Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linafungua rasmi Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, uliotangazwa na Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 2 Februari 2015, Siku kuu ya kutolewa Bwana Hekaluni, sanjari na maadhimisho ya siku ya kumi na tisa ya watawa duniani, iliyoanzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II. Maadhimisho haya yanafanyika katika ngazi ya Kijimbo na katika baadhi ya Majimbo makuu.
Hayo yamesemwa na Askofu Renatus Nkwande, Mwenyekiti wa Tume ya Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican. Kwa namna ya pekee anasema, Watawa wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa imani dhidi ya ukanimungu, kwa kujikita katika maongozi ya Mungu, Injili ya Kristo na Mashauri ya Kiinjili.
Watawa wanachangamotishwa na Mama Kanisa kuwa ni Manabii kwa kufundisha, lakini zaidi kwa njia ya mfano bora wa maisha na huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Watawa wakumbuke kwamba, wao ni vyombo muhimu sana vya Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili, kumbe, ni jukumu lao kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji ili tunu msingi za Kiinjili ziweze kuwafikia watu wengi zaidi. Watekeleze dhamana hii kwa ari, moyo mkuu na sadaka, hata ikibidi kumimina maisha yao kwa Kristo na Kanisa lake, wawe tayari!
Watawa wanapaswa kuwa ni chemchemi ya furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake, kwa kusali na kutafakari Neno la Mungu, kwa njia ya maisha ya Sakramenti na Mashauri ya Kiinjili. Pale ambapo watawa watashindwa kutekeleza dhamana na wajibu wao kutokana na ubinafsi na hata pengine kumezwa na malimwengu, hapo watambue kwamba, furaha ya kweli itatoweka na hapo wakaanza kukiona cha mtema kuni!
Mashirika ya kitawa anasema Askofu Nkwande yawe makini katika kuwateuwa watu wanaotaka kujiunga na maisha ya kitawa, vinginevyo wanaweza kujikuta wanakusanya watu wenye malengo tofauti kabisa na maisha ya kitawa! Hapa kuna umuhimu wa kuhakikisha kwamba, Mashirika ya kitawa yanajikita katika maisha ya kijumuiya, sala, tafakari ya Neno la Mungu na huduma kwa jamii, ili kukoleza karama ya Shirika husika na moyo wa mwanzilisho wao!
No comments:
Post a Comment