenu na tumaini lenu liwe kwa Mungu.

INJILI. :Lk. 24:13-35
Siku ile watu wawili miongoni mwa wafuasi wa Yesu walikuwa wakienda kijiji kimoja, jina lake Emau, kilichokuwa mbali na Yerusalemu kama mwendo wa saa mbili. Nao walikuwa wakizungumza wao kwa wao habari za mambo hayo yote yaliyotokea. Ikawa katika kuzungumza na kuulizana kwao Yesu mwenyewe alikaribia, akaandamana nao. Macho yao yakafumbwa wasimtambue. Akawaambia, ni maneno gani haya tangu yalipotendeka mambo haya; tena wanawake kadha wa kadha wa kwetu walitushitusha, walivyokwenda kaburini asubuhi na mapema, wasiuone mwili wake; wakaja wakasema ya kwamba wametokewa na malaika waliosema kwamba yu hai. Na wengine walikuwa pamoja nasi walikwenda kaburini wakaona vivyo hivyo kama wale wanawake walivyosema, ila yeye hawakumwona. Akawaambia, enyi msiofahamu, wenye mioyo mizito ya kuamini yote waliyoyasema manabii! Je! Haikupasa Kristo kupata mateso haya na kuingia katika utukufu wake? Akaanza kutoka Musa na manabii wote, akawaeleza katika maandiko yote mambo yaliyomhusu yeye mwenyewe. Wakakaribia kile kijiji walichokuwa wakienda, naye alifanya kama anataka kwendelea mbele. Wakamshawishi wakisema, kaa pamoja nasi, kwa kuwa kumekuchwa, na mchana unakwisha. Akaingia ndani kukao nao. Ikawa alipokuwa ameketi nao chakulani, alitwaa mkate, akaubariki, akaumega,akawapa.yakafumbuliwa macho yao, wakamtambua; kasha akatoweka mbele yao. Wakaambiana, je! Mioyo yetu haikuwaka ndani yetu hapo alipokuwa akisema nasi njiani, kutufunulia maandiko? Wakaondoka saa ile ile, wakarejea Yerusalemu,wakawakuta wale kumi na moja wamekutanika, wao na wale waliokuwa pamoja nao, wakisema, Bwana amefufuka kweli kweli, naye amemtokea Simoni. Nao waliwapa habari ya mambo yale ya njiani, na jinsi alivyojitambulisha nao katika kuumega mkate.


  1.  form za ziara ya uinjilishaji parokia ya Dareda na ziara ya mbuga ya wanyama ya ngorongoro zipo tayari na nafasi zimebaki chache wahi sasa nafasi ikiwa kama kijana mkatoliki askari kamili wa Yesu,...twende tuungane pamoja katika kumtangaza yeye aliye njia ya uzima na ukweli mchango na tshs 180,000 tu na mwisho wa kupokea michango ni tarehe 18/06/2014.
  2. tunawakumbusha vijana wote kuendelea kulipa ada kwa maendeleo ya chama chetu..... mapendo sana malipo kwa njia ya benk kwa jina na number hii :viwawa parokia ya boko account no 01524526820100 crdb bank tegeta branch
JIANDAE NA ZIARA YA UINJILISHAJI MWAKA 2014.....................

Tuesday, March 25, 2014

Ujumbe wa Kwaresima Mwaka 2014 Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania




kwa wasomaji wa Blog yetu tunawaletea ujumbe wa Kwaresima kwa Mwaka 2014 kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania unaoongozwa na kauli mbiu "Ukweli utawaweka huru. Yn. 8:32". Maaskofu wanazungumzia kuhusu umuhimu wa wongofu wa kweli unaomweka mwamini huru; wajibu wa kuuishi, kuulinda na kuusimamia ukweli kishuhuda mintarafu hali halisi ya Tanzania.

UTANGULIZI

Wapendwa Taifa la Mungu,


“Ukweli utawaweka huru”. Safari ya maisha ya mwanadamu ni safari ya kutafuta uhuru, uhuru ambao unamfungua mtu kutoka katika minyororo inayomfunga na kumfanya kuwa mhudumu wa mazingira na hali yake. Chimbuko la uhuru wa kweli ni Mungu mwenyewe katika mpango wake wa milele na huruma yake ya milele. Mungu ndiye asili na chanzo cha uhuru wa kweli na tunafanywa kuwa huru kweli pale tunapoamua kwa dhati kuupokea ukweli utokao kwa Mungu. Mungu ndiye ukweli wenyewe: “Ukweli wowote, bila kujali anayeusema, unatoka kwa Roho Mtakatifu”, na popote tunapoukuta ukweli huo ni mali ya Mungu.


Wapendwa Taifa la Mungu, tunapoanza safari ya Kwaresima ya mwaka huu, sisi Maaskofu wenu, tungependa kuwakumbusheni ninyi na watu wote wenye mapenzi mema juu ya umuhimu wa kuishi katika ukweli. Kuuishi ukweli na kuishi maisha yaliyojengwa juu ya msingi wa ukweli ni kushiriki hasa maisha ya Mungu. Kama tunataka kujenga jamii yenye utu, haki, amani, upendo na mshikamano wa kweli, ni lazima tuanze kwanza kujenga dhamiri zinazothamini na kuuenzi ukweli. Pasipo ukweli jamii itasambaratika kwa sababu itakuwa imejengwa bila msingi.


Wapendwa Taifa la Mungu, Ukweli utawapeni uhuru kwa kuwa toka kuumbwa kwa ulimwengu, Mungu aliye ukweli wenyewe alipanga na kunuia kwamba mwanadamu aliyemuumba kwa sura na mfano wake, aishi katika uhuru kamili akimiliki na kuutiisha ulimwengu wote (Mwa 1:28 ). Ni katika ukweli tunamjua, tunampenda na kumtumikia Mungu. Ni katika ukweli tunadhihirisha kuwa tumeitwa kuwa wana huru katika ufalme wa Baba wa milele.


Ukweli na uhuru ni dhana zinazoenda pamoja. Penye ukweli pana uhuru na penye uhuru pana ukweli. Kama vile mtu huru awezavyo kuuishi ukweli kwa kuwa uhuru wake humfanya ajitegemee kifikra, kimaamuzi na kiutendaji ndivyo pia jamii ya watu na hata taifa huru liwezavyo kujitegemea kifikra, kimaamuzi na kiutendaji.


Kwa maisha, kifo na ufufuko wa Kristo, waamini wamewekwa huru na wanaitwa kuutafuta na kuusimamia ukweli. Waamini wanaalikwa kuutafuta, kuujua na kuulinda ukweli katika nyanja zote za maisha.


SURA YA KWANZA
WONGOFU WA KWELI HUTUWEKA HURU


Mungu alipenda kujifunua kwa wanadamu kupitia manabii na mwanawe wa pekee Bwana wetu Yesu Kristo. Hata leo, Roho Mtakatifu analiongoza Kanisa katika kuendelea kuujua ukweli wa kiimani katika safari ya pamoja ya kiroho kuelekea uhuru kamili wa roho zetu. Ukweli wa kiimani huleta uhuru wa kiroho. Mwaka uliopita Kanisa liliadhimisha Mwaka wa Imani ikiwa ni sehemu ya kuwakumbusha wanakanisa wote juu ya wajibu wao wa kiimani katika Kanisa na katika jamii.

Kwa kuishi ipasavyo imani yetu ya kikristo tunashiriki wajibu wa kuujenga Ufalme wa Mungu ambao mojawapo ya nguzo zake saba za msingi ni ukweli! Hakika, ufalme wa Mungu, kama Mama Kanisa anavyotangaza katika utangulizi wa Misa ya sherehe ya Kristo Mfalme ni ufalme wa UZIMA na KWELI, ufalme wa NEEMA na UTAKATIFU, ufalme wa HAKI, MAPENDO na AMANI. Mungu wetu ni UKWELI na ni MKWELI. Tunasadiki na kukiri kwamba hadaganyi wala hadanganyiki. Imani ni wajibu wa kushiriki kuujenga Ufalme wa Mungu, ufalme ambao msingi wake ni ukweli, kwa sababu Mungu ni ukweli.

Mwanadamu aliyekombolewa kwa damu ya thamani kubwa sana ya Kristo iliyomwagika pale Kalvari, amepata kurudishiwa hadhi ya kuwa mwana huru wa Mungu akikombolewa kutoka utumwa wa dhambi. Uhuru anaoupata mwanadamu una gharama kubwa na thamani kubwa. Uhuru wa kweli ni uhuru ndani ya Mungu; ni uhuru katika Mungu. Uhuru wa kweli huambatana na utii wa sheria ya Mungu na uwajibikaji unaodai unyenyekevu na nidhamu ya hali ya juu. Uhuru huu ni kinyume na uhuru usio na mipaka ambao jamii ya sasa inadai,uhuru ambao hupingana na malengo ya Muumba na taratibu na miongozo halali mbele za Mungu iliyowekwa na jamii.
Kanisa, ukweli na uhuru

Kanisa ambalo ni ishara ya wokovu na alama ya uwepo hai wa Kristo aliye njia, ukweli na uzima katika ulimwengu wa sasa ni sisi tulioalikwa kuwa Familia ya Mungu. Kwa kumkiri Kristo na kwa kubatizwa kwetu tumekuwa Rafiki na wadau wake Yesu Kristo (Yn 15: 14). Kwa namna hiyo sisi sote Familia ya Mungu – Wakleri, Watawa na Waumini Walei – tu chombo mikononi mwa Kristo kwa kushiriki kikamilifu kazi ya Kristo ya kuwakomboa watu.

Kwa mantiki hiyo, Kanisa linao wajibu wa kwanza kabisa kuulinda ukweli, kuusimamia, kuushi na kuutangaza. Kanisa ni chombo kiletacho wokovu kwa ulimwengu na kuwaweka huru wanadamu walio katika utumwa unaojidhihirisha katika sura mbalimbali kama vile, umasikini, ufisadi, rushwa, ushirikina, magonjwa, siasa chafu, kutokuwajibika, ubinafsi,nk.

Kanisa ni chombo cha Kristo cha kuwaletea watu uhuru wa kweli. Roho wa Bwana, aliye juu ya Yesu (Lk 4:18,19) yuko pia juu ya Kanisa lake ambalo analituma kuwafungulia watu vifungo vyao mbalimbali na kuwaachia huru waliosetwa (Lk 4:18-19).

Ukweli kama tunu ya kimungu lazima uote mizizi katika mioyo ya wanadamu walioumbwa kwa sura na mfano wake (Kut 1:26). Ni wajibu wa kila mwanadamu kuutafuta ukweli na kuujua. Kwa njia ya ufahamu, mwanadamu anaalikwa kuutafuta ukweli kwani ndio njia pekee ya kumweka huru na kuufikia wokovu. Maana Mungu amemwachia mwanadamu uhuru kusudi aifuate nia yake (YBS 14:15), na hivyo amtafute Muumba wake kwa hiari, na hatimaye aufikie ukamilifu ulio bora na wenye heri, pasipo shuruti na kwa kuambatana na Mungu. Kanisa linamsaidia mwandamu kufanikisha kuufikia ukweli na kwa uhuru kupitia neema za Mungu.



SURA YA PILI
WAJIBU WA KUUISHI, KUULINDA NA KUUSIMAMIA UKWELI KISHUHUDA

Waamini waliowekwa huru na Kristo, wanao wajibu wa kuujua ukweli, kuutafuta, kuulinda na kuusimamia kwa lengo la kuleta huru wa kweli kwa manufaa ya wote. Huko ndiko kuwa mfuasi wa Kristo aliyesema: “Mimi nilikuja ulimwenguni; ili niishuhudie kweli. Kila aliye wa hiyo kweli hunisikia sauti yangu” (Yn 18:38).

Jamii leo hii imegawanyika juu ya uhuru ambao wanajamii wanapaswa kuwa nao. Wazazi wanaamini kuwa uhuru ni kutenda jambo lolote bila kubughudhiwa na yeyote, hata kama tendo hilo ni kinyume na misingi ya maadili. Watoto wanataka uhuru binafsi katika kupanga na kuamua mambo yanayowahusu. Watoto wasingependa kupokea malezi na maelekezo iwe ni ya wazazi au ya jamii. Vijana wanapenda kuamua mambo yao kama wanavyoona, wakipuuzia uzoefu na ushauri wa wakubwa wao. Tujiulize: Je, huu ndiyo uhuru tuutafutao? Katika mazingira kama haya kinachotafutwa si uhuru bali kuishi kwa kuheshimu vionjo binafsi. Ni muhimu sana kwa wanafamilia kuwa na uhuru wa pamoja katika kupanga na kuamua masuala kifamilia.

Tukijiruhusu kama wanajamii kuishi katika uholela upendo unatoweka. “Usikubali kitu chochote kuwa ni ukweli kama kinakosa upendo. Na usikubali kitu chochote kuwa ni upendo kama kinakosa ukweli! Hali moja bila nyingine ni uongo unaoharibu”. Kwa sababu “ni katika ukweli tu ndipo upendo inang’aa, ni katika ukweli tu ndipo tunapoweza kuuishi upendo kwa hakika”.
SURA YA TATU
HALI HALISI YA TAIFA LETU


Taifa lenye umri wa miaka 50 ya uhuru ni taifa lililokwishavuka uchanga. Ni taifa kijana lililo katika umri wa kujenga juu ya misingi iliyowekwa kwa manufaa ya wote. Ni taifa linalojitegemea. Bila msingi huo, mengine yote, hata kama yanaonekana yanang’aa yatakuwa yanasaliti mustakabali wa kweli wa taifa letu. Tusijidanganye. Bila msingi wa kujitegemea na kutafuta manufaa ya wote (common good) taifa hili litaanguka. Kama halianguki leo, kesho ni lazima litaanguka. Tunajiuliza, uko wapi ujasiri wa Taifa letu? Imepotelea wapi fahari ya kujitawala, si kisiasa tu, bali kiuchumi, kifikira na kijamii? Imepotelea wapi ile mbegu ya uzalendo iliyopandwa na waasisi wa taifa letu? Imeishia wapi heshima ya kuthamini utu, kuheshimu imani ya asiyeamini kile nisichokiamini na kutafuta ufumbuzi halisi wa matatizo yanayotukabili?


Tumepoteza dira ya kujitegemea kimaamuzi na kimkakati. Tumefikia mahali pa kuamini kwamba maendeleo yataletwa kwa kaulimbiu zinazobadilika badilika kila siku. Katika mazingira ya sasa, watu wachache, kwa sababu binafsi na kwa manufaa binafsi wanapotosha ukweli na kutafuta njia za kulinda maslahi yao kwa kutumia mifumo isiyokubalika, lakini inayosimikwa na kuhalalishwa ili kulinda maslahi binafsi. Hali hii inajidhihirisha kupitia matumizi mabaya ya madaraka, mikataba mibovu, kupindisha sheria, kufumbia macho uhalifu, nk. Uhuru wa kweli haujengeki katika misingi dhaifu ya ubinafsi na haulengi kumfanya mtu yeyote yule awe juu ya sheria za haki na taratibu za uadilifu. Na kimsingi, hakuna maendeleo ya kweli kama watu hawaheshimu haki ya msingi ya kuujua ukweli na kuishi kadiri ya ukweli huo.

Katika mazingira kama haya Kanisa haliwezi kukaa pembeni na kutazama tu kwa sababu nalo lina wajibu wa kuijenga jamii. Kanisa lina wajibu wa kuangalia, kuboresha na kuikosoa mienendo ya kijamii na kisiasa inayohatarisha ustawi wa jamii nzima na hivyo kuathiri kazi ya Kristo ya kumkomboa mwanadamu na kuusimika Ufalme wa Mungu; ufalme unaojidhihirisha katika kutamalaki kwa ukweli, haki na amani. Kanisa litaendelea kusisitiza ukweli huu kwamba; “Ili kuunda maisha ya kisiasa yaliyo kweli ya kibinadamu, hakuna lililo bora zaidi kuliko kustawisha ndani ya watu hisia za haki, upendo na huduma kwa manufaa ya wote”. Hapa tungependa kuelezea mambo machache yanayoivuruga nchi yetu.
Uvunjifu wa amani

Taifa letu linazidi kupoteza tunu bora ya amani ambayo waasisi wa taifa letu wametuachia. Katika siku za karibuni yamekuwepo matukio ya mauaji, watu kumwagiwa tindikali kwa sababu ya imani yao au visasi na hata mauaji kwa kutumia mabomu. Uhasama wa kidini na matukio ya kijasusi na ugaidi dhidi ya raia yanaonekana kushamiri. Kumekuwapo na matumizi makubwa ya nguvu upande wa vyombo vya dola vikitumia silaha za moto na za kivita. Wimbi la wananchi kutotii sheria na taratibu za nchi linakua. Tunakwenda wapi?

Amani lazima ilindwe ndani na nje ya mipaka ya nchi yetu. Hata hivyo, amani sio tunu inayojitegemea peke yake kwa kuwa amani ya kweli inazaliwa ndani ya mioyo yenye kujali misingi ya utu, haki, heshima, ukweli na umoja. Fikra tofauti na hizo, huzaa mioyo potofu, na mioyo potofu haiwezi kutoa amani.
Rushwa na madawa ya kulevya

Mapambano dhidi ya rushwa na madawa ya kulevya yamegeuka kuwa wimbo unaochosha kwa sababu hakuna dhamira ya dhati ya kuitokomeza. Uongozi wa juu unapotamka hadharani kuwafahamu watoa rushwa, wapokea rushwa na wafanyabiashara wa madawa ya kulevya lakini hakuna hatua zozote zinazochukuliwa ni hali inayotisha sana. Wakati umefika ambapo lazima tuwe wakweli kuhusu mapambano dhidi ya rushwa na madawa ya kulevya. Hatuwezi kuwa huru kuhusu rushwa na madawa ya kulevya kama hatujawa wakweli kuhusu mapambano dhidi ya rushwa na madawa ya kulevya. Wanaopiga vita rushwa majukwaani, ndio wanaoomba na kupokea nje ya jukwaa. Isitoshe rushwa ndiyo ngazi waliyoitumia na wanayoitumia kufika jukwaani. Katika mazingira kama haya hatujengi Taifa bali tunalibomoa na historia itatuhukumu. Hatuna budi kuunda misingi imara ya utawala bora. Tukumbuke daima kuwa utawala bora bila uwajibikaji na kuwajibishana ni kiini macho.
Kukua kwa matabaka katika jamii

Tofauti kubwa sana za kiuchumi zinazidi kupanua utengano wa kimatabaka kati ya wenye nguvu za kiuchumi na wasio na kitu. Wenye nguvu kiuchumi sasa wanamiliki uchumi, wanamiliki siasa na hatima ya fukara, na kwa fedha wananunua haki ya wanyonge.


Mgawanyo mbovu wa rasilimali za nchi unatisha. Ardhi inamilikiwa na wachache kwa kivuli cha uwekezaji mkubwa huku wananchi wakiahidiwa ajira kwa kuwa vibarua kwenye mashamba hayo badala ya kuwezeshwa kumiliki ardhi na kuitumia kwa faida. Haya ni masuala yanayomtia hofu mtu yeyote anayejali na kuthamini mustakabali wa taifa letu.
Siasa kuingilia weledi

Tatizo la siasa kutawala mifumo ya ujenzi wa misingi ya maendeleo linakua kwa kiwango cha kutia hofu. Kwa mfano, siasa na wanasiasa wanaathiri mfumo wa utoaji wa elimu nchini kiasi cha kulifanya taifa hili kuwa kama taifa lisilojali mustakabali wake. Yamekuwepo maneno mengi na mipango ya zimamoto isiyofanyiwa utafiti wa kina na utendaji umekuwa hafifu sana. Uthabiti katika kusimamia utekelezaji wa mipango ya maendeleo hauonekani na badala yake porojo zimetawala. Imejitokeza hali ya wale waliopewa dhamana ya kusimamia masuala ya elimu kwa mfano kukosa unyenyekevu wa kuwasikiliza na kushauriana na wataalamu katika nyanja hizi. Kila mara zinaibuka sera ambazo msingi wake ni ubunifu usiozingatia weledi na hivi kuifanya elimu kudidimia.
Mchakato wa Katiba mpya

Katiba kama moyo wa taifa ni chombo kinachopaswa kutengeneza misingi ya mfumo wa maisha mazima na uhai wa Taifa letu. Ukweli wote na uhuru wote wa Taifa unabebwa na Katiba. Iwapo mchakato wa katiba mpya hautaendeshwa kwa ukweli na uhuru, hatutaweza kupata katiba yenye kubeba ukweli na uhuru wote kuhusu taifa letu. Tunarudia tena kutamka kuwa zoezi hili adhimu na la muhimu kwa mustakabali wa Taifa limeharakishwa mno. Sasa tunaona zoezi zima limehodhiwa na wanasiasa. Mchakato wa katiba mpya unadai kuwepo kwa fadhila ya kijamii ya kutafuta manufaa ya wote (common good). Katiba si mali ya wanasiasa bali ni mali ya wananchi. Tunapenda kuialika jamii yote kuitendea haki nchi yetu. Tukae chini na tuzipime kila hatua zetu katika zoezi hili na tuone kama zinakidhi kipimo cha «Hekima, Umoja na Amani». Hekima ituongoze kulinda umoja wa Taifa letu na utuepushe na kishawishi cha kubaguana na kutengana. Kwa kuzingatia hilo umoja huo utatuongoza katika njia ya amani.

Uharibifu wa mazingira

Tishio kubwa la kimaangamizi kwa vizazi vijavyo linatokana na ukweli kuwa kumekuwepo na uharibifu mkubwa wa mazingira. Maendeleo yanagharama yake. Kiu ya kweli ya maendeleo ni lazima iambatane na ulazima wa kuwa makini katika kutunza mazingira na uthabiti wa uumbaji. Vyanzo vya maji na kingo za mito zimeharibiwa kwa kuruhusu shughuli za kilimo kufanyikia maeneo hayo, kwa kuruhusu makazi ya watu, viwanda kujengwa na kuruhusu takataka ya sumu kutoka viwandani na migodini kutiririkia kwenye vyanzo vya maji, nk. Ukataji wa miti umeshamiri na baadhi ya misitu ya asili imepotea. Kwa sababu hiyo tumechangia sana katika kusababisha mabadiliko ya tabia nchi ambayo athari zake sasa zinajionesha waziwazi. Ukame, njaa, mafarakano kati ya wakulima na wafugaji na kuenea kwa jangwa ni vitisho vilivyo dhahiri mbele yetu. Huu ni ukweli kuwa tumeshindwa kuzingatia agizo la Mungu la kuitawala na dunia kuutiisha ulimwengu. Tunahitaji sasa kubadilika ili ukweli utawale, tupate uhuru kamili kwa kuwajibika kuyalinda na kuyatunza mazingira kwa faida ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.
Ni wajibu wetu Waamini Wakatoliki kuulinda ukweli na kuusimamia kiushuhuda. Jitahada za namna hii zina gharama yake kwa kuwa zinahitaji ujasiri wa kinabii na utayari wa kuteseka na hata ikibidi kutoa sadaka kubwa ya uhai.
HITIMISHO

Wapendwa Taifa la Mungu, tunapenda kuwahimiza kwa maneno haya tukisema: “Inunue kweli, wala usiiuze. Naam, hekima na mafundisho na ufahamu” (Mith 23:23). Ukweli ni msingi wa lazima na unapaswa kuwa wa kudumu kwa tendo lolote ili liweze kuitwa kuwa ni adilifu. Ukweli unapaswa kuzijenga dhamiri zetu ili kumsaidia mwanadamu kupata mwanga unaofukuza mikanganyiko.


Katika ulimwengu usiojali ukweli, uhuru unapoteza msingi wake na mwanadamu anakuwa mhanga wa vurugu ya vionjo na kutawaliwa kwa hila, iliyojidhihirisha waziwazi au iliyojificha. Hivi ni mwaliko kwetu sote “tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, Kristo” (Efe 4:15). Kwa sababu upendo “haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli” (1Kor 13:6).










Ni sisi Maaskofu wenu,

Mhashamu Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Iringa
Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Dar es Salaam
Mhashamu Askofu Mkuu Josaphat Lebulu, Arusha
Mhashamu Askofu Mkuu Paul Ruzoka, Tabora
Mhashamu Askofu Mkuu Yuda Thaddaeus Ruwa’ichi, Ofm Cap, Mwanza,
Mhashamu Askofu Telesphor Mkude, Morogoro
Mhashamu Askofu Gabriel Mmole, Mtwara

Mhashamu Askofu Bruno Ngonyani, Lindi
Mhashamu Askofu Anthony Banzi, Tanga
Mhashamu Askofu Agapiti Ndorobo, Mahenge
Mhashamu Askofu Evaristo Chengula, IMC, Mbeya
Mhashamu Askofu Augustino Shao, CSSp, Zanzibar
Mhashamu Askofu Damian Kyaruzi, Sumbawanga

Mhashamu Askofu Severine NiweMugizi, Rulenge-Ngara
Mhashamu Askofu Desiderius Rwoma, Bukoba
Mhashamu Askofu Method Kilaini, Bukoba
Mhashamu Askofu Damian Dallu, Geita
Mhashamu Askofu Ludovick Minde, OSS, Kahama
Mhashamu Askofu Alfred Leonard Maluma, Njombe

Mhashamu Askofu Castor Paul Msemwa, Tunduru-Masasi
Mhashamu Askofu Beatus Kinyaiya, Ofm Cap, Mbulu
Mhashamu Askofu Michael Msonganzila, Musoma
Mhashamu Askofu Issack Amani, Moshi
Mhashamu Askofu Almachius Rweyongeza, Kayanga
Mhashamu Askofu Rogath Kimaryo, CSSp Same
Mhashamu Askofu Salutaris Libena, Ifakara
Mhashamu Askofu Eusebius Nzigilwa, Dar es Salaam
Mhashamu Askofu Renatus Nkwande, Bunda
Mhashamu Askofu Gervas Nyaisonga, Dodoma
Mhashamu Askofu Bernadin Mfumbusa, Kondoa
Mhashamu Askofu John Ndimbo, Mbinga
Mhashamu Askofu Titus Mdoe, Dar e
s Salaam.

Tuesday, March 11, 2014

UJUMBE WA BABA MTAKATIFU FRANCISCO KWA KIPINDI CHA KWARESMA 2014

Mama Kanisa anakianza kipindi cha Kwaresima, yaani siku arobaini za toba na wongofu wa ndani; kusali na kufunga; kusoma na kulitafakari Neno la Mungu pamoja na kumwilisha imani katika matendo, kwa Jumatano ya Majivu. Waamini wanakumbushwa kwamba, wao ni mavumbi na mavumbini watarudi tena.

Hizi ni nyakati za toba na zimewekwa na Mama Kanisa kwa ajili ya mazoezi ya maisha ya kiroho; zinajikita katika liturujia ya toba, kuhiji kama ishara ya toba, kujinyima kwa hiyari kama sehemu ya kufunga na kutoa sadaka kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii; ni mwaliko wa kushiriki kidugu kazi za mapendo na kimissionari zinazotekelezwa na Mama Kanisa.

Ujumbe wa Kwaresima kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa Mwaka 2014 unaongozwa na kauli mbiu “Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, Jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba, ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake”. Huu ni mwaliko kwa waamini kuonesha moyo wa ukarimu kwa jirani zao kama ilivyokuwa nyakati za Mtakatifu Paulo aliyewahimiza Wakorintho kuwasaidia ndugu zao waliokuwa wanateseka mjini Yerusalemu.

Baba Mtakatifu katika tafakari hii anaonesha jinsi ambavyo Mwenyezi Mungu ambaye ni tajiri na mwingi wa rehema kwa njia ya Yesu Kristo, Mwanaye wa pekee amejinyenyekesha na kuwa maskini, ili aweze kuwa karibu na binadamu kwa njia ya Fumbo la Umwilisho. Hiki ni kielelezo cha upendo wa Mungu ambao ni neema na baraka inayotolewa kwa binadamu anayependwa na Mwenyezi Mungu, kiasi cha hata Kristo kujisadaka maisha yake.

Huu ndio upendo unaoshirikisha, unajenga na kuimarisha umoja na udugu kwa kuvunjilia mbali kuta za utengano. Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Mwenyezi Mungu amefikiri na kutenda kama binadamu katika mambo yote isipokuwa hakutenda dhambi.

Kwa njia ya umaskini wa Yesu, Mwenyezi Mungu amependa mwanadamu aweze kutajirika, hii ndiyo mantiki ya Fumbo la Umwilisho na Fumbo la Msalaba. Alibatizwa mtoni Yordani si kwa vile alikuwa anahitaji toba, wongofu wa ndani na msamaha, bali alipenda kuonesha mshikamano wa dhati na binadamu mdhambi kwa kujitwika dhambi zake mabegani mwake, ili aweze kuwafariji, kuwaokoa na kuwakomboa kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake wa Kwaresima kwa Mwaka huu anasema, Yesu alijifanya kuwa jirani na Msamaria mwema, kwa kuguswa na mahangaiko ya binadamu, ili hatimaye, aweze kumwonjesha huruma na mapendo yanayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Utajiri wa Yesu unajionesha kwa namna ya pekee kwa kumtegemea Baba yake wa mbinguni, katika kutekeleza mapenzi yake na hatimaye kuvikwa taji la utukufu. Yesu anatambua kwamba, ni Mwana pekee wa Mungu, Masiha anayewaalika wafuasi wake kujitajirisha kutoka kwake na kushiriki udugu na kujitahidi kuchuchumilia utakatifu wa maisha kwa kuishi kama watoto wa Mungu na ndugu zake Kristo.

Kila wakati Mwenyezi Mungu anaendelea kumkomboa mwanadamu kutoka katika umaskini wake kwa njia ya umaskini wa Yesu, kwa kuonja na kuguswa na umaskini wa jirani zao tayari kujifunga kibwebwe kusaidia kupambana na umaskini: wa hali, kipato na maadili. Umaskini ni kielelezo cha kukosa imani, mshikamano na matumaini. Umaskini wa kipato unawakumba wote wanaoishi katika mazingira ambayo ni kinyume kabisa cha utu na heshima ya binadamu.

Hawa ni watu wanaopokonywa haki na mahitaji msingi kama vile: chakula, maji, malazi, huduma bora za afya, fursa za kazi na ajira, maendeleo na ukuaji wa kitamaduni. Kanisa linaendelea kujisadaka kwa ajili ya kupambana na umaskini wa kipato katika mikakati yake ya kichungaji inayopania kumkomboa mtu mzima: kiroho na kimwili. Kanisa linaiona na kuitambua sura ya Kristo miongoni mwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Kanisa linapania kuhakikisha kwamba, utu na heshima ya binadamu vinaendelea kupewa kipaumbele cha pekee kwa kukomesha ubaguzi ambao wakati mwingine ni chanzo kikuu cha umaskini. Kanisa linahimiza matumizi bora ya rasilimali ya dunia kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Jamii iongozwe katika misingi ya haki, usawa, kiasi na ushirikiano.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kuna umaskini wa kimaadili, unaomfanya mwanadamu kuwa ni mtumwa wa dhambi, ulevi wa kupindukia, mcheza kamari na mtazamaji wa picha za ngono. Hili ni kundi la watu lililopoteza dira na mwelekeo wa maisha kwa kukata tamaa! Ni watu wanaoogelea katika utupu kwa kukosa fursa za ajira pamoja na kuendelea kudhalilishwa utu na hehima yao kama binadamu: wanakosa chakula na malazi; hawana haki ya kupata huduma bora katika sekta ya elimu, afya na maendeleo. Matokeo yake ni watu kuelemewa mno na umaskini wa kimaadili kiasi hata cha kutema zawadi ya maisha!

Umaskini huu ni chanzo kikuu cha myumbo wa uchumi kimataifa na matokeo yake ni umaskini na utupu wa maisha ya kiroho. Hali hii inajionesha pale mwanadamu anapomn’goa Mwenyezi Mungu katika maisha na vipaumbele vyake, kiasi hata cha kutema upendo na huruma yake. Hapa mwanadamu anadhani kwamba, anaweza kujitegemea mwenyewe na wala haitaji msaada kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Lakini ikumbukwe kwamba, ni Mungu peke yake anayeweza kukomboa na kumwokoa mwanadamu.

Baba Mtakatifu anasema, Injili ni dawa inayoponya umaskini wa maisha ya kiroho, changamoto na mwaliko kwa kila Mkristo kuhakikisha kwamba, anashiriki kutangaza Injili ya Kristo katika medani mbali mbali za maisha, ili watu waonjeshe upendo na huruma ya Mungu; ili hatimaye, waweze kushirikishwa maisha ya uzima wa milele. Waamini wawe ni watangazaji amini wa Injili ya Furaha inayojikita katika huruma na matumaini; mwanga na faraja kwa wote wanaotembea katika giza na uvuli wa mauti. Ni mwaliko wa kumfuasa Kristo aliyethubutu kuwaendea maskini; akaonesha sifa ya kuwa mchunga mwema kwa kumwendea Kondoo aliyekuwa amepotea, ili kumwonjesha upendo wake. Kwa kushikamana na Yesu, waamini wanaweza kuwa na ujasiri wa kushiriki katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya na maendeleo endelevu.

Baba Mtakatifu Francisko katika Kipindi hiki cha Kwaresima anawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuonesha ushuhuda wa pekee kwa maskini wa hali, maadili na maisha ya kiroho wanaokutana nao kila siku ya maisha yao, ili waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Yesu Kristo. Kwaresima ni muda muafaka wa kujisadaka kwa ajili ya kuwasaidia wengine, kwa kutambua kwamba, kwa njia hii pia tunafanya toba.

Waamini wanaweza kuwatajirisha jirani zao na hivyo kushiriki katika mchakato wa kuganga na kuponya umaskini unaomwandama binadamu. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, waamini wataweza kukitumia kipindi hiki cha Kwaresima ili kupata neema na baraka zinazobubujika kutoka kwa Kristo mwenyewe!

Ujumbe huu umehaririwa na

Padre Richard A. Mjigwa.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican

Monday, March 3, 2014

Mafungo ya Kwaresima Consolata Mission Centre - Bunju

Kituo cha Consolata mission center Bunju, kinawaalika Vijana wote katika Mafungo ya kwaresima, yatakayofanyika  siku ya jumamosi tarehe 08/03/2014 siku ya jumamosi

Mada ni: "INJILI YA FURAHA:EVANGELII GAUDIUM"

Ada ya ushiriki kwa kila Kijana ni TSHS 5000 kwa ajili ya chakula na chai .Fika bila kukosa na jitahidi ufike kabla ya saa Mbili asubuhi .......

MAANA YA KIPINDI CHA KWARESIMA

Hii ni Kwaresima

Nini maana ya Kwaresima?Kwa Kilatini na Kiitaliano neno Kwaresima lilimaanisha “40” yaani siku 40 za kufunga za wiki kati ya Jumatano ya Majivu hadi Jumamosi Kuu. Kwa Kijerumani Kwaresima maana yake “Kipindi cha kufunga.”

Kwaresima ilianzaje?
Kabla ya kuona Kwaresima jinsi ilivyoanza, ni vizuri kuongea kidogo kuhusu Sikukuu ya Pasaka ili tuweze kupata mwanga wa kuelewa mwanzo wa kipindi hiki muhimu cha Kwaresima.

Habari Njema yatuambia kwamba YESU KRISTO alifufuka “Siku ya kwanza ya juma.” “Hata sabato ilipokwisha, ikipambazuka siku ya kwanza ya juma, Mariamu Magdalene, na Mariamu yule wa pili, walikwenda kulitazama kaburi.” (Mt.28:1) Hii ni kwasababu Wakristo walianza kukutana pamoja kwa sikukuu ya ufufuko wa BWANA kila wiki sio Jumamosi kama Wayahudi, bali siku iliyo fuata. “Hata siku ya kwanza ya juma, tulipokuwa tumekutana ili kumega mkate, Paulo akawahutubu, akiazimu kusafiri siku ya pili yake, naye akafuliza -`maneno yake hata usiku wa manane.” (Mdo.20:7). “Siku ya Kwanza ya juma kila mtu kwenu na aweke akiba kwake, kwa kadiri ya kufanikiwa kwake: ili kwamba michango isifanyike hapo nitakapokuja.” (1Kor.16:2), siku ambayo Warumi waliita “Siku ya Jua”. Mara moja jina hilo lilibadilika na kuwa “Siku ya BWANA”

Kanisa la mwanzoni halikusherehekea sikukuu kama vile Noel, Sikukuu kwa heshima ya Mama Bikira Maria au sikukuu yeyote ile. Kulikuwepo na adhimisho la ufufuko wa BWANA kila wiki na hakuna zaidi.

Miaka mingi ikapita kanisa likiwa katika hali hii. Baadaye kulikuwepo na hitaji la kusherehekea tukio la kiini cha imani yetu kwa namna ya pekee. Wakristo waliona umuhimu wa kuwa na muda kwa sikukuu ya kwanza kati ya sikukuu zao yaani “Jumapili ya Pasaka”, ambayo ilifikiriwa kama “Mama wa Jumapili zote”, “Mama wa skikukuu zote”. Waliiona sikukuu hiyo kama “Malkia wa sikukuu zote, wa Jumapili zote, na kiujumla kama Malkia wa siku zote za mwaka. Tangu mwanzoni mwa karne ya pili, Jumuiya zote za Kikristo walikuwa wanasherehekea sikukuu hii ya Pasaka. Sherehe zilikuwa zinahitimishwa na kusanyiko la sala lililofanyika usiku na kumalizikia na Ekaristi. Ushiriki wa kwenye ibada hiyo, ulichukuliwa kama ni kitu muhimu sana kwa mkristo.



Kuanza kwa Kwaresima

Wote tunafahamu kwamba, ufanisi au mafanikio yoyote ya sikukuu au ya jambo lolote yanategemea sana maandalizi yake. Miaka miambili hivi baada ya KRISTO, Wakristo walitaka kuvuna matunda ya kiroho ya Paska kwa wingi. Ili kufanikisha hili, walianzisha utamaduni wa kuwa na siku tatu kabla ya Pasaka kwa sala, tafakari na kufunga kwa nia ya kuonyesha masikitiko yao juu ya kifo cha YESU KRISTO. Kutokana na ukubwa na umuhimu wa sikukuu hii, mbali ya kuona umuhimu wa maandalizi, walitafuta njia za kuongeza muda wa furaha na utajiri wa kiroho utokanao na Pasaka. Hivyo walianzisha “Wiki Saba,” yaani siku 50 za Pentekoste ambapo walisherehekea na kuzipitisha siku hizo kwa hali ya furaha. Askofu Mt. Ireneus alisema kuwa muda huo wa siku 50 ni kama Sikukuu ya Siku moja yenye umuhimu sawa na Jumapili. Katika kipindi cha siku za Pentekoste, sala zilikuwa zinasaliwa hali wamesimama, kufunga kulikatazwa na sakramenti ya ubatizo ilikuwa ikiadhimishwa. Ni kama vile sikukuu ya Pasaka ilidumu kwa kipindi chote cha siku 50. Miaka 150 ilipita na mwishoni mwa mwaka 350 B.K., Wakristo waliona kama siku tatu hazikutosha kwa maandalizi ya sikukuu kama hii. Hivyo waliongeza hadi kufikia siku 40. Hivi ndivyo Kwaresima ilivyoanza.

Kwa nini siku 40?
Tunaposema kuku wanne au kilo saba za mchele tuna maana kama ilivyo yaani kuku wanne na kilo saba za mchele. Si zaidi au pungufu.

Namba au tarakimu mbalimbali tunazokutana nazo katika Biblia zinaashiria lugha za picha na siyo kuchukulia katika thamani ya kuhesabu. Hivyio basi, tunapokutana na namba kama 40 huenda isimaanishe 40 kama tunavyo hesabu fedha. Kati ya maana nyingi zilizotolewa kwa namba 40, kuna moja yenye maana ya pekee, inamaana ya kipindi cha maandalizi cha kutosha kisichokuwa na muda maalum, kwa tukio kubwa. Kwa mfano , Gharika ilidumu kwa siku 40 usiku na mchana…na ilikuwa ni maandalizi ya ubinadamu mpya; Waisraeli walitumia muda wa miaka 40 jangwani…maandalizi ya kuingia nchi ya ahadi; watu wa Ninawi walifunga na kufanya kitubio siku 40…maandalizi ya kupokea msamaha wa MUNGU; Elia alitembea kwa siku 40 mchana na usiku…kama maandalizi ya kufika mlima wa MUNGU; Musa na YESU walifunga kwa siku 40 mchana na usiku… kama maandalizi kabla ya kuanza utume wao. “Kisha ROHO alimwongoza YESU mpaka jangwani ili ajaribiwe na ibilisi. Akafunga siku arobaini usiku na mchana, na mwishoe akaona njaa” (Mt.4: 1-4)

Natumaini hadi hapo tumeelewa nini maana ya namba 40. Je, ni siku ngapi ambazo zinahitajika kwa ajili ya maandalizi ya sikukuu kubwa kuliko zote za kikristo? Bila shaka ni 40. (Kuanzia Jumatano ya majivu hadi Jumamosi Kuu ukiondoa Jumapili zote) Siku 40 ni muda wa kutosha wa kufanikisha kitu fulani chema, kizuri na chenye thamani.

Lengo la Kwaresima ni nini?

Lengo kuu la Kwaresima ni kufanya upya maisha yetu ya kiroho na kutufanya kuwa watu ambao MUNGU anataka tuwe yaani ni kipindi chenye kutupatia utakatifu, tukikumbuka kuwa sote tumeitwa kuwa watakatifu kama BABA yetu wa mbinguni alivyo mtakatifu (Mt. 5:48). Ni kipindi cha kuuvua utu wetu wa kale na kuvaa utu mpya. Kwani tunasoma:- “Mvue kwa habari ya mwenendo wa kwanza utu wa zamani, unao haribika kwa kuzifuata tamaa zenye kudanganya; na mfanywe wapya katika roho na nia zenu; mkavae utu mpya, ulioumbwa na MUNGU katika haki na utakatifu wa kweli. Basi uvueni uongo, mkaseme kweli kila mtu na jirani yake…Mwibaji asiibe tena…Neno lolote lililo ovu lisitoke vinywani mwenu, bali lililo jema na kufaa…tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama MUNGU katika KRISTO alivyowasamehe ninyi.” (Efe.4:22-32.)

Kwaresima kwa hakika ni kipindi pia cha kuachana na matendo ya mwili. “Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya: uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo;” (Gal.5:19 – 20)

Kwa ufupi Kwaresima ni kipindi cha kuachana na maisha ya dhambi na kurudi kwa MUNGU kwa kuishi maisha yanayompendeza MUNGU kwa njia ya kufanya toba ya kweli isiyo ya mazoea, na malipizi yasiyo ya nje tu, bali hasa mapinduzi ya kiroho. Katika kipindi hiki tunalazima ya kubadili hali yetu ya ndani. Badala ya kujitafuta wenyewe na kufuata mapenzi yetu, inatupasa sisi kumwelekea MUNGU na kuyatimiza mapenzi yake katika mawazo, maneno na matendo yetu.

Nguzo tatu kuu za Kwaresima ni:

i. Sala.Wewe usalipo, ingia katika chumba chako cha ndani. Usali mbele ya BABA yako aliye sirini; na BABA yako aonaye sirini atakujazi.” (Mt. 6:6)
Kupata muda wa sala pamoja na MUNGU. Sio tu kunena maneno ya sala fulani, lakini pia kumsikiliza MUNGU akizungumza mioyoni mwetu. Kumuomba MUNGU nguvu ya kubadilika, yaani uongofu wa kweli. Ndiyo maana tunaambiwa. “Tubuni na kuiamini Injili”. Hayo ndiyo MUNGU aombayo kwetu wakati wa Kwaresima. MUNGU anatuita kutoka kwa dhambi, na tuupokee ujumbe wake kwetu – Injili, na kuwa waamninfu kuishi kadiri ya Injili. Ni wakati pia wa kuhudhuria misa mara kwa mara kwa ibada na uchaji, kuhudhuria ibada mbalimbali, kama vile Baraka ya Sakramenti Kuu, Kuabudu Ekaristi Takatifu, kusoma Neno la MUNGU na kuliishi baada ya kuyatafakari maneno hayo ya MUNGU ambayo ndiyo sauti yake MUNGU na kutumia muda wetu kwa mambo ya ki-MUNGU yaliyo matakatifu.

ii. Kufunga. “Bali wewe ufungapo, jipake mafuta kichwani, unawe uso wako ili usionekane na watu ukifunga, ila na BABA yako aliye sirini; na BABA yako aonaye sirini atakutuza.” (Mt. 6:17-18). Kufunga sio tu kujinyima kutokunywa pombe, kutokula chakula, kutovuta sigara n.k. Kifupi ni kwamba kufunga kuondokana na ubinafsi wetu na kuwafikiria na kuwasaidia wenye shida. Uovu hauwezi kushindwa bila kujitoa nafsi na bila kutoa na kuwapa wahitaji vile tuvipendavyo. MUNGU hapendezwi na kufunga tu, bali upendo kwa wanaoteseka utusukume na kufunga tupendavyo kwa ajili ya kuwasaidia wahitaji. Hivyo kuna mahusiano makubwa sana kati ya kufunga na ukarimu. Kufunga lazima kuendane na ukarimu. Kufunga bila ukarimu huo ni mfungo tasa.

iii. Kutoa Sadaka.Angalieni msifanye wema wenu machoni pa watu kusudi mtazamwe nao. Bali wewe utoapo sadaka hata mkono wako wa kushoto usijue ufanyalo mkono wa kuume; na BABA yako aonaye kwa siri atakujazi.” (Mt. 6:1) Hayo yanamaanisha kwamba usidai shukurani wala malipo kwa wema wowote uwatendeao jirani zako kwa sadaka yako. Malipo utakayopata uyatazamie tu kutoka kwa BABA yako wa mbinguni. Kutoa tunachojinyima kwa kumsaidia KRISTO anayeteseka kwa wenzetu. Kushirikiana na wengine tulivyo navyo kama vile fedha, nguo, chakula, ama kuwakaribisha wahitaji nyumbani.

Hivyo basi, Mazoezi tunayofanya katika kipindi cha Kwaresima kama kusali zaidi, kusikiliza au kusoma Neno la MUNGU, kutenda matendo ya huruma kwa wahitaji, kufunga chakula na kujihinisha kinywaji pamoja na kuzuia tamaa potovu za mwili wetu, yawe na kusudi la kuibadili hali yetu, kutufanya kuwa na upendo zaidi na huruma kwa wenzetu na kutufanya tuweze kuunganika zaidi na KRISTO MFUFUKA. Tumvue mtu wa zamani katika nafsi zetu na tumvae mtu mpya, yaani KRISTO Mfufuka.

Nini makusudi ya kufunga?YESU alifunga ili awape wanadamu mfano au kielelezo halisi na sahihi cha kuiga, na apate kuokoa roho zetu. Watu wawe na namna bora ya kufanya malipizi, kuuadibisha na kuutumikisha mwili na tamaa kwa kuwa anatenda dhambi.

Nani anapaswa kufunga?Inatubidi tujiangalie sana kwani miili yetu ni midhaifu na myepesi kwa kutenda dhambi na kuipeleka roho motoni. Tusiiendekeze miili yetu, bali tuitawale kwa kufuata maadili ya kimungu na kuinyima madai yake, ambayo ni kishawishi kinachotupeleka upotevuni. Tunapoamua kufuata njia hii, hakika, KRISTO atatuimarisha na kutuongoza kwenye uzima wa milele; na kutupa neema ya kupambanua mema na dhambi, huku tukielekea uzimani. Mdomo unao nena dhambi, na mwili unaotenda dhambi, sherti vyote vitende pia mema, siyo dhambi.

Mtu asiyetenda dhambi hana haja ya kufunga. Lakini hakuna mtu anyefikia utu uzima ambaye hatendi dhambi machoni pa MUNGU hata Wacha MUNGU wana dosari. Kwa hiyo, kila mtu afunge kufidia dhambi zake. Tusipofunga kuna hatari kubwa ya kuungua moto. Ni vizuri waamini wote wafunge ili kulipia fidia ya dhambi zinazotendwa. Tumwabudu KRISTO kwa unyofu na unyenyekevu, ili kwa huruma yake kuu atusamehe dhambi zetu na adhabu tunazostahili.

Ngazi tatu za kufunga chakula:

(a) Ngazi ya kwanza, ni kuacha chakula kimoja fulani, au kitu kingine unachopendelea. Kufunga huku ni rahisi hata kwa watoto. Kwa mfano, kuacha kula nyama au kunywa soda yoyote kwa kipindi kizima cha Kwaresima; au kula chakula bila chumvi, au kunywa chai bila sukari kwa kipindi kizima cha mfungo. Huu ni mfungo rahisi.

(b) Ngazi ya pili, ni kuacha kabisa kula siku nzima. Hii ni ngazi ya kawaida, yaani mfungo wa kawaida. Huku ni kula mlo mmoja tu kwa siku hadi utosheke. Yawezekana ikawa ukala mlo wa mchana au wa jioni tu. Asubuhi au jioni (au asubuhi na mchana) ule kidogo sana. Katikati ya hapo usile chochote tena wala kunywa chochote.

(c) Ngazi hii ya tatu ni ya wale wanaotaka kufanya malipizi makali zaidi. Huu ni Mfungo mkali. Katika ngazi hii ya kufunga watu wengi huaacha kabisa kula na kunywa siku nzima, wakawa na huo mlo mmoja tu. Wanaotaka malipizi makali zaidi siku ya kufunga chakula, asubuhi pokea Ekaristi Takatifu, na wala usiguse chakula au kinywaji chochote kingine. Mchana unaweza kula slesi moja (kipande) tu ya mkate na unywe glasi moja tu ya maji ya kawaida. Jioni pia ule slesi moja ya mkate na unywe glasi moja tu ya maji. Na endapo utaamua kutokula kabisa na kutokunywa kabisa hadi asubuhi kesho yake, itampendeza zaidi Mwenyezi MUNGU. Hii ndiyo toba ya kweli.

Tukumbuke kwamba kile tunachofunga kiwasaidie wasiojiweza. Si kufunga kwa nia ya kuweka akiba ili baada ya mfungo uweze kutumia wewe mwenyewe! La hasha. Huo si mfungo wenye kuleta faida kiroho, bali ni mfungo tasa.

Kuacha kula nyama Ijumaa Kuu na Ijumaa nyingine za mwaka.
Ufungapo au uachapo kula nyama, funga kweli na acha kweli kula nyama kwa dhati kwa toba ya dhambi. Vinginevyo utakuwa unajidanganya mwenyewe. Papo uutolee mfungo wako na kutokula nyama huku kwa Mwenyezi MUNGU, kwamba unafanya hivyo kwa kudhamiria. La sivyo utadhania unafunga na unaacha kula nyama kwa manufaa ya kiroho wakati unashinda tu na njaa ! Kuacha kula nyama maana yake ni kula vyakula vitokanavyo na ardhi tu; ndivyo vyakula vya mfungo. Acha kula kila aina ya nyama, na mafuta yanayotokana na wanyama. Usile nyama, mayai, mafuta ya wanyama, siagi na jibini, wala maziwa. Kula vitu vyovyote vitokanavyo na wanyama au ndege hurahishisha mfungo wako. Kumbuka pia kwamba siku za kufunga na kuacha kula nyama, uwe macho sana, maana shetani mshawishi atakuja kupima utashi wako. Shinda mwili (njaa na kiu) wako, mshinde shetani anyekuongoza dhambini. Jambo la muhimu hasa ni kwamba matendo hayo yote yatendeke kwa ajili ya BWANA. Tuyafanye kama alama ya kwamba tunataka kurudi kwake. Yawe ni matendo kati ya MUNGU na mimi. Kwa sababu hiyo lazima kulinda siri ya jambo lolote tutakalo tenda. “BABA yako aonaye sirini atakujazi.”

Nini thamani na maana ya kujinyima jambo fulani ambalo kimsingi ni zuri na inafaa kwa ajili ya afya ya mwili?

Thamani na maana ya kufunga tunaiona na kupata mfano kwa YESU. Ni vema tukumbuke kwamba Kwaresima inatukumbusha siku 40 za mfungo wa BWANA wetu jangwani, alivyofanya kabla ya kuanza Utume wake hadharani, (Mt. 4:1-2). Pia, kama Musa alivyofunga kwa siku 40 usiku na mchana kabla ya kupokea zile Mbao za Sheria (Kut. 34:28). Eliya naye alifunga kabla ya kukutana na BWANA katika Mlima Horeb (1 Wafal. 19:8), YESU vile vile kwa njia ya sala na kufunga, akijitayarisha kwa ajili ya majukumu yaliyokuwa mbele yake, alituonesha tangu mwanzo mapambano makali dhidi ya Shetani.

Hivyo basi, Maandiko Matakatifu na mafundisho yote ya desturi za ukristo yanafundisha kuwa mfungo ni msaada mkubwa katika kukwepa dhambi na vishawishi vinavyoweza kutupeleka katika dhambi yenyewe. Kwa kuwa kila mmoja wetu anaelemewa na dhambi na mafuatano yake, kufunga kumependekezwa kwetu kama njia ya kurudisha urafiki wetu na MUNGU. Hivi ndivyo alivyofanya Ezra (8:21), walivyofanya watu wa Ninawi (Yona 3:9).

Je, unajua mfungo wa kweli ni upi?
Mfungo wa kweli kama YESU alivyorudia mahali pengi, ni kufanya mapenzi ya Baba aliye Mbinguni, “na BABA yako aonaye sirini, na atakujazi” (Mt. 6:18). Mfungo wa kweli unaelekezwa katika kula chakula cha kweli; yaani “kufanya mapenzi ya MUNGU” (Yn. 4:34).

Hivyo basi, kama katika Kwaresima hii UMEAMUA kweli kusali, basi funga; kama unafunga, onesha huruma; kama unataka maombi yako yasikiwe, sikiliza maombi ya wengine. Endapo hufungi masikio yako kwa wengine, unafungua masikio ya MUNGU kwa ajili yako.

Kwa hakika mfungo unaleta faida za kimwili, lakini kwa Mkristo mfungo upo kwa ajili ya “Tiba” ya kuponya yale yote yanayouzuia mwili kutekeleza utashi wa MUNGU. Pia kufunga ni njia ya kuonesha “huzuni” (1 Sam 31:13; 1 Fal 21:27; Neh1:4); toba (1 Sam 7:6; Yoe 2:12; Dan 9:3-4) au hali ya “unyofu katika maombi” (2 Nya 20:3-4; Ezra 8:23).

Mpenzi msomaji wa kijitabu hiki, nakutakia Kwaresima njema na mfungo wenye heri na toba ya kweli mbele za MUNGU kwa kuleta mabadiliko ya kweli katika maisha yetu ili kufungua mifereji ya neema na baraka katika mtu binafsi, familia na Jumuiya. Tukumbuke kwamba dhambi huzuia baraka na neema toka kwa MUNGU hata kurudisha nyuma maisha yetu ya kiroho na maendeleo katika familia. Hivyo, katika kipindi hiki cha Kwaresima tukitumie kwa kufanya toba ya kweli kimatendo ili kuondoa vikwazo vyote vinavyo zuia maendeleo yetu kiroho na ya kifamilia kwa kuwa tayari kumegwa kuwa chakula kwa wengine kwa njia ya ukarimu wetu. Tujitahidi katika kushiriki Ibada ya Njia ya Msalaba ikichukuliwa katika mtazamo wa kufanya toba na kuomba msamaha kwa MUNGU. Kushiriki Sakramenti vema hasa Sakramenti ya upatanisho ili mfungo, na toba yetu vipate kibali machoni pake MUNGU na kushiriki matakatifu.
MUNGU akubariki na kukulinda. Nakutakia kwaresima njema.

“Wakati umetimia na ufalme wa MUNGU umekaribia, Tubuni na kuiamini Injili.” (Mk 1:16).


NJIA YA MSALABANjia ya Msalaba ni ibada ya Mateso na Kifo cha KRISTO. Tunasafiri naye kiroho kutoka kwenye nyumba ya Pilato hadi Kalvari. Tunakumbuka yote yaliyotukia tangu alipohukumiwa hadi alipozikwa karibuni. Tunafanya ibada hii kwa kuwa karibu na YESU anayeteseka kwa ajili yetu na kuwa karibu na Bikira MARIA Mama wa Mateso. Hivyo, tufikiri juu ya ubaya wa dhambi zetu na kuzijuta na kudhamiria kuziacha kweli. Pili, tufikiri juu ya Fumbo la Mapendo ya YESU kwa BABA yake na kwetu sisi wanadamu. Ibada hii itusaidie kuonja wokovu uliotujia kwa Mateso, Kifo na Ufufuko wa Mkombozi wetu, YESU KRISTO.




Sala mbele ya AltareEe, Mkombozi wangu, ninakuja leo kufuata njia ile uliyoshika siku ya kufa sadaka yetu. Nimetubu dhambi zangu zote; ninataka kugeuza mwendo wangu; ninaomba kwako niwapatie roho za waamini marehemu waliomo toharani, rehema zote zilizotolewa na Kanisa kwa Njia ya Msalaba. Nawe MARIA Bikira Mtakatifu, uliyefuata njia ile nyuma ya mwanao YESU, uniangalie kwa wema, unitie Moyo Mkuu, nisipende dhambi tena, nikivumilia kazi na usumbufu na mateso na matukano yatakayonipata.

**************
Umekosa nini we YESU,/ Kushtakiwa bure kwa Pilato
Wenye kustahili hukumu, Si wewe, si wewe BWANA, ni sisi.

KITUO CHA KWANZA - YESU anahukumiwa afe
- Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
- Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.

Pilato anamhukumu YESU ingawa haoni kosa lake, anawaogopa Wayahudi. Anabembeleza urafiki wa Kaysari. Ee YESU usiye na kosa, hata mimi ningeweza kutenda mema mengi, lakini naogopa macho ya wenzangu, na maneno yao. Ee BWANA, uniima-rishie utashi wangu, nijitegemee katika kushika madaraka yangu.

BABA yetu… – Salamu MARIA… -Atukuzwe BABA…
K. Ee BWANA, Utuhurumie. W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.

**************
Ole Msalaba huo mzito, / Apagazwa mwana mpenzi wa MUNGU. / Mwili waenea mateso, / Alipa, alipa madhambi yetu
KITUO CHA PILI - YESU anapokea msalaba
- Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
- Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.

YESU anakubali kuelemewa na msalaba kwa ajili ya wokovu wa watu. Ndivyo anavyonifundisha moyo wa sadaka, moyo wa kujitolea na kujisahau kwa ajili ya wengine. Ee YESU wangu mkarimu, mimi pia ninao msalaba wangu: jirani zangu, mwenzangu wa ndoa, watoto, wazazi wangu, kazi zangu, joto, baridi, njaa, kiu, vishawishi, magonjwa na matatizo mengine ya maisha, wajibu wangu kwa MUNGU, kwa umma na kwa Kanisa. Hayo yote ni msalaba. Unipe ukarimu wako ee YESU, niyapokee bila kunung’unika, na kuyabeba vema.

BABA yetu… -Salamu MARIA… -Atukuzwe BABA…
K. Ee BWANA, Utuhurumie. W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.

**************
Ona Muumba mbingu na nchi, / Yupo chini mzigo wamwelemea, / Na mtu kiumbe chake kwa ukali, / Ampiga, ampiga bila huruma.
KITUO CHA TATU - YESU anaanguka mara ya kwanza
- Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
- Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.

YESU amedhoofika sana, anaanguka chini, kisha anasimama, anaendelea na safari ya ukombozi. Ee YESU uliyeanguka chini ya msalaba kwa ajili ya udhaifu, ukasimama tena; usiniache katika tamaa nikianguka dhambini, bali nisimame mara moja, nikufuate.

BABA yetu… -Salamu MARIA… -Atukuzwe BABA…
K. Ee BWANA, Utuhurumie W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.

**************
Huko njiani we MARIA, / Waonaje hali ya mwanao, / Ni damu tupu na vidonda, / Machozi, machozi yamfumba macho.
KITUO CHA NNE - YESU anakutana na mama yake
- Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
- Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.

Wote wawili mama na mwanawe wanaumia sana moyoni kwa ajili ya dhambi zangu. Ee YESU, Mwana wa MARIA, unitilie moyoni mwangu upendo na ibada kwa Bikira MARIA; unijalie na ulinzi wake, nisitende dhambi tena.

BABA yetu… -Salamu MARIA… -Atukuzwe BABA…
K. Ee BWANA, Utuhurumie. W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.

**************
Kwa Simoni heri ya kweli, / Mimi pia YESU nisaidie, / Kuchukua mzigo wa ukombozi, / Kuteswa, kuteswa pamoja nawe.
KITUO CHA TANO - Simoni wa Kirene anamsaidia YESU
- Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
- Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.

Nausifu ukarimu wa Simoni wa Kirene. Ee BWANA unijalie ukarimu kama huo, niitikie nami wito wa kukusaidia kuchukua msalaba. Nitoe zaka na michango yote ya uenezaji wa dini; nijitolee mimi mwenyewe katika kazi ya maendeleo ya dini. Uwajalie vijana wengi wito wa Upadre, waweze kuchukua msalaba pamoja nawe kwa ajili ya wokovu wa dunia. Uwaimarishe viongozi wa dini. Ustawishe moyoni mwa waamini wote mwamko wa utume.

BABA yetu… -Salamu MARIA… -Atukuzwe BABA…
K. Ee BWANA, Utuhurumie. W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.

**************
Uso wa YESU Malaika, / Betlehemu walikuabudu, / Bahati yake Veronika, / Kupangusa, kupangusa Mfalme wa Mbingu.
KITUO CHA SITA - Veronika anapangusa uso wa YESU
- Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
- Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.

Mama huyu ni kinyume kabisa cha Pilato. Veronika anajua analopaswa kutenda, na analitenda bila kujali macho na maneno ya makundi ya watu waovu. Ee YESU, uliyemtuza Veronika zawadi ya picha ya uso wako juu ya kitambaa, unijalie ushupavu na ujasiri wake wa kutenda mema, ili roho yangu ipambwe kwa chapa ya uungwana na utakatifu wako.

BABA yetu… -Salamu MARIA… -Atukuzwe BABA…
K. Ee BWANA, Utuhurumie. W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.

Wakimvuta huku na huku, / Wauaji wanamchokesha bure, / Chini wanamtupa bado kwa nguvu, / Aibu, aibu yao milele.
KITUO CHA VII - YESU ANAANGUKA MARA YA PILI
- Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
- Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.

Ee YESU uliyelegea mno kwa mateso makali, unapoanguka mara ya pili kwa ajili ya udhaifu wa mwili, wanionya kwamba hata mimi naweza kurudi dhambini kwa udhaifu wa moyo. Nipe basi neema ya kuepuka nafasi za dhambi na visa vyenye kunikwaza na kunirudisha dhambini.

BABA yetu -Salamu MARIA -Atukuzwe BABA.
K. Ee BWANA, Utuhurumie W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amni. Amina.

Wanawake wa Israeli, / Msilie kwa sababu hiyo, / Muwalilie hao kwa dhambi, / Upanga, upanga ni juu yao.
KITUO CHA VIII - AKINA MAMA WANAMLILIA YESU
- Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
- Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.

Asanteni sana akina mama kwa moyo wenu wa huruma. Ee YESU uliyetulizwa na wanawake, unipe moyo wa kuwaheshimu akina mama wote. Uwaite na wasichana wengi waingie utawa, ili watulize moyo wako Mtakatifu kwa sala na sadaka zao.

BABA yetu -Salamu MARIA -Atukuzwe BABA.
K. Ee BWANA, Utuhurumie W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.

Mwokozi sasa ni ya tatu, / Waanguka chini ya msalaba, / Katika dhambi za uregevu, / Nijue, nijue kutubu hima.

KITUO CHA IX - YESU ANAANGUKA MARA YA TATU
- Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
- Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.

Ee YESU unayezidi kudhoofika kwa mateso unaanguka mara ya tatu, upate kunistahilia neema ya kuutiisha mwili wangu na kuusulibisha, licha ya kuepuka nafasi za dhambi. Mara nyingi mno ninajibovusha kwa kupenda mno starehe, anasa na tafrija. Ee YESU mwema, nisaidie kuufuata mfano wa Mtakatifu Paulo, niutese mwili wangu na kuutumikisha, ili nipate siku moja tuzo mbinguni.

BABA yetu -Salamu MARIA -Atukuzwe BABA.
K. Ee BWANA, Utuhurumie W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.

Muje Malaika wa Mbingu, / Funikeni mwiliwe kwa huruma, / Vidonda vyake na utupu, / Askari, askari wamemvua.
KITUO CHA X - YESU ANAVULIWA NGUO
- Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
- Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.

Askari wanamvua kwa nguvu nguo yake, iliyogandamana na madonda yake; wanayaamsha mara moja mateso yote aliyoteswa tangu mwanzo. Ee YESU, unayavumilia mateso makali haya, upate kunifundisha kuuvua kwa nguvu moyoni mwangu urafiki mbaya, au kitu kingine chochote kile kinachoharibu urafiki wa MUNGU, hata ikipasa kutoa sadaka kubwa.

BABA yetu -Salamu MARIA -Atukuzwe BABA.
K. Ee BWANA, Utuhurumie W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.

Hapo MKRISTO ushike moyo, / BWANA wako alazwa msalabani, / Mara miguu na mikono, / Yafungwa, yafungwa kwa misumari

KITUO CHA XI - YESU ANASULIBIWA MSALABANI
- Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
- Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.

Ee YESU uliyepigiliwa misumari msalabani, nakutolea akili na utashi wangu, vifungwe pamoja na miguu yako, nipate kuwaza, kusema na kutenda siku zote yale tu yanayolingana na utukufu wa msalaba wako Mtakatifu. Ee YESU, mimi ni mfungwa wako. Nisaidie kuimarisha kifungo hicho kwa sala, Sakramenti na fadhila za KiKRISTO.

BABA yetu -Salamu MARIA -Atukuzwe BABA
K. Ee BWANA, Utuhurumie W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.

**********
YESU mpenzi nakuabudu, / Msalabani unapohangaika, / Nchi yatetemeka kwa hofu, / Na jua, na jua linafifia.
KITUO CHA XII - YESU ANAKUFA MSALABANI
- Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
- Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.

Ee YESU uliyekufa msalabani kwa ajili ya dhambi zangu, unijalie niichukie dhambi, nisiishi kamwe katika dhambi. Nifahamu kwamba nilipobatizwa kwa jina lako, nilibatizwa katika mauti yako ili utu wangu wa kale usulibishwe nawe, mwili wa dhambi uangamizwe nisitumikie tena dhambi.

BABA yetu -Salamu MARIA -Atukuzwe BABA.
K. Ee BWANA, Utuhurumie W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.

**********
Mama MARIA mtakatifu, / Upokee maiti ya Mwanao, / Tumemwua kwa dhambi zetu, / Twatubu kwake na kwako.

KITUO CHA XIII - YESU ANASHUSHWA MSALABANI
- Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
- Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.

Ee YESU uliyeshushwa msalabani baada ya kufa, unijalie nidumu katika maisha ya kujitoa sadaka mpaka siku ya kufa kwangu. Nielewe na kukubali kwamba baada tu ya kufa ndio mwisho wa vita na mashindano ya KiKRISTO.

BABA yetu -Salamu MARIA -Atukuzwe BABA.
K. Ee BWANA, Utuhurumie W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.

Pamoja nawe kaburini, / Zika dhambi na ubaya wa moyo, / YESU tuwe Wakristo kweli, / Twakupa twakupa sasa mapendo.
KITUO CHA XIV - YESU ANAZIKWA KABURINI
- Ee YESU, tunakuabudu, tunakushukuru.
- Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.

Ee YESU, ulizikwa kaburini, ukafufuka siku ya tatu. Mimi pia nilizikwa pamoja nawe kwa njia ya ubatizo katika mauti yako. Kwa vile wewe ulifufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa BABA, unijalie nami nifufuke, yaani nishike mwenendo mpya, mwenendo wa uzima wa milele.

BABA yetu -Salamu MARIA -Atukuzwe BABA.
K. Ee BWANA, Utuhurumie W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.

**********
Katika roho yangu BWANA, / Chora mateso niliyokutesa, / Nisiyasahau madeni, / Na kazi, na kazi ya kuokoka.(Hiari yako - Mbele ya Altare)

KITUO CHA XV - YESU AMEFUFUKA
- Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
- Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu

Habari njema aliyotuletea YESU ni kwamba baada ya kila Ijumaa Kuu huja sikukuu ya Pasaka; kwamba punje ya ngano isipoanguka ikafa, hukaa hali hiyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa maozo mengi. Twakushukuru, ee YESU, kwa mateso yako, lakini twakushukuru hasa kwa ufufuko wako, kwa kuwa huo ndio unaotupa hakika ya kuwa hatukuzaliwa kwa ajili ya mateso na maumivu, bali kwa ajili ya heri ya milele.

BABA yetu -Salamu MARIA -Atukuzwe BABA.
K. Ee BWANA, Utuhurumie W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.

*********
SALA YA MWISHO
Mbele ya Altare: YESU wangu, kwa uchungu wote ulioona juu ya msalaba, na kwa kuzimia kwako kwa ukali wa mateso, unijalie nguvu ya kuvumilia kwa moyo taabu zote sasa na saa ya kuzimia kwangu. Nawe MARIA Mamangu, kwa uchungu wote ambao moyo wako umejaa ulipomwona mwanao mpenzi kuinama kichwa na kuzimia, unifadhili nife kifo chema.

SALA YA KUMWOMBA YESU ALIYETESWA
YESU wangu,/ kwa masikitiko uliyoyaona hata ya kuzimia roho,/ na kwa jasho la damu ulilotoka kwa sababu ya dhambi zangu,/ unitie uchungu wa kweli juu ya makosa yangu! YESU wangu, / kwa msongo wa moyo uliouona kutolewa na Yuda,/ unifanyizie nikae amini kwako,/ nisikutoe bado vile nilivyofanya mpaka leo!/ YESU wangu, uliyefungwa kama mtu mwovu,/ niunganishe nawe kwa vifungo vya mapendo yako! YESU wangu,/ kwa madharau uliyodharauliwa, / na machukizo uliyochukizwa mbele ya Ana,/ Kaifa na Herodi,/ uniwezeshe kuvumilia kwa saburi matukano nitakayotukanwa na watu! / YESU wangu, kwa maumivu uliyovumilia mwilini mwako ulipopigwa fimbo nyingi mno,/ nijalie nguvu ya kustahimili maumivu ya ugonjwa, / na kukataa furaha zote mbaya!/ YESU wangu, /kwa mateso uliyoona ulipotiwa taji la miiba,/ unipe neema ya kutokubali tena mawazo yoyote ya majivuno na ya uchafu!/ YESU wangu, /uliyechukua msalaba wako mzito kwa ajili ya dhambi zangu, / unitie moyo mkuu, / nikubali kwa uvumilivu taabu na sulubu zote za maisha yangu! / YESU wangu, uliyemwaga damu yako yote juu ya msalaba kwa ajili yetu,/ nifanyizie niwe hai kwa ajili yako tu!/ YESU wangu, kwa kiu kikali ulichoona kwa ajili yangu,/ nifanyizie nisikukasirishe tena kwa kupenda mno chakula au kileo!/ YESU wangu, kwa uchungu wote uliouona juu ya msalaba,/ na kwa kuzimia kwako kwa ukali wa mateso,/ nijalie nguvu za kuvumilia kwa moyo taabu zote saa ya kuzimia kwangu!/ Nawe MARIA Mama yangu, kwa uchungu wote ambao moyo wako umejaa / ulipomwona Mwanao mpenzi akiinama kichwa na kuzimia,/ unifadhili nife kifo chema! Amina. 

na Abel Reginald

NCHI YANGU FAHARI YANGU TOUR