Sunday, March 15, 2015

Download Picture za Hija ya Vijana iliyofanyika Parokiani Boko tarehe 14/03/2015 hapa

Dominika ya 4 ya Kwaresima tarehe 15/03/2013(Masomo ya Jumapili)

15

 Marchi
 Jumapili ya 4 ya Kwaresima Masomo ya Mwaka "B".
Mwanzo

Furahi, Jerusalemu, mshangilie ninyi nyote mmpendao; furahini, ninyi nyote mliao kwa ajili yake, mpate kunyonya, na kushibishwa kwa maziwa na faraja.
SOMO  1: 2Nya. 36:14- 16, 19-23
Somo katika kitabu cha pili cha Mambo ya Nyakati.
Wakuu wote wa makuhani, na watu,wakakosa mno sawasawa na machukizo yote ya mataifa; wakainajisi nyumba ya Bwana aliyoitakasa katika Yerusalemu. Naye Bwana, Mungu wa baba zao akatuma kwao kwa mikono wajumbe wake, akiondoka mapema, na kutuma; kwa sababu aliwahurumia watu wake, na makao yake; lakini walidhiaki wajumbe wa Mungu, na kuyadharau maneno yake; na kuwacheka manabii wake, hata alipozidi ghadhabu ya Bwana juu ya watu wake, hata kusiwe na kuponya.
wakaiteketeza nymba ya Mungu wakaubomoa ukuta wa Yerusalemu, wakayateketeza kwa moto majumba yake yote, wakaviharibu vyombo vyake vyote vya thamani. Na wale waliookoka na upanga akawachukua mpaka Babeli; wakamtumikia yeye na wanawe hata kulipoingia milki ya Uajemi; ili kulitimiza neno la Bwana kwa kinywa cha Yeremia, hata nchi itakapofurahia sabato zake; kwa maana siku zote ilipokaa ikiwa ilishika sabato, kutimiza miaka sabini.
Ikiwa katika mwaka wa kwanza wa Koreshi, mfalme wa Uajemi, ili kwamba neno la Bwana alilolisema kwa kinywa cha Yeremia lipate kutimizwa. Bwana akamwamsha roho yake Koreshi, mfalme wa Uajemi, hata akapiga mbiu katika ufalme wake wote, akaiandika pia akisema. Koreshi, mfalme wa Uajemi asema hivi; Bwana, Mungu wa mbinguni, amenipa falme zote za dunia; naye ameniagiza nimjengee nyumba katika Yerusalemu, ulioko Yuda. Basi kila mtu katika nyinyi nyote mlio watu wake, Bwana, Mungu wake, na awe pamoja naye, na akwee.

WIMBO WA KATIKATI. 
Zab. 19:7-10. 
Kiitikio. Ulimi wangu na ugandamane 
            Na kaakaa la kichwa changu, nisipokumbuka..

Friday, March 6, 2015

Masomo ya Dominika ya 3 ya Kwaresima, Jumapili ya tarehe 08/03/2015

08

 Marchi
 Jumapili ya 3 ya Kwaresima Masomo ya Mwaka "B".
Mwanzo

Macho yangu humwelekea Bwana daima, naye atanitoa miguu yangu katika wafu. uniangalie na kunihifadhi, Maana mimi ni Mkiwa na mteswa.
SOMO  1: Kut. 20:1- 17
Somo katika kitabu cha Kutoka.
Mungu alinena maneno haya yote akasema, mimi ni Bwana, Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa. Usiwe na miungu ila mimi. Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu ya mbinguni, wala kilicho chini duniani. Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi, Bwana Mungu wako, ni Mungu wenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wananichukiao, nami nawarehemu maelfu elfu wanipendao, na kuzishika amri zangu. usilitaje bure jina la Bwana, Mungu wako, maana Bwana hatamhesabia kuwa hana hatia mtu alitajaye jina lake bure. Ikumbuke siku ya sabato uitakase. Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote; lakini siku ya saba ni sabato ya Bwana, Mungu wako, siku hiyo usifanye kazi yo yote, wewe wala mwanawako, wala binti yako, wala mtumwa wako,  wala mjakazi wako, wala mnyama wako wa kufuga, wala mgeni aliye ndani ya malango yako. Maana, kwa siku sita Bwana alifanya mbingu, na nchi, bahari , na vyote vilivyomo, akastarehe siku ya saba; kwa hiyo Bwana akaibariki siku ya Sabato akaitakasa. Waheshimu baba na mama yako; siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi upewayo na Bwana, Mungu wako. Usiue. Usizini. Usiibe. Usimshuhudie jirani yako uongo. Usitamani nyumba ya jirani yako, usitamani mke wa jirani yako; wala mtumwa wake, wala mjakazi wake, wala ng'ombe wake, wala punda wake, wala cho chote alicho nacho jirani yako.

WIMBO WA KATIKATI. 
Zab. 19:7-10. 
Kiitikio. Wewe, Bwana, Ndiwe Mtakatifu wa Mungu..

Wednesday, March 4, 2015

Tafakari ya Masomo ya Dominika ya 3 ya Kwaresima


Ni Dominika nyingine tena katika kumega mkate, Neno la Mungu litupalo furaha na tumaini la kweli. Basi karibuni tuendelee na wajibu wetu wa kutafakari Neno la Mungu ili kwa njia hii tuweze kuliweka Neno la Mungu katika matendo na kisha lizae matunda. Ni Dominika ya tatu ya Kwaresima na Neno linatualika kusafisha kwa ndani Hekalu la Mungu, ndiyo mioyo yetu.  

Mpendwa somo la kwanza linatoka katika kitabu cha kutoka likiweka mbele yetu amri za Mungu na linatupa mwaliko wa kushika amri hizo. Mungu anaweka amri ili ziwe ni dira ya kuongoza maisha ya watu. Mpendwa kabla ya kuwekwa amri hizi Waisraeli kwa sababu ya kutotii mapenzi ya Mungu walienda utumwani na hivi anapowatoa katika utumwa huo hapendi tena shida hii itokee na hivi anaweka dira na mwongozo wa mapendo yake.

Mpendwa, amri za Mungu hazikuwekwa tu kwa ajili ya kuzishika au kuzikariri bali ni namna ya kujibu mapendo kwa Mungu, ni njia ya kuelekea furaha ya kimungu, ni njia ya kukutana na Mungu atupendaye daima. Amri za Mungu ni namna ya kuongoza maisha ya watu yakae katika msimamo thabiti wa kimaadili ambao huruhusu amani na uelewano kati ya watu. Basi mpendwa unayenisikiliza shikeni amri za Mungu si tu kwa woga bali kama nyenzo, taa, na dira ya maisha yako.

Katika somo la pili, Mtume Paulo anawaandikia Wakorinto akiwataka watambue kuwa wale wote walioitwa na Kristu na watakaoitwa naye baadaye, kwao Kristu ni nguvu na hekima ya Mungu. Fundisho hili linalenga kuvunjilia mbali fikira potofu za Kiyahudi na Kiyunani. Fikira ambazo zilmweka Kristu katika nafasi ya waliolaaniwa na kwamba Mungu ni jambo la kutafuta kwa akili, ni jambo la kifalsafa tu na hivi hakuna haja ya imani. 

Basi anakukumbusha wewe pia, kuwa uwe macho na wale wote ambao wanafikiria dini au imani ni jambo la miujiza na maajabu. Anakutahadharisha usije ukaanguka katika falsafa ya ujanjaujanja ambao huiweka imani katika kipimo lelemama yaani kutowajibika kwa sababu hakuna mahakama. Imani yetu, Neno la Mungu ni maisha na hivi yatupasa kuweka chachu ya Injili katika maisha ya kijamii. Dini si njia ya kujipatia kazi bali njia ya kwenda mbinguni.

Katika somo la Injili, Bwana yuko Yerusalemu, na ni muda mfupi umebaki ili pasaka ya Wayahudi iwadie. Anaona jinsi wafanya biashara ambavyo wanahangaikia mambo ya nje yaani biashara na wanasahau hekalu la Baba yake. Wanalifanya hekalu sehemu ya kawaida ambapo mambo ya kidunia yanaweza kusonga mbele! Anawakemea na anasafisha hekalu la Baba yake akisema: “msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa nyumba ya biashara” Bwana anatimiza lile andiko lililonenwa na Nabii Zakaria yakuwa Masiha ajapo hakutakuwa na biashara katika nyumba ya Mungu, Zk 14:21. 

Tunafundisha kuondoa ubaya wote moyoni ili Bwana aiingie na kupata kukaa nasi. Atufundisha kuwa mioyo yetu kwa njia ya ubatizo ni hekalu la Mungu, ni kikao cha hekima ya Mungu yaani Roho Mtakatifu. Bwana anatangaza ufalme wa kimasiha na hivi mchanganyo wa uchumi na dini anautupilia mbali.

Sehemu ya pili ya Injili yatufundisha juu ya NGUVU ya BWANA kujenga hekalu kwa siku tatu!, Umungu wake na Habari ya Ufufuko upeo wa wokovu wetu. Anatangaza mwanzo mpya wa ufalme wa Mungu, na anataka wale wote watakaomfuata watambue kuwa hekalu si jengo bali ni ufufuko wa Mwana wa Mungu. Hekalu ni jumuiya ya watu walio na imani ya kweli na wako chini ya Kristu mwenyewe aliye Masiha.

Kumbe mpendwa, ninakusindikizeni daima katika kukua na kutambua wajibu wako wa kusafisha hekalu kwa njia ya kitubio na Ekaristi na kwa namna hiyo Mwana wa Mungu ataweza kuja kwako nawe utazidi kusonga mbele katika safari ya wokovu ukiwa jiwe hai na hekalu safi lisilo na doa.

Nakutakieni heri na baraka za Mungu katika Dominika hii, tukutane tena siku kama ya leo kwa chakula zaidi cha roho zetu. Tumsifu Yesu Kristo.

Ni Padre Richard Tiganya, C.PP.S.

Friday, February 27, 2015

Masomo ya Jumapili ya Pili ya Kwaresima Mwaka B (Tarehe 01/03/2015)

01

 Marchi
 Jumapili ya 2 ya Kwaresima Masomo ya Mwaka "B".
SOMO  1: Mwa. 22:21- 2, 9a, 10-13, 15-18

Somo katika kitabu cha Mwanzo.
Mungu alimjaribu Ibrahimu, akamwambia, Ee Ibrahimu! Naye akasema, Mimi hapa. Akasema, Uchukue mwanao, mwana wako wa pekee, umpendaye, Isaka, ukaende zako mpaka nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya Kuteketezwa huko juu ya mlima mmojawapo nitakaokuambia. Wakafika mahali pale alipoambiwa na Mungu. Ibrahimu akanyosha mkono wake, akakitwaa kisu ili amchinje mwanawe. Ndipo malaika wa Bwana akamwita kutoka mbinguni, akasema, Ibrahimu! Ibrahimu! Naye akasema, Mimi hapa. Akasema, usimnyoshee kijana mkono wako, wala usimtendee neno; kwa maana sasa ninajua ya kuwa unamcha Mungu, iwapo hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee. Ibrahimu akainua macho yake, akaangalia, na tazama, Kondoo mume yuko nyuma yake, amenaswa pembe zake katika kichaka. Basi Ibrahimu akaenda akamtwaa huyo kondoo, akamtoa awe sadaka ya kuteketeza badala ya mwanae. Malaika wa Bwana akamwita Ibrahimu mara ya pili kutoka mbinguni, akasema, Nimeapa kwa nafsi yangu asema Bwana, kwa kuwa umetenda neno hili, wala hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee, katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga uliopo pwani; na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao; na katika uzao wako mataifa yote duniani watajibarikia; kwa sababu umetii sauti yangu.

WIMBO WA KATIKATI. Zab. 116:10, 15-19. 
K. Nitaenenda mbele za Bwana
         Katika nchi za walio hai..

Tafakari ya Masomo ya Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Kwaresima mwaka B wa kanisa( tarehe 1/3/2013)

Ninjesusakuleteeni tafakari ya Neno la Mungu, tukitafakari masomo Dominika ya II ya Kwaresima. Mama Kanisa ametuwekea Neno la Mungu linalotutaka kuimarisha imani yetu kwa Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo.
Mpendwa mwana wa Mungu katika tafakari yetu Dominika ya kwanza ya kwaresima tuliona majaribu dhidi ya Bwana wetu Yesu Kristu na sasa Dominika hii tumewekewa majaribu dhidi ya Ibrahimu. Ibrahimu ni Baba mnyenyekevu ambaye kwanza aliambiwa na Mungu aende nchi asiyoijua na alitii wito huo wa Mungu bila kuangalia usalama wake bali tegemeo katika Mungu anayemwita. Baadaye katika uzee wake akiwa amempata mtoto, mwanae wa pekee Isaka, ghafla anaombwa na Mungu akamtoe sadaka ya kuteketezwa na anaitika bila kusita.
Ibrahimu anakubali ombi la Mungu na anaanza safari kuelekea mlima wa kafara! Mara anapofikia wakati wa shughuli yenyewe malaika wa Bwana anamwambia usitende jambo hilo, tayari ninajua unamcha mwenyezi Mungu. Mara kondoo anaonekana kwa ajili ya kafara badala ya mtoto Isaka! Kwa tendo la imani hii kuu, Mungu anamwahidia Ibrahimu uzao kama nyota za angani, mchanga wa pwani na baraka tele zisizo na mwisho. Kwa sababu ya imani kuu ya Ibrahimu Kanisa humwita Baba wa Imani.
Mpendwa mwanatafakari, kwangu mimi yatosha tu kufurahia matunda ya imani ya Ibrahimu! Kumbe imani inazaa na kujenga upya utajiri usioisha, kizazi kisichoisha na baraka zisizo na mwisho. Basi tufanye nini? Ni kusadiki na kujiimarisha katika kutekeleza mpango wa Mungu daima tulioupokea kwa njia ya ubatizo na hasa wakati huu wa kwaresima. Wote twafahamu kuwa katika kipindi hipi wapo wakatekumeni wanaojiandaa kwa ubatizo, hawa wanaitwa na Mungu kuacha yote ya kipagani, chuki, rushwa, ulevi na mambo kama hayo na wanatakiwa kujikabidhi mikononi mwa yule anayewaita pasipo kuwa mashaka. Wanaalikwa kuiga mfano wa Ibrahimu Baba wa imani anayejitoa bila kuangalia usalama wake, aliye tayari kutoa sadaka ya mwanae bila woga bali akiwa na tumaini yakwamba Mungu atatenda yote.
Katika somo la pili Mtume Paulo anawaandikia Warumi sura ya 8 akiwaimarisha katika imani yao. Anajua wakati fulani wanapata mateso kwa sababu ya imani hiyo, lakini anawaambia cha msingi ni kujenga imani kama ya Ibrahimu ili Mungu akae pamoja nao. Na hivi Mungu akiwa upande wao hakuna nguvu nyingine ya kuweza kuwashinda. Kristu mzaliwa wa kwanza amekuja kwa ajili ya wokovu, amekufa na kufufuka taji ya ushindi dhidi ya dhambi. Kristu ametuletea upendo usiokwisha hata kama tunamkosea, yeye hubaki akitupenda bila kurudi nyuma.
Mpendwa msikilizaji, somo la Injili toka Mwinjili Marko sura 9 linaweka mbele yetu Yesu akiwa mlimani katika faragha pamoja na Yakobo, Petro na Yohane. Jambo la Bwana kuwa mlimani ni alama ya uwepo na utukufu wa Mungu. Daima Mungu anaongea na watu wake akiwa mlimani. Katika mantiki ya kuwa mlimani katika Innjili tunakumbuka mara moja, jinsi Mungu alivyomkabidhi Musa amri akiwa mlimani Sinai (Kut. 24:15). Ni pale mlimani Mungu anajionesha kwa Eliya (1Wafalme 19:8). Jambo la pili ni lile la kugeuka sura na mavazi meupe kumetameta. Weupe ni alama ya Mungu, alama ya furaha na dhihirisho la Kristu aliye Mtakatifu na Mungu.
Alama ya tatu ni ile ya Musa na Eliya wanapozungumza na Yesu. Hawa ni viwakilishi vya Agano la kale yaani sheria na Manabii na hivi kazi yao ni kumweka mbele yetu Bwana na kisha watatoweka. Kutoweka kwao kuna maana yakuwa sasa Agano la Kale limekwisha na linaanza agano Jipya. Mpendwa msikilizaji, kazi yetu waamini ni kutangaza ukuu wa Mungu na baada ya hapo kupisha njia ili Mungu daima akue wakati huo tukipungua.
Mtakatifu Petro anamwomba Bwana wakajenge vibanda vitatu kimoja cha Bwana, vingine vya Musa na Eliya. Hii ni alama ya sikukuu, kama tujuavyo sikukuu ya vibanda kwa Waisraeli ilikuwa ya maana sana na hasa ilipowakumbusha vibanda vyao huko jangwani. Mtume Petro hajaelewa nini hasa mpango wa Bwana, yeye anaona ni sherehe tu, haoni mateso yaliyo mbele ya Bwana.
Wakiwa bado mlimani linatoka wingu na kuwafunika na sauti inatoka juu ikisema “Huyu ni mwanangu mpendwa msikieni yeye! Wingu katika agano la kale liliwaongoza wana wa Israeli kupita jangwani, baharini kumbe uwepo wa wingu ni uwepo wa Mungu na hivi sauti inapotoka juu katika wingu si kitu kingine bali Kristu anadhihirishwa kuwa mmoja na Baba, yeye ni wa juu na wala si wa dunia hii.
Mara hawa Mitume walipotazama hawakuona mtu bali Yesu peke yake ndiyo kusema wale akina Musa na Eliya hawapo, kama nilivyokwishasema kazi yao imekwisha na anabaki Bwana mkuu wa Agano Jipya na la milele. Baada ya matukio hayo yote Bwana pamoja na Mitume wanaanza kushuka chini mlimani na wananaposhuka anawakataza wasimweleze mtu mpaka Mwana wa mtu atakapofufuka toka wafu.
Hii ni siri ya kimasiha, hataki wasimulie mambo yake mpaka wawe wameelewa vizuri mpango wake wa wokovu kwa njia ya msalaba. Daima Mwinjili Marko atajitahidi kumficha Masiha mpaka atakapowekwa wazi katika sura ya 15 ya Injili yake. Tunatafakari maneno ya akida mpagani anayesema baada ya Yesu kukata roho “hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu” Mk. 15:39. Wito kwako wewe unayenisikiliza ni kujifunza vizuri na kumtambua Bwana ni nani, ili utume wako ulale katika uhakika wa Bwana anayekualika daima kumtumikia kwa uchaji. Kumbuka bila toba ya ndani si rahisi kupokea mafundisho ya imani, Neno la Mungu na yote mema yatokayo kwa Mungu.
Mpendwa ninakuageni kwa furaha nikitumaini utaendelea kuongozwa na Neno la Mungu daima. Utaendelea kuongozwa na Mwana wa Mungu kwa maana ndivyo ulivyoamriwa katika injili “ Huyu ndiye Mwanangu mpendwa msikieni yeye”. Tumsifu Yesu Kristu. Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya, C.PP.S.

NCHI YANGU FAHARI YANGU TOUR