Tuesday, February 26, 2013

Kwaresima ni kipindi cha toba, matendo ya huruma na utii kwa maagizo ya Mwenyezi Mungu

Wakati huu wa Kipindi cha Kwaresima sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu, tayari kuanza hija ya maisha mapya, kwa kumtii Mwenyezi Mungu. Inafahamika kuwa, Imani bila matendo hiyo imekufa ndani mwake! Kumbe, kuna haja kwa waamini kumwilisha imani yao kwa Kristo na Kanisa lake kwa njia ya matendo ya huruma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, kila mtu akijitahidi kuwa kweli ni Msamaria mwema kwa jirani yake. Ni mwaliko wa kuwa na mwono mpana zaidi kwa kuwaangalia wote wanateseka kutokana na majanga asilia, vita na madhulumu.

Kwaresima kiwe ni kipindi cha maandalizi ya kina katika Maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, yaani, mateso, kifo na ufufuko wa Kristo. Kwaresima iwawezeshe waamini kujenga fadhila ya imani, matumaini na mapendo katika Fumbo la Ufufuko wa Kristo, ili hatimaye, kuweza kulitolea ushuhuda.  Imani ya Wakristo wa mwanzo ilijikita katika Ufufuko, wakaliona Kaburi wazi, hapo ukawa ni mwanzo wa Habari Njema ya Wokovu inayojikita katika: maisha, maneno na matendo ya Yesu Kristo kwa ajili ya wokovu wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

No comments:

Post a Comment

NCHI YANGU FAHARI YANGU TOUR