Monday, September 29, 2014

TAFAKARI YA NENO LA MUNGU DOMINIKA YA 24 YA MWAKA A, 28SEPTEMBA

TAFAKARI YA NENO LA MUNGU DOMINIKA YA 24 YA MWAKA A, 28SEPTEMBA



Tunakualika katika tafakari yetu, Dominika ya 24 ya mwaka A wa Kanisa tukilenga kukua katika toba na msamaha wa Mungu ulio wa kudumu. Katika historia, kadiri ya mangamuzi ya watu njia rahisi ya kujibu dhuluma ilikuwa ni kwa njia ya hasira na zaidi jino kwa jino (Kut 21:24) wakijaribu kutafuta mlinganyo sahihi (proportionality to the offence) lakini leo hii kadiri ya somo la kwanza toka kitabu cha Hekima ya Yoshua bin Sira tunaalikwa kutawala hasira zetu, kuacha chuki na kuacha kulipiza kisasi maana haya ni machukizo mbele ya Mungu. Ni hali ambayo huongeza taabu katika jumuiya badala ya kupunguza taabu. Basi kama mmoja wetu atashupaa katika haya, naye vivyohivyo atatendewa vivyohivyo yaani atajiondoa katika ufalme wa Mungu. Kumbe ndugu yangu mpendwa, leo tunaalikwa kupiga hatua katika safari ya kiroho tukiunganika na mausia ya Bwana kadiri ya Injili.

Mtume Paulo akiendeleza fundisho tunalolipata katika somo la kwanza anasema sisi hatuishi kwa ajili yetu wenyewe kama watu wenye chuki na visasi waishivyo bali twaishi kwa ajili ya Bwana. Anafundisha hili kwa sababu katika jumuiya ya kirumi mjini Roma kuna utengano kati ya wanaoshika sheria ya kufunga kadiri ya utamaduni wa mwanzo walipopokea imani na wale wanaojiona wa kisasa wanoshika sheria ya mapendo kwa ndugu. Kumbe ili kusahihisha dosari hii Mt. Paulo anasema sisi sote ni mali ya Bwana katika yote na hata tukifa tunakufa katika yeye. Ndiyo kusema matendo, maneno yetu, nyajibu zetu, sheria tunazoshika, familia zetu, parokia zetu, majimbo yetu tunayoyasimamia ni mali ya Kristu. Kwa hivi tuwajibike tukitambua hilo na mwishoni mapenzi ya Mungu yafanyike. Mafundisho ya Mt Paulo ni msaada kwa jumuiya zetu zinapojikuta ziko katika mgongano kwa sababu ya mwono tofauti. Zinaalikwa pande mbili pinzani kuketi na kutatua shida kwa pamoja kwa kuheshimiana.

Tunaendelea bado kutafakari Injili ya Mathayo, na leo Mwinjili atuambia kuwa msamaha ni wa kudumu. Msamaha hauna mipaka bali kama ulivyo upendo unaovumilia basi na msamaha wapaswa kuwa namna hii. Mt Petro akiwa bado katika mawazo ya kiyahudi ya kusamehe kimahesabu, yaani mara saba, anamwuliza Kristu nisamehe mara ngapi ndugu akinikosea? Kristu anakuja na fundisho jipya ya kwamba hakuna tena suala la mahesabu katika kusamehe bali mapenzi ya Mungu yatimizwe daima. Kristu anataka tuondoke katika mazoea ya kila siku na hivi tuingie katika mpango wa milele ambao ni msamaha wa kudumu. Mfano wa mtumwa katika Injili, mtumwa aliyesamehewa deni, deni ambalo asingeweza kulilipa mpaka anakufa kwa hakika ni kielelezo cha huruma ya Mungu iliyo milele!

Pamoja na huruma ya Mungu iliyo milele bado mwanadamu ni dhaifu, haoni vema. Huyu mtumwa aliyesamehewa deni lote yeye mwenyewe hakuweza kuwasamehe wajoli wake. Hiki ni kielelezo cha udhaifu wa mwanadamu ambaye daima hushindwa kusamehe na hasa kosa au dhambi inapojirudia. Ni picha ya kuwa tunahitaji daima huruma ya Mungu. Basi ndugu yangu mpendwa, tukumbuke kuwa kusamehe ni zawadi, ni fadhila tunayopaswa kuiomba daima ili tuweze kuunganika na Kristu mfufuka anayetutaka kusamehe daima na anayesamehe daima. Kinyume cha fadhila hii basi tutakuwa tumejiweka pembeni katika ufalme wa Mbinguni.

Tumalizie tukisema, Suala la kusamehe ni wajibu wa kila mtu awaye yote si wenye mamlaka ya juu tu katika jumuiya bali na wale wanaoongozwa na tukumbuke kuanguka katika dhambi ya kutosamehe na kukuza chuki zisizoisha ni hatari kubwa iliyo mbele yetu. Yaweza kuzuia na hivi tukakosa kuingia mbinguni. Fikiri kidogo mtu asemaye “Mimi nitakapokufa mtu fulani asikaribie na hata kuweka udongo kwenye kaburi langu!! Chuki ya ujazo huu haina maelezo lakini yatishishia usalama wa roho ya mtu huyo aliyefariki!! Tafakari kidogo!Tumwombe Mungu daima atutangulie na kutulinda katika kutekeleza wajibu wa kusamehe. Tumsifu Yesu Kristu.
Tafakari hii imeletwa kwako na Pd Richard Tiganya Cpps
TAFAKARI YA NENO LA MUNGU DOMINIKA YA 24 YA MWAKA A, 28SEPTEMBA

MASOMO YA JUMAPILI TAREHE 28/09/2014 MWAKA" A" WA KANISA

28
 SEPTEMBER
 JUMAPILI YA 26 YA MWAKA "A" 2014.


RATIBA ZA IBADA

KIGANGO CHA BOKO.
IBADA YA MISA YA KWANZA 12:15 – 1:45 ASUBUHI
IBADA YA MISA YA PILI 2:00 – 3:50 ASUBUHI
IBADA YA MISA YA TATU SAA 4:00-5:20 ASUBUHI
KIGANGO CHA MBWENI.
IBADA YA MISA YA KWANZA 1:15 – 2:55 ASUBUHI
IBADA YA MISA YA PILI 3:00 – 4:50 ASUBUHI
KIGANGO CHA MT. RAFAEL.
IBADA YA MISA YA KWANZA 1:00 – 2:55 ASUBUHI
IBADA YA MISA YA PILI 3:00 – 4:50 ASUBUHI
KIGANGO CHA ANTHONY WA PADUA – MBWENI MPIJI.
IBADA YA MISA NI 3:00 – 5:00ASUBUHI

SOMO  1. Eze. 18:25-28
Bwana ameniambia hivi: Ninyi mwasema; Njia ya Bwana ni sawa. Sikilizeni sasa, Enyi nyumba ya Israeli; je! njia yangu siyo iliyo sawa? Njia zenu sizo zisizo sawa? Mwenye haki atakapoghairi, na kuiacha haki yake, na kutenda uovu, atakufa katika uovu huo; katika uovu wake alioutenda atakufa. Tenamtu mwovu atakapoghairi, na kuuacha uovu wake alioutenda, na kutenda yaliyo halali na haki, ataponya roho yake, nayo itakuwa hai. kwa sababu atafakari, na kughairi, na kuyaacha makosa yake yote aliyoyatenda, hakika ataishi, hatakufa. 

SOMO  2. Flp. 2:1-11


Ikiwako faraja yo yote katika Kristo, yakiwako matulizo yo yote ya mapenzi, ukiwako ushirika wo wote wa Roho, ikiwako huruma yo yote na rehema, ijalizeni furaha yangu, ili mwe na nia moja, mwenye mapenzi mamoja, mwenye Roho moja, mkinia mamoja. Usitende neon lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa na bora kuliko nafsi yake. kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo yake mwenyewe. Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu;ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa binadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa Yesu Kristo ni Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba.

  INJILI.Mt. 21:28-32


 Yesu aliwaambia wakuu wa makuhanina wazee, Mwaonaje? mtu mmoja alikuwa na wana wawili; akamwendea yule wa kwanza, akasema, mwanangu, leo nenda kafanya kazi katika shamba la mizabibu. Akajibu akasema, Naenda, Bwana;  asiende. Akamwendea yule wa pili, akasema vile vile. Naye akijibu akasema, sitaki; baadaye akatubu, akaenda. je! katika hao wawili ni yupi aliyefanya mapenzi ya babaye? Wakamwambia, Ni yule wa pili. Basi Yesu akawaambia, Amin, nawaambia, watoza ushuru na makahaba wanatangulia mbele yenu kuingia katika ufalme wa Mungu. kwa sababu Yohana alikuja kwenu kwa njia ya haki, ninyi msimwamini; nanyi hata mlipoona, hamkutubu baadaye, ili kumwamini.


Matangazo
jiandaye na Kongamano la ujirani kati ya Parokia ya Boko na bunju' mwema, nunue Ticketi yako sasa kwa Tshs 18,000. Kongamano litafanyika kuanzia tarehe 28-29/11/2014, Parokiani Boko w

 

 

 


Sunday, September 28, 2014

SALA YA KUMWOMBEA MGOJWA


Ee Bwana Yesu Kristo, ulishirikisha ubinadamu wetu kwa hiari yako upate kuwaponya wagojwa na kuwaokoa wanadamu wote.
Sikiliza kwa huruma sala zetu, umjalie afya ya mwili na roho huyu ndugu (taja jina lake) yetu. Mfariji kwa kinga yako, mpe nafuu kwa nguvu yako.
Msaidie atumaini kuokoka kwa njia ya mateso, kama ulivyotufundisha kutumaini hapo ulipoteswa kwa ajili yetu.
Utujalie sisi sote amani na furaha zote za ufalme wako huko unakoishi daima na milele. Amina

Thursday, September 25, 2014

Hawa Wote Walikuwa na sisi na Wengine Bado wapo na sisi Utume wa Viwawa unazidi kusonga mbele




 vijana wa Parokia ya Bunju wakiwa na mlezi wao kipindi hicho 2012 kutoka kushoto ni Getruda, Fr, Paul Malewa, Lucy Linuc

Vijana wa Parokia ya Boko wakiwa kijiji cha furaha mbweni waliposhiriki semina ya siku moja(2012) 


Ruben, Diana na wengine ambao kwa sasa hatujui utume wao wanafanyia wapi
Vijana wa Kigango cha Bunju(kwa sasa Parokia) wakiwa katika ibada ya Matawi 2012 Don Bosco Upanga

Viongozi wa Kigango cha Bunju(kwa sasa Parokia)kutoka kushoto ni Lily Machota na Fredinando
Sister mlezi wa VIWAWA Parokia ya Boko Sir. Sabina

Aliyekuwa Padre Mlezi wa VIWAWA Parokia ya Boko PD. Dominiki Mwaluko kwa sasa ni Paroko Parokia ya Kunduchi
vijana wakitumbuiza kwenye sherehe ya Pentekoste


Monday, September 22, 2014

MASOMO YA DOMINIKA YA TAREHE 21/09/2014, JUMAPILI 25 MWAKA A


21
 SEPTEMBER
 JUMAPILI YA 25 YA MWAKA "A"
2014 


RATIBA ZA IBADA
KIGANGO CHA BOKO.
IBADA YA MISA YA KWANZA 12:15 – 1:45 ASUBUHI
IBADA YA MISA YA PILI 2:00 – 3:50 ASUBUHI
IBADA YA MISA YA TATU SAA 4:00-5:20 ASUBUHI
KIGANGO CHA MBWENI.
IBADA YA MISA YA KWANZA 1:15 – 2:55 ASUBUHI
IBADA YA MISA YA PILI 3:00 – 4:50 ASUBUHI
KIGANGO CHA MT. RAFAEL.
IBADA YA MISA YA KWANZA 1:00 – 2:55 ASUBUHI
IBADA YA MISA YA PILI 3:00 – 4:50 ASUBUHI
KIGANGO CHA ANTHONY WA PADUA – MBWENI MPIJI.
IBADA YA MISA NI 3:00 – 5:00ASUBUHI

SOMO  1. isa. 55:6-9
Mtafutuni Bwana, maadamu anapatikana,
Mwiteni, maadamu anapatikana,Mwiteni, maadamu yu karibu;
Mtu mbaya na aache njia yake,
Na mtu asiye haki aache mawazo yake;
Na amrudie bwana. naye atamrehemu;
Na arejee kwa Mungu wetu,
Naye atamsamehe kabisa.
maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; asema Bwana. Kwa maana kwa vile mbingu zilivyo juu sana kuliko nchi, kadhalika njia zangu zi juu sana kuliko njia zenu, na mawazo yangu kuliko mawazo yenu.
SOMO 2.Flp.1:20-24,27
Kristo ataadhimishwa katika mwili wangu; ikiwa kwa maisha yangu, au ikiwa kwa mauti yangu. Kwa maana kwangu mimi kuishi ni Kristo, na kufa ni faida. Ila ikiwa kuishi katika mwili, kwangu mimi ni matunda ya kazi; basi nitakalolichagua silitambui. Ninasogwa katikati ya mambo mawili; ninatamani kwenda zangu nikae na Kristo; maana ni vizuri zaidi sana; bali kudumu katika mwili kwahitajiwa zaidi kwa ajili yenu. Lakini mwenendo wenu na uwe kama inavyoipasa Injili ya Kristo.
INJILI. Mt. 20:1-16
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: ufalme wa mbinguni umefanana na mtu mwenye nyumba, aliyetoka alfajiri kwenda kuajiri wakulima awapeleke katika shamba lake la mizabibu. Naye alipokwisha kupatana na wakulima kuwapa kutwa dinari, aliwapeleka katika shamba lake la mizabibu. Akatoka mnamo saa tatu, akaona wengine wamesimama sokoni wasiokuwa na kazi; na hao nao akawaambia, Enendeni nanyi katika shamba langu la mizabibu, na iliyo haki nitawapa. Wakaenda. Akatoka tena mnamo saa sita na saa kenda, akafanya vile vile. Hata kama saa kumi na moja akatoka, akakuta wengine wamesimama, akawaambia, Mbona umesimama hapa mchana kutwa bila kazi? Wakamwambia, kwa sababu hakuna mtu aliyetuajiri. Akawaambia, enendeni nanyi katika shamba la mizabibu. Kulipokuchwa, yule bwana wa shamba akamwambia msimamizi wake, waite wakulima, uwalipe ujira wao, ukianzia wa mwisho hata wa kwanza. Na walipokuja wale wa saa kumi na moja,walipokea kila mtu dinari. Na wale wa kwanza walipokuja, walidhani kwamba watapokea zaidi; na hao pia wakapokea kila mtu dinari. Basi wakiisha kuipokea, wakamnng’ukia mwenye nyumba, wakisema, Hao wa mwisho wametenda kazi ya saa moja tu, nawe umewasawazishia na sisi tuliostahimili taabu na hari za mchana kutwa. Naye akamjibu mmoja wao, akamwambia, Rafiki, sikudhulumu; hukupatana nami kwa dinari? Chukua iliyo yako, uende zako; napenda kumpa huyu wa mwisho sawa na wewe. Si halali yangu kutumia vilivyo vyangu kama nipendavyo? Au jicho lako limekuwa ovu kwa sababu ya mimi kuwa mwema? vivyo hivyo wa mwisho watakuwa wa kwanza, na wa kwanza watakuwa wa mwisho.

Sunday, September 21, 2014

KWANINI UFUNGE NDOA

“Kamba yenye nyuzi tatu haiwezi kukatika upesi.”—MHUBIRI 4:12.
JE, UNAPENDA kwenda kwenye harusi? Wengi wanapenda, kwa sababu mara nyingi hizo huwa pindi zenye kufurahisha sana. Bwana na bibi-arusi wanavalia mavazi yenye kupendeza kwelikweli. Zaidi ya hilo, nyuso zao zinaonyesha kwamba wana shangwe nyingi! Siku hiyo, wana furaha nyingi na inaonekana wana matazamio mengi mazuri ya wakati ujao.
2 Hata hivyo, ukweli ni kwamba ndoa nyingi leo ziko mashakani. Ingawa tunawatakia mema wenzi wapya wa ndoa, nyakati nyingine tunajiuliza: ‘Je, ndoa hii itakuwa na furaha? Itadumu?’ Majibu ya maswali hayo yanategemea ikiwa mume na mke wanaamini na kutumia shauri la Mungu kuhusu ndoa. (Methali 3:5, 6) Wanahitaji kufanya hivyo ili waendelee kukaa katika upendo wa Mungu. Acheni tuchunguze majibu ya Biblia kwa maswali haya manne: Kwa nini ufunge ndoa? Ikiwa utafunga ndoa, utachagua mwenzi wa aina gani? Unaweza kujitayarisha jinsi gani kwa ajili ya ndoa? Na ni nini kinachoweza kuwasaidia wenzi wa ndoa waendelee kuwa na furaha?
KWA NINI UFUNGE NDOA?
3 Watu fulani wanaamini kwamba siri ya kuwa na furaha ni kufunga ndoa na kwamba huwezi kamwe kutosheka au kuwa na furaha maishani ikiwa huna mwenzi wa ndoa. Hilo si kweli hata kidogo! Yesu, ambaye alikuwa mseja, alisema useja ni zawadi, naye aliwahimiza wale wanaoweza waupe nafasi. (Mathayo 19:11, 12) Mtume Paulo pia alizungumzia faida za useja. (1 Wakorintho 7:32-38) Hata hivyo, Yesu na Paulo hawakuweka sheria kuhusu jambo hilo; na ‘kukataza kufunga ndoa’ ni ‘fundisho la roho waovu.’ (1 Timotheo 4:1-3) Lakini wale wanaotaka kumtumikia Yehova bila kukengeushwa wanaweza kufaidika kwa kuendelea kuwa waseja. Basi, si jambo la hekima kufunga ndoa kwa sababu ndogo-ndogo, kama vile kufunga ndoa kwa sababu tu wenzako wamefunga ndoa au kwamba wanakutia moyo ufanye hivyo.
4 Kwa upande mwingine, je, kuna sababu nzuri za kufunga ndoa? Ndiyo. Ndoa pia ni zawadi kutoka kwa Mungu mwenye upendo. (Mwanzo 2:18) Kwa hiyo, inatimiza mambo fulani mazuri na inaweza kuleta furaha. Kwa mfano, ndoa nzuri ndio msingi bora wa maisha ya familia. Watoto wanahitaji kulelewa katika mazingira yanayofaa wakiwa na wazazi wanaowapenda, wanaowatia nidhamu, na kuwapa mwongozo. (Zaburi 127:3; Waefeso 6:1-4) Hata hivyo, kusudi la ndoa si kupata na kulea watoto tu.
5 Fikiria andiko la msingi la sura hii pamoja na mistari inayotangulia: “Wawili ni afadhali kuliko mmoja, kwa maana wana thawabu nzuri kwa ajili ya kazi yao ngumu. Kwa maana mmoja wao akianguka, yule mwingine anaweza kumwinua mwenzake. Lakini itakuwaje kwa yule aliye peke yake akianguka wakati ambapo hakuna mwingine wa kumwinua? Tena, wawili wakilala pamoja, watapata joto; lakini aliye peke yake anawezaje kupata joto? Na mtu akiweza kumshinda nguvu mmoja aliye peke yake, wawili wakiwa pamoja wataweza kusimama dhidi yake. Nayo kamba yenye nyuzi tatu haiwezi kukatika upesi.”—Mhubiri 4:9-12.
6 Andiko hilo linazungumzia hasa faida ya urafiki. Bila shaka, ndoa ni muungano wa marafiki wa karibu zaidi. Kama andiko hilo linavyoonyesha, katika muungano huo wenzi wa ndoa wanaweza kupata msaada, faraja, na ulinzi. Ili kifungo cha ndoa kiwe imara zaidi, mengi zaidi yanahitajika. Kamba yenye nyuzi mbili, kama mstari huo unavyodokeza, inaweza kukatika. Lakini kamba yenye nyuzi tatu zilizosokotwa au kufumwa pamoja haikatiki kwa urahisi. Lengo kuu la mume na mke linapokuwa kumpendeza Yehova, ndoa yao ni kama kamba yenye nyuzi tatu. Kwa kuwa Yehova anahusishwa kabisa, ndoa hiyo inakuwa muungano imara sana.
7 Pia, katika ndoa ndipo tu tamaa za ngono zinaweza kutoshelezwa inavyofaa. Ni katika kifungo hicho tu ambapo mahusiano ya kingono huonwa kwa kufaa kuwa chanzo cha shangwe. (Methali 5:18) Hata baada ya mtu kupita kipindi ambacho Biblia inakiita “upeo wa ujana”—wakati ambapo tamaa za ngono huanza kuwaka—huenda bado akahitaji kuzuia tamaa hizo. Zisipozuiliwa, tamaa hizo zinaweza kumwingiza katika mwenendo mchafu au usiofaa. Paulo aliongozwa na roho ya Mungu kuwapa watu ambao hawajafunga ndoa shauri hili: “Ikiwa hawawezi kujizuia, acheni wafunge ndoa, kwa maana ni bora kufunga ndoa kuliko kuwaka tamaa.”—1 Wakorintho 7:9, 36; Yakobo 1:15.
8 Hata kuwe na sababu gani za kufunga ndoa, mtu anapaswa kuona mambo kihalisi. Kama Paulo alivyosema, wale wanaofunga ndoa “watakuwa na dhiki katika mwili wao.” (1 Wakorintho 7:28) Watu waliofunga ndoa hupata matatizo fulani ambayo waseja hawapati. Hata hivyo, ukiamua kufunga ndoa, unaweza kufanya nini ili upunguze matatizo na kuwa na furaha zaidi? Njia moja ni kuchagua mwenzi wa ndoa kwa hekima. Etaendelea

Tafakari ya Neno la Mungu Domonika ya 25 ya Mwaka A,

Mpendwa, tunatafakari masomo ya Jumapili ya 25 ya mwaka wa A wa Kanisa, tukialikwa kuwa na matumaini daima katika kumtafuta Bwana na kutambua kuwa wema wa Mungu ni wa milele kwa watu wote na fikra zake ni tofauti na fikra za kibinadamu. Katika somo la kwanza Waisraeli wako utumwani Babeli kwa sababu hawakutii mausia ya Bwana na zaidi wanaona hawawezi kusamehewa dhambi zao, wamepoteza tumaini na wanaona kana kwamba Mungu amewatupa na kuwaacha kabisa. Zaidi ya hilo wanaongeza kosa jingine tena la kumwona Mungu anayefikiri kama wao, wanafikiri hawezi kuwasamehe tena.


Mpendwa, katika shida yao hiyo Mungu anamtuma Nabii Isaya awaambie kuwa fikra na njia za Mungu ni za juu mno ni tofauti na fikira za kibinadamu kiasi kwamba si rahisi kuzielewa. Zaidi ya hilo Isaya anawakumbusha kuacha njia zao mbaya na kumrudia Bwana. Kumrudia Bwana si tu kuacha dhambi, bali pia kubadili namna ya kumtazama Mungu, Mungu aliye haki na mkamilifu. Mawazo haya yatajitokeza waziwazi katika Injili ambapo tunaona Mungu anayewapenda wote wadhambi kwa wema.


Mtume Paulo akikoleza ujumbe wa nabii Isaya anawaambia Wafilipi, hata kama kuna shida katika maisha yao watambue kuwa kuishi kwao ni Kristu, ndiyo kusema la maana katika maisha yao ni Kristu mfufuka. Mara kadhaa watu wapatapo shida huanza manunguniko dhidi ya Mungu na kusahau kwamba yote waliyonayo yametoka kwake. Wanasahau kuwa, kwa njia ya msalaba yaani njia ya mateso, Kristu ametustahilisha kwenda mbinguni. Ndiyo kusema, hata sisi tuliodhaifu tunapaswa kupitia njia ya mateso ili kuweza kufika Mbinguni. Kwa hakika mtume Paulo anapoandika barua hii kwa Wafilipi yuko katika wakati mgumu yaani kuchagua kufa ili akae na Kristu au kuendelea kuhubiri Injili kwa mataifa, na mwisho anaona ahitimishe fikra zake akisema kuishi kwangu ni Kristu na kufa ni faida. Hapa tunaonja imani ya Paulo ilivyozama katika Mwana wa Mungu.

Tujiulize je kwetu sisi kuishi na kufa, twaweza kuvipokea kama alama ya ushindi katika imani kama Mtume Paulo? Mpendwa msikilizaji jitafiti na hivi unapokuwa umechoka, unapokuwa umefikia mwisho wa maisha yako uweze kusema nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza na imani nimeilinda sasa kufa kwangu ni faida na kuishi kwangu ni Kristu!


Mpendwa mwana wa Mungu tukiongozwa na mwinjili Mathayo, tunapata kuonja kuwa mawazo ya Mungu ni ya juu sana kuliko yetu. Jambo hili linajionesha wazi katika Injili ya leo pale ambapo Bwana wa shamba anawaajiri watu mbalimbali katika masaa tofauti na mwishoni anawalipa ujira sawa. Mpendwa katika hali ya kawaida, Bwana huyu angepaswa kuwalipa tofauti kwa maana muda wa kazi ulikuwa tofauti. Kuwalipa ujira sawa pia ni namna ya kusema kuwa uvivu uendelee katika ulimwengu, tuseme hakuna ile haki ya kawaida yaani common justice! Hii ni namna yetu ya kufikiri na hata namna ya watu wa wakati huo, lakini je Mwinjili anataka kutuambia nini? Je Bwana afikiri kama sisi?


Kwa hakika kuwalipa ujira sawa maana yake, wema wa Mungu ni kwa ajili ya wema na wabaya. Wale walioajiriwa kwanza ndio walisadikiwa kuwa wema na wale wa baadaye ndio kundi wakilishi la walio wabaya. Pamoja na hilo kuna jambo jingine jema, kwamba mwenye shamba anapenda kila mmoja afanye kazi, asiishi bila wajibu, ajisikie katikati ya jumuiya ya watu kwa maana kazi huleta heshima. Kwa jinsi hiyo kazi ya wokovu inaendelea na inawaletea heshima watu wote.
Mfano huu wa mwenye shamba unatufundisha kuwa Mungu si mhasibu wala meneja anayewalipa watu kulingana na jasho lao tu, bali kulingana na upendo wake aliokusudia tangu alipoumba ulimwengu. Hatuna uwezo wa kupata stahili yoyote toka kwa Mungu kwa nguvu zetu bali kwa uweza wake, huruma yake na mapendo yake ya milele. Kwa wazo hili tunarudi kwa nabii Isaya anayetuambia kuwa njia zake ni za juu mno na mawazo yake hatuwezi kuyafikia. Tunaalikwa kutambua kuwa wokovu si kwa maveterani peke yao bali hata vijana wanaokuja saa kumi na moja jioni! Hakutakuwa na upendeleo wowote katika wokovu cha msingi ni kumtafuta Bwana madamu anapatikana. Tumsifu Yesu Kristu.

Tafakari hii imeletwa kwako na Pd Richard Tiganya Cpps

NCHI YANGU FAHARI YANGU TOUR