Wednesday, November 6, 2013

Mnaalikwa kwenye Karamu ya Bwana! Wakristo msiridhike kuwa katika orodha ya wageni waalikwa! Mnatakiwa kufanya makubwa zaidi!




Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, Jumanne, tarehe 5 Novemba 2013 anawaalika waamini kuhakikisha kwamba, wanasherehekea kikamilifu Karamu ya Bwana. Wakristo watambue kwamba, wanaalikwa na Mwenyezi Mungu kushiriki karamu hii wakiwa na dhamiri safi na nyofu.

Karamu ya Bwana ni sherehe inayobubujika furaha, matumaini na mapendo kutoka kwa Kristo; sherehe ambayo inawakumbatia wote pasi na ubaguzi kwani wao ni sehemu ya viungo vya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa, kila mtu ana wajibu na dhamana ya kutekeleza kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa. Wakristo wajitambue kwamba, wao ni sehemu muhimu sana ya Kanisa la Kristo! Karamu hii ni mwaliko wa kujenga na kudumisha umoja miongoni mwa Wakristo, kila mwamini akijitahidi kujitakatifuza kwa nyenzo mbali mbali zinazotolewa na Mama Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, Kanisa linawakumbatia watakatifu na wadhambi; na kwamba, kila mmoja wao ana karama na zawadi ambayo amekirimiwa na Roho Mtakatifu; zawadi ambayo anapaswa kuifanyia kazi barabara kwa ajili ya mafao ya Kanisa. Kanisa linapaswa kuwakumbatia wote kwa kuanzia na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Inasikitisha kuona kwamba, kuna baadhi ya Wakristo wamepewa mwaliko na wako kwenye orodha ya waalikwa, lakini bado wanagoma kuhudhuria Sherehe ya Mwanakondoo wa Mungu kwa visingizio kibao! Wanashindwa kutambua kwamba, kuingia ndani ya Kanisa ni mwaliko na neema inayowataka waamini kujenga na kuimarisha Jumuiya ya Kikristo, kila mtu akitumia kikamilifu karama na vipaji vyake kwa ajili ya Kanisa na Jirani zake. Kristo anaendelea kuwaalika waamini kufanya hija inayowapeleka kwenye maisha ya uzima wa milele na kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye kiongozi mkuu wa safari hii ya maisha ya kiroho.

Baba Mtakatifu anasema, Yesu ni mwingi wa huruma na mapendo, hata kwa wale wanaoonesha shingo ngumu kwa mwaliko wake. Anaendelea kuwasubiri kwa saburi na mapendo makuu. Yesu anawapenda watu ambao ni wanyofu na wa kweli katika maisha yao: kwa maneno na matendo.

Inapendeza ikiwa kama Wakristo wote wataweza kushiriki katika Karamu ya Bwana, ili kuonja furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo na wala wakristo wasiridhike kwamba, majina yao yameandikwa kwenye orodha ya waalikwa kwenye Karamu ya Bwana, bali wanatakiwa kushiriki bila kutoa visingizio!

Monday, November 4, 2013

Kilele cha Mwaka wa Imani Kitaifa, Bagamoyo kufunika!



Maadhimisho ya Mwaka wa Imani  limekuwa ni tukio ambalo limeasidia kukuza na kuimarisha imani ya waamini kwa Kristo na Kanisa lake. Waamini katika ngazi mbali mbali wamefanya tafakari ya kina kuhusu: Fumbo la Msalaba, Sakramenti za Kanisa na umuhimu wake, Maisha ya Sala na Ushuhuda wa maisha ya Kikristo kama kielelezo makini cha imani tendaji.

Maadhimisho ya Mwaka wa Imani nchini Tanzania yanakwenda sanjari na Jubilee ya Miaka 150 ya Ukristo nchini Tanzania. Katika kipindi chote hiki Kanisa Katoliki limejikita katika Uinjilishaji unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Mheshimiwa Padre Patern Patrick Mangi, Katibu mtendaji Idara ya Liturujia ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania  anafafanua kuhusu mikakati ya Maaskofu Katoliki Tanzania katika kufunga Mwaka wa Imani huko Bagamoyo.

Maadhimisho haya yataanza hapo tarehe 8 Novemba 2013 na kilele cha Maadhimisho ya Kufunga Mwaka wa Imani Kitaifa ni hapo tarehe 10 Novemba 2013, ili kutoa nafasi kwa Familia ya Mungu Majimboni, kushiriki na Baba Mtakatifu Francisko katika kuufunga rasmi Mwaka wa Imani wakati wa Sherehe za Kristo Mfame wa dunia. Familia ya Mungu itapata nafasi ya kutafakari mada mbali mbali zilizoandaliwa na Maaskofu Katoliki Tanzania.

Sunday, November 3, 2013

Tafakari ya masomo ya leo dominika ya 31 mwaka C 03/11/13

Somo La Kwanza: Hek. 11:22-12:2
Wimbo Wa Katikati: Zab. 145: 1-2, 16-18, 123-14 (K)
Somo La Pili: 2 Thes.1: 11-2:2
Injili: Lk. 19: 1-10
Tafakari y ya masomo:
Injili ya leo, inatuadithia juu ya mtosa ushuru Zakayo. Zakayo alikuwa na mapungufu makuu mawili. Moja, alikuwa na upungufu wa asili, alikuwa mfupi wa kimo. Katika msongamano mkubwa uliokuwa unamfuata Yesu, alikuwa hana nafasi ya kumwona kwani watu warefu wangemzuia. Pili, alikuwa na upungufu wa kijamii. Kazi yake ya kutosa ushuru ilimfanya achukiwe na Wayahudi wenzake. Kwani, watosa ushuru walikuwa wadanganyifu kwa waliwatosa watu ushuru mkubwa zaidi, huku wakijitajirisha na pesa za ziada walizotosa watu. Hivyo basi, hawakupendwa na jamii ya  Wayahudi.

Pamoja na mapungufu haya ya kiasili na hata ya kijamii, ambayo yangekuwa sababu ya kutosha kabisa ya kumzuia Zakayo asimuone Yesu. Zakayo hakukubali, nafasi hii ya kumuona Yesu, impite. Alitoka mbio, akapanda juu ya mkuyu ili amuone Yesu. Yesu alizizawadia juhudi za Zakayo kwa kumuita, “Zakayo, shuka upesi, kwa kuwa leo imenipasa  kushinda nyumbani mwako.”

Yesu anamtumia Zakayo kutuonesha jinsi Mungu anavyozijali juhudi za wale wajitahidio bila kukata tamaa kutokana na mapungufu waliyonayo. Kama Zakayo asingejitahidi kutafuta mbinu za kumuona Yesu, hata kwa kupanda mkuyuni, angekufa bila kutimiza ndoto yake ya kutaka kumuona Yesu. Mara nyingi tumejiona kuwa kutokana na mapungufu yetu hatuwezi kutimiza ndoto zetu maishani. Tunapoteza muda tukisema kama ningekuwa na hili ama lile ningefanya hivi ama vile. Kama ningezaliwa mwanamke ama mwanaume ningefanya hili wala lile. Kama ningezaliwa katika familia iko hivi ningefanya hili ama lile; Kama ningekuwa na uwezo huu ama ule basi mambo yangu yangeenda vizuri; Kama muda huu, ndio ningekuwa mwanafunzi, ningesoma sana ili niwe na maisha mazuri zaidi. Mwanafunzi naye anasema, ningekuwa na akili kama fulani, ningefanya vizuri; ama ningekuwa shule bora zaidi ningesoma kwa bidii sana. Hizi ndoto za mchana hazitatusaidia. Kitakachotusaidia ni kukubali mapungufu yetu na hapo kuangalia ni kitu gani Mungu ametuwekea karibu kitakachotuwezesha kutimiza ndoto zetu. Kama Zakayo asingekuwa mtu wa jitihada, asingeona kuwa angeweza kupanda mtini na hivyo kuyashinda mapungufu yake. Kama Zakayo asingekuwa ni mtu wa maono, mkuyu ungeendelea kubakia mkuyu tu huenda ungekuwa mojawapo ya vikwazo vya kumzuia asimuone Yesu. Angeendelea kulalamika na hata kuulalamikia mkuyu. Zakayo alipoutazama mkuyu aliona jinsi unavyoweza kutumika kuwa kifaa cha kumwezesha kumuona Yesu na siyo kikwazo cha kumuona Yesu. Ufupi wake, japo ulikuwa ni upungufu wa asili ulikuwa sababu yake ya kuzitumia jitihada zake. Zakayo alikuwa na mtazamo chanya katika maisha. Mtazamo huu ulimfanya kuweza kuvibadilisha vizingiti katika njia yake ya maisha na kuvifanya ngazi ya kumwezesha kutimiza ndoto yake katika maisha. 

Sisi pia, inatubidi, kuangalia kwa makini kabisa ni mapugufu gani yanayotufanya tushindwe kutimiza ndoto zetu maishani.(ulevi? Wivu? Tamaa? Hasira? Uwongo? Uadui? Chuki? Uvivu? Nk.) Baada ya kuyaona mapungufu hayo, tuangalie kwa makini, tena sana, ni kitu gani Mungu ametuwekea karibu nasi ambacho kitatufanya tuweze kuyashinda mapungufu haya. Hakuna na tatizo lisilo na suluhu kwa wale wanaoamini. Ila tu ni lazima tukazie macho mapungufu yetu, tuangalie pia na zile nyenzo Mungu alizoweka karibu nasi ambazo zitatuwezesha kukwea na kuvishinda vikwazo hivvyo na baada ya kuviona tumuombe Mungu kwa bidii zote, kwani  yeye alikuja ili tuwe na uzima kamili (Jn 10:10) na siyo mapungufu. Zakayo aliona mti wa mkuyu, wewe pia inakubidi utafute mkuyu wako utakao panda, na hapo utamsikia Bwana akikuambia, “Leo, imenipasa niwe nyumbani mwako.” AMINA

Friday, November 1, 2013

Maadhimisho ya Siku ya Watakatifu wote na siku ya Marehemu wote

Papa afafanua kiini cha Maadhimisho ya Siku ya Watakatifu wote na siku ya Marehemu wote.



BabaMatakatifu Francisko akiendelea kutoa tafakari juu ya sala ya Nasadiki, kwa Jumatano hii, alilenga zaidi katika usharika na Watakatifu, kama Kateksimu ya Kanisa Katoliki inavyotukumbusha sisi kwamba, usharika huu ni kwa Mambo Matakatifu na kati ya watu Watakatifu (No. 948 ).

Papa alizama zaidi katika sehemu ya Pili ya kuw ana usharika na Marehemu Watakatifu , ukweli unaohitaji ufafanuzi zaidi katika imani yetu, akieleza pia kwamba, hutukumbusha pia kwamba, hatuko pweke, lakini kuna uwepo wa usharika wa maisha kwa wale wanaokuwa wa Kristu. Usharika mmoja unaoundwa na imani , katika ukweli wake, neno hili Watakatifu hurejea wale wanao mwamini Yesu Kristu kuwa ndiye Bwana wa Maisha na hivyo humwilishwa kwake Yeye ndani ya kanisa kupitia ubatizo. Na kwa namna hiyo , Wakristu wa kwanza waliitwa pia Watakatifu.

Papa aliendelea kufundisha , Usharika wa Watakatifu ni kina halisi cha maana ya Kanisa kwa sababu kama wakristu kupitia Ubatizo , tunafanywa kuwa washiriki wa maisha ya usharika mmoja na upendo wa Utatu Mtakatifu. Na hivyo sote tunaunganishwa mmoja kwa mwingine na kiungo cha ubatizo katika Mwili wa Kanisa. Na kupitia usharika huu wa kidugu, tunawekwa karibu zaidi na Mungu, na tukitakiwa kusaiidiana mmoja kwa mwingine kiroho.

Papa alieleza na kuirejea Injili Yohana ambayo inasema kwamba , kabla ya mateso yake, Yesu aliomba kwa Baba kwa ajili ya umoja kwa wanafunzi wake kwa maneno haya : “Naomba ili wote wawe kitu kimoja kama wewe, Baba , ulivyo ndani yangu , nami ndani yako. Naomba wawe kitu kimoja kusudi ulimwengu upate kuamini kwamba wewe ndiye uliyenituma "( 17:21). Kanisa , katika kweli yake kamili , ni usharika na Mungu , usharika wa upendo na Kristo na Baba katika Roho Mtakatifu shina la usharika huo. . Uhusiano huu baina ya Yesu na Baba ni dhamana kati ya Wakristo, iwapo pia sisi tumo ndani yake katika umoja huu, na tanuru la moto huu wa upendo katika Utatu Mtakatifu, basi tunaweza kweli kuwa na moyo na roho moja kati yetu kwa sababu upendo wa Mungu unauguza ubinafsi wetu , chuki zetu, utengano na miganyiko yetu ya ndani na nje.

Papa Francisko amesema, iwapo ushariki huu chanzo chake ni mzizi wa upendo ambao ni Mungu, basi pia kuna sababu za kufanya hima kutoa jibu landiyo katika muungano huu na Mungu, maisha ya ushirika wa udugu unaoongoza katika kuwa msharika na Mungu.

Hii ni sehemu ya pili ya usharika, ambayo Papa alitoa msisitizo zaidi, kuwataka watu wa Mungu,kupta uelewa mpana kwamba, imani yetu inahitaji msaada wa wengine , hasa katika nyakati ngumu. Alisema, tazama pia jinsi ilinavyokuwa vizuri kutoa msaada kwa mwingine katika maajabu haya ya imani! Papa alieleza kukemea mwelekea kukubatia tabia ya kutaka kujifungia binafsi, hata katika mazingira ya kidini, kiasi kwamba, inakuwa hata vigumu kwa wengine, hata kuomba msaada wa kiroho, kwa wale wenye uzoefu katika maisha haya ya Kikristu.

Papa alihimiza katika nyakati hizi ngumu ni muhimu kuwa imani kwa Mungu kupitia sala, na wakati huo huo, ni muhimu kupata ujasiri na unyenyekevu kuwa wazi kwa wengine. Papa amekumbusha ushirika wa watakatifu ni familia kubwa, ambapo vipengele vyote ni kusaidia na kusaidiwa yaani kusaidiana mmoja kwa mwingine. Kushirkiana na wengine katika parokia zetu, katika vyama , jumuiya, harakati na vikundi, kama sehemu ya maisha katika safari yetu ya imani, ni kutochoka kuomba msaada wa maombezi na faraja ya kiroho. Ni wakati wetu wa kusikiliza na kuwasaidia wale ambao hawaja jiunga nasi katika safari hii.

Papa alikamilisha Katekesi yake kwa kuchambua kipengele kingine cha usharika wa watakatifu, akisema kwamba, ushariki wa wakatifu huenda zaidi ya maisha ya dunia, inakwenda zaidi ya kifo kwa kuwa huduma milele. Usharika wa kiroho tunaopokea wakati wa Ubatizo hauvunjwi na kifo , lakini umeinuliwa na ufufuko wake Kristu, unao ipeleka roho katika mapito ya utimilifu wa maisha ya milele.

Papa aliendelea kubaini kwmba, kuna dhamana ya kina na isiyokuwa na mwisho kati ya wale ambao bado mahujaji katika dunia hii na wale ambao wamevuka kizingiti cha kifo na kuingia katika umilele. Wote hao huuundwa wakati wa ubatizo hapa duniani,na nafsi hutakatifushwa toharani na kufanywa wenye heri, kuingia katika makazi ya mbinguni ambako ni makazi ya familia moja kubwa. Ushirika huu kati ya nchi na mbinguni ni barabara ya maombezi , ambayo ni aina ya juu ya mshikamano, na pia ni msingi wa maadhimisho ya kiliturujia ya Watakatifu wote na Maadhimisho ya Marehemu wote kama itakavyokuwa siku chache zijazo.

Papa alimalizia kwa kumtaka kila mmoja alifurahie fumbo hili , na kumwomba Bwana neema zake , ili tuweze kuwa karibu zaidi naye na katika usharika na waamini wote, wake kwa waume ndani ya kanisa.
Wito wa Kuombea Iraki
Baada ya Katekesi, Papa akisalimia makundi mbalimbali, pia alilitaja kundi la mahujaji kutoa Iraki ambao walikuwa wakiwakilisha makundi mbalimbali ya kidini, toka yanayojionyesha kama ni utajiri wa Ukristu katika taifa la Iraki . Kundi hili liliongozwa na Kardinali Tauran Rais wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya majadiliano na dini zingine. Papa alitoa wito kwa watu wote kukumbuka kuliombea taifa la Iraki ambalo kila kukicha hukumbana na majanga ya fujo na ghasi za kusitisha zinazofaywa na makundi mabalimbali. Tusali ili Iraki ipate kurejea katika njia ya majadiliano, maridhianao , amani, umoja na utulivu wa kudumu kitaifa.

Sikuku ya Watakatifu woteleo tarehe 01/11/2013

Somo La Kwanza: Ufunuo.7:2-4, 9-14
Wimbo Wa Katikati: Zaburi: 24:1-6 (K) 6
Somo La Pili: 1 Yoh. 3:1-3
Injili: Mathayo 5:1-12
Sikukuu ya Watakatifu wote
Kalenda ya Kanisa Katoliki inajumuisha sikukuu za watakatifu wengi na hata wafia dini. Lakini Novemba mosi, ni sikukuu ya watakatifu wote. Kweli tunasherehekea sikukuu za watakatifu fulani fulani katika siku tofauti lakini Novemba Mosi, tunasherehekea sikukuu ya watakatifu wote, wale tunaowajua na wale tusiowajua. Watakatifu ni wengi na wamefanya kazi nyingi tofauti tofauti lakini zote zikiwa na umuhimu wake katika kuiendeleza na kuikuza imani yetu. Watakatifu ni wengi na hatuwezi kuwajua wote. Hivyo sikukuu hii inawajumuisha pamoja kama kundi moja la watu walioyaishi maisha yao vyema hapa duniani. Sikukuu hii ni kichocheo katika maisha yetu ya imani kwani inatubidi tufuate nyayo zao, tuishe tukimtegemea Mungu zaidi ya chochote. Watakatifu walio pamoja na Mungu mbinguni wanatuombea na kutupa moyo sisi watakatifu tulio safarini kwenda mbinguni. Watakatifu tunao sherekea siku yao leo ni  mashujaa wa imani na kielelezo kwetu, wanatupa moyo kuwa, “Ndiyo kumfuata Kristo kunawezekana.” Kesho Novemba mbili tutawakumbuka marehemu wote. Hawa ni ndugu zetu, wasafiri wenzetu ambao tayari wameiacha dunia hii lakini bado hawajafika mbinguni, wanavikwa mavazi meupe (Ufu.7:9) wanatakaswa kabla ya kuingia mbinguni
Sherehe ya watakatifu wote inatukumbusha kuufuata wito wetu wa kuwa wana wa Mungu. Baada ya mwanadamu kuupoteza utu wake kwa kutenda dhambi, Mungu alimtuma mwanae ulimwenguni ili wale wote wamuaminio wapate ufalme wa milele (Yn. 3:16). Watakatifu wameshaupata ufalme huu wa milele ni wajibu wetu sisi wakristo kufuata mfano wao. Wao walishinda adui wa roho kwa kutumaini neema za Mungu.
Injili ya leo inatuonesha furaha ya watakatifu ilivyo, na njia inayotuwezesha kufika kufika mbinguni. Tunasikia kwamba, “Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao.” Kumbe basi, tukitaka vita vya miaka michache hapa duniani vitatuletea furaha na heri ya milele. Inatubidi basi tuvumilie kabisa katika imani yetu, tujaribu kila tuwezavyo tuvishinda vishawishi kwani Mungu hatajaribu zaidi ya neema aliyotupa kuvishinda vishawishi hivyo.  Watakatifu tunaowakumbuka leo, wanatupenda wanatuombea kwa Mungu  ili tuwe pale walipo, karibu na Mungu na kwenye heri ya milele.  Sikukuu hii haina budi kuamsha matumaini makubwa mioyoni mwetu.
Sala:
Ee Mungu niongezee kiu na njaa ya kuyafanya mapenzi yako na siku moja niwe pamoja na watakatifu mbinguni tukikusifu na kuiombea dunia.
Amin

Thursday, October 31, 2013

Sherehe za Nadhari za kwanza Wanovisi wa Shirika la Carmelite sisters

Wanavosisi watano wa shirika la masista wakarmel wamisionari wa Mt. teresia wa Mtoto Yesu, watarajia kufunga naziri za kwanza za kitawa, ambao ni
  1. Betrice Faustine Urio
  2. Dorice Kalebi Tarimo
  3. Emeritha Joseph Kavishe.
  4. Hemilete Masika Sivatungika
  5. Salange Kavuke Syaghuswa.
 Ibada itafanyika katika Parokia ya Ekaristi Takatifu Lushoto, siku ya Ijumaa ya tarehe 01/11/2013,siku ya  Sherehe ya Watakatifu wote, Na itaongozwa na Askofu wa Jimbo la Tanga: Mhashamu Askofu Anthony Banzi.
 Na baada ya Ibada itafuata Tafrija fupi ya kuwapongeza katika nyumba ya wito wa kitawa ya Jumuiya ya Bikira Maria wa Mlima Karmel - lushoto KIALO,

Mungu awaongeze na Mt. Teresia wa Mtoto Yesu awe Mlinzi wako...

Tuesday, October 29, 2013

MASOMO YA DOMINIKA YA 31 YA MWAKA C. JUMAPILI TAREHE 03/11/13

JUMAPILI DOMINIKA YA 31 ya Mwaka C.
      RATIBA ZA IBADA 
KIGANGO CHA MH. ISIDORI BAKANJA- BOKO.
MISA YA KWANZA 12:15-2:00 ASUBUHI
MISA YA PILI     SAA 2:00-4:00 ASUBUHI
MISA YA TATU SAA 4:00-5:30 ASUBUHI
KIGANGO CHA MT. FRANCIS WA ASIZ-MBWENI 
MISA YA KWANZA SAA 1:10-3:00 ASUBUHI
MISA YA PILI SAA 3:00-4:30 ASUBUHI

KIGANGO CHA MT. RAFAEL-MBWENI MALINDI
IBADA NI MOJA TU ITAANZA SAA 3:00-5:00 ASUBUHI.


KIGANGO CHA ANTHONY WA PADUA-MBWENI TETA
MISA NI SAA 3:00-5:00.




DOMINIKA 31 ya mwaka C (masomo)
SOMO 1. HEK. 11:22- 12:2
Ulimwengu wote mbele zako Bwana, ni kama chembe moja katika mizani, na mfano wa tone moja la umande lishukalo asubuhi juu ya ardhi. Lakini wewe unawahurumia watu wote, kwa sababu unao uweza wa kutenda mambo yote; nawe wawaachilia wanadamu dhambi zao, ili wapate kutubu. Kwa maana wewe wavipenda vitu vyote vilivyopo, wala huchukii kitu cho chote ulichokiumba. Kwa kuwa hungalifanya kamwe kitu cho chote kama ungalichukia; tena kitu cho chote kingaliwezaje kudumu, ila kwa mapenzi yako? Au kitu kisichoumbwa nawe kingaliwezaje kuhifadhika? Lakini wewe unaviachilia vyote, kwa kuwa ni vyako, Ee Mfalme mkuu, mpenda roho za watu; maana roho yako isiyoharibika imo katika vyote. Kwa hiyo wawathibitishia kidogo kodogo hatia yako, wale wanaokengeuka kutoka katikala  njia njema; wawaonya, ukiwakumbusha kwa mambo yale yale wanayokosa, ili waokoke katika ubaya wao, na kukuamini wewe Bwana.

SOMO 2. 2THE. 1:11- 2:2
Kwa hiyo twawaombea ninyi sikuzote, ili Mungu wetu awahesabu kuwa mmekustahili kuitwa kwenu, akatimiza kila haja ya wema na kila kazi ya imani kwa nguvu; jina la Bwana wetu Yesu litukuzwe ndani yenu, nanyi ndani yake, kwa neema ya Mungu wetu na ya Bwana Yesu Kristo. Basi, ndugu, tunakusihini, kwa habari ya kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo, na kukusanyika kwetu mbele zake, kwamba usifadhaishwe upesi hata kuicha nia yenu, wala msisitushwe, kwa roho, wala kwa neno, wala kwa waraka unaodhaniwa kuwa ni wetu, kana kwamba siku ya Bwana imekwisha kuwapo.

INJILI. LK. 19:1-10
Yesu alipoingia Yeriko alipita katikati yake. Na tazama, palikuwa na mtu, jina lake Zakayo, mkubwa mmoja katika watoza ushuru, naye ni tajiri. Huyu alikuwa akitafuta kumwona Yesu ni mtu wa namna gani, asiweze kwa sababu ya umati wa watu, maana ni mfupi wa kimo. Akatangulia mbio, akapanda juu ya mkuyu apate kumwona, kwa kuwa atakuja kupita njia ile. Na Yesu, alipofika mahali pale, alitazama juu, akamwambia, Zakayo, shuka upesi, kwa kuwa leo imenipasa kushinda nyumbani kwako. Akafanya haraka, akashuka, akamkaribisha kwa furaha. Hata watu walipoona, walinung’unika wote, wakisema, ameingia kukaa kwa mtu mwenye dhambi. Zakayo akasimama,  akamwambia Bwana, Tazama, Bwana nusu ya mali yangu nawapa maskini, na ikiwa nimenyang’anya mtu kitu kwa hila namrudishia mara nne. Yesu akamwambia, leo wokovu umefika nyumbani humu, kwa sababu huyu naye ni mwana wa Ibrahimu. Kwa kuwa mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuoka kile kilichopotea.
             
  1.  Jumapili ya tarehe 03/11/13 tutakuwa na kikao cha halmashauri ya VIWAWA Parokia, kikao kitaanza mara baada ya misa ya pili...mahali na parokiani boko fika bila kukosa.
  2. Kigango cha mt. Raphael jumapili tarehe 3/11/2013 ni siku ya mnada wa mavuno waamini wote, ndugu jamaa na marafiki unaalikwa kuungano nao.
  3. jiandae na semina ya vijana wote wa parokia ya boko pamoja na parokia jirani tarehe 23/11/2013 taarifa kamili utazipata jumapili.


  1. tunawakumbusha vijana wote kuendelea kulipa ada kwa maendeleo ya chama chetu..... mapendo sana malipo kwa njia ya benk kwa jina na number hii :viwawa parokia ya boko account no 01524526820100 crdb bank tegeta branch
JIANDAE NA ZIARA YA UINJILISHAJI MWAKA 2014.....................

NCHI YANGU FAHARI YANGU TOUR